Raia wa Syria wanaorejea nyumbani wakabiliwa na tishio la mabomu yaliotegwa ardhini

Ayghad hakuwahi kufikiria kuwa ndoto yake ya kurudi kwenye shamba lake inaweza kugeuka kuwa mbaya.
Anapambana na machozi yake anapotuonyesha picha ya marehemu babake, akitabasamu na kuzungukwa na miti mingi ya mizeituni katika ardhi yao katika jimbo la Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria.
Picha hiyo ilipigwa miaka mitano iliyopita, miezi michache kabla ya vikosi vinavyohusishwa na serikali ya zamani kuchukua kijiji chao, karibu na mji wa Saraqeb.
Mji huo ulikuwa ngome ya kimkakati ya makundi ya upinzani ya Syria kwa miaka kadhaa, kabla ya vikosi vinavyoshirikiana na serikali iliyoanguka ya Bashar al-Assad kuanzisha mashambulizi dhidi ya waasi katika jimbo la Idlib mwishoni mwa 2019.
Mamia ya maelfu ya wakazi walikimbia majumbani mwao , huku wanajeshi wa Assad wakiteka ngome zingine kadhaa za waasi kaskazini magharibi mwaka 2020.
Ayghad na baba yake walikuwa miongoni mwa wale waliohamishwa.
"Ilitubidi kuondoka kwa sababu ya mapigano na mashambulizi ya anga," Ayghad anasema, huku machozi yakimlenga machoni. "Baba yangu alikuwa akikataa kuondoka. Alitaka kufia katika ardhi yake."

Baba na mwana walitamani kurudi tangu wakati huo. Na wakati vikosi vya upinzani vilipodhibiti tena kijiji chao mwezi Novemba 2024, ndoto yao ilikuwa karibu kutimia. Lakini maafa yalitokea hivi karibuni.
"Tulienda katika ardhi yetu kuvuna mizeituni," Ayghad anaelezea. "Tulienda kwa magari mawili tofauti. Baba yangu alichukua njia tofauti kurudi nyumbani kwetu katika jiji la Idlib. Nilimwonya dhidi ya hatua hiyo, lakini alisisitiza. Gari lake lilikanyaga bomu la ardhini na kulipuka."
Babake Ayghad alikufa papo hapo kwenye eneo la tukio. Sio tu kwamba alimpoteza baba yake siku hiyo, lakini pia alipoteza chanzo kikuu cha mapato ya familia yake. Mashamba yao, yaliyoenea katika mita za mraba 100,000, yalijaa miti ya mizeituni yenye umri wa miaka 50. Sasa eneo hilo lote limetejwa kuwa hatari kutokana na mabomu ya ardhini.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Takriban watu 144, wakiwemo watoto 27, wameuawa na mabomu yaliyotegwa ardhini na mabaki ya vita ambayo hayakulipuka tangu utawala wa Bashar al-Assad ulipoanguka mapema mwezi Desemba, kulingana na Halo Trust, shirika la kimataifa linalojihusisha na kutengua mabomu na vifaa vingine vya vilipuzi.
Jeshi la Ulinzi la Raia la Syria - linalojulikana kama White Helmets - liliambia BBC kwamba wengi wa waliouawa walikuwa wakulima na wamiliki wa ardhi ambao walikuwa wakijaribu kurejea katika ardhi yao baada ya utawala wa Assad kuporomoka.
Mabaki ya vita ambayo hayajalipuka ni tishio kubwa kwa maisha nchini Syria. Silaha hizo huwa zimeorodheshwa katika makundi mawili. La kwanza ni vifaa visivyolipuka (UXOs) kama vile mabomu ya kutapakaa.
Hassan Talfah, ambaye anaongoza timu ya Helmeti Nyeupe inayoondoa vilipuzi vya UXO kaskazini-magharibi mwa Syria, anaelezea kuwa vifaa hivi vina changamoto ndogo kuondolewa kwa sababu kwa kawaida vinaonekana juu ya ardhi.
The White Helmets wanasema kwamba, kati ya tarehe 27 Novemba na 3 Januari, walisafisha baadhi ya UXO 822 kaskazini-magharibi mwa Syria.
Changamoto kubwa zaidi, Bw Talfah anasema, iko katika aina ya pili ya silaha - mabomu ya kutegwa ardhini. Anaelezea kuwa vikosi vya serikali ya zamani vilitega mamia kwa maelfu ya silaha hizo katika maeneo mbalimbali nchini Syria - hasa katika mashamba.

Vifo vingi vilivyorekodiwa tangu utawala wa Assad uanguke vilitokea kwenye mstari wa mbele wa vita, kulingana na White Helmets. Wengi wa waliouawa walikuwa wanaume.
Bwana Talfah alitupeleka kwenye mashamba makubwa mawili yaliyokuwa na mabomu yaliotegwa ardhini. Gari letu lilimfuata kwenye barabara ndefu, nyembamba na yenye kupindapinda. Ndiyo njia pekee salama ya kufika mashambani.
Kando ya barabara, watoto walionekana wakikimbia kuzunguka eneo hilo. Hassan anatuambia wanatoka katika familia ambazo zimerejea hivi karibuni. Lakini hatari za mabomu yaliotegwa ardhini inawazunguka.
Tunaposhuka kwenye gari, anaashiria kizuizi kwa mbali.
"Hii ilikuwa hatua ya mwisho kutenganisha maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa vikosi vya serikali kutoka kwa yale yanayoshikiliwa na vikundi vya upinzani" katika jimbo la Idlib, anatuambia.
Anaongeza kuwa vikosi vya Assad vilitega maelfu ya mabomu katika mashamba nje ya kizuizi, ili kuzuia vikosi vya waasi kusonga mbele.
Mashamba karibu na mahali tunaposimama hapo zamani yalikuwa mashamba muhimu sana. Leo, yote ni tasa, na hakuna kijani kibichi kinachoonekana isipokuwa vilele vya kijani vya mabomu ya ardhini ambavyo tunaweza kuona kwa kutumia darubini.
Bila kuwa na utaalamu wa kuondoa mabomu ya ardhini, kile ambacho Jeshi la White helmet linaweza kufanya ni kuziba maeneo haya, na kuweka alama kwenye mipaka yao kuwaonya watu wasikaribie
Pia wanachora ujumbe wa onyo kwa kutumia rangi kwenye vizuizi vya uchafu na nyumba karibu na kingo za shamba. "Hatari - mabomu ya ardhini mbele," zinasoma.
Wanaongoza kampeni za kuongeza ufahamu miongoni mwa wenyeji kuhusu hatari ya kuingia katika ardhi zilizotegwa mabomu.
Tukiwa njiani kurudi, tunakutana na mkulima mmoja mwenye umri wa miaka 30 ambaye amerejea hivi majuzi. Anatuambia kwamba baadhi ya ardhi ni ya familia yake.
"Hatukuweza kutambua lolote kati ya hayo," Mohammed anasema. "Tulikuwa tunapanda ngano, shayiri, bizari na pamba. Sasa hatuwezi kufanya lolote. Na mradi hatuwezi kulima mashamba haya, tutakuwa katika hali mbaya ya kiuchumi kila wakati," anaongeza, akionekana kuchanganyikiwa.

The White Helmets wanasema wametambua na kuzingira maeneo ya mabomu 117 yaliotegwa ardhini katika muda wa mwezi mmoja tu.
Sio wao pekee wanaofanya kazi ya kusafisha mabomu na UXO, lakini inaonekana kuwa kuna ushirikiano mdogo kati ya juhudi za mashirika mbalimbali.
Hakuna takwimu sahihi za maeneo yaliyochafuliwa na UXO au mabomu ya ardhini. Lakini mashirika ya kimataifa, kama vile Halo Trust, yamechora ramani za takwimu hizo.
Meneja wa programu ya Halo Syria Damian O'Brien anasema kuwa uchunguzi wa kina unahitaji kufanywa ili nchi kuelewa ukubwa wa uchafuzi. Anakadiria kuwa karibu vilipuzi milioni vitahitajika kuharibiwa ili kulinda maisha ya raia nchini Syria.
"Nafasi yoyote ya jeshi la Syria kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na baadhi ya mabomu ya ardhini kuwekwa karibu nayo kama mbinu ya kujihami," Bw O'Brien anasema.
"Katika maeneo kama Homs na Hama, kuna vitongoji vizima ambavyo vimekaribia kuharibiwa kabisa. Mtu yeyote anayeingia kwenye majengo hayo kutathmini, kwa kubomoa au kujenga upya, anapaswa kufahamu kwamba kunaweza kuwa na vitu ambavyo havijalipuka ndani yake. iwe ni risasi, mabomu ya kutapakaa au makombora."

Jeshi la The White Helmet lilikutana na hazina ambayo inaweza kusaidia juhudi za kuondoa migodi katika ofisi yao katika jiji la Idlib, Bw Talfah anatuonyesha rundo la ramani na hati, zilizoachwa nyuma na vikosi vya serikali.
Zinaonyesha maeneo, idadi na aina za migodi iliyopandwa katika maeneo tofauti kaskazini magharibi mwa Syria.
"Tutakabidhi hati hizi kwa mashirika ambayo yatashughulikia mabomu ya ardhini moja kwa moja," Bw Talfah anasema.
Lakini utaalamu wa ndani unaopatikana kwa sasa nchini Syria hauonekani kuwa wa kutosha kukabiliana na hatari kubwa ambayo silaha zisizolipuka huleta kwa maisha ya raia.
Bw O'Brien anasisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa inahitaji kufanya kazi pamoja na serikali mpya nchini Syria ili kuboresha utaalamu nchini humo.
"Tunachohitaji kutoka kwa wafadhili ni ufadhili, ili tuweze kupanua uwezo wetu, ambao inamaanisha kuwajiri watu wengi, kununua mashine nyingi na kufanya kazi katika eneo kubwa zaidi," anasema.
Kuhusu Bw Talfah, kuondoa UXO na kuongeza ufahamu kuhusu hatari yao imekuwa kazi ya kibinafsi. Miaka kumi iliyopita, alipoteza mguu wake mwenyewe wakati akiondoa bomu la kutapakaa.
Anasema kwamba jeraha lake, na matukio yote ya kuvunja moyo ambayo ameshuhudia miongoni mwa watoto na raia walioathiriwa na UXOs, yamechochea tu kuendelea kwake kufanya kazi.
"Sitaki kamwe raia au mwenzangu katika timu kupitia kile nilichonacho," anasema.
"Siwezi kuelezea hisia ninazopata ninapoondoa hatari inayotishia maisha ya raia."
Lakini hadi pale juhudi za kimataifa na za ndani zitakaporatibiwa kupunguza hatari ya mabomu ya ardhini, maisha ya raia wengi hasa watoto yanasalia hatarini.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












