Ebola: Watu wanaoeneza habari potofu mtandaoni nchini Uganda

Chanzo cha picha, Getty Images
"Nadhani hakuna Ebola nchini Uganda." Hayo ni maneno ya Battle Kay, kama anavyojulikana mtandaoni - mwenye umri wa miaka 28 anayeishi katika mji mkuu, Kampala, na anatengeneza video za mitandao ya kijamii akikosoa vitendo vya serikali.
Lakini pia ni sehemu ya wimbi jipya la watu wanaotoa madai ambayo hayajathibitishwa kwamba mlipuko wa sasa wa Ebola umetiwa chumvi au umeundwa kabisa na mamlaka.
Uganda imekuwa ikipambana na Ebola kwa miezi miwili sasa.
Kufikia sasa, kumekuwa na maambukizi ya watu 141 na vifo 55 - vilivyothibitishwa na Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, Medecins Sans Frontieres (MSF) - kati ya watu wake milioni 44.7.
Ukosoaji mkubwa wa rekodi ya serikali umechanganywa na uvumi na madai yasiyo na msingi kuhusu ugonjwa huo.
Kuna madai gani kuhusu Ebola?
Ujumbe wa kupotosha ambao unaenea umekuwa:
- Serikali inaitumia kuhalalisha kuwafungia na kuwadhibiti wananchi.
- Mlipuko huo ni kificho cha kuvuna viungo vya mwili ili kuuza kinyume cha sheria.
- Serikali inaghushi namba za kesi ili kuvutia ufadhili au tu kuwatisha watu.
Kwa mfano, chapisho la mtandao wa kijamii lililodai kuwa viungo vya mwili vilivunwa na Ebola kama jalada lililoangazia ziara ya mwezi Oktoba ya Princess Anne wa Uingereza, dadake Mfalme Charles.
Ilisema hakuna jinsi angeweza kuzuru nchi ambayo ilikuwa na kesi "halisi" za Ebola.

Hatahivyo, Princess Anne alitembelea akijua kulikuwa na mlipuko unaendelea, kwa sababu ya kuhusika kwake na Shule ya Usafi na Tiba ya Kitropiki ya London, ambayo inasaidia kukabiliana na mlipuko huo.
Ingawa ni hatari zaidi, Ebola inaambukiza kidogo sana kuliko virusi vya corona kwani haisambai kwa njia ya hewa.
Huenea kati ya binadamu kwa kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili yaliyochafuliwa - damu, mate, matapishi, mbegu za kiume, uchafu ukeni, mkojo, kinyesi na jasho.
Waziri wa Afya wa Uganda Jane Ruth Aceng amekanusha madai kuhusu uvunaji wa viungo vya mwili kuwa ni uongo kabisa.

Na kutokana na kukaribia kutolewa kwa chanjo ya majaribio dhidi ya virusi hivyo, baadhi ya madai yanadai kuwa Waganda watatumika kama nguruwe.
Kuna chanjo mbili zinazotumika dhidi ya aina tofauti, inayojulikana zaidi ya Ebola, lakini mlipuko huu unasababishwa na aina ya Sudan - ambayo kwa sasa hakuna chanjo iliyoidhinishwa kutumika.
Washiriki watatu wa chanjo wameidhinishwa kufanyiwa majaribio katika jaribio la kimatibabu.
Lakini chanjo bado hazijajaribiwa, achilia mbali kutolewa kwa idadi ya watu kwa ujumla.
Ni nani wanaotoa madai hayo?
Kundi la kwanza la watu, kama Bw Kay, kwa ujumla wanaikosoa serikali ya Yoweri Museveni. Anamuunga mkono kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi - almaarufu Bobi Wine ambaye alishindwa katika uchaguzi wa urais wa Uganda wa 2021 na Bw Museveni.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kura hiyo iligubikwa na shutuma za kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria, kuteswa na mauaji ya waandamanaji yaliyofanywa na vikosi vya usalama.
Matukio haya yamesababisha baadhi, kama Bw Kay, kutoamini chochote ambacho mamlaka inasema. Patricia Ssewungu ni muuguzi anayeishi Uingereza, ambaye anaendelea kujihusisha sana na harakati za kisiasa dhidi ya serikali.
Aliiambia BBC kwamba ingawa aliamini kuwa kulikuwa na maambukizi ya Ebola, alidhani vimetiwa chumvi.
Aliongeza kuwa hii ni kwa sababu ya kile alichokiona kama njia "isiyowajibika" ambayo pesa hutumiwa na serikali mahali pengine kwenye afya, elimu na virusi vya corona.
Wengine wanaohoji mlipuko wa Ebola hapo awali walieneza habari potofu kuhusu virusi vya corona.
Joseph Kabuleta, mgombea mwingine wa kiti cha urais mwaka 2021, amedai serikali inatumia mlipuko huo kujipatia fedha.
Lakini ameenda mbali zaidi akidai chanjo za Ebola si salama, bila kutoa ushahidi wowote. "Lengo kuu la haya yote ni kutumia Waganda kama panya wa maabara kwa chanjo ya majaribio, ambayo athari zake zinaweza kuwa mbaya sana," alichapisha hivi karibuni kwenye mtandao wa Twitter. Pia alikuwa ametoa madai kuhusu usalama wa chanjo za Covid, ambazo haziungwi mkono na ushahidi.
Serikali imekuwa ikisema nini?
Waziri wa Afya Margaret Muhanga hivi karibuni aliliambia bunge la nchi hiyo kuwa siasa kuhusu janga hilo ni mojawapo ya changamoto zinazoikabili serikali.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Baadhi ya wanasiasa... wanachanganya umma kwa kusema hakuna Ebola na janga hili ni propaganda za serikali za kukusanya rasilimali," alisema.
"Hata kwa kujiamini wanasema Wizara ya Afya inapaswa kuacha ugonjwa huo kuenea na watu kukuza kinga, wakisahau yaliyotokea Afrika Magharibi."
Anasema mazungumzo hasi yanaweza kusababisha mlipuko wa kesi - hata katika maeneo ambayo serikali imepata maendeleo dhidi ya kuenea kwa ugonjwa huo.
Marion Apio, ambaye anafanya kazi katika mpango huru wa kuangalia ukweli nchini Uganda, alisema jambo la kawaida ambalo timu yake imegundua sio habari potofu, lakini mapungufu katika ufahamu wa watu kuhusu ugonjwa huo, jinsi unavyoenea na jinsi ya kuzuia, haswa katika maeneo ambayo hayajaathiriwa na mlipuko huo.












