Mahmoud Yussouf Ali achaguliwa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika

x

Chanzo cha picha, Sourced

    • Author, Na Laillah Mohammed
    • Nafasi, BBC Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Djibouti Mohammed Ali Youssouf anasubiria kutangazwa rasmi kama mrithi wa Moussa Faki Mahamat baada ya kuibuka mshindi kwenye kinyang'anyiro kikali dhidi ya wagombea wa Kenya na Madagascar.

Baada ya raundi saba za upigaji kura, Raila Odinga alijiondoa kwenye kinyang'anyiro alipopata matokeo ya chini.

Safari ya aliyekuwa Waziri Mkuu nchini Kenya Raila Odinga kuwa Mwenyekiti wa Tume ya AUC inafikia kikomo, baada ya taifa lake kumpigia kampeni kali.

Kura zilivyopigwa

Kinyanga'anyiro hicho kilikuwa kigumu huku wajumbe wakipiga kura kwa raundi saba, bila ya mshindi wa moja kwa moja kupatikana.

Matokeo ya awali yaliyotangazwa pindi tu kura zilipohesabiwa na baraza la mawaziri ambalo lilisimamia uchaguzi huo wa Februari 15 ni kama ifuatavyo:

Awamu ya Saba:

DJIBOUTI: Mohammmed Ali Youssouf – 33

Awamu Sita:

Djibouti - 26

Kenya- 22

Kura zilizoharibika - 0

Waliokosa kupiga kura – 1

Awamu ya Tano:

Djibouti - 26

Kenya- 21

Kura zilizoharibika - 0

Waliokosa kupiga kura – 1

Awamu ya Nne:

Djibouti - 25

Kenya- 21

Kura zilizoharibika - 1

Waliokosa kupiga kura – 2

Awamu ya Tatu:

Djibouti - 23

Kenya- 20

Madagascar- 5

Waliokosa kupiga kura – 1

Awamu ya Pili:

Kenya – 22

Djibouti – 19

Madagascar – 7

Awamu ya Kwanza:

Djibouti - 18

Kenya- 20

Madagascar- 10

Pia unaweza kusoma:

Ili kutangazwa mshindi, mgombea anapaswa kuwa na uungwaji mkono wa athuluthi mbili ya jumla ya kura zilizopigwa. Katika kikao cha februari 15, Marais 49 au wawakilishi wao wanaotamubiliwa na baraza linaloandaa uchaguzi huo walikuwa na uwezo wa kupiga kura baada ya mataifa sita yaliyosimamishwa uanachama wao kutoweza kufanya hivyo.

Huku Raila Odinga akiuguza jeraha la kushindwa kwenye ulingo wa bara Afrika, si mgeni katiak mashindano makali, kwani aliwahi kuwania Urais nchini Kenya na kuibuka nambari mbili mara tatu.

Raila Odinga

Raila alishindwa uchaguzi wa urais wa mwaka 2022 na Rais wa sasa William Ruto kwa chini ya kura milioni tatu.

Matokeo ya uchaguzi wa leo yanarejesha makovu ya ushindi wa wa Mwanyekiti wa AUC anayeondoka Moussa Faki Mahamat mnamo 2018 dhidi ya mgombea mwengine wa Kenya Balozi Amina Mohammed.

Kinyang'anyiro cha wakati huo pia kilikwenda raundi saba, na hatimaye mgombea wa Chad akatangazwa mshindi.

Wataalaam wa masuala ya Diplomasia na siasa za kanda wanasema kwamba suala la ushindani dhidi ya mataifa yanayozungumza Kifaransa na yale yanayozungumza Kiingereza huenda likawa mojawapo ya sababu kuu kwa Odinga kukosa kutamba kama wengi katika Ukanda wa Afrika Mashariki walivyotarajia.

Hatua pia ya SADC kutaka wanachama wake kumuunga mkono Randriamandrato wa Madagascar limetajwa pia kama sababu nyinginea ya kura za , "Baba" kupungua.

Raila Odinga

Chanzo cha picha, Getty Images

Raila alipotangaza rasmi nia yake ya kuwania kiti hicho, viongozi kadhaa kutoka EAC akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan walizuru Nairobi, Kenya kwa mualiko wa Rais William Ruto kama njia ya kutafuta ungwaji mkono kwa Raila Odinga.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa nchini Kenya, wakati huu ni nafasi ya Kenya kwa kuwa Tanzania iliwahi kushikilia nafasi hii kati ya 1989 na 2001 Salim Ahmed Salim alipokuwa katibu Mkuu wa Umoja wa nchi huru za Afrika (OAU).

Aidha ilipotajwa kwamba Rais wa zamani Jakaya Mrisho Kikwete, angewania kiti hicho, alitangaza wazi katika uzinduzi wa ugombea wa Raila kwamba hakuwa na nia ya kuwania kiti hicho.

Je, kura hupigwa vipi?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Watatu hao walishiriki kwenye uchaguzi ambao upigaji kura ulifanyika kwa njia ya siri. Marais wa mataifa wanachama wa AU, ndio walikuwa wajumbe maalum wenye uwezo wa kupiga kura.

Kulingana na sheria za Jumuiya ya Afrika, ni mataifa ambayo hayakabiliwi na adhabu yoyote ndio yatakayopata fursa ya kupiga kura. Kwa sababu hiyo, ni mataifa 49 pekee ambayo yana uwezo wa kuamua ni nani atakayemrithi Moussa Fakii kama Mwenyekiti wa tume ya AU.

"Kura itakapopigwa, maafisa wa kusimamia uchaguzi huo, watakusanya kura hizo na kuzihesabu.Kisha atahitajika kuwa na uungwaji mkono wa thelithi mbili ya jumla ya kura zilizopigwa , mgombea ambaye atatangazwa mshindi. Ikiwa hakutakuwa na aliyefikisha kiwango hiki, basi kengele itapigwa na kura kupigwa kwa raundi ya pili, ambapo wagombea wawili wa kwanza wataminyana debeni ten ana kulingana na itifaki za kuhesabu kura zitalia kama hapo awali, na kama mambo yatakataa kukamilisha mahitaji ya jinsi sheria za AU zinasema, kura itapigwa kwa mara ya tatu.Ikiwa katika raundi hii hakuna mshindi wa moja kwa moja, basi kura ya Naibu Mwenyekiti inaendelea na akipatikana mshindi atashikilia wadhifa huo kwa muda wa miezi sita, ambapo uchaguzi wa Uenyekiti utahitajika kuandaliwa upya.' Alisema Balozi Mwencha.

Wakati wa uchaguzi wa 2017, Balozi Amina Mohammed alipomenyana na Waziri Mkuu wa zamani wa Chad, Moussa Fakii Mahamat, kura hiyo ilipigwa kwa raundi saba na hatimaye kuamuliwa kwa kura moja tu, kati ya mashindi na aliyeshindwa.

Wataalamu wa Diplomasia kama daktari Peter Mwencha kutoka IRSK wanasema kwamba kuangushwa kwa Bi Mohammed ambaye alikuwa Waziri wa mambo ya kigeni wakati huo chini ya uongozi wa Uhuru Kenyatta, alikosa kupata uungwaji mkono kwa sababu ambazo zilikuwa zaidi ya upinzani kati ya mataifa yanayozunga Kiingereza na yale yanayozungumza Kifaransa.

Wajumbe sasa watasubiri uchaguzi wa Naibu mwenyekiti ambao una wagombea sita kutoka Libya, Algeria na Morrocco kufanyika.

Baada ya hapo wajumbe watawachagua makamishena sita, wawili kutoka majimbo matatu ambayo wakati huu hayajawasilisha mgombea kwenye viti vikuu viwili.

Tume hiyo kwa mujibu wa sheria za AU, inaweza kuhudumu kwa miaka minne na vile vile kuongezewa mingine minne ya kazi kama alivyofanyiwa Moussa Fakii Mahamat ambaye anaondoka baada ya miaka minane kazini.

Nini kitakachofuata Raila kurejea nyumbani mikono mitupu?

Mchambuzi wa siasa nchini Kenya, Barack Muluka anasema kwamba Raila atarejea nyumbani na kuendeleza siasa za ndani kama kawaida.

"Kwa sasa kiti chake cha mwenyekiti wa chama cha ODM kinaweka moto na Prof. Peter Anyang' Nyong'o -ambaye ni gavana wa jimbo la Kisumu – kwa muda. Na vile amepoteza hana pengine pa kurejea isipokuwa nyumbani kwao,"alisema Muluka huku akiongeza kwamba; " Raila, ndio amekuwa kidonda sugu kwa Rais William Ruto, ambaye kwa sasa amemunga mkono kwa asilimia 100 katika kampeni hii.

Wachambuzi wanasema Rais Ruta hangetaka azimio lake la 2027 kuwa na kizingiti kikibwa na ndio maana amefanya kampeni ya kukata na shoka kumhakishia Raila ushindi.

Zimwi la 2017 lililompata Amina lamfuata Raila

Tulipozungumza naye awali Daktari Peter Mwencha alisema kwamba itakuwa vigumu kutabiri kwa sasa lakini kulingana na uchambuzi uliochapishwa kwenye magazeti makuu ya nchini Kenya, siasa za wakati huo zilikuwa kali na wengi walihisi kwamba huenda labda, Kenya ingelifikiria kumuangazia Mkenya ambaye tayari alikuwa akihudumu kama Naibu Mwenyekiti wa AUC wakati huo. Kwa sasa hayo ni maji yaliyomwagika ambayo hayaweza kuzoleka.

Muluka anasema pia alisema, hadhi ya kimataifa ya Raila Odinga huenda ikampa nafasi bora, mbali na kampeni iliyopigwa kumtafutia uungwaji mkono lakini mambo yameenda vingine.

Ila wanavyosema wahenga, kura ni kwa debe, na debe limeamua hatima yake Odinga.

Baada ya kivumbi kutifulia, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Djibouti Mohammed Ali Youssouf ameibuka kidedea.

Maelezo zaidi:

Imehaririwa na Ambia Hirsi