Kipi kilichomsaidia Rais Yoweri Museveni kumpiku Bobi Wine

Chanzo cha picha, Getty Images
Uchaguzi wa Uganda uliokuwa unashindaniwa vilivyo na kufuatiliwa kwa karibu ulimalizika huku kiongozi ambaye amekuwa madarakani kwa muda mrefu nchini humo akitangazwa mshindi dhidi ya mwanamuziki wa pop.
Hata hivyo uchaguzi huo haukukosa vioja vyake ila swali ambalo wengi wamekuwa wakijiuliza ni je umeleta mabadiliko yoyote?
Mwanahabari wa BBC Patience Atuhaire kutoka kampala anatufafanulia zaidi:
Wengine wameutathmini kama uchaguzi wa kipekee ambapo mwanamuziki, 38, aliyekulia eneo la kitongoji duni alikuwa anakabiliana na ambaye mara yake ya kwanza kuwa rais ni miaka 35 iliyopita.
Pale Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, alipoanzisha kampeni yake ya kwanza ya kutaka kuwa rais, baadhi katika chama tawala kinachoongozwa na Rais Yoweri Museveni wa chama cha National Resistance Movement (NRM) walitupilia mbali taarifa hizo wakisema kwamba huo ni uvumi tu.
Walisema kuwa Bobi Wine ni maarufu tu katika mji mkuu lakini aliendelea kuvutia wafuasi wengine kutoka kila pembe ya nchi hiyo.
Na kama alivyosema mmoja wa mawaziri, ilidaiwa kuwa watu walimfurahia kwasababu tu alikuwa ni msanii maarufu.
Ila kidogo kidogo, hali ikaanza kuwabadilikia na kwenda kinyume na matarajio yao.
Inasemekana kuwa Bobi Wine alitumia mitandao ya kijamii kutoa wito kwa vijana wa Uganda ambao ndio idadi kubwa ya watu nchini humo kushirikiana naye katika kufikia "Uganda mpya".
Na wakaitikia wito tena kwa shauku kubwa.
Mitandao ya kijamii sio kura
Ghafla, mamlaka ikaonekana kushutuka ikawa ni kana kwamba imechokozwa. Na wakati kampeni zinafikia kilele chake, mabomu ya kutoa machozi, risasi na kukamatwa ni baadhi ya yale yaliyomuandama Bobi Wine na wafuasi wake, ambao walisema wazi kuwa hakuna kitakachowafanya kulegeza msimamo wao.
Upande wa chama cha NRM ukawa unamtegemea Rais aliye madarakani na vikosi vya serikali.

Chanzo cha picha, AFP
Bobi Wine ambaye ni msanii wala sio Robert Kyagulanyi mwanasiasa, aliyetawala kipindi cha kampeni.
Alikuwa na ushawishi wa kuvutia umati mkubwa - hata kukusanya watu licha ya wasiwasi juu ya virusi vya corona huku wakipaza sauti, "nguvu ya raia, nguvu yetu".
Lakini kile hasa alichotaka kufanya na nguvu hiyo, ilikuwa ni nadra sana kujitokeza. Hata katika nyakati chache ambapo vikosi vya usalama viliamua kuchukua mapumziko na kutomvamia, ni mara chache sana alizungumza juu ya masuala ya manifesto yake.
Yaani, ilifika wakati kuangazia uchaguzi huo, ilikuwa sawa na kuripoti kuhusu vurugu kutoka upande wa upinzani badala ya ajenda za wagombea kwa wapiga kura.
Lakini "nguvu ya watu" moto ambao ulikuwa umewashwa miongoni mwa Waganda na Bobi Wine, ulionekana kuchoma hadi kwenye masanduku ya kupiga kura na baada ya hapo ukafifia.
Idadi rasmi ambayo upinzani inasema kura ziliingiliwa, baadaye kukaonesha kuwa mikutano mikubwa na umaarufu kwenye mitandao ya kijamii, haikumaanisha kwamba hiyo ni idadi kubwa ya wapiga kura.

Chanzo cha picha, Getty Images
Bobi Wine alipata asilimia 35 ya kura zilizopigwa lakini idadi hii ikawa ni sawa na aliyopata mgombea mkuu wa upinzani Kizza Besgye, mwaka 2016. Na tena kama ilivyotokea kwa Dkt. Besigye, Bobi Wine pia naye alifungiwa nyumbani kwake asiruhusiwe kutoka na vikosi vya usalama.
Kilichotokea baada ya uchaguzi kilionekana kuwa jambo ambalo sio kigeni.
Kabla ya hapo, asubuhi ya kupiga kura - wakati upinzani bado ulikuwa na imani ya kutimiza ndoto yake ya kuwa na mwanzo mpya- kulikuwa na utulivuna usio wa kawaida, hali tofauti ikilinganishwa na jinsi mji wa Kampala ulivyozoeleka hasa mwezi wa Januari.
'Kipi kinachosubiriwa?'
Niliwasili katika eneo la kupiga kura la Nsambya, kusini mwa mji saa moja unusu, ambako niliona kundi la watu wachache tu waliokuwa wamepanga mstari wakiwa kimya. Uwanja huo mkubwa ulikuwa na vituo vitano vya kupiga kura.
Nyenzo za kupiga kura zilikuwa zimewasili lakini upigaji kura ulikuwa bado haujaanza.
Wakati foleni inazidi kuongezeka, hisia nazo ziliendelea kubadilika. Kijana mmoja akapaza sauti na kusema kile ambacho pengine kila mmoja alikuwa anakifikiria: "Tuliwasili hapa saa kumi na mbili asubuhi! Kipi kinachosubiriwa?"

Chanzo cha picha, Reuters
Wengine wakaanza kulalamika, kuna wale waliorushia wahudumu wa zoezi la kupiga kura matusi.
Pengine uzungumzaji wa kijana huyo ulimsaidia au maafisa walitaka kumuondoa. Na hatimaye upigaji kura ulipoanza saa mbili baadaye, alipishwa na kuruhusiwa na maafisa kwenda mbele kabisa na kuanza kupiga kura yake.
Nikavuka eneo jingine la Nansana upande wa kaskazini ambapo upigaji kura ulicheleweshwa hadi saa nne. Huku milolongo ikiwa mirefu niliweza kutabiri jinsi watu walivyokereka kwa kuangalia nyuso zao tu.
"Nimefika hapa nikaambiwa kuwa hili sio eneo langu sahihi la kupiga kura. Nilipokwenda ule upande mwingine, nikarejeshwa tena hapa, sasa nasubiri tu. Rafiki yangu alikuwa na kikaratasi kinachoonesha eneo lake la kupiga kura lakini jina lake haliko kwenye daftari la hapa la usajili. Amekata tamaa na ameondoka," alisema Fatuma Namuleme.
Nakumbuka nikiona milolongo sawa na hiyo mwaka 2016, wapiga kura wakiwa wanatiririkwa na jasho kwasababu ya jua lililokuwa linapiga wakisubiri kuwasili kwa nyenzo za kupiga kura.
Siku hiyo, nyenzo za kupiga kura katika maeneo mengi ya mjini Kampala zilifika kuchelewa na pia kukawa na maandamano katika baadhi ya maeneo huku uchaguzi ukilazimika kusongezwa mbele hadi siku nyingine.
Lakini safari hii kulikuwa na maafisa kadhaa wa polisi kuhakikisha kuwa mchakato huo unafanyika kwa mpangilio.
Kukiwa hakuna mtandao na upatikanaji wa taarifa kutoka sehemu nyingine ikiwa vigumu kufikiwa, siku ya kupiga kura ilikuwa ni kama ndio mwanzo wa kujionea yanayojiri, watu wakiwa wamepoteza matumaini.

Chanzo cha picha, AFP
Wakati Tume ya Uchaguzi ilipoanza kutoa majibu, ikawa wazi kuanzia mapema kabisa kutoka sehemu ambayo matokeo yalikuwa yakitangazwa, kuwa Museveni ameongezwa miaka mingine mitano ya uongozi.
Licha ya milolongo mirefu kushuhudiwa katika mji wa Kampala, ni asilimia 57 pekee ya wapiga kura milioni 18 waliosajiliwa waliopiga kura, idadi hiyo ikiwa chini kwa asilimia 10 ikilinganishwa na uchaguzi uliotangulia.
Pia ushindi wa rais umekuwa ukipungua katika chaguzi tatu zilizotangulia; kuanzia asilimia 68 mwaka 2011 hadi asilimia 60.6 mwaka 2016 huku mwaka huu akipata asilimia 58.6.
Na pia upinzani, umepata viti vingi katika mji mkuu wa Kampala na eneo la kati nchini humo.
Wabunge walipoteza viti vyao
Chama kipya cha National Unity Platform (NUP) kilichoanzishwa na Bobi Wine kilipata viti vingi zaidi vya ubunge katika eneo la kati na kitakuwa na jumla ya wabunge 56 kati ya 500, na kukifanya kuwa chama kikubwa cha upinzani bungeni.
Chama cha NUP kimekuwa ndio nyumbani kwa vijana wengi, wanasiasa wenye utashi wa muungano mpya ambao wanaweza kutikisa.
Uchaguzi wa mwaka 2021, ulimrejesha rais yule yule lakini ni wengi walioachwa nje, wanasiasa ambao wamekuwa bungeni kwa mingo mitatu.
Wabunge 25 wa baraza la mawaziri akiwemo makamu rais Edward Ssekandi walipoteza viti vyao bungeni.
Na ikiwa kuna chochote kilichojitokeza katika uchaguzi huu, ni ukosefu wa uaminifu. Miongoni mwa waliopoteza viti vyao katika uchaguzi huu ni wabunge wa upinzani ambao mara moja walibadilika na kuunga mkono chama cha NRM na kujipatia nafasi za uwaziri.

Chanzo cha picha, AFP
Katika hotuba yake baada ya kutangazwa mshindi, Bwana Museveni aliitikia wito wa kuimarisha vituo vya afya na elimu na pamoja na kilimo na sekta ya viwanda. Pia alikosoa wanasiasa wanaoweka maslahi yao mbele badala ya wananchi.
Hata hivyo, viongozi wa chama cha NUP, wamedhamiria kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo.
Lakini huenda wakawa na changamoto na hilo kwasababu Lina Zedriga, makamu rais wa chama hicho eneo la kaskazini, alisema kwamba maajenti wa kituo chake waliokuwa na ushahidi wa wizi wa kura ama wamekamatwa au hawajulikani walipo.
'Hakuna kukata tamaa'
"Tutaendelea kusalia humu almradi tunataka kuona mabadiliko," alisema.
"Mradi tunataka kuona matakwa ya raia wa Uganda yakitimia, hatutatikisika. Tumesubiri kwa miaka 30. Hatuwezi kukata tamaa kabisa."
Hata hicyo, ari ya kutaka kuendelea kuwa na matumaini itategemea vijana ambao wametiwa motisha na Bobi Wine ikiwa wataendelea kutaka kujitolea.
La sivyo, kile kile ambacho kimekuwa kikijitokeza katika kipindi cha miongo mitatu kitajirudia, huku Bwana Museveni na chama chake cha NRM kikiendelea kungangania madaraka.













