Vita ya Sudan: Ushahidi waonyesha ndege zisizo na rubani za Iran na UAE zilitumika

A city battered by the year-long civil war in Sudan residents in Omduran have found themselves besieged in their homes

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mji uliokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa mwaka mzima nchini Sudan, wakazi wa Omduran wamenaswa majumbani mwao.
    • Author, Abdelrahman Abu Taleb
    • Nafasi, BBC News Arabic
    • Akiripoti kutoka, Cairo

Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zimeshutumiwa kwa kukiuka vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa kwa kutoa ndege zisizo na rubani kwa pande zinazozozana katika mzozo wa miezi 14 ambao umeiharibu Sudan.

Tunaangazia ushahidi unaounga mkono madai hayo.

Asubuhi ya tarehe 12 Machi 2024, wanajeshi wa serikali ya Sudan walikuwa wakisherehekea hatua iliyofanywa kijeshi ambayo haiyajawahi kutokea.

Hatimaye walikuwa wameteka tena makao makuu ya shirika la utangazaji la serikali katika mji mkuu, Khartoum.

Kama sehemu kubwa ya jiji, jengo hilo lilikuwa limeangukia mikononi mwa wanajeshi wa Rapid Support Forces (RSF) mwanzoni mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe miezi 11 kabla.

Kilichojulikana kuhusu ushindi huu wa kijeshi ni kwamba video zilionesha shambulio hilo lilitekelezwa kwa msaada wa ndege zisizo na rubani zilizotengenezwa na Iran.

Pia unaweza kusoma:

Ndege zisizo na rubani zimeonekana Sudan

Wakati wa mwanzo wa vita, jeshi la Sudan lilitegemea jeshi la anga, kulingana na Suliman Baldo, mkurugenzi wa Sudan Transparency and Policy Observatory.

"Vikosi vya jeshi vilijikuta katika hali ambayo vikosi vyao wanavyovipendelea vimezingirwa, na kukosa vikosi vya ardhini," anasema.

Vikosi vya RSF viliendelea kudhibiti maeneo mengi ya Khartoum na Darfur magharibi mwa Sudan, wakati vikosi vya SAF vilidumisha uwepo wake angani.

Mapema Januari 2024, video iliibuka kwenye mtandao wa x ikionesha ndege isiyo na rubani ya jeshi iliyodunguliwa na RSF.

Kwa mujibu wa Wim Zwijnenburg, mtaalamu wa ndege zisizo na rubani na mkuu wa Mradi wa kuondokana na Silaha zenye madhara kwa Binadamu katika shirika la amani la Uholanzi, mabaki yake, injini, na mkia wake ulifanana na ndege isiyo na rubani iliyotengenezwa na Iran iitwayo Mohajer-6.

Ndege ya Mohajer-6 ina urefu wa mita 6.5, inaweza kupaa hadi kilomita 2,000 na kufanya mashambulizi ya angani kwa kutumia silaha za kuongozwa.

The drone identified at Wadi Seidna had a length of 6.5m and wingspan of 10m

Chanzo cha picha, Planet Labs

Maelezo ya picha, Ndege isiyo na rubani iliyotambuliwa katika kituo cha kijeshi cha Wadi Seidna ilikuwa na urefu wa mita 6.5 na ilikuwa na mabawa ya mita 10.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Zwijnenburg alibainisha toleo jingine la ndege hiyo isiyo na rubani katika picha ya satelaiti ya kambi ya jeshi ya Wadi Seidna, kaskazini mwa Khartoum, iliyochukuliwa siku tatu baadaye.

"Droni hizi ni nzuri sana kwa sababu zinaweza kutambua malengo kwa usahihi na zinahitaji mafunzo kidogo," Zwijnenburg anasema.

Wiki tatu baada ya ndege ya Mohajer-6 kudunguliwa, video iliibuka ya ndege nyingine isiyo na rubani iliyoangushwa na RSF.

Zwijnenburg ililinganisha hii na Zajil-3, toleo la ndani la ndege isiyo na rubani ya Ababil-3 ya Iran.

Ndege zisizo na rubani za Zagjil-3 zimetumika nchini Sudan kwa miaka mingi.

Lakini Januari ilikuwa ni matumizi yao ya kwanza katika vita hivi, kama ilivyoangaziwa na BBC na PAX.

Mnamo mwezi Machi, Zwijnenburg iligundua toleo moja zaidi la Zajil-3 lililonaswa katika picha ya satelaiti ya Wadi Seidna.

"Ni dalili ya uungaji mkono wa Iran kwa jeshi la Sudan," anasema, ingawa baraza la uongozi la Sudan limekanusha kupata silaha kutoka Iran.

"Ikiwa ndege hizi zisizo na rubani zina vifaa vya kuongozwa, inamaanisha zilitolewa na Iran kwa sababu silaha hazitengenezwi nchini Sudan," Zwijnenburg anaongeza.

Mapema mwezi Disemba, ndege ya abiria ya Boeing 747 ya shehena ya Iran ya Qeshm Fars Air ilipaa kutoka uwanja wa ndege wa Bandar Abbas nchini Iran, kuelekea Bahari ya Shamu kabla ya kutoweka kwenye rada.

Saa chache baadaye, satelaiti zilinasa picha ya ndege ya aina hiyo katika uwanja wa ndege wa Port Sudan mashariki mwa nchi, ambako maafisa wa jeshi la Sudan wana makao yao.

Picha ya ndege hiyo hiyo kwenye njia ya kupaa ndege ilisambaa kwenye mtandao wa X

Qeshm Fars Air Boeing 747 in Port Sudan airport

Chanzo cha picha, X @SudanSena

Maelezo ya picha, Picha iliyotumwa kwenye mtandao wa X na @SudanSena iliyoratibiwa na BBC hadi uwanja wa ndege wa Port Sudan ilipendekeza usafirishaji wa silaha.

Safari hii ya ndege ilirudiwa mara tano hadi mwisho wa Januari, mwezi huo huo matumizi ya ndege zisizo na rubani za Iran yalirekodiwa.

Shirika la ndege la Qeshm Fars Air linakabiliwa na vikwazo vya Marekani kutokana na shutuma nyingi za kusafirisha silaha na wapiganaji Mashariki ya Kati, hasa kuelekea Syria, mojawapo ya washirika wakuu wa Iran.

Kila upande una malengo yake

Sudan ilikuwa na historia ndefu ya ushirikiano wa kijeshi na Iran kabla ya uhusiano kumalizika mwaka 2016 kutokana na mzozo kati ya Saudi Arabia na Iran, huku Sudan ikiegemea Saudi Arabia.

"Silaha nyingi za Sudan zilitengenezwa kienyeji kwa modeli za Iran," anasema Suliman Baldo.

Tangu kuanza kwa mzozo wa sasa, serikali ya Sudan imerejesha uhusiano na Tehran.

Kulingana na Baldo, kila upande una malengo yake.

"Iran inatafuta kuwa na ushawishi katika kanda. Iwapo watapata makubaliano ya kijiografia, bila shaka watatoa ndege zisizo na rubani za hali ya juu zaidi," anasema.

BBC iliwasiliana na jeshi la Sudan, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na Qeshm Fars Air ili kutoa maoni yao kuhusu madai kwamba ndege zisizo na rubani za Iran zinatumiwa katika mzozo huo lakini haijapata jibu.

Lakini katika mahojiano na BBC, Malik Agar, makamu wa rais wa Baraza Kuu la Sudan, alisema: "Hatupokei silaha yoyote kutoka kwa chama chochote... Silaha zinapatikana katika soko la magendo, na sasa soko la magendo limegeuka kuwa soko lisilo rasmi".

A PAX drones expert suggested this photo posted on X by an account called @RapidSupportSdn shows a Zagil 3 drone

Chanzo cha picha, @RapidSupportSdn

Maelezo ya picha, Mtaalamu wa ndege zisizo na rubani za PAX alipendekeza picha hii iliyowekwa kwenye mtandao wa X na akaunti iitwayo @RapidSupportSdn kuonyesha droni ya Zagil 3

Marufuku ya silaha ya Umoja wa Mataifa yapuuzwa

Wakati huo huo, ushahidi uliibuka mapema katika vita kwamba RSF wametumia droni za quadcopter zenye uwezo wa kuangusha makombora ya ukubwa wa milimita 120mm.

Picha kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha jeshi lilikuwa limedungua nyingi za ndege hizi zisizo na rubani.

Brian Castner, mtaalamu wa silaha katika Amnesty International, ananyooshea kidole cha lawama UAE.

"UAE imewapa washirika wake ndege zisizo na rubani kama hizo katika maeneo mengine yenye migogoro kama vile Ethiopia na Yemen," anasema.

Quadcopter drone

Chanzo cha picha, X @war_noir

Maelezo ya picha, Jeshi la Sudan lilikuwa limekamata droni nyingi za quadcopter zinazotumiwa na RSF

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama mapema mwaka huu, wataalam wa ufuatiliaji wa anga waliona ndege ya kiraia inayodaiwa kusafirisha silaha kutoka UAE hadi kwa vikosi vya RSF - madai ambayo UAE inakanusha.

Njia hiyo inaanzia uwanja wa ndege wa Abu Dhabi, inapitia viwanja vya ndege vya Nairobi na Kampala, kabla ya kuishia katika uwanja wa ndege wa Amdjarass nchini Chad, kilomita chache kutoka mpaka wa magharibi wa Sudan, ambako RSF ina ngome yake.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa pia inanukuu vyanzo vya ndani na vikundi vya kijeshi vinavyoripoti kuwa magari yaliyokuwa yamebeba silaha yanashukisha ndege katika uwanja wa ndege wa Amdjarass mara kadhaa kwa wiki, kabla ya kusafiri hadi Darfur na maeneo mengine ya Sudan.

"UAE pia ina maslahi ya kiuchumi nchini Sudan na inatafuta kujikita kwenye Bahari ya Shamu," anasema Baldo.

UAE imekanusha mara kwa mara kuwa ndege hizi zimesafirisha silaha, ikisema badala yake, zilikuwa zikitoa misaada ya kibinadamu.

Katika taarifa, afisa wa serikali aliiambia BBC, UAE imejitolea kutafuta "suluhisho la amani kwa mzozo unaoendelea".

RSF haijajibu ombi la BBC la kutoa maoni.

Ndege zisizo na rubani ambazo pande zote mbili zinazopambana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe zinadaiwa kuziingiza nchini humo zinakiuka azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililotolewa mwaka 2005, ambalo linapiga marufuku usambazaji wa silaha kwa serikali ya Sudan na makundi yenye silaha huko Darfur.

"Baraza la Usalama lazima lichukue jukumu na kuzingatia hali ya Sudan, njaa inayokaribia, na idadi ya watu waliouawa na waliokimbia makazi yao, na kutekeleza mara moja hatua ya kuiwekea vikwazo vya silaha Sudan yote," anasema Castner.

Kunusurika kwa muujiza

Tangu kuonekana kwa ndege zisizo na rubani katika anga ya Sudan, hali ardhini imebadilika kiasi.

Jeshi la Sudan limefanikiwa kukabiliana na hatua ya wanajeshi wake kuzingirwa katika maeneo kadhaa.

Na RSF imejiondoa katika baadhi ya vitongoji magharibi mwa mji mkuu.

Kwa mujibu wa Suliman Baldo, mabadiliko haya yametokea kutokana na ndege zisizo na rubani za Iran.

Baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa vita, takriban raia 16,650 wameuawa, kulingana na Armed Conflict Location & Event Data Project (ACLED).

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) linakadiria kuwa watu milioni 12 wamelazimika kuhama makazi yao.

Abdullah Makkawi ni mmoja ambaye sasa amekimbilia Misri. Alipokuwa bado kusini mwa Khartoum Julai iliyopita, anasema aliponea chupuchupu kifo wakati ndege zisizo na rubani, ambazo anasema zilikuwa za vikosi vya RSF, ziliposhambulia eneo alilokuwa.

"Nilikimbilia ndani ya nyumba, na tukajificha kwenye chumba chenye paa la zege... Mama yangu, ndugu zangu wanne na mimi tulijificha chini ya vitanda," anasema.

Abdullah anasema walisikia sauti ya ndege isiyo na rubani ikiangusha kombora kwenye chumba kilichofuata, ambacho kilikuwa na paa la mbao.

"Kama tungekuwa katika chumba hicho, sote tungeuawa. Tulinusurika kimiujiza,” amesema

Mwanzoni mwa 2024, mzozo ulienea katika maeneo mapya nje ya mji mkuu.

Vifo vya raia kutokana na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani viliripotiwa kwa mara ya kwanza kaskazini, mashariki na kati mwa Sudan.

Kabla ya kukimbilia Misri, Abdullah aliiacha familia yake huko Bandari ya Sudan Mashariki, akichukulia kuwa ni sehemu salama.

Lakini sasa anahofia ndege zisizo na rubani zinaweza kuwafikia huko pia.

“Watu wa Sudan wamechoshwa na vita. Tunachotaka ni vita ikome. Ikiwa nchi za kigeni zitaacha kuunga mkono pande zote mbili kwa silaha, itaisha.

Soma zaidi:

Imetafsiriwa na Asha Juma