Kwa nini majibu ya Iran dhidi ya shambulio la Marekani yanaweza kuwa tofauti safari hii

Chanzo cha picha, Mike Blake/Reuters
Kuwasili kwa manowari ya kubeba ndege ya Marekani, USS Abraham Lincoln, katika eneo la operesheni la Kamandi ya Kati ya Marekani karibu na maji ya Iran, kumezidisha hisia kwamba huenda makabiliano makubwa ya kijeshi yanakaribia kutokea.
Hatua hii ya kijeshi inajiri wakati Iran inapitia mojawapo ya vipindi vigumu zaidi katika historia yake ya hivi karibuni, ikikabiliwa na ukandamizaji mkubwa na wa kikatili dhidi ya maandamano ya wananchi.
Hali hii inaonyesha wazi kuwa Washington na Tehran huenda ziko karibu zaidi na mapambano ya moja kwa moja kuliko ilivyokuwa wakati wowote katika miaka ya karibuni.
Viongozi wa Iran wanajikuta katika hali ya mashinikizo makubwa kutoka pande mbili: maandamano yanayozidi kuongezeka na kudai kuangushwa kwa utawala, pamoja na rais wa Marekani ambaye kwa makusudi anaacha nia yake ikiwa haijulikani wazi.
Mchanganyiko huu umeongeza wasiwasi si tu Tehran, bali pia katika eneo lote la Mashariki ya Kati, ambalo tayari linajulikana kwa ukosefu wa utulivu wa kudumu.
Katika mazingira haya, majibu ya Iran kwa shambulio lolote la kijeshi la Marekani huenda yasifuate mtindo wa tahadhari na usawazishaji ulioshuhudiwa katika makabiliano ya awali na Washington.
Vitisho vya hivi karibuni vya Rais Donald Trump vinakuja katika wakati ambao Jamhuri ya Kiislamu iko katika mvutano mkubwa wa ndani, kufuatia ukandamizaji mkali wa machafuko ya kisiasa na kijamii.
Kwa mantiki hiyo, shambulio lolote la Marekani kwa sasa lina hatari kubwa zaidi ya kusababisha mzozo kuongezeka kwa kasi, ndani ya Iran na katika eneo zima.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ameonya kwamba shambulio lolote la Marekani litasababisha vita vya kikanda, huku Marekani ikiendelea kuimarisha uwepo wake wa kijeshi katika eneo hilo.
"Wamarekani wanapaswa kufahamu kuwa wakianzisha vita, safari hii haitakuwa vita ya kawaida, bali vita ya kikanda," alisema Khamenei, kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim.
Katika miaka ya hivi karibuni, Tehran imekuwa ikipendelea majibu ya kulipiza kisasi yenye mipaka na yaliyopimwa kwa uangalifu.
Baada ya mashambulio ya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran mnamo tarehe 21 na 22 Juni 2025, Iran ilijibu siku iliyofuata kwa mashambulio ya makombora dhidi ya Kituo cha Anga cha al-Udeid nchini Qatar, kinachotumiwa na majeshi ya Marekani.
Kwa mujibu wa Rais Trump, Iran ilitoa onyo mapema kabla ya mashambulio hayo, hatua iliyoruhusu mifumo ya ulinzi wa anga kudhibiti makombora mengi.
Hakuna vifo vilivyoripotiwa.
Mashambulio hayo yalitafsiriwa kama ujumbe wa kisiasa na kijeshi uliolenga kuonyesha msimamo wa Iran, bila kuchochea vita vikubwa.
Mtindo huu wa kujibu kwa tahadhari ulionekana pia Januari 2020, wakati wa muhula wa kwanza wa Donald Trump.
Tarehe 3 Januari mwaka huo, Marekani ilimuua Qassem Soleimani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq.
Iran ililipiza kisasi siku tano baadaye kwa kushambulia kwa makombora kambi ya anga ya Ain al-Asad nchini Iraq, inayotumiwa na majeshi ya Marekani.
Kama ilivyokuwa katika tukio la hivi karibuni, Tehran ilitoa onyo mapema.
Hakuna wanajeshi wa Marekani waliouawa, ingawa kadhaa waliripotiwa kupata majeraha ya ubongo kutokana na mshtuko wa milipuko.
Matukio haya yaliimarisha dhana kwamba Iran ilikuwa ikijaribu kudhibiti kiwango cha mvutano, badala ya kuuchochea. Hata hivyo, hali ya sasa ni tofauti kwa kiasi kikubwa.

Chanzo cha picha, Reuters
Iran inajipata katika mojawapo ya mawimbi makubwa zaidi ya machafuko ya ndani tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Kiislamu mwaka 1979.
Maandamano yaliyozuka mwishoni mwa Desemba na mwanzoni mwa Januari yalikandamizwa kwa nguvu kubwa.
Mashirika ya haki za binadamu na wataalamu wa afya wameripoti vifo vya maelfu ya raia, huku wengi zaidi wakijeruhiwa au kukamatwa.
Uhakiki wa idadi kamili ya vifo umekuwa mgumu kutokana na ukosefu wa takwimu na kukatika kwa huduma ya intaneti kwa zaidi ya wiki mbili.
Mamlaka za Iran zimekanusha kuhusika moja kwa moja na vifo hivyo, zikilaumu kile walichokiita "makundi ya kigaidi" na kuituhumu Israel kwa kuchochea machafuko.
Mtazamo huu umeungwa mkono na ngazi za juu za dola.
Katibu wa Baraza la Juu la Usalama wa Taifa alisema kuwa maandamano hayo yanapaswa kutazamwa kama mwendelezo wa vita vya siku 12 dhidi ya Israel mwaka uliopita.
Kauli hii inaonyesha msimamo wa serikali wa kuweka usalama mbele ya mazungumzo, na huenda ilitumika kuhalalisha kiwango kikubwa cha ukandamizaji.
Ingawa ukubwa wa maandamano ya wazi umepungua, bado hayajakomeshwa kabisa. Malalamiko ya wananchi hayajapatiwa ufumbuzi, na pengo kati ya jamii na mfumo wa utawala halijawahi kuwa pana kiasi hiki.
Mnamo tarehe 8 na 9 Januari, taarifa zinaeleza kuwa vikosi vya usalama vilipoteza udhibiti wa baadhi ya maeneo katika miji kadhaa, kabla ya kurejesha hali kwa kutumia nguvu kali.
Tukio hili linaonekana kuwatia hofu kubwa viongozi wa nchi, na utulivu uliokuja baadaye uliwekwa kwa mabavu, si kwa maridhiano, jambo linaloifanya hali kubaki tete.
Kauli kali na zisizolegeza msimamo
Katika mazingira haya, aina na ukubwa wa shambulio lolote la Marekani vinakuwa na uzito mkubwa.
Shambulio dogo linaweza kuiruhusu Marekani kudai ushindi wa kijeshi bila kuchochea vita vikubwa, lakini pia linaweza kuwapa viongozi wa Iran kisingizio cha kuanzisha duru mpya ya ukandamizaji wa ndani.
Kwa upande mwingine, kampeni kubwa ya kijeshi ya Marekani inayodhoofisha au kupooza dola ya Iran inaweza kuisukuma nchi hiyo katika machafuko makubwa.
Kuporomoka kwa mamlaka ya kati katika nchi yenye zaidi ya watu milioni 90 kunaweza kusababisha kipindi kirefu cha vurugu, mapigano ya makundi na athari mbaya kwa eneo lote, athari ambazo zinaweza kudumu kwa miaka mingi.
Hatari hizi zinaeleza kwa nini kauli za Tehran zimekuwa ngumu zaidi.
Viongozi wa juu wa Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, jeshi la kawaida, na wanasiasa wakuu wameonya kuwa shambulio lolote la Marekani, bila kujali ukubwa wake, litachukuliwa kama tangazo la vita.
Kauli hizi zimezitia wasiwasi nchi jirani, hasa mataifa ya Ghuba yanayohifadhi kambi za kijeshi za Marekani.
Jibu la haraka la Iran lingeziweka nchi hizo pamoja na Israel katika hatari ya moja kwa moja, na hivyo kufungua uwezekano wa mzozo kusambaa nje ya mipaka ya Iran na Marekani.
Marekani nayo inakabiliwa na mipaka yake ya kisiasa.
Trump amewaonya mara kwa mara viongozi wa Iran dhidi ya kutumia nguvu kwa waandamanaji, na wakati wa kilele cha machafuko alitangaza kuwa "msaada unakuja," kauli iliyosambaa kwa kasi ndani ya Iran na kuongeza matarajio miongoni mwa waandamanaji.

Chanzo cha picha, Maxar Technologies/EPA
Pande zote mbili zinafahamu mizani ya nguvu na mazingira ya kimkakati.
Trump anatambua kuwa Iran leo ni dhaifu kijeshi ikilinganishwa na ilivyokuwa wakati wa vita vya siku 12, na Tehran inajua kuwa rais wa Marekani hana hamu ya vita vikubwa vya wazi.
Hata hivyo, ufahamu huu unaweza pia kuzaa makadirio potofu na hatari, kila upande ukikosea kutafsiri uwezo au nia ya mwenzake.
Kwa Trump, changamoto ni kupata matokeo yanayoweza kuwasilishwa kama ushindi bila kuisukuma Iran katika ukandamizaji mpya au machafuko makubwa.
Kwa viongozi wa Iran, hatari kubwa iko katika muda na mtazamo.
Mtindo wa awali wa kulipiza kisasi kwa ishara huenda usitoshe tena ikiwa viongozi wataamini kuwa hatua za haraka ni muhimu kurejesha udhibiti wa ndani na hofu ya kuzuia mashambulio ya nje.
Hata hivyo, jibu la haraka linaongeza kwa kiasi kikubwa hatari ya makosa ya kimkakati na mzozo wa kikanda ambao wachache wanaweza kuhimili.
Hatimaye, kushindwa kupata uwiano sahihi kutaathiri si tu serikali husika, bali pia mamilioni ya raia wa kawaida wa Iran na mustakabali wa eneo lote.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












