Kwanini nchi za Magharibi zimeiwekea Ukraine ukomo katika kutumia makombora yao?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Frank Gardner
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kuna dalili kubwa kwamba Marekani na Uingereza ziko tayari kuondoa vikwazo vyao ndani ya siku chache, ili Ukraine itumie makombora ya masafa marefu kulenga shabaha ndani ya Urusi. Ukraine imekuwa ikiomba ruhusa hii kwa muda mrefu sasa.
Storm Shadow ni kombora la masafa marefu la Uingereza na Ufaransa lenye uwezo wa kusafiri hadi kilomita 250 (maili 155).
Hufyatuliwa kutoka katika ndege kisha huruka kwa kasi inayokaribiana na kasi ya sauti, hutembea karibu na ardhi, kabla ya kushuka chini kabisa na kulipuka.
Storm Shadow inachukuliwa kuwa silaha bora ya kupenya kwenye mahandaki magumu na ghala za kihifadhi silaha, kama yanayotumiwa na Urusi katika vita vyake dhidi ya Ukraine.
Lakini kila kombora hugharimu karibu dola za Kimarekani milioni 1 (£767,000), kwa hivyo linarushwa kwa uangalifu mkubwa, kwa kutanguliza droni za bei nafuu kwanza ili kuivuruga mifumo ya ulinzi wa anga ya adui, kama Urusi inavyofanya kwa Ukraine.
Uingereza na Ufaransa tayari wametuma makombora haya kwa Ukraine - lakini kwa sharti kwamba Kyiv inaweza tu kuyatumia kulenga shabaha ndani ya mipaka yake ya nchi.
Yametumiwa kwa ufanisi mkubwa, kushambulia makao makuu ya jeshi la wanamaji wa Urusi katika Bahari Nyeusi huko Sevastopol na kufanya eneo lote la Crimea kutokuwa salama kwa jeshi la wanamaji wa Urusi.
Justin Crump, mchambuzi wa masuala ya kijeshi, afisa wa zamani wa Jeshi la Uingereza na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la ushauri la Sibylline, anasema Storm Shadow imekuwa silaha yenye ufanisi mkubwa kwa Ukraine, ikishambulia kwa usahihi shabaha zilizolindwa vyema katika eneo la Ukraine linalokaliwa kwa nguvu.
"Haishangazi kwamba Kyiv imeshawishi litumike ndani ya Urusi, hasa kulenga viwanja vya ndege vinavyotumiwa kuanzisha mashambulizi ambayo hivi karibuni yamevuruga vita vya mstari wa mbele vya Ukraine," anasema.
Kwanini Ukraine inataka ruhusa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Miji ya Ukraine ilio katika mstari wa mbele wa vita, yako chini ya mashambulizi ya kila siku ya Urusi. Makombora ya masafa marefu husababisha uharibifu kwenye maeneo ya kijeshi, nyumba za ghorofa na hospitali - kutoka ndege za Urusi zilizo mbali ndani ya Urusi yenyewe.
Kyiv inalalamika kwamba kutoruhusiwa kushambulia maeneo ambayo mashambulizi haya ndio hutoka ni sawa na kupigana vita hivi ikiwa imefungwa mkono mmoja nyuma ya mgongo wake.
Katika kongamano la usalama la Globsec nililohudhuria huko Prague mwezi huu, Ukraine ilisema vituo vya kijeshi vya Urusi vina ulinzi mzuri kuliko raia wa Ukraine wanaoshambuliwa kwa sababu ya vizuizi hivi.
Ukraine ina droni zake za masafa marefu. Wakati fulani, mashambulizi ya ndege hizi, yamefika mamia ya kilomita ndani ya Urusi. Lakini zinaweza kubeba tu vilipuzi kidogo na hugunduliwa na kudunguliwa.
Kyiv inasema ili kurudisha nyuma mashambulizi ya anga ya Urusi, inahitaji makombora ya masafa marefu, ikiwa ni pamoja na Storm Shadow na makombora ya Marekani ya Atacms, ambayo yanasafiri masafa marefu zaidi ya kilomita 300.
Kwanini Magharibi haikutoa ruhusa?

Chanzo cha picha, EPA
Washington ina wasiwasi kwamba kuiruhusu Ukraine kulenga shabaha ndani ya Urusi kwa makombora yaliyotolewa na nchi za Magharibi kunaweza kumfanya rais Vladimir Putin kulipiza kisasi.
Hofu ya Ikulu ya White House ni kwamba watu wenye msimamo mikali huko Kremlin wanaweza kusisitiza kulipiza kisasi kwa kushambulia vituo vya kusafirishia makombora kwenda Ukraine, kama vile kambi ya anga nchini Poland.
Iwapo hilo litatokea, Kifungu cha 5 cha Nato kinaweza kutumiwa, kumaanisha muungano huo utakuwa vitani na Urusi.
Tangu uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine tarehe 24 Februari 2022, lengo la Ikulu ya White House limekuwa kuipa Kyiv uungaji mkono kadiri inavyowezekana bila kuingia kwenye mzozo wa moja kwa moja na Moscow, jambo ambalo linahatarisha vita vya nyuklia.
Lakini baadhi ya wachambuzi wanasema; Kyiv imekuwa ikiomba kutumia makombora ya masafa marefu ya Magharibi kushambulia Urusi kwa muda mrefu sasa, na hivyo Moscow tayari imechukua tahadhari ikiwa vizuizi vitaondolewa.
Imehamisha ndege, makombora na baadhi ya miundombinu mbali na mpaka wake na Ukraine na mbali zaidi ambapo haviwezi kufikiwa na kombora la Storm Shadow.
Hata hivyo Justin Crump wa Sibylline anasema, ulinzi wa anga wa Urusi umebadilika ili kukabiliana na tishio la Storm Shadow ndani ya Ukraine, lakini itakuwa ngumu kuzuia kombora hilo ndani ya Urusi kutokana na ukubwa wa nchi hiyo.
"Kuruhusu mashambulizi ndani ya Urusi kutafanya vifaa vya kijeshi, vituo vya kamandi na udhibiti, na ulinzi wa anga kutofanya kazi vizuri, na ikiwa Urusi itazidi kurudi nyuma kutoka katika mipaka ya Ukraine ili kuepusha kushambuliwa na kombora, itapata hasara ya muda na kifedha kushambulia mstari wa mbele."
Matthew Savill, mkurugenzi wa sayansi ya kijeshi wa shirika la Rusi, anaamini kuondoa vikwazo kutatoa manufaa mawili makubwa kwa Ukraine.
Kwanza, inaweza kutumia mfumo wa makombora ya masafa marefu ya Atacms.
Pili, italeta mkanganyiko kwa Urusi kuhusu mahali pa kuweka ulinzi wao wa anga, jambo ambalo anasema linaweza kurahisisha ndege zisizo na rubani za Ukraine kushambulia.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












