Tunachokijua kuhusu miji ya mahandaki ya Iran yaliyojaa makombora

gg

Chanzo cha picha, Noghteh Zan

Muda wa kusoma: Dakika 5

''Ikiwa tutaanza leo na kufichua miji ya roketi kila wiki, mfululizo huu hautaisha ndani ya miaka miwili. Kuna idadi kubwa ya miji hiyo.''

Maneno ya Amir Ali Hajizadeh, kamanda wa Kikosi cha Anga cha Walinzi wa Mapinduzi, alilotoa katika mahojiano na vyombo vya habari vya Iran karibu mwezi mmoja uliopita.

Tangu wakati huo, kauli hii imeenezwa sana katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vinavyounga mkono serikali ya Iran.

Neno "Mji wa Roketi" linatumiwa na Walinzi wa Mapinduzi kumaanisha kambi zao za chini ya ardhi inayohifadhi makombora.

Kambi hizi ziko katika mahandaki iliyo chini ya ardhi, inayojengwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Inadhaniwa kuwa mahandaki haya yako katika milima na maeneo ya kimkakati ya Iran, ikiwa ni sehemu za kutengeneza na kuhifadhi makombora ya balestiki, makombora ya meli, pamoja na silaha nyingine kama ndege zisizo na rubani na mifumo ya ulinzi.

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, Walinzi wa Mapinduzi wameachilia picha za kambi hizi mara chache.

Jumanne iliyopita, Walinzi wa Mapinduzi walitangaza kuwa wangeufichua mji mpya wa makombora, na masaa machache baadaye, picha zilionyesha Amir Ali Hajizadeh na Jenerali Mkuu Mohammad Bagheri, kamanda mkuu wa Jeshi la Iran, wakisafiri kwa gari la kijeshi lililobeba makombora.

Tangazo la mji huu mpya wa makombora linakuja wakati ambapo Iran imekuwa ikiendelea kutishia kulipiza kisasi tangu shambulizi la pili la Israel mnamo Novemba 25.

Hata hivyo, kwa upande mwingine, mkuu wa jeshi la Uingereza, Admiral Tony Radakkin, anaamini kuwa Israel imeiondoa Iran uwezo wake wa kujenga makombora ya balestiki kwa mwaka mmoja.

Ni kipi tunajua kuhusu 'miji ya makombora' ?

gg

Chanzo cha picha, Noghteh Zan

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Iran imekuwa ikifichua makombora ili kuonyesha nguvu zake na kukabiliana na vitisho kutoka kwa mataifa kama Israel na Marekani, na kuviweka kama mafanikio makubwa katika sekta ya silaha za kijeshi, ingawa imekuwa ikificha programu na kambi zake za makombora.

Walinzi wa Mapinduzi wanadai kuwa wana kambi nyingi za makombora zilizojengwa katika mahandaki kupitia 'uhandisi maalum'.

Mnamo 2015, kwa mara ya kwanza, Amir Ali Hajizadeh alitangaza uwepo wa kambi za makombora "mita 500 chini ya ardhi" katika mikoa mbalimbali.

Hakuna taarifa kamili inayopatikana kuhusu lini kambi hizi zilijengwa, lakini Mehdi Bakhtiari, mwandishi wa habari wa Fars News Agency, alieleza katika mahojiano na Al Jazeera kuwa "kambi ya kwanza ya makombora ya chini ya ardhi nchini Iran ilijengwa mwaka 1984, wakati Iran ilianza programu yake ya makombora."

Programu ya makombora ya Iran ilianza katikati ya Vita vya Iran-Iraq kwa msaada wa mataifa kama Korea Kaskazini na China.

Vyombo vya habari vya Kiirani na Walinzi wa Mapinduzi hadi sasa vimechapisha picha za kambi kadhaa za makombora ya chini ya ardhi wanayoita 'miji ya makombora ya Walinzi wa Mapinduzi'.

Hata hivyo, maeneo halisi ya kambi hizi hayajawahi kutangazwa rasmi.

Lakini maeneo ambayo yalizinduliwa hivi karibuni ni kambi iliyoko mlima wa Zagros, jiji la Bushehr na pia katika mkoa wa Hormozgan.

Pia unaweza kusoma:

Moja kati ya video zilizosambaa zimeonyesha ushoroba ukiwa umejaa makombora na pia eneo ambalo makombora hayo hupitia yakisafrishwa kupitia treni iliyo chini ya handaki.

Miji hii ya makombora imekuwa ikionyeshwa mara kwa mara, hasa wakati walinzi wa Mapinduzi walipovamia ISIS nchini Syria au walipofanya operesheni ijulikanayo 'Operation True Promise One and Two'.

Mnamo Machi 2020, Walinzi wa Mapinduzi walizindua 'mji wa kombora la baharini' kwenye pwani ya Ghuba ya Uajemi.

Mahali pa kituo hicho hakikutangazwa, lakini vyombo vya habari vya ndani katika mkoa wa Hormozgan viliripoti kuhusu kambi hiyo.

Kamanda Mkuu wa Walinzi wa Mapinduzi Hossein Salami alisema kuhusu 'mji huu wa makombora' kwenye pwani ya Ghuba ya Uajemi kwamba 'kiwanda hiki ni mojawapo ya vituo kadhaa vinavyohifadhi makombora ya kimkakati ya Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi.'

Mbali na Jeshi la Wanaanga la IRGC, Jeshi la Wanamaji la IRGC pia lina makombora ya kutoka ufukweni hadi baharini, nchi kavu hadi baharini, na kutoka bahari hadi bahari, kama vile makombora ya 'Ya Ali' na 'Hawiza'.

Idadi kamili ya kambi hizo za makombora za siri za Iran hazijulikani, lakini Ahmad Reza Pourdastan, Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Kistratejia na Utafiti cha jeshi la Iran mnamo Januari 2015 alisema mbali na Walinzi wa Mapinduzi, jeshi la Iran pia lina miji mingi ya makombora ya siri.

gg

Chanzo cha picha, Noghteh Zan

Kwa mujibu wa Amir Ali Hajizadeh, kamanda wa Kikosi cha Anga cha Walinzi wa Mapinduzi, "Ikiwa watafichua mji mmoja wa makombora kila wiki, mfululizo huu hautaisha ndani ya miaka miwili."

Hii inaashiria kuwa Iran inaweza kuwa na miji takriban 104 ya makombora, ingawa hili ni jambo lisiloweza kuthibitishwa kwa urahisi kutokana na ukosefu wa taarifa za kina kuhusu hilo.

Vyanzo vinavyokaribu na Walinzi wa Mapinduzi pia vimeripoti uwepo wa 'miji mia ya makombora' nchini Iran.

Mji wa makombora uliozinduliwa hivi karibuni ulionyesha makombora kama vile Khyber Shakan, Hajj Qasim, Imad, na Sajjeel.

Kombora la balestiki la Emad lilikuwa miongoni mwa makombora yaliyotumika katika shambulizi la Iran dhidi ya Israel, likiharibu Kituo cha Anga cha Navatim kilichoko katikati ya Israel.

gg

Chanzo cha picha, Tasnim

Kwanini Iran imejenga miji ya makombora

Lengo la miji hii ya makombora ni kupinga mashambulizi ya angani na kujikomboa, kwa kuwa Iran imefanikiwa kwa kiasi fulani kuonyesha kwamba ina uwezo wa kudumisha uwezo wake wa makombora hata wakati ambapo kambi zake za makombora ardhini zinashambuliwa.

Katika mahojiano na Al Jazeera, Mehdi Bakhtiari alitangaza uwepo wa miji ya makombora ya siri nchini Iran ambayo itawashangaza maadui.

Kwa mujibu wa wachambuzi, kambi hizi, au kama Walinzi wa Mapinduzi wanavyoielezea, "miji ya makombora ya chini ya ardhi," inaweza kuwa maandalizi kwa vita visivyo vya kawaida, kwani inaruhusu makombora kurushwa kutoka maeneo yasiyojulikana na kuchanganya adui kuhusu uwezo wa Iran.

Kwa mujibu wa makamanda wa Walinzi wa Mapinduzi, miji hii ya makombora siyo tu sehemu za kuhifadhi makombora, bali baadhi yao ni "vituo vya kutengeneza makombora na kuandaa makombora kabla ya kuwa tayari kwa mashambulizi."

Mnamo Juni 2017, Amir Ali Hajizadeh alitangaza uwepo wa viwanda vitatu vya chini ya ardhi nchini Iran vinavyozalisha makombora kwa ajili ya Walinzi wa Mapinduzi.

Mada zinazofanana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi