Baada ya kuanguka AU, nini mustakabali wa Odinga na siasa za Kenya?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Yusuph Mazimu
- Akiripoti kutoka, Nairobi, Kenya
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Viongozi wa Afrika, wamemchagua Waziri wa mambo ya nje wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), akimshinda mpinzani wake wa karibu, Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, na mwanasiasa mkongwe wa nchi hiyo, Raila Odinga.
Youssouf alishinda kwa kupata kura 33 katika raundi ya 7, ambayo alisalia kama mgombea pekee baada ya Raila kujiondoa katika raundi ya sita kufuatia kupitwa kura na Youssof katika raundi ya tatu, nne, tano na raundi hiyo ya sita.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Jumamosi hii katika makao makuu ya Umoja wa Afrika, mjini Addis Ababa, Ethiopia, Odinga aliongoza katika raundi mbili za mwanzo, akipata kura 20 na 21 dhidi ya 18 na 19 za Youssouf.
Youssouf, mwanadiplomasia anayeiongoza wizara ya mambo ya nje ya Djibouti kwa karibu miongo miwili chini ya marais watatu tofauti, alimpiku Odinga katika raundi ya tatu mpaka ya sita akipata kura 23 dhidi ya 20 za Odinga katika raundi ya tatu.
Katika raundi ya nne alipata kura 25 kwa 21, 26 kwa 21 raundi ya tano na 26 kwa 22 katika raundi ya sita. Wakati Youssouf, akienda kuanza maisha mapya katika siasa za Afrika, nini hatma ya Odinga na siasa za Kenya?
Athari kwa Raila Odinga

Chanzo cha picha, Reuters
Raila Odinga ana umri wa miaka 80 sasa, zaidi ya nusu ya umri wake ameutumia kwenye siasa za Kenya. Hakuna shaka, ukizungumza siasa za Kenya, katika miongo minne iliyopita, jina la Raila Odinga litatawala mazungumzo.
Amewania urais wa Kenya mara tano, na mara zote akishindwa, akianza harakati zake kwenye uchaguzi wa mwaka 1997, mpaka uchaguzi wa hivi karibuni (mwaka 2022) na kushindwa dhidi ya rais wa sasa, William Ruto.
Kuingia kwenye siasa za Afrika kupitia uchaguzi wa AUC, kunaonekana na baadhi kama kutamuongezea nguvu kwenye siasa za Kenya, ingawa kuna mtazamo mwingine kuwa, kushindwa kwake, kunakwenda kupunguza mvuto wake kwenye siasa za kiwango cha bara (Afrika) na hilo linasogea pia mpaka kwenye siasa za ndani za Kenya.
Ikisalia muda mfupi kabla ya hekaheka za uchaguzi mkuu ujao wa nchi hiyo utakaofanyika mwaka 2027, Raila anapaswa kutafakari zaidi mustakabali wake kwenye siasa za Kenya, akitafakari umri wake lakini pia ajiulize iwapo atakuwa katika nafasi ile ile ya mwanasiasa mwenye nguvu, ushawishi na mwenye kukubalika na wafuasi wake walio wengi. Anaweza kuwa na nafasi nyingine moja ya mwisho ya dhahabu ya kujaribu kuingia Ikulu mwaka 2027 dhidi ya rais wa sasa wa Kenya, William Ruto, ambaye katika miezi ya hivi karibuni wameonekana kuwa 'maswahiba' wa kisiasa, huku Ruto na serikali yake anayoiongoza walikuwa wakimpigia debe Odinga kwenye uchaguzi wa AUC.
Uhusiano wake na Rais Ruto

Chanzo cha picha, Getty Images
Usingedhani kama Odinga na Ruto, wangewahi kushikana mikono, kufuatia upinzani mkali wa kisiasa waliokuwa nao kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022. Kauli za Ruto na Odinga zilikuwa hazionyeshi kama watu hawa wanaweza 'kupikika chungu kimoja'. Lakini sasa wanazungumza na walikuwa na mikakati ya pamoja ili kushinda uchaguzi wa AUC.
Ni wazi Odinga alihitaji uungwaji mkono wa Ruto na serikali yake, ili kushinda uchaguzi wa AUC. Hakukua na namna nyingine zaidi ya kukubali Ruto awe sehemu yake ya safari ya kutaka kushinda uchaguzi huo.
Kwa upande wa Ruto, nae kwa vyovyote alitaka Odinga ashinde, ili kuipa nafasi na nguvu Kenya kwenye siasa za Afrika, lakini cha pili ambacho wengi wanakiona ni kwamba, pengine ingesaidia kupunguza nguvu ya upinzani kwenye uchaguzi mkuu ujao, ambao Ruto ameonyesha kutaka kuwania muhula wake wa pili wa urais wa Kenya.
Mustakabali wa Upinzani Kenya

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Upinzani Kenya ni Raila na Raila ni upinzani. Japo wapo viongozi wengi wa upinzani, lakini huwezi kupuuza nguvu ya mwanasiasa huyu dhidi ya serikali. Ushawishi wake unaufanya upinzani kuwa na nguvu kubwa. Hofu ya wengi ni je, baada ya kushindwa uchaguzi wa AUC, nguvu ile ile ya upinzani chini ya Odinga itaendelea kusalia Kenya?
Wapinzani wake hawatamzodoa kwa kushindwa kwake uchaguzi wa AUC? achilia mbali umri wake ambapo atafikisha miaka 82 wakati wa uchaguzi mkuu ujao. Lakini kwa upande mwingine angeshinda uchaguzi wa AUC, pengine upinzani ungejipanga upya kutafuta 'kinara' mwingine wa kuongoza mapambano na kujenga upya ushawishi wa kisiasa, kama alio nao Odinga.
Bado ana nafasi ya kuendelea kuongoza upinzani wa Kenya kuelekea uchaguzi Mkuu ujao, lakini 'uswahiba' wake wa hivi karibuni na rais Ruto, unatikisa upinzani. Kwa sababu si wapinzani wote wanafurahia ukaribu wao.
Wakati wanararuana kwenye uchaguzi, Ruto mara kadhaa amekuwa akimtaja kama 'mzee wa kitendawili', na kuonyesha kama kiongozi asiyepaswa kupewa nafasi, lakini kwenye uchaguzi huu wa AUC, amekuwa akimsifia na kumpigia debe.
Bado ni kitendawili, kwamba je Waziri mkuu huyo wa zamani wa Kenya, ataendelea kuwa karibu na Ruto, na ikiwa hivyo itamaanisha nini kwenye siasa za Kenya? je zitaimarika? ama zitatetereka?
Imehaririwa na Asha Juma












