Tisho kwa Raila baada ya SADC kuwaomba wanachama kumuunga mkono mgombea wa AUC wa Madagascar

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Ambia Hirsi
- Nafasi, BBC Swahili Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Matumaini ya kiongozi wa upinzani wa Kenya Raila Odinga ya kupata kiti cha Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika yameingia mashakani baada ya SADC kuziandikia nchi 16 za muungano huo izikiomba kumuunga mkono mgombea wa Madagascar katika uchaguzi wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC..
Sekretarieti ya SADC imeziandikia barua nchi zote wanachama ikiwasihi wa kumuunga mkono Richard J. Randriamandrato, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Madagascar.
Hatahivyo haijabainika iwapo nchi zote 16 zitampigia kura mgombea wa Madagascar.
Baadhi ya nchi wanachama wa SADC pia ni wajumbe wa Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki, eneo ambalo Raila anatoka.
Kura ya Umoja wa Afrika itapigwa na wajumbe kwa njia ya simu.
Umoja wa Afrika umetoa majina ya wagombea wanne wanaowania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Wagombea walioidhinishwa wanatokea mataifa ya Afrika mashariki ikiwa ni pamoja na Kenya, Djibouti, Mauritania, na Madagascar.
Hii ni kwa sababu nchi wanachama wa Muungano wa Afrika Mashariki EAC, zimepewa nafasi ya kutoa mrithi wa mwenyekiti wa sasa Mousa Faki, raia wa Chad ambaye amekuwa akishikilia wadhifa huo tangu mwaka wa 2017.
Uchaguzi wa AUC umepangwa kufanyika Februari 2025 wakati wa Mkutano wa Umoja wa Afrika, AU.
Kila mgombea kati wa wagombea hao wanne ni jina tajika katika nchi yake. Lakini wao ni kina nani? Tunawaangazia katika taarifa hii.
Raila Odinga - Kenya
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kiongozi wa upinzani wa Kenya Raila Odinga,79, sio jina geni katika ulingo wa siasa nchini mwake na pia barani Afrika.
Amejaribu kuwania urais wa Kenya na kushindwa mara tano - ya mwisho katika uchaguzi wa 2022 ambapo alishindwa na Rais William Ruto.
Uamuzi wake wa kuwania uenyekiti wa Tume ya Muungano wa wa Afrika bila shaka utafuatiliwa kwa karibu kote barani.
Wakati akiwasilisha hati zake, Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Kenya anasema ana uwezo wa kutatua changamoto zinazokabili muungano huo na kufanikisha malengo yake kama mwenyekiti wa AUC, iwapo atashinda kinyang'anyiro hicho.
Bw Odinga ni mwanasiasa mkongwe ambaye anasifika kupigania mageuzi ya kisiasa nchini Kenya, harakati ambazo zilimfanya kukamatwa na kuachiliwa mara kwa mara tangu mwaka 1982 hadi 1991 wakati wa utawala wa rais wa pili wa Kenya Hayati Daniel arap Moi.
Pia aliwahi kuhudumu kama waziri mkuu wa kwanza wa Kenya, wadhifa ulioundwa kufuatia Mkataba wa Kitaifa ulioafikiwa kumaliza ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007-2008, ambapo aligawana mamlaka na Rais Mwai Kibaki.
Mahmoud Ali Youssouf - Djibouti

Chanzo cha picha, Djib/Facebook
Mahmoud Ali Youssouf mwenye umri wa miaka 58 amehudumu kama Waziri wa Mambo ya Nje wa taifa hilo dogo lakini lenye umuhimu wa kimkakati katika eneo la upembe wa Afrika tangu 2005.
Amekuwa mfanyakazi wa umma kwa miaka mingi nchini mwake lakini anahoji kuwa uzoefu ambao unaweza kuwa wa manufaa kwa Afrika, ikiwa atachaguliwa Mwenyekiti ajaye wa Tume ya Umoja wa Afrika.
"Lengo langu kuu ikiwa nitachaguliwa ni kutuliza milio ya risasi" katika bara hili, aliiambia shirika la habari la AFP katika mahojiano mwezi uliopita.
Anasema kuwa tume hiyo inahitaji mageuzi na kuongeza kuwa mageuzi hayo yanastahili kuanzia kwenye uongozi na uwajibikaji wa hali ya juu.
Mbali na kudumisha amani na usalama barani anasema azma yake ni kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Anajivunia kuwa na uwezo wa kuzungumza lugha tofauti na ana imani kuwa uwezo huo wa mawasilaino utamwezesha kuwa 'daraja' litakalounganisha maeneo ya kaskazini na kusini, mashariki na magharibi.
Richard James Randriamandrato - Madagascar
Richard James Randriamandrato, ni Waziri wa Mambo ya Nje wa wa zamani wa Madagascar, ambaye alifutwa kazi Oktoba 2022 kwa kulipigia kura azimio la Umoja wa Mataifa lililolaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Wakati huo Madagascar ilisema alikuwa amekiuka msimamo wao wa kutoegemea upande wowote.
Nchi hiyo sasa imeamua kumuunga mkono kugombea uwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.
Je, tajiriba ya Randriamandrato inatosha kumpatia ushindi? Hili ni swali ambalo jibu lake litapatikana baada ya uchaguzi wa AUC kufanyika Februari 2025 wakati wa Mkutano wa Umoja wa Afrika, AU.















