Muhoozi Kainerugaba - Jenerali mashuhuri wa Uganda mwenye 'uchu' wa madaraka

Chanzo cha picha, AFP
Akiwa amefunzwa katika vyuo vya kijeshi vya hadhi duniani kote, mtoto wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni amegeuka kuwa jenerali wa jeshi ambaye amepata sifa mbaya kwa ujumbe wake wa kisiasa katika mtandao wa Twitter ambazo zimepelekea siasa za ndani na za kikanda kuingia doa.
Jenerali Muhoozi Kainerugaba alijigamba kwamba jeshi lake linaweza kuuteka mji mkuu wa Kenya, Nairobi, chini ya wiki mbili, na kuwaonya wapinzani wa Misri kwamba Uganda itaingia katika vita vyovyote upande wa taifa la Afrika Kaskazini, huku kwa upande wa ndani akionyesha nia ya kumrithi baba yake mwenye umri wa miaka 78.
Amekaidi agizo la kuacha kuweka ujumbe wenye utata kwenye Twitter kwa kuandika: ‘’Mimi ni mtu mzima na HAKUNA MTU atanipiga marufuku kwa chochote!’’
Mwandishi wa habari mpelelezi wa Uganda Solomon Serwanjja alisema ujumbe huo wa Twitter ulionyesha kwamba Jenerali Kainerugaba - ambaye kwa kawaida hujulikana kama Muhoozi, maana yake ni ‘’mlipiza kisasi’’ - ni afisa wa kijeshi anayehudumu na malengo ya kisiasa.
‘’Anataka kuwathibitishia wafuasi wake kwamba anaweza kujitegemea na kufanya maamuzi peke yake. Hata hivyo, anabaki kuwa mtoto wa kiume anayepaswa kuzingatia maagizo ya baba yake,’’ alisema.
Akiwa madarakani tangu 1986, Bw Museveni amekuwa akishukiwa kwa muda mrefu kumuandaa jenerali huyo mwenye umri wa miaka 48 kumrithi ili kukita kile ambacho wakosoaji wanakiita utawala wa kifalme nchini Uganda.
‘’Familia hiyo inadhibiti Uganda. Mama yake yuko kwenye baraza la mawaziri, na yeye ndiye mtoto wa mfalme, akisubiri kumrithi baba yake,’’ alisema Peter Kagwanja wa Taasisi ya Sera ya Afrika yenye makao yake makuu nchini Kenya.
Kama Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alivyofanya, jenerali huyo anatumia Twitter kuongeza wasifu wake.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
‘’Prof Kagwanja anamchukulia kama ‘’mchochezi’’ ambaye anatuma ujumbe kwenye Twitter ili kuweza kufikia viongozi wa Afrika, na kuendeleza malengo ya kisiasa ya Uganda: ‘’Muhoozi anachokoza, kisha baba yake anapanga aende kuomba msamaha, na kwa njia hii anaingizwa kwenye miduara ya viongozi.’’
Mkakati huu ulionekana wakati Jenerali Kainerugaba alipoikashifu serikali ya Ethiopia alipojitokeza kuunga mkono sana Misri wakati ambapo iko kwenye mzozo mkali na Ethiopia kuhusu bwawa kubwa linalojengwa kwenye mkondo wa Mto Nile.
Baadaye alisifu ari ya ‘’kupata ushindi’’ ya vikosi vya Tigray vilivyohusika katika vita vya kikatili na wanajeshi wa shirikisho la Ethiopia, na kusema kwamba ‘’wale waliobaka dada zetu wa Tigray na kuua ndugu zetu lazima waadhibiwe!’’
Badala ya kumgeuza kuwa mtu wa nje nchini Ethiopia, ujumbe huo wa Twitter ulimfungulia njia ya kuzuru nchi hiyo kukutana na Waziri Mkuu Abiy Ahmed na maafisa wakuu wa kijeshi mapema mwaka huu.
Ilipelekea jenerali huyo kubadilisha wimbo wake, na kuanza kumsifu Bw Abiy - ambaye, akiwa na umri wa miaka 46, ni mdogo kwake - kama ‘’ndugu yangu’’, na kusema kwamba ‘’tunaamini katika suluhu za Afrika kwa matatizo ya Afrika’’, akielezea mtazamo sawa na ule wa kiongozi wa Ethiopia kusisitiza sifa zake kama mwana-Afrika.
Baba na mwana wanafanya kazi pamoja
Jenerali Kainerugaba anapenda kutumia maneno ya kifamilia, akifichua katika mchakato huo jinsi anavyowaona viongozi mbalimbali wa Afrika na uhusiano wake nao ukoje.
Anamtaja Rais wa Rwanda Paul Kagame kama ‘’mjomba wangu’’, na amemtembelea katika shamba lake.
Mzozo uliposababisha kufungwa kwa mpaka wa Rwanda na Uganda, alijaribu kurekebisha uhusiano kwa kupanga mkutano kati ya babake na ‘’mjomba’’.

Chanzo cha picha, AFP
Ilipofika Kenya, Jenerali Kainerugaba aliweka ujumbe kwenye Twitter kwamba alizungumza na Rais wa zamani Uhuru Kenyatta baada ya kujiuzulu baada ya kumalizika kwa mihula yake miwili mwezi Agosti: ‘’Tatizo langu pekee na kaka yangu mpendwa ni kwamba hakusimama kwa ajili ya muhula wa tatu. Tungeshinda kirahisi!’’
Hili lilizua taharuki miongoni mwa Wakenya kwenye Twitter, ambao walimshutumu jenerali huyo kwa kujaribu kuhujumu demokrasia yao.
Prof Kagwanja alisema hatua ya jenerali huyo kuingilia kati ilikuja kinyume na hali ya uhusiano mbaya huku rais wa Uganda akipinga Bw Kenyatta kumuunga mkono mwanasiasa mkongwe wa upinzani Raila Odinga katika kampeni za uchaguzi, akimwona kama ‘’mradi wa ubeberu’’ wa mataifa ya Magharibi.
Bw Museveni alimpendelea William Ruto, ambaye alishinda urais baada ya mchuano mkali.
Nia ya ujumbe huo wa Twitter ilikuwa kumfurahisha Kenyatta ili asimpoteze kwa sababu bado ni muhimu katika siasa za Kenya,’’ Prof Kagwanja alisema.
‘’Baba na mwana walikuwa wakifanya kazi pamoja. Muhoozi anajifanya kuwa kinyume na baba yake, kuwa mtu wa machafuko - hiyo inamfanya baba yake aonekane mzuri.’’
Jenerali Kainerugaba pia alitoa ujumbe wa kichochezi zaidi kwa wafuasi wake zaidi ya 600,000, akisema kwamba haitatuchukua sisi, jeshi langu na mimi, wiki 2 kuuteka [mji mkuu wa Kenya] Nairobi’’.
Prof Kagwanja alisema ujumbe huo uliibua kumbukumbu za madai ya dikteta wa wakati huo wa Uganda Idi Amin katika miaka ya 1970 kwamba sehemu kubwa ya Kenya ni ya Uganda, na ilikuwa ukumbusho wa haja ya kutatua mzozo wa muda mrefu kati ya Uganda na Kenya kuhusu kisiwa cha Migingo.
Alipokabiliwa na upinzani kutoka kwa Wakenya ambao walimkanyaga kwa matamshi yake ‘’ya kizembe’’, kamanda huyo wa jeshi aliwataka ‘’watulie’’: ‘’Sitawahi kulipiga jeshi la Kenya kwa sababu baba yangu aliniambia nisijaribu kamwe!’’
Serikali ya Kenya haikuzungumza hadharani, lakini huku mabishano hayo yakiendelea kushika kasi, Bw Museveni alilazimika kumpigia simu Bw Ruto ili kumuomba msamaha kwa “kosa” la mwanawe.
Hili lilifungua njia kwa Bw Ruto kuhudhuria sherehe za kuadhimisha miaka 60 ya uhuru wa Uganda, na kwa Jenerali Kainerugaba kutoa ‘’uungwaji mkono usio na kikomo na kamili katika kutatua matatizo ya zamani’’.
Huku jeshi la Uganda pia likielezea wasiwasi wao kuhusu ‘’jenerali wao wa kutwiti’’, Bw Museveni aliamua kuwaweka sawa kwa kumfukuza kama kamanda wa vikosi vya nchi kavu.
‘’Majenerali wakuu walizungumzia suala la nidhamu, ambalo ni la msingi katika jeshi, na Bw Museveni hakuwa na chaguo,’’ Bw Serwanjja alisema.
‘’Kama angekuwa mtu mwingine, wangefikishwa mahakamani.’’
Lakini Bw Museveni pia alichukua fursa hiyo kumpandisha cheo mwanawe hadi afisa wa ngazi ya juu - jenerali wa nyota nne - huku akimuweka kama mshauri wake.
‘’Tamaa ya kupitiliza’’
Baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu cha kijeshi cha Sandhurst nchini Uingereza, Jenerali Kainerugaba alianza kupanda cheo katika jeshi la Uganda, ambalo alijiunga rasmi mwaka wa 1999. Akiwa ameoa na watoto wanne, anafanya mengi ya imani yake ya Kikristo na maadili ya familia kwenye Twitter.
Alichukua jukumu muhimu katika uundaji wa Kamandi ya Kikosi Maalum (SFC), kitengo kinachohusika na usalama wa baba yake.
Pia kimeshutumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu - ikiwa ni pamoja na kuwaweka kizuizini na kuwatesa wanaharakati wa upinzani.
‘’Muhoozi alipanda cheo na kuwaongoza walinzi wa babake mwaka 2008, wadhifa alioshikilia hadi 2017. Alirejea kwenye kitengo hicho wakati wa msimu wa uchaguzi wa 2020 wenye ghasia,’’ aliandika mwandishi wa habari wa Uganda Musinguzi Blanshe katika The Africa Report.
Bw Serwanjja alisema baada ya kutimuliwa kama kamanda wa vikosi vya nchi kavu, haijafahamika ni kiasi gani jenerali huyo sasa ana ushawishi katika jeshi.
Jambo lililo wazi ni kwamba Bw Museveni amekatiza matumaini yoyote aliyokuwa nayo mwanawe ya kumrithi katika uchaguzi wa 2026 baada ya wenzake wa zamani - akiwemo makamu wa rais na waziri wa mambo ya ndani - kuanzisha kampeni ya kumtaka agombee tena wadhifa huo.
Hili lilikuwa pigo kubwa kwa makundi mengi ambayo yalikuwa yameibuka kwenye Twitter - chini ya lebo za hashtags kama vile #MKArmy na #MK26 - kutafuta uungwaji mkono kwa jenerali huyo kuchukua nafasi kutoka kwa baba yake.
‘’Wale wote wanaotaka nisimame mwaka wa 2026, wale wote ambao hawapendi,’’ alisema kwenye Twitter mnamo Mei.

Chanzo cha picha, AFP
Hili liliungwa mkono na kampeni ya mashinani iliyoshuhudia sherehe za kuadhimisha miaka 48 ya kuzaliwa kwa jenerali huyo mwezi Aprili, na uungaji mkono wake kwa mipango mbalimbali katika kile kilichoonekana kama nia ya kukuza sifa zake, hasa miongoni mwa vijana.
‘’Muhoozi ana jeshi kubwa la vijana. Wafuasi wake wanajaribu kutafuta uungwaji mkono na vijana,’’ Bw Serwanjja alisema.
Hili linaonekana kuwa muhimu kukabiliana na kukua kwa umaarufu wa viongozi vijana wa upinzani kama mwanasiasa aliyegeuka kuwa mwanamuziki Bobi Wine ambaye jenerali anajaribu kumdharau kwa kumtaja kwa Kiswahili kama ‘’Kabobi’’, kumaanisha ‘’Bobi mdogo’’.
Bw Serwanjja anahisi kuwa jenerali huyo ‘’anatamaa ya kupitiliza’’ kwa matumaini yake ya kupigiwa kura 2026: ‘’Rais Museveni hataacha lolote, ikiwa ni pamoja na kujitolea mhanga kwa chake mwenyewe, ili kusalia madarakani.’’
Na ikiwa Bw Museveni atathibitisha kwamba atawania urais, mwanawe - anayejulikana kama Kiongozi Mkuu wa Vizazi kwa baadhi ya wafuasi wake kwenye Twitter - anakaribia kuhakikisha kumfanyia kampeni.















