Mkataba wa kibiashara wa Kenya na EU: Kwa nini Jumuiya ya Afrika Mashariki iliachwa nje

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Kenya William Ruto alisifu "ushirikiano wa ajabu" wa nchi yake na Umoja wa Ulaya (EU) huku pande hizo mbili zikisaini mkataba wa kibiashara wa miaka 25, lakini imezua maswali kuhusu umoja wa Afrika Mashariki.
Je, Kenya imedhoofisha umoja uliopo au haikuwa na budi ila kwenda peke yake?
Hilo limekuwa suala kubwa la mjadala wiki nzima - na huenda likaongezeka mara tu tutakapopata majibu rasmi kutoka kwa mataifa mengine sita katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) - jumuiya ya kibiashara ya kikanda ambayo, wengine wanaamini, inapaswa kuwa kiini cha makubaliano na EU ambayo ni kubwa na yenye nguvu zaidi.
Hadi sasa, wamekuwa kimya, lakini mpango huo – mkataba wa kina zaidi ambao Kenya imewahi kujadiliana na EU, ukifunga pande zote mbili kwa miaka 25 – unaonekana kutotarajiwa na serikali ya Tanzania.
Ilisema katika taarifa yake mwaka jana kwamba ingeunga mkono tu makubaliano ambayo yatanufaisha EAC kwa ujumla - si Tanzania pekee.
Uamuzi wa Kenya umelichukiza kundi la Econews Africa, kiasi kwamba linatishia kwenda mahakamani kuupinga.
Kenya ilitia saini mkataba ulioidhinishwa na EAC na Umoja wa Ulaya mwaka wa 2016, lakini haujaanza kutekelezwa kikamilifu kwani wanachama wengine wengi wa kanda hiyo walikataa kutia saini.
Wanaounga mkono mpango huo wa Rais Ruto wanawashutumu kwa kujikokota katika kukamilisha makubaliano hayo, na kusababisha Kenya kuteseka zaidi.
Wanaeleza kuwa Kenya ndiyo pekee mwanachama wa EAC ambayo iko katika kundi la nchi "zinazochipukia", huku nyingine zikitajwa kuwa "zinazoendelea kidogo", kumaanisha mauzo yao ya nje yanaweza kuendelea kuingia katika soko la Umoja wa Ulaya bila makubaliano.
Kwa hivyo, Kenya ililazimika kukiuka makubaliano yake - au kuhatarisha kupoteza ufikiaji wa soko lenye faida kubwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
EU yenye mataifa 27 ni mshirika wa pili kwa ukubwa wa kibiashara wa Kenya, baada ya Uchina, na soko kuu la nje la Kenya.
EU inaagiza zaidi mboga, matunda na maua kutoka Kenya ya hadi $1.3bn (£1bn), huku ikisafirisha bidhaa za madini na kemikali, pamoja na mashine, kwa Kenya zenye thamani ya $2.2bn.
Msemaji wa rais wa Kenya Hussein Mohammed alipongeza makubaliano hayo, akisema yatakuwa:
- kuongeza uwekezaji katika sekta ya viwanda
- kutengeneza ajira katika tasnia mbalimbali
- kuiweka nchi kama kitovu cha makampuni ya Ulaya yanayojaribu kuingia katika soko la Afrika Mashariki
- kuwapa wakulima wa Kenya ufikiaji bila ushuru kwa soko lao kubwa zaidi la kuuza nje.
Hata hivyo, maafisa Kenya wamesema machache sana kuhusu ukweli kwamba mpango huo unaipa EU ufikiaji usio na vikwazo katika soko la Kenya, na kupunguzwa kwa ushuru katika kipindi cha miaka 25.
Wasiwasi ni mkubwa kwamba hii inaweza kusababisha bidhaa za Ulaya kujaa Kenya na kuathiri viwanda vya ndani.
Ili kushughulikia maswala haya, serikali italazimika kusaidia wafanyabiashara wa Kenya kujiinua ili kuzuia ushindani kutoka wafanya biashara wakubwa wa Ulaya, huku ikihakikisha mauzo ya nje kwa soko la faida kubwa la EU kuongezeka.
Ina imani kwamba itashughulikia changamoto hiyo, kiasi kwamba inaangazia kufikia makubaliano ya kibiashara na Marekani mwaka ujao, na kuibua swali la hii ina maana gani kwa juhudi za mataifa ya Afrika kuunda mwelekeo wa kibiashara wa pamoja.












