Taliban yapinga ndoa za wake wengi miongoni mwa makamanda wake

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiongozi wa Taliban nchini Afghanistan ametoa amri ya kuwasihi makamanda wa kundi hilo kuachana na utamaduni wa kuoa wanawake wengi, ambao unawafanya "kukosolewa na maadui wetu".
Wanaume wa Kiislamu wanaruhusiwa kidini kuoa hadi wanawake wanne na ndoa ya mke zaidi ya mmoja bado ni halali nchini Afghanistan, Pakistan na mataifa mengine ya Kiislamu
Lakini vyanzo vya habari vya Taliban vimeiambia BBC utamaduni huo umechangia makamanda wengi kuitisha fedha zaidi kulipia "mahari" - utamaduni unaokumbatiwa na jamii ya Pashtun nchini Afghanistan na Pakistan ambapo pesa zinapewa familia ya mwanamke kabla hajaolewa.
Amri hiyo inakuja wakati nyeti wa kisiasa kwa Taliban nchini humo inapoanza mazungumzo na serikali kuhusu hatma ya baadae ya nchi hiyo.
Vyanzo hivyo vilisema kwamba uongozi wa Taliban una wasiwasi kuhusu madai ya ufisadi dhidi ya wanachama wake ambao wanajaribu kutafuta kiwango kikubwa cha fedha za kutunza familia zao kubwa.
Baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu wa Taliban wana zaidi ya mke mmoja, lakini amri hiyo mpya haiwajumuishi wale ambao tayari wako katika ndo ya mke zaidi ya mmoja.
Amri hiyo inasema nini?
Amri hiyo ya kurasa mbili, ilitolewa na kiongozi wa Taliban nchini Afghanistan Mullah Hibatullah, haipigi marufuku ndoa ya pili, tatu, na ya nne, lakini inaonya kuwa kiwango kikubwa cha fedha zinazotumika katika sherehe za harusi kinaweza kuvutia ukosoaji kutoka kwa wapinzani wa Taliban.
"Ikiwa viongozi wote na makamanda watajiepusha na ndoa ya mke zaidi ya mmoja, hawatajihusisha na ufisadi na maovu mengine," amri hiyo ilisema.
Amri hiyo haipingi ndoa ya mke zaidi ya mmoja kwa wanaume ambao pengine hawana watoto au hawajapata watoto wa kiume katika ndoa zao za awali, wale ambao wanaoa wajane ama familia zao zina mali ya kuwawezesha kuoa wanawake kadhaa.
Amri hiyo inasema wale walio katika kundi hilo, na wanataka kuoa mke zaidi ya mmoja wanastahili kuomba idhini ya moja kwa moja kutoka kwa wakubwa wao kabla ya kuinga katika ndoa nyingine.
Vyanzo vya habari vya Taliban vimeiambia BBC kwamba barua zinawasilishwa kwa viongozi wanaolengwana na amri hiyo nchini Afghanistan na Pakistan.
Suala la kuoa mke zaidi ya mmoja ni kubwa kiasa gani?
Utamaduni wa kuoa mke zaidi ya mmoja ni maarufu sana miongoni mwa jamii za Pashtun nchini Afghanistan na Pakistan, ambako wanawake wana usemi mdogo kuhusu suala la ndoa.
Ukosefu wa mtoto katika ndoa - hasa mtoto wa kiume - ni sababu kubwa inayochangia kuoa mke zaidi ya mmoja hususan katika jamii nyingi za Pashtun zinazoishi maeneo ya vijijini. Sababu nyingine ni mzozo wa kinyumbani, ambao mara nyingi wanawake hulaumiwa.
Mwanamke mjane mara nyingi huozwa kwa ndugu ya mume wake aliyefariki - hatua ambayo huchukuliwa kama kulinda heshima ya mjane na familia japo wakati mwingine ndugu huyu huenda tayari ameoa. Na kwa wale walio na mali, kuwa na mke zaidi ya mmoja ni ishara ya kuwa na hadhi katika jamii.

Chanzo cha picha, Anadolu
Ndoa kama hizo zinawezeshwa na utamaduni wa "walwar" - au mahari - ambayo hupokelewa na familia ya bibi harusi kabla ya binti yao kuolewa.
Hali ngumu ya kiuchumi na kubadilika kwa mtazamo wa jamii kuhusiana na ndoa ya wake wengi katika miongo ya hivi karibuni imechangia kufifia kwa utamaduni huo wa "tamaa ya wanaume", alisema Rita Anwari, mwanaharakati wa Afghanistan anayeishi Australia.
Dini ya Kiislamu inaruhusu wanaume kuoa wanawake hadi wanne "katika hali fulani", Bi Anwari alisema, "kwa mfano kama mke wa awali ni mgonjwa au hana uwezo wa kuzaa na kadhalika".
"Cha kusikitisha ni kwamba, siku hizi wanaume walio na uwezo wamepuuza hali hiyo na kuweka mbele tamaa za kimwali," aliongeza, akiwalaumu kwa kutumia "vijisababu vidogo" kuoa mke mwingine.
"Haifai kabisa kuwa na wanawake kadhaa wakati hauna uwezo kuwatunza kwa kuzingatia usawa - kifedha, kimaungo, kimwili na kiakili,"alisema .
Baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu wa Taliban wana wanawake kadhaa. Mwanzilishi wa vuguvugu hilo, marehemu Mullah Mohammad Omar, na mrithi wake, Mullah Akhtar Mansoor, wote walikuwa na wake watatu. Kiongozi wa sasa wa Taliban, Mullah Hibatulah, ana wake wawili.
Afisa wa ngazi ya juu wa Taliban , Mulah Abdul Ghani Baradar, ana wake watatu - wa mwisho akiripotiwa kumuoa alipokuwa amezuililwa nchi Pakistan.

Chanzo cha picha, Getty Images
Karibu viongozi wate wa kundi hilo wanaoishi mjini Doha - wana wake kadhaa, ikiwa ni pamoja na wale ambao waliachiliwa kutoka gereza la Guantanamo nchini Marekani. Wengine wao wameoa wake wangine baada ya kuachiliwa huru, na hulazimika kulipa fedha nyingi kwa wakwe zao wapya.
BBC ilipojaribu kuwasiliana na vyanzo vya Taliban kuuliza ni viongozi wapi wana wanawake zaidi ya mmoja, walijibu kwa kuuliza: "Ni yupi hajafanya hivyo?"
Kwa nini kuna juhudi za kudhibiti ndoa hizo sasa?
Kwa miaka mingi, maafisa wa serikali nchini Afghanistan wamegusia kuwa wakati viongozi wa Taliban wanaishi maisha ya ya kifahari wakati maafisa wa ngazi ya chini wanaishi maisha ya hali ya chini.
"Habari njema ni kwamba wapiganaji wa Taliban wamechoshwa na [viongozi wao] jinsi wanaojivinjari na wake wanne hadi watano," alisema Rais wa Afghan Ashraf Ghani katika jopo la mashauriano lililoandaliwa wakati wa kongamano la kimataifa la uchumi (WEF) mjini Davos.
Kumekuwa na taarifa kuwa makomanda wa Taliban huko Afghanistan wamechukuwa wake kwa kutumia nguvu wakati kundi hilo linafanya mazungumzo na serikali.
Na jinsi mahari inavyozidi kuongezeka ni suala ambalo limekuwa likiendelea kutia wasiwasi viongozi wa Taliban.
Taarifa zaonesha kwamba makomanda na wapiganaji wamelipa mahari kati ya dola 26,000 na zaidi ya 100,000 ama inalipwa kutoka kwa mfuko wa kundi hilo au zinapatikana kwa njia zinazotiliwa mashaka.












