Binadamu kuanza kuchimba madini angani?

Muda wa kusoma: Dakika 5

Na Josh Sims

S

Chanzo cha picha, Getty Images

Miaka 30 iliyopita, kipindi cha sayansi cha BBC Tomorrow's World kilitabiri kuwa kufikia mwaka 2025, binadamu wangeweza kuchimba madini kutoka kwenye miamba ya angani (asteroids). Ingawa hili bado halijatimia kikamilifu, makampuni kadhaa binafsi yamepiga hatua kubwa kuelekea kufanikisha azma hiyo, kinyume na matarajio ya wengi.

Kampuni ya AstroForge yenye makao yake California imeleta matumaini ya kuwa Kampuni ya kwanza kufanikisha uchimbaji wa madini angani. Mnamo Februari 27, kampuni hiyo ilizindua chombo chake cha uchunguzi, Odin, kwa kutumia roketi ya SpaceX Falcon 9 kutoka Kituo cha Anga cha Kennedy, Florida.

Lengo lake kuu ni kufika kwenye kwenye miamba (OB5), umbali wa kilomita milioni 8 kutoka Dunia, ili kuchunguza madini yaliyoko huko. Safari hii inatarajiwa kuchukua miezi tisa.

Hata hivyo, chombo cha Odin kilipata matatizo makubwa ya mawasiliano, hali inayofanya iwe vigumu kufuatilia mahali kilipo na harakati zake. Licha ya hayo, wataalamu wa AstroForge wanajitahidi kurejesha mawasiliano, wakitumaini kuwa chombo hicho kinaendelea na safari yake kama ilivyopangwa.

.

Chanzo cha picha, SpaceX

Maelezo ya picha, Moja ya vifaa vya uchunguzi wa uchimbaji madini kwenye anga za mbali vya Kampuni ya AsroForge, Odin.

Teknolojia mpya zinaongeza uwezekano wa kufanikisha uchimbaji wa madini angani. Kwa mfano, darubini ya kisasa ya Vera C. Rubin nchini Chile, ambayo iko karibu kukamilika, itasaidia kutambua na kufuatilia miamba ya angani kwa urahisi zaidi. Vifaa vya ujenzi wa vyombo vya anga pia vinazidi kupatikana kwa urahisi, huku gharama za safari za anga zikishuka kwa kiasi kikubwa.

Miaka 15 iliyopita, iligharimu takriban dola 10,000 kupeleka mzigo wa kilo 0.45 angani. Lakini sasa, gharama hiyo imeshuka hadi chini ya dola 2,000, na kwa teknolojia mpya kama SpaceX Starship, kuna matumaini kuwa gharama inaweza kushuka hadi mamia ya dola tu. Kupungua kwa gharama za safari za anga ni mojawapo ya sababu zinazoharakisha ndoto ya uchimbaji wa miamba ya angani.

Faida ya uchimbaji wa madini Angani

Mwanasayansi maarufu wa anga, Neil deGrasse Tyson, aliwahi kusema kuwa bilionea wa kwanza wa trilioni atatokana na uchimbaji wa madini angani. Hii ni kwa sababu miamba ya angani ina utajiri mkubwa wa madini adimu kama platinamu, nikeli, kobalti, na hata helium-3, ambayo ni muhimu katika uzalishaji wa nishati ya nyuklia.

Wataalamu wengine wanahoji kuwa uchimbaji huu unaweza kusaidia kuhifadhi mazingira ya Dunia kwa kupunguza utegemezi wa madini ya ardhini, ambayo uchimbaji wake unasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira. Kwa mfano, uchimbaji wa platinamu ardhini unahitaji nishati kubwa na hutoa kiasi kikubwa cha gesi chafu.

Kulingana na utafiti wa mwaka 2018 wa Chuo Kikuu cha Paris-Saclay, uchimbaji wa platinamu kwenye miamba ya angani ungetoa kilo 150 za hewa chafu kwa kila kilo moja ya platinamu inayopatikana. Kwa kulinganisha, uchimbaji wa madini hayo duniani hutoa hadi kilo 40,000 za hewa chafu kwa kiasi hicho hicho cha platinamu.

Kwa mujibu wa Daynan Crull, mwanzilishi wa kampuni ya Karmen+, uchimbaji wa madini angani unaweza kuchochea uchumi wa anga, ambao Kituo cha Kiuchumi Duniani (WEF) kinatabiri kufikia thamani ya dola trilioni 1.8 ifikapo mwaka 2035.

Changamoto zinazokabili uchimbaji wa madini angani

.

Chanzo cha picha, AstroForge

Maelezo ya picha, Wafanyakazi wa AstroForge wakiwa nyuma ya chombo cha anga cha Odin, na paneli zake za umeme wa jua, mnamo Januari 2025 kabla ya uzinduzi wake wa Februari, 2025
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Licha ya matumaini makubwa, wapo wanaohoji uhalisia wa uchimbaji wa madini angani. Profesa Lang, mtaalamu wa masuala ya madini, anasema kuwa ingawa kiteknolojia inawezekana, gharama kubwa za mradi huu zinaweza kufanya biashara hii isiwe na faida. Anaeleza kuwa madini kama platinamu bado yanapatikana ardhini, hata kama yapo chini ya bahari, na teknolojia mpya zinaweza kuwezesha uchimbaji wake kwa urahisi zaidi kuliko kutumia mabilioni ya dola kusafiri angani.

Mtaalamu wa mazingira Kathryn Miller, kutoka Chuo Kikuu cha Lancaster, anaamini kuwa uchimbaji wa madini angani ni bora zaidi kwa mazingira kuliko uchimbaji wa kina kirefu cha baharini. Anasema kuwa kuchimba madini kwenye sakafu ya bahari kunasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira ya baharini, ikiwemo kuteketeza viumbe wa baharini na mifumo yao ya ikolojia.

Hata hivyo, uchimbaji wa miamba ya angani pia unakabiliwa na changamoto za kimazingira. Wanamazingira wana wasiwasi kuwa mabaki na vumbi litakavyotokana na uchimbaji angani vinaweza kuzidisha tatizo la uchafuzi wa anga. Pia, kuna hofu kwamba vipande vya miamba vilivyopasuka vinaweza kuanguka na kuingia tena kwenye anga ya Dunia.

"Anga za juu zinapaswa kubaki safi. Tunapaswa kuhakikisha tunasafisha baada ya shughuli zetu angani," anasema Dkt. Monica Grady, mhadhiri wa sayansi ya anga na sayari katika Chuo Kikuu Huria cha Uingereza.

Hata hivyo, wawakilishi wa sekta hii wanapinga hoja hiyo, wakisema kuwa rasilimali za anga zinapaswa kutumiwa kwa manufaa ya wanadamu.

"Anga ina rasilimali zisizo na mwisho, lakini Dunia yetu ni moja tu. Lazima tutafute njia za kuhifadhi rasilimali za Dunia kwa manufaa ya vizazi vijavyo," alisema mmoja wa wakurugenzi wa AstroForge.

Masuala ya Kisheria

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Watu wakitazama roketi ya SpaceX Falcon Heavy ikirusha chombo cha Psyche kutoka katika Kituo cha Anga cha Kennedy huko Cape Canaveral, Florida, Marekani mnamo Oktoba 13, 2023. Chombo hicho cha anga za juu cha NASA kitafanya safari ya miaka sita hadi kwenye miamba ya mbali ya Psyche wenye utajiri mkubwa wa madini.

Changamoto nyingine kubwa inayowakabili waendeshaji wa miradi ya uchimbaji wa madini angani ni suala la haki za kisheria.

Mkataba wa Anga za Juu wa 1967 unasema kuwa anga ni mali ya wanadamu wote na haipaswi kumilikiwa na taifa moja au mtu binafsi. Hata hivyo, haujaweka wazi ikiwa mtu binafsi au kampuni inaweza kumiliki madini yanayochimbwa angani.

Mkataba wa Mwezi wa 1979 unazuia umiliki binafsi wa rasilimali za angani, lakini ni nchi saba pekee zilizouridhia, nchi nyingi zikiwa hazina mipango ya anga.

Mnamo mwaka 2027, Umoja wa Mataifa umepanga kufanya mkutano maalum kujadili sheria za uchimbaji wa rasilimali za anga, lakini maamuzi yatakayofikiwa hayatakuwa na nguvu ya kisheria.

Dkt. Rosanna Deplano, mtaalamu wa sheria za anga, anaeleza kuwa mataifa mengi yanatafsiri sheria kwa maslahi yao wenyewe, jambo linalofanya uchimbaji wa madini angani kuwa sekta yenye mvutano mkubwa wa kisiasa na kiuchumi.

"Kama uchimbaji wa madini angani ungeshughulikiwa tu kwa madhumuni ya kisayansi, basi isingekuwa tatizo kubwa. Lakini kwa kuwa sasa ni biashara, inazua changamoto nyingi za kisiasa," alisema Deplano.

"Hakuna shaka kwamba uchimbaji wa madini angani utafanyika siku za usoni, lakini swali ni nani atafaidika na nani atabaki nyuma?" aliongeza.

Kwa mwelekeo wa sasa wa teknolojia, uchimbaji wa madini kwenye miamba ya angani si suala la kama utafanikiwa, bali lini utafanikiwa. Kama changamoto za kisheria, kiuchumi, na kimazingira zitashughulikiwa ipasavyo, basi anga za juu zinaweza kuwa mgodi mpya wa thamani kwa binadamu.