Zifahamu kambi za kijeshi za Marekani Mashariki ya Kati zinazolengwa na Iran

.

Chanzo cha picha, Allen J. Schaben / Los Angeles Times via Getty Images

Maelezo ya picha, USS Carl Vinson ni mojawapo ya meli za kubeba ndege za Marekani zinazofanya kazi katika eneo hilo.
Muda wa kusoma: Dakika 5

Marekani inamiliki kikosi muhimu cha kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati, na wanajeshi katika zaidi ya nchi kumi mbali na meli za kijeshi katika maji ya eneo hilo. Kwa jumla, Marekani ina kambi za kijeshi katika angalau maeneo 19, nane kati yao inachukuliwa kuwa kambi za kudumu na wachambuzi wengi wa kikanda.

Kambi hizi kwa sasa zina wanajeshi 40,000, wakiwemo raia, pamoja na mifumo ya ulinzi wa anga, ndege za kivita, na meli za kivita.

Kufuatia shambulio la Marekani dhidi ya vituo vitatu vya nyuklia nchini Iran, vituo hivyo vimekuwa shabaha ya kulipiza kisasi kwa Iran, huku serikali ya Iran ikiwa tayari imeonya kwamba "inahifadhi chaguzi zote" kujibu.

Uwepo wa Marekani katika eneo hilo ambalo wakati wa vita vya Iraq na Afghanistan ulifikia zaidi ya wanajeshi 160,000 uliimarishwa mwaka jana kutokana na mvutano kati ya Israel na Iran na kujibu mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Wahouthi wa Yemen dhidi ya meli za kibiashara na kijeshi katika Bahari Nyekundu.

Lakini katika siku za hivi karibuni, kwa kutarajia mashambulizi na kulinda wafanyakazi katika tukio la jibu kubwa la Tehran, Marekani ilikuwa imeomba kuondoka kwa hiari kwa wanajeshi kutoka kambi za kikanda.

Kwa jumla, Marekani inamiliki vituo vya kijeshi katika angalau maeneo 19 katika eneo hilo, nane kati ya hayo wachambuzi wengi wa kikanda wanaona kuwa za kudumu: Bahrain, Misri, Iraq, Israel, Jordan, Kuwait, Qatar, Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, na Syria.

Kulingana na kundi huru la utafiti la Baraza la Mahusiano ya Kigeni, jeshi la Marekani pia linatumia kambi kubwa nchini Djibouti na Uturuki, ambazo ni sehemu ya amri nyingine za kikanda lakini mara nyingi huchangia pakubwa katika operesheni za Marekani katika Mashariki ya Kati.

Ifuatayo ni orodha ya kambi kuu za Marekani katika eneo hilo, ambazo zote ziko chini ya Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM).

Bahrain

Ufalme huu mdogo ni nyumbani kwa Kikosi cha Tano cha cha Wanamaji wa Marekani , kinachohusika na vikosi vya wanamaji katika Ghuba ya Uajemi, Bahari Nyekundu, Bahari ya Arabia, na pwani ya Afrika Mashariki kusini hadi Kenya.

Kituo hicho kinajulikana kama Shughuli ya Usaidizi wa Wanamaji Bahrain na pia kina makao makuu ya Kamandi Kuu ya Kikosi cha Wanamaji cha Marekani.

Wanajeshi 9,000 wa Marekani wametumwa kwenye kisiwa hicho.

Meli kadhaa za Jeshi la Wanamaji la Marekani ziko katika bandari ya Bahrain, ambayo ina maji yenye kina kirefu yanayoweza huruhusu kuingia kwa meli za kina kirefu, kama vile UUS Carl Vinson na nynegine za kubeba ndege za kivita .

Pia miongoni mwao ni vyombo vinne vya kusafisha maeneo ya mgodi na vyombo viwili vya msaada wa vifaa vya kimkakati.

Walinzi wa Pwani wa Marekani pia wana meli nchini humo, zikiwemo boti sita zenye kasi , kulingana na AFP.

Kuwait

Kuwait ni mojawapo ya nchi zenye idadi kubwa ya kambi za kijeshi za Marekani katika eneo hilo.

Miongoni mwao ni Camp Arifjan, nyumbani kwa makao makuu ya kitengo cha CENTCOM cha Jeshi la Marekani.

Kituo hiki kinatumika kama kitovu cha uendeshaji na vifaa kwa vikosi vya Marekani katika Mashariki ya Kati, kikiwa na akiba kubwa ya nyenzo za kusambaza shughuli mbalimbali.

Pia kuna Kambi ya Anga ya Ali al-Salem, ambapo ni nyumbani kwa kitengo cha 386 cha Usafiri wa Anga, "kitovu kikuu cha usafirishaji wa ndege na lango la kupeleka nguvu za kivita kwa vikosi vya pamoja na vya muungano katika kanda," kulingana na AFP.

Marekani vilevile ina ndege zisizo na rubani, ikiwemo ile ya MQ-9 Reaper, huko Kuwait.

Katika Kambi ya Arifjan na Ali al-Salem Air Base pekee, jeshi la Marekani limetuma wanajeshi 13,500, kulingana na Idara ya masuala ya kigeni ya taifa hilo .

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Trump alitembelea wanajeshi wa Marekani katika kambi ya Al Udeid nchini Qatar mwezi Mei mwaka jana.

Qatar

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kambi ya Anga ya Al Udeid nchini Qatar ndiyo kubwa zaidi katika eneo hilo, ina makao makuu ya Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) na kikosi chake cha anga.

Al Udeid imekuwa muhimu katika operesheni za kijeshi za Marekani huko Iraq, Syria na Afghanistan.

KItengo cha 379 cha Usafiri wa Anga wa Jeshi la Anga la Marekani pia kimetumwa huko.

Rais Donald Trump aliitembelea kambi hiyo tarehe 15 mwezi Mei wakati wa ziara yake ya Mashariki ya Kati.

Katika siku za hivi karibuni, Washington iliondoa makumi ya ndege kutoka kwa uwanja wa ndege wa Al Udeid, kama inavyoonyeshwa kwenye picha za satelaiti, na kuibua shaka kwamba ilitaka kuzilinda dhidi ya mashambulio ya Iran kujibu uingiliaji wa Marekani.

Kati ya ndege 40, zikiwemo za usafiri na ndege za upelelezi za C-130 Hercules, ambazo zingeweza kuonekana kwenye picha zilizochapishwa na Planet Labs mnamo Juni 5, ni tatu pekee zilizosalia wiki mbili baadaye, kulingana na AFP, ambayo iliweza kuchambua picha hizo.

Kuna takriban wanajeshi 10,000 wa Marekani nchini Qatar.

Umoja wa Falme za Kiarabu UAE

Wanajeshi wa Marekani wanamiliki Kambi ya wanaanga ya Al Dhafra katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kituo cha kimkakati kinachojishughulisha na upelelezi, kukusanya taarifa za kijasusi na kuunga mkono operesheni za anga.

Kambi hiyo ni nyumbani kwa kitego cha wanaanga cha 380, kikosi kinachojumuisha vikosi 10 vya ndege na pia ndege zisizo na rubani kama vile MQ-9 Reapers.

.

Chanzo cha picha, United States Air Force via EPA

Maelezo ya picha, Ndege isiyo na rubani ya RQ-4 Global Hawk ya upelelezi katika Kambi ya Anga ya Al Dhafra katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

Iraq

Marekani ilikuwa na hadi wanajeshi 160,000 waliotumwa nchini Iraq katika kambi zaidi ya 500 wakati wa uvamizi uliompindua Saddam Hussein, uliodumu kutoka 2001 hadi 2003.

Hata hivyo kwasasa kuna wanajeshi 2,500 wa Marekani walioko nchini humo, na Washington inafanya mazungumzo na serikali ya Baghdad ili kuwaondoa polepole.

Wanajeshi hawa ni sehemu ya muungano wa kimataifa unaopambana na kundi la wanajihadi la Islamic State, na wanafanya hivyo hasa kutoka katika kambi mbili za anga, Al Asad na Erbil, huko Kurdistan Iraq.

Kambi hizi, pamoja na zingine ndogo ambazo zimesalia wazi nchini, zimekuwa zikilengwa na vikundi vya washirika wa Iran tangu vita vya Gaza vilipoanza mnamo Oktoba 2023.

Syria

Uwepo wa jeshi la Marekani nchini Syria pia unahusishwa na mapambano dhidi ya Islamic State, ambayo yaliibuka kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka nchini humo mwaka 2011 na hatimaye kuteka sehemu kubwa ya ardhi ya Syria na Iraq.

Jeshi la Marekani lina takriban wanajeshi 2,000 katika kambi mbalimbali nchini Syria, wakishirikiana na vikosi vya usalama vya ndani ili kuzuia kuibuka tena kwa kundi hilo la kijihadi.

Mwezi Juni, Washington ilitangaza kuwa itapunguza idadi ya kambi za kijeshi inazoendesha nchini humo kutoka nane hadi moja, na kwamba itabadilisha sera zake nchini humo "kwa sababu hakuna hata moja iliyofanya kazi."

Trump bila kutarajia aliamua kuondoa vikwazo dhidi ya Syria mwezi uliopita wa Mei, na utawala wake umeonyesha nia ya kufanya mazungumzo na kiongozi mpya wa nchi hiyo, Ahmed Sharaa, ambaye wanamgambo wake walifanikiwa kumpindua Bashar al-Assad mwishoni mwa 2024.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla