Mataifa manane ya Afrika yenye utajiri wa madini

l

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 5

Hamu ya mataifa ya kigeni (Marekani, China, Urusi, Canada, Uingereza, Umoja wa Ulaya, India, na nchi za Kiarabu) na makampuni yao, kupata madini kutoka Afrika, ndio kiini cha ajenda za kidiplomasia wanapokutana na viongozi wa Afrika.

Wakati makampuni ya kigeni yakiendelea kukusanya mabilioni ya dola kutokana na madini hayo barani humo, Afŕika inasalia katika dimbwi la umaskini na ukosefu wa ajiŕa miongoni mwa vijana wake.

Nchi nyingi za Kiafrika zina madini muhimu ambayo kwa sasa yanahitajika sana. Rasilimali hizi ni pamoja na cobalt, grafiti, lithiamu, bauxite, nikeli, manganese, PGMs (Platinum Group Metals) na madini adimu duniani.

Baadhi ya madini haya muhimu hutumika kuboresha utendakazi wa betri, huku mengine hutumika katika utengenezaji wa magari ya umeme, simu janja, mitambo ya kuzalisha umeme wa upepo, pia hutumiwa katika kuunda mifumo ya akili mnemba na nishati mbadala.

Afrika inaelezwa kuwa na takriban aina 60 tofauti za madini, jumla ya thuluthi moja ya hifadhi ya madini duniani, madini yote kwa pamoja.

Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu inakadiria kuwa bara hili lina asilimia 90 ya hifadhi ya madini ya kundi la platinamu duniani; 80% ya coltan; 60% ya cobalt; 70% ya tantalum; 46% ya hifadhi ya almasi; 40% ya akiba ya dhahabu; na 10% ya akiba ya mafuta.

Rasilimali hizi za madini ndio chanzo kikuu cha uchumi na huwakilisha sehemu kubwa ya mapato ya nje kwa nchi kadhaa Afrika.

Pia unaweza kusoma

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo

DRC ni maarufu kutokana na rasilimali zake mbalimbali na nyingi za madini. Nchi hii ina shaba, cobalt, coltan, lithiamu, dhahabu, almasi, urani, nk.

Ni nchi inayoongoza duniani kwa uzalishaji wa cobalt, malighafi ya muhimu kwa uzalishaji wa magari, DRC pia ni shaba na ndio mzalishaji wa kwanza wa shaba kwa Afrika.

Kulingana na IMF, nchi hii inachangia zaidi ya 70% ya uzalishaji wa cobalt duniani, inashikilia 51% ya hifadhi ya cobalt duniani, na 2.2% ya hifadhi ya shaba duniani. Pia ina bati na tantalum, kati ya madini mengine muhimu.

Katika bajeti ya 2025, mchango wa sekta ya madini unakadiriwa kuwa 30% ya faranga za Congo bilioni 49.8 ($ 16.9 bilioni). Sekta ya madini inachangia dola bilioni 5, ikiwa ni ongezeko la 41% ikilinganishwa na bajeti iliyopita.

Afrika Kusini

Nchini Afŕika Kusini, sekta ya madini imekuwa msukumo mkuu nyuma ya historia na maendeleo ya nchi hiyo.

Kama nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika na nchi iliyoendelea zaidi Afrika, Afrika Kusini ina rasilimali nyingi za almasi, dhahabu, shaba, chrome, manganese, platinamu, palladium, rhodium, iridium, ruthenium, nk.

Afrika Kusini ina moja ya hifadhi kubwa zaidi ya uranium duniani. Nchi hiyo ndiyo inayoongoza duniani kwa uzalishaji wa paladiamu na platinamu, ikichukua 43% na 73% ya uzalishaji wa kimataifa.

Pia inashikilia 90% ya hifadhi ya kimataifa, ikiwa na takriban tani milioni 63 za madini haya. Afrika Kusini ina hifadhi ya pili kwa ukubwa ya uranium duniani baada ya Australia. Sekta ya madini ilichangia Dola za Marekani bilioni 15.5 katika Pato la Taifa mwaka 2021.

Botswana

Ikiwa na Pato la Taifa la dola bilioni 19, Botswana ni nchi kubwa katika uchimbaji madini barani Afrika.

Kulingana na Shirika la Taifa la Takwimu, sekta ya almasi inawakilisha karibu 90% ya mapato ya nje ya nchi na inachangia kati ya 30% na 40% ya mapato ya serikali.

Kando na almasi, Botswana ina shaba, nikeli, kaboni ya sodiamu, potashi, makaa ya mawe, chuma na fedha.

Zimbabwe

Kulingana na Chama cha Wachimbaji Madini cha Zimbabwe, nchi hiyo imejaliwa kuwa na zaidi ya hifadhi 60 tofauti za madini. Hizi ni pamoja na dhahabu, metali za kundi la platinamu, almasi, nikeli, chromium, makaa ya mawe, lithiamu, na granite nyeusi.

Nchi hiyo inasemekana kuwa na madini ya chuma, tungsten, na grafiti, ambayo bado hayajachimbwa. Udongo wake una fosforasi, mawe ya thamani ya (aquamarine, rubi, amethisto, zumaridi), tantalite, manganese, vermiculite, chokaa, na mica, kati ya madini mengine.

Sekta ya madini inachangia 12% ya Pato la Taifa na 70% ya mapato ya mauzo ya nje ya nchi, kulingana na Shirika la Biashara la Shirikisho la Marekani.

Zambia

Zambia, nchi ya pili barani Afrika kwa uzalishaji wa shaba, inaorodheshwa miongoni mwa wazalishaji 10 bora wa shaba duniani. Akiba kubwa zaidi ya bara Afrika, iko kati ya DRC na Zambia katika eneo linaloitwa Copperbelt. Nchi hizo mbili zina akiba ya saba na ya kumi na moja kwa ukubwa duniani.

Mbali na madini hayo, nchi hiyo ina utajiri mkubwa wa rasilimali nyingine kama vile kobalti, urani, manganese na zumaridi. Shaba, hata hivyo, inasalia kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa taifa, ikichangia 18% katika Pato la Taifa na kutoa zaidi ya 70% ya mapato ya nje ya nchi, kulingana na data rasmi ya serikali.

Angola

Inajulikana kuwa mzalishaji mkuu wa mafuta (ya pili barani Afrika baada ya Nigeria) ambayo hutoa 95% ya mapato yote ya nchi, 80% ya mapato ya ushuru na zaidi ya 45% ya Pato la Taifa kwa mujibu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Angola ina sekta ya madini yenye nguvu sana inayoendeshwa na madini ya almasi. Nchi hiyo ni mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa almasi barani Afrika na uzalishaji unaofikia takriban karati milioni 9 kwa mwaka.

Almasi huzalisha takriban dola bilioni 7 kwa mwaka kwa Angola. Mbali na rasilimali hii, udongo wa Angola una chuma, fosforasi, shaba, dhahabu, bauxite, urani, manganese, nk.

Jamhuri ya Guinea

Jamhuri ya Guinea, nchi ya pili duniani kwa uzalishaji wa bauxite baada ya Australia, ina akiba kubwa zaidi duniani (25%) ya madini haya yanayotumika kwa uzalishaji wa alumini.

Kulingana na Wizara ya Madini na Jiolojia ya Guinea, hifadhi ya nchi hiyo inakadiriwa kuwa zaidi ya tani bilioni 40, zikiwemo tani bilioni 23 zinazopatikana katika eneo la Boké. Nchi hiyo pia ina (tani bilioni 4) za akiba ya chuma, karati milioni 30 hadi 40 za akiba ya almasi iliyothibitishwa, tani 700 za dhahabu.

Kulingana na barua kutoka Wizara ya Uchumi, Fedha, na Viwanda ya Ufaransa, manganese, cobalt, nikeli na urani ni sekta ya pili ya na madini, inawakilisha 18% ya Pato la Taifa.

Ghana

Iliyokuwa ikijulikana zamani kama Gold Coast. Nchi hiyo ndiyo inayoongoza kwa uzalishaji wa dhahabu barani Afrika (tani 136), na inashika nafasi ya kumi kwa uzalishaji wa dhahabu duniani. Dhahabu inachimbwa zaidi katika mikoa ya Magharibi na Ashanti (Kusini). Madini hayo yanawakilisha 97% ya madini yanayochimbwa na nchi hiyo.

Kulingana na serikali ya Ghana, sekta ya madini inachangia 39% ya mapato ya nje ya nchi, 18.6% ya mapato ya moja kwa moja ya kodi ya ndani, na karibu 14% ya Pato la Taifa mwaka 2024.

Uzalishaji wa dhahabu, rekodi ya wakia milioni 4.8 (tani 136) mwaka 2024, ulizalisha dola bilioni 5 katika mapato rasmi ya nje ya nchi. Mbali na dhahabu, Ghana pia ina manganese, bauxite, almasi, lithiamu, kati ya madini mengine.