Njaa yatanda Sudan,manusura wa vita wasimulia madhila ya mauaji na ubakaji

Chanzo cha picha, Dany Abi Khalil / BBC
- Author, Feras Kilani - Sudan, Mercy Juma- Chad
- Nafasi, BBC NEWS
Raia walionaswa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan wametoa maelezo ya wazi kwa BBC kuhusu ubakaji, ghasia za kikabila na kunyongwa mitaani. Wanahabari wetu wamefanikiwa kufika mstari wa mbele wa mapigano karibu na mji mkuu, Khartoum.
Maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa wamesema mzozo huo umeitumbukiza nchi hiyo katika "mojawapo ya jinamizi baya zaidi la kibinadamu katika historia ya hivi karibuni" na linaweza kusababisha janga kubwa zaidi la njaa duniani.
Pia kuna hofu kwamba huko Darfur, magharibi mwa nchi, marudio ya kile Marekani ilichoita mauaji ya halaiki miaka 20 iliyopita huenda yanaanza kujitokeza.
ONYO: Makala haya yana simulizi za unyanyasaji wa kimwili na kingono
Mlipuko mkubwa unatikisa barabara huko Omdurman. Watu wanapiga kelele na kukimbia pande zote, wakipiga kelele: "Rudi nyuma, rudi, kutakuwa na mwingine." Moshi mzito unafunika kila kitu.
Muda mfupi kabla, barabara iliyoharibiwa ilikuwa imejaa watembea kwa miguu wakinunua mchele, mkate na mboga kutoka kwenye maduka, ambayo yalikuwa yameanza kufunguliwa tena hivi karibuni.
Katikati ya mwezi wa Februari, jeshi la Sudan lilitwaa tena mji huo, moja kati ya mitatu kando ya Mto Nile unaounda mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
Kwa vyombo vya habari vya kimataifa, kupata fursa ya kuangazia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka Aprili mwaka jana imekuwa vigumu, lakini BBC imeweza kufika mstari wa mbele.
Timu yetu iliupata mji uliokuwa na shughuli nyingi wa Omdurman ukibadilishwa kuwa nyika iliyo na watu wengi.

Chanzo cha picha, Dany Abi Khalil / BBC
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mapambano makali ya madaraka kati ya jeshi la nchi hiyo na mshirika wake wa zamani, kundi la wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), yamesababisha vifo vya takribani watu 14,000 kote nchini au pengine wengi zaidi.
Kwa karibu mwaka mmoja, jeshi na RSF limepigana Khartoum na miji ya karibu.
RSF imechukua udhibiti wa maeneo ya kusini mwa mji mkuu, pamoja na maeneo makubwa ya Darfur, ambayo yamekuwa katika machafuko kwa miaka mingi kutokana na ghasia kati ya jumuiya zake mbalimbali za Kiafrika na Kiarabu.
Wanawake ambao walitorokea Darfur hadi nchi jirani ya Chad wameilezea BBC kuhusu matukio ya kubakwa, wakati mwingine mara nyingi na wanamgambo.
Wanaume katika kambi walituambia walikuwa wametoroka kunyongwa mitaani na kutekwa nyara.
Ikiwekwa kwenye mstari wa mbele na jeshi huko Omdurman, mienendo ya timu ya BBC ilidhibitiwa kwa uangalifu, tulikuwa na mshauri nasi na hatukuruhusiwa kurekodi shughuli za kijeshi.
Jeshi linahofia taarifa kuhusu shughuli zake kuvuja.
Wakati mpigapicha wetu alipoanza kupiga picha baada ya mlipuko, watu wenye silaha waliovalia kiraia walimzunguka, mmoja akimnyooshea bunduki kichwani.
Tunabaini ni wanaintelijensia wa kijeshi, inatoa ishara ya jinsi hali ilivyo hapa.
Licha ya mafanikio ya hivi karibuni ya jeshi huko Omdurman, bado tunaweza kusikia kurushiana risasi za moto katika eneo hilo mara kwa mara.

Chanzo cha picha, Dany Abi Khalil / BBC
Sehemu ya mstari wa mbele sasa inapita kando ya Mto Nile, ambayo inatenganisha Khartoum upande wa mashariki kutoka Omdurman, ambayo ni magharibi mwa mto huo.
Wanajeshi wanatuambia wavamizi wa RSF wamekaa katika vyumba vya ghorofa kando ya maji kutoka maeneo ya jeshi la Sudan kwenye jengo la bunge lililoharibiwa vibaya.
Soko la zamani la Omdurman, ambalo hapo awali lilikuwa na shughuli nyingi na wenyeji na wageni, limeharibika, maduka yake yameporwa. Magari mengi barabarani ni ya kijeshi.
Zaidi ya watu milioni tatu wamekimbia Jimbo la Khartoum katika kipindi cha miezi 11 iliyopita, lakini baadhi ya wakazi wa Omdurman wamekataa kuondoka. Wengi tunaokutana nao ni wazee.

Chanzo cha picha, Dany Abi Khalil / BBC
Chini ya kilomita moja kutoka mstari wa mbele, Mukhtar al-Badri Mohieddin anatembea na fimbo karibu na msikiti wenye mnara ulioharibika.
Eneo la wazi limefunikwa na makaburi ya muda, vilima vya ardhi vilivyo na alama za matofali yaliyovunjika, mbao na saruji.
"Kuna watu 150 hapa. Niliwajua wengi wao, Mohamed, Abdullah... Jalal," anasema, akisimama kwa muda mrefu, Dk Youssef al-Habr, profesa maarufu wa fasihi ya Kiarabu.
"Ni mimi tu nimesalia," anaongeza.
Jeshi la Sudan limekosolewa kwa matumizi makubwa ya mabomu ya angani, ikiwa ni pamoja na katika maeneo ya kiraia ambako wapiganaji wa RSF wanajificha, ingawa linasema inachukua "hatua muhimu" kulinda raia.
Watu hapa wanashikilia pande zote mbili kuwajibika kwa uharibifu ndani na karibu na mji mkuu.
Lakini wengi wanaishutumu RSF kwa uporaji na mashambulizi wakati ilipodhibiti eneo hilo.
"Walisafisha nyumba kwa kuchukua mali, waliiba magari, TV, waliwapiga wazee, hata wanawake," mkazi Muhammad Abdel Muttalib anatuambia.
"Watu walikufa kwa njaa, niliwatoa baadhi yao nje ya nyumba zao ili miili isiozee ndani," anaongeza.
Anasema "inajulikana sana" kwamba wanawake walibakwa majumbani mwao na kuwapapasa wakati wa ukaguzi wa usalama.

Chanzo cha picha, Dany Abi Khalil / BBC
Afaf Muhammad Salem, mwenye umri wa karibu miaka hamsini, alikuwa akiishi na kaka zake huko Khartoum wakati vita vilipoanza.
Anasema alihamia ng'ambo ya mto hadi Omdurman baada ya kushambuliwa na wapiganaji wa RSF, ambao anasema walipora nyumba yao na kumpiga risasi kaka yake mguuni.
"Walikuwa wakiwapiga wanawake na wazee na kuwatishia wasichana wasio na hatia," anasema.
Ni rejeleo lililofichwa la unyanyasaji wa kijinsia, mada ambayo ni mwiko nchini Sudan.
"Kuivunja heshima kunadhuru zaidi kuliko kuchukua pesa," anaongeza.
'Silaha ya kulipiza kisasi'
Waathiriwa wa ubakaji wanaweza kukabiliwa na unyanyapaa na kutengwa maisha yao yote kutoka kwa familia na jamii zao. Watu wengi huko Omdurman hawakutaka kuzungumzia suala hilo.
Lakini zaidi ya kilomita 1,000 (maili 621) kuelekea magharibi, katika kambi za wakimbizi zinazosambaa mpakani mwa Chad, wingi wa shuhuda zinazoibuka za unyanyasaji wa kijinsia unalazimisha kiwango kipya, cha kutisha cha uwazi kuhusu vitendo hivi.

Chanzo cha picha, Marek Polaszewski / BBC
Amina, ambaye jina lake tumebadilisha ili kuuficha utambulisho wake, amekuja kwenye kliniki ya muda inayoendeshwa na shirika la misaada la Médecins Sans Frontières, akitaka kuavya mimba. Anatusalimia bila kututazama.
Msichana huyo mwenye umri wa miaka 19, ambaye ametoroka kutoka Darfur nchini Sudan, aligundua kuwa alikuwa mjamzito siku iliyotangulia. Anatumai familia yake haitawahi kujua.
"Sijaolewa na nilikuwa bikira," Amina anasema kwa sentensi akionesha kugugumia.
Mnamo Novemba, wanamgambo walimkamata, pamoja na shangazi yake na binamu zake, walipokuwa wakikimbia kutoka mji wa kwao wa Ardamata hadi jiji la karibu la Geneina, anatuambia.
"Wengine walitoroka lakini walinihifadhi kwa siku nzima. Walikuwa wawili, na mmoja alinibaka mara nyingi kabla sijafanikiwa kutoroka," anasema.

Chanzo cha picha, Marek Polaszewski / BBC
Kupanuka kwa utawala wa RSF huko Darfur, ukiungwa mkono na wanamgambo washirika wa Kiarabu, umeleta ongezeko la mashambulizi ya kikabila dhidi ya wakazi weusi wa Afrika, hasa kabila la Masalit.
Hadithi ya Amina ni moja tu ya shuhuda nyingi za mashambulizi dhidi ya raia yaliyotokea karibu tarehe 4 Novemba wakati RSF na washirika wake walipoteka ngome ya kijeshi ya Sudan huko Ardamata.
Inafuatia ghasia za mwanzoni mwa mwaka, ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa iliyoonekana na BBC inasema kuwa zaidi ya watu 10,000 wanaaminika kuuawa katika eneo hilo tangu Aprili mwaka jana.
Umoja wa Mataifa umeandika waathiriwa wapatao 120 wa unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro nchini kote, ambao unasema "ni uwakilishi mdogo wa hali halisi".
Inasema wanaume waliovalia sare za RSF na watu wenye silaha wanaoshirikiana na kundi hilo waliripotiwa kuhusika na zaidi ya asilimia 80 ya mashambulizi hayo. Kando, pia kumekuwa na ripoti za unyanyasaji wa kijinsia na jeshi la Sudan.
Nje kidogo ya kambi hiyo hiyo, ambayo iko katika mji wa mpakani wa Adré, takribani wanawake na wasichana 30 hukutana kwenye kibanda saa sita mchana.
Puto za waridi na buluu zinaning'inia kutoka kwenye kamba juu ya vichwa vyao, pamoja na noti zilizoandikwa kwa mkono. "Ubakaji sio majaliwa; ni mazoea ambayo yanaweza kukomeshwa," mmoja anasoma.
Machozi hutiririka wanawake wanapozungumza juu ya madhila wanayopitia ya unyanyasaji wa kimwili na kingono.

Chanzo cha picha, Marek Polaszewski / BBC
Maryamu, sio jina lake halisi, anasema alibakwa na watu wenye silaha waliokuwa wamevalia vilemba vya wapiganaji wa Kiarabu katika eneo hilo, mwezi Novemba nyumbani kwake huko Geneina.
Alikuwa na ugumu wa kutembea baadaye, anasema, huku akilia huku akielezea kukimbia: "Watu walikuwa wakikimbia, lakini hatukuweza kwa sababu bibi yangu hawezi kukimbia. Pia nilikuwa navuja damu."
Zahra Khamis, mfanyakazi wa kijamii ambaye ni mkimbizi mwenyewe, anaendesha kikundi.
Amina na Maryamu wote wanatoka katika jamii za Waafrika weusi, na Bi Khamis anasema hawa, hasa wa kabila la Masalit, wanalengwa huko Darfur.

Chanzo cha picha, Marek Polaszewski / BBC
Wakati wa vita huko Darfur miaka 20 iliyopita, wanamgambo wa Kiarabu walioitwa Janjaweed, ambapo RSF ina mizizi yake, walihamasishwa na Rais wa zamani Omar al-Bashir kukomesha uasi wa makabila yasiyo ya Kiarabu.
Umoja wa Mataifa unasema watu 300,000 waliuawa na ubakaji ulitumiwa sana kama njia ya kutisha jamii za Waafrika weusi na kuwalazimisha kukimbia.
Baadhi ya viongozi wa Janjaweed na Bw Bashir wamefunguliwa mashtaka na ICC kwa tuhuma za mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Wamekana mashtaka na hakuna mtu aliyehukumiwa.
Bi Khamis anaamini ubakaji unatumiwa katika mzozo huu "kama silaha ya kulipiza kisasi".
"Wanafanya hivi kwa wanawake kwa sababu ubakaji unaacha athari kwa jamii na familia," anaongeza.
Katika ufahamu adimu wa mitazamo inayoendesha unyanyasaji dhidi ya wanawake, mwanachama mmoja wa RSF ambaye anajielezea kama "field commander'' alichapisha video kwenye mitandao ya kijamii mnamo Novemba.
"Tukibaka binti yako au msichana wako, ni jicho kwa jicho(adhabu). Hii ni nchi yetu na hii ni haki yetu na tuliichukua," anasema kwenye kipande hicho ambacho sasa kimefutwa.
Katika kujibu maswali ya BBC kuhusu ubakaji na mashambulizi mengine, RSF ilisema upelelezi wa kijeshi wa Sudan ulikuwa "ukiwaandikisha watu kuvaa nguo za RSF na kufanya uhalifu dhidi ya raia ili isemekane kwamba RSF wanafanya uhalifu, unyanyasaji wa kingono na utakaso wa kikabila".
"Labda tukio moja au mawili yalifanywa na wapiganaji wa RSF na waliwajibishwa," Omran Abdullah Hassan kutoka ofisi ya ushauri ya kiongozi wa RSF aliiambia BBC.
Mwaka jana, RSF ilisema itaanzisha mchakato wa kuchunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na vikosi vyake, lakini Umoja wa Mataifa unasema hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa.
'Kama wewe ni kabila la Masalit, wanakuua'
Katika makazi mengine katika kambi hiyo hiyo, mikono ya Ahmat inatetemeka anaposhika simu, akitazama video, ambayo imethibitishwa na BBC, inayoonesha watu watano wasio na silaha wakiwa wamejipanga kwenye barabara moja huko Ardamata mnamo Novemba.
"Nitawamaliza," sauti inapazwa kwa Kiarabu cha Sudan, kabla ya watu hao kufyatuliwa risasi na bunduki.
"Huyu ni Amir, na huyu ni Abbas...," Ahmat anasema, chozi likishuka shavuni mwake.

Chanzo cha picha, SOCIAL MEDIA
Hii ni mara ya kwanza kwa kijana huyo mwenye umri wa miaka 30, ambaye jina lake tumelibadilisha, kuona picha za wakati alipopigwa risasi. Ilirekodiwa, inaonekana na mmoja wa watu wenye silaha, tarehe 5 Novemba, siku moja baada ya RSF kukamata ngome na kuwekwa mtandaoni.
Ahmat anasema binamu yake Amir na rafiki yake Abbas walikufa papo hapo, lakini yeye na wale wengine wawili walinusurika.
Kovu kubwa mgongoni mwake linaonesha jeraha ambapo risasi ilipita kwenye bega lake. Anasema alikuwa mwalimu kabla ya vita na kwamba wote watano walikuwa raia.
"Tulijilaza kana kwamba tumekufa," anasema. "Nakumbuka nikiomba. Nilikuwa nikifikiri ulikuwa mwisho."
Ahmat anasema alitekwa nyara kutoka karibu na nyumba yake na wanachama wa RSF na washirika wao. Video inaonesha wanaume waliovaa mtindo wa kawaida wa vikosi hivi.
Wanaume wengine wawili walitoa ushuhuda wa kina kwa BBC wa kutekwa nyara na kujeruhiwa na watu wenye silaha wanaoamini kuwa walihusishwa na RSF wakati huo huo huko Ardamata.
Mmoja wao, Yussouf Abdallah mwenye umri wa miaka 55, alitueleza kuwa alifanikiwa kutoroka baada ya kushikiliwa na watu waliokuwa na silaha. Anasema aliona wakimuua mama na mtoto wake mchanga.

Chanzo cha picha, Marek Polaszewski / BBC
"Waliuliza ikiwa tunatoka katika jamii ya Masalit na, kama wewe ni wa jamii hiyo, wanakuua moja kwa moja," aliongeza.
Sudan iliingia katika kipindi kipya cha ukosefu wa utulivu mwaka wa 2019, wakati maandamano ya mitaani na mapinduzi ya kijeshi yalipomaliza utawala wa karibu wa miongo mitatu wa Bw Bashir.
Serikali ya pamoja ya kijeshi na ya kiraia ilianzishwa, lakini hiyo ilipinduliwa katika mapinduzi mengine na jeshi na RSF mnamo Oktoba 2021.
Lakini washirika hao wawili walitofautiana kuhusu hatua iliyopendekezwa kuelekea utawala wa kiraia na jinsi RSF inapaswa kuunganishwa katika vikosi vya kawaida vya kijeshi.
Aprili mwaka jana, wakati RSF ilipotuma tena wanachama wake kote nchini, jeshi la Sudan liliona hatua hiyo kama tishio, na ghasia zilianza, na hakuna upande uliotaka kuacha mgao wa faida wa madaraka.
'Hatari ya kukumbwa na njaa'
Takribani mwaka mmoja sasa, mashirika ya misaada yameonya juu ya hali ya kibinadamu inayozidi kudorora, huku shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, Unicef, likisema baadhi ya jamii zinakaribia kupata baa la njaa.
Manasek mwenye umri wa miaka mitatu ni mmoja wa mamia ya maelfu ya watoto ambao tayari wana utapiamlo mkali. Hana nguvu za kutembea na hawezi kuinua kichwa chake.
Mama yake Ikram anamlaza katika hospitali ya Unicef huko Port Sudan, mji ulio kwenye Bahari ya Shamu ambako maelfu ya watu wanaokimbia mapigano huko Khartoum wametafuta hifadhi na ambako taasisi nyingi za serikali na mashirika ya kibinadamu pia yamehamia.
"Tulipoteza maisha yetu, tukapoteza kazi zetu," anasema, akielezea kuwa mumewe amekwenda kaskazini mwa Sudan kutafuta kazi ya shamba na jinsi bei ya chakula ilivyopanda bila kufikiwa. Anainamisha kichwa, huku akifuta machozi, akashindwa kusema zaidi.

Chanzo cha picha, Dany Abi Khalil / BBC
Tunatembelea shule huko Port Sudan. Madarasa ambayo wanafunzi walijifunza mara moja sasa yamejaa familia zilizokata tamaa.
Mkondo wa maji taka unatiririka kando ya ua, ambapo watoto hucheza bila viatu kwenye rundo la takataka. Tunaambiwa watu watano wamekufa kwa kipindupindu hapa.
Zubaida Ammar Muhammad, mama wa watoto wanane, anakohoa huku akituambia ana saratani ya damu na amekuwa na maumivu tangu Aprili, wakati dawa zake zilipokwisha. Hakuweza kupata zaidi wakati vita vilipozuka na familia ikakimbia kutoka eneo la Khartoum.
Mumewe alijitolea kupigana na jeshi la Sudan, na hajamsikia kwa miezi miwili. Mama yake, bibi yake na watoto watatu wanaokaa nao wanaweza kumhudumia kidogo lakini wakiangalia afya yake ikizorota.
Katika Bandari ya Sudan pia tunakutana na kundi la Wakristo wa Coptic ambao wamekimbia mji mkuu, kuepuka vitisho na mashambulizi ya RSF, na mashambulizi ya anga ya kijeshi.
"Jeshi la anga huko Khartoum lilituangamiza," anasema mmoja wao, Sarah Elias.
Anasema shambulizi la anga lilimuua mumewe, na jingine lilipiga nyumba ya jirani, na kuua watu tisa, huku wanajeshi wakiwalenga wapiganaji wa RSF waliokuwa wamejificha katika maeneo ya makazi na makanisa.
Marekani inasema pande zote mbili zimefanya uhalifu wa kivita, na RSF na wanamgambo washirika pia wamefanya uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya kikabila.
Pande zote mbili zinakanusha madai hayo.
Miezi kumi na moja ya vita, kuna dalili ndogo ya nia ya pande zote mbili kumaliza mapigano.
Wengi wa walio na uwezo wa kuondoka wameikimbia nchi na wakati migogoro, njaa na magonjwa yanaendelea, watu wengi hapa wanashangaa ni nini kitasalia kwa mtu yeyote kutangaza ushindi.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga.












