Mfahamu Asma, mke wa Rais aliyepinduliwa Bashar al Assad

Asma al Assad aliwahi kuelezewa kuwa mwanamke "mzuri sana" na mke wa rais "mwenye mvuto wa asili.
Hizi zilikuwa baadhi ya sifa zilizotumiwa na majarida mbalimbali katika ripoti zao ikiwemo Vogue katika ripoti ya mwaka 2011 kuhusu mke wa rais wa Syria wakati huo, ambayo baadaye iliondolewa na jarida hilo kufuatia ukandamizaji wa kikatili wa serikali ya mumewe dhidi ya waandamanaji wanaodai demokrasia zaidi na uhuru.
Mnamo mwaka wa 2016, katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Urusi Rossiya 24, Asma al-Assad alisema alikuwa amekataa maombi ya hifadhi ili kuondoka katika taifa hilo lililokumbwa na vita vilivyochochewa na ukandamizaji wa maandamano.
Mnamo mwaka 2016 akihojiwa na Televisheni ya Urusi Channel Rssiya 24, Asma Assad alisema alikataa hifadhi alizopewa bure ili kuondoka katika taifa hilo lililogubikwa na maandamano na ukandamizaji.
"Nimekuwa hapa tangu mwanzo na sijawahi kufikiria kwenda mahali pengine popote," alisema wakati huo.
Hata hivyo, hali ilibadilika mwishoni mwa juma hili baada ya kuwasili kwa vikosi vya waasi huko Damascus, jambo ambalo lilipelekea kuanguka kwa utawala wa mumewe, Bashar al Assad, ambaye alitawala nchi hiyo ya Kiarabu kwa zaidi ya miongo miwili kwa mkono wa chuma.
Asma al-Assad aliondoka Syria na mumewe na watoto watatu kuelekea Urusi, ambako walipata hifadhi kwa "misingi ya kibinadamu," vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vilithibitisha Jumapili.
Katika kumtetea mumewe
Wakati wafuasi wa mume wake wakimtaja kama "yasmine wa Damascus," baadhi ya maadui zake wamempa jina la utani "bibi kifo au mke wa muuaji."
Asma Al Assad ameelezea mara kwa mara utiiifu kwa mumewe na serikali yake.
Mnamo Aprili 2017, Asma alichapisha kwenye mtandao wa kijamii taarifa kutoka kwa rais wa Syria akikosoa shambulio la kombora la Marekani kwenye kambi ya anga katika taifa hilo la Kiarabu.
Iliidhinishwa na Rais wa wakati huo Donald Trump kujibu shambulio la kemikali linalodaiwa kutekelezwa na jeshi la Syria mnamo Aprili 4, 2017 huko Khan Sheikhun, mji unaodhibitiwa na waasi.
Serikali ya Assad ilikanusha vikali kutumia silaha za kemikali katika operesheni zake kaskazini mwa Idlib, ikitaja mlipuko katika kiwanda cha silaha za kemikali cha al-Qaeda kama sababu ya mlipuko.
Zaidi ya watu 80 walikufa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Miaka ya awali, Agosti 2013, mamia ya watu waliuawa katika shambulio la silaha za kemikali katika eneo linalodhibitiwa na waasi karibu na Damascus.
Mataifa ya Magharibi na upinzani yalilaumu utawala wa Assad, ingawa serikali ilikanusha kuhusika. Hatimaye, chini ya shinikizo la kimataifa, ilikubali kuteketeza silaha zake za kemikali.
Lakini hilo halikumaliza orodha ndefu ya ukatili katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Kulikuwa na mashambulizi zaidi ya kemikali na tume za Umoja wa Mataifa zilishutumu pande zote zinazopigana kwa uhalifu wa kivita.
Katika majibu yake kwa mgomo ulioagizwa na Ikulu ya Marekani mwaka 2017, Asma al Assad alibainisha:
"Kile ambacho Marekani imefanya ni kitendo cha kutowajibika ambacho kinaonyesha tu kutoona mbali, upeo mdogo wa mambo, upofu wa kisiasa na kijeshi kwa ukweli na harakati za kijinga za kampeni ya uwongo ya uwongo," ulisema ujumbe huo uliowekwa kwenye Instagram na Facebook.
Kutokana na hali hiyo, chama cha Liberal Democrats cha Uingereza ndipo kilimtaka Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, Amber Rudd, kumvua uraia wa Uingereza Asma al-Assad, mzaliwa wa Uingereza.
Katika ksehemu ya jarida hilolililochochapishwa katika The Guardian, Mbunge wa Conservative Nadhim Zahawi aliandika:
"Asma al Assad hastahili tena uraia wa Uingereza. Sio wakati aliotumia mitandao ya kijamii kumtetea mumewe, kukana matumizi ya silaha za kemikali na kushambulia nchi za Magharibi, huku akionyesha maisha katika nchi iliyokumbwa na vita kuwa ya kawaida
''Sijawahi kufikiria kuondoka"
Hii haikuwa mara ya kwanza kwa Asma al Assad kusababisha mzozo.
Mnamo Oktoba 2016, aliamua kuzungumza na ulimwengu katika mahojiano ambayo aliweka wazi kwamba hataondoka Syria na angebaki upande wa mumewe.
"Nimekuwa hapa tangu mwanzo na sijawahi kufikiria kwenda mahali pengine popote," Asma al Assad alisema katika mahojiano ya 2016 na kituo cha televisheni cha Urusi Rossiya 24.
Aliongeza kuwa amekataa fursa za kuondoka katika taifa hilo lililokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Chanzo cha picha, Aleppo Media Center
"Ndiyo, nilipewa fursa ya kuondoka Syria, au tuseme kutoroka Syria. Hatua hiyo ilijumuisha hakikisho la usalama na ulinzi kwa watoto wangu na hata usalama wa kifedha," alisema.
Alisema waliotoa fursa hiyo walikuwa wakijaribu kuhujumu urais wa mumewe.
"Haihitaji akili kujua watu hawa wanafuata nini. Hili halikuwa kamwe kuhusu ustawi wangu au ustawi wa watoto wangu. Hili lilikuwa jaribio la makusudi la kuharibu imani ya watu kwa rais wao," alisema.
Alipoulizwa kwa nini alipendelea kubaki Damascus, alisema: "Si suala la upendeleo. Niko pamoja naye kwa sababu imani yangu inanielekeza hivyo."
Muhudumu wa zamani katika Benki nchini Uingereza
Ilikuwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minane kwa Asma al-Assad kufanya mahojiano ya televisheni.
Mwanzoni mwa vita mwaka 2011, mama huyo wa watoto watatu wa Rais Assad alikuwa aligonga vichwa vya habari katika mfululizo wa kuonekana kwenye vyombo vya habari akimuunga mkono mumewe, ambaye serikali yake tayari ilikuwa inashutumiwa kuua maelfu ya waandamanaji na wapinzani wakati wa mzozo huo.
Miaka sita baadaye, alikuwepo hasa kwenye mitandao ya kijamii, ambapo alihifadhi kurasa zilizojaa picha za mikutano yake na watoto yatima na ziara zake katika kliniki na hospitali.

Chanzo cha picha, LOUAI BESHARA/AFP via Getty Images
Yalikuwa ni mazingira tofauti sana na Acton, magharibi mwa London, ambako alizaliwa na kukulia kama Asma Akhras, kwenye familia aliyotoka yenye asili ya Syria.
Baba yake, Fawaz Akhras, alikuwa daktari wa magonjwa ya moyo na alifanya mazoezi ya udaktari katika kliniki ya kibinafsi.
Mama yake, Sahar, alikuwa mwanadiplomasia na alifanya kazi kama katibu wa kwanza katika ubalozi wa Syria huko London.
Asma, ambaye ni Mwislamu wa Kisunni, alisoma shule ya kibinafsi ya wasichana, Chuo cha Queen, kisha akasomea sayansi ya kompyuta katika Chuo cha kifahari cha King's College, alihitimu mwaka wa 1996, kabla ya kuanza kazi ya benki katika Jiji la London.
Huko alikutana na mumewe. Bashar alikuwa amehitimu udaktari huko Damascus na alikuwa katika mji mkuu wa Uingereza akisomea taaluma ya ophthalmology.
Sura mpya ya Syria
Wakati Rais Hafez al Assad, ambaye alitawala nchi tangu 1971, alipofariki Juni 2000, mwanawe Bashar alichukua urais.
Mnamo Novemba mwaka huo, Asma alisafiri kwenda Syria kufunga ndoa na Bashar katika harusi ambayo iliwashangaza wengi kwani hapakuwa na taarifa zozote kuhusu uhusiano wao au uchumba wao.
Wengi walifikiri kwamba ndoa na mwanamke huyo kutoka Uingereza - Muislamu wa Kisunni - ingeweza kuwa ishara ya maendeleo na ushirikiano na ingehimiza mageuzi katika nchi yenye Wasunni wengi ambayo ilitawaliwa na familia ya Al Assad.

Chanzo cha picha, LOUAI BESHARA/AFP via Getty Images
Lakini kama mwandishi wa zamani wa BBC Mashariki ya Kati Kim Ghattas anavyoeleza, kwa miaka mingi ilidhihirika kuwa Bashar alikuwa kama babake, "kiongozi mgumu ambaye alijifanya kuwa mwanamageuzi".
"Katika majaribio yake ya kuonyesha sura ya kiuongozi wa Magharibi, Assad alisaidiwa na Asma, mke wake mrembo wa Syria aliyelelewa London," Ghattas alielezea.
"Chanzo cha familia ambacho hakikutajwa jina kilieleza kuwa Assad alioana na Asma akijua kwamba angekuwa hatua nzuri sana katika kuonyesha sura ya kisasa nchini Syria."
Assads hata walitafuta usaidizi wa kampuni ya mawasiliano ya umma ya Uingereza, Bell Pottinger, ili kukuza taswira ya Asma - na ya Syria - kwenye jukwaa la kimataifa.
Hata hivyo, anasema Kim Ghattas, "Mtazamo wa Asma katika nafasi yake kama mke wa rais ulisababisha mvutano ndani ya familia ya Assad, hasa na dada wa rais, Bourhra, na mama, Anisseh, ambaye hakujali sana mahusiano ya umma."
Waridi jangwani
Juhudi hizo zilileta mafanikio kadhaa.
Mnamo Februari 2011, jarida la Vogue lilichapisha wasifu wa maneno 3,200 kuhusu mke wa rais wa Syria uitwao "A Rose in the Desert."ikimaanisha uaridi jangwani.
Ndani yake lilimtaja Asma kama "mrembo" na kudai kwamba Syria ilikuwa "nchi salama zaidi katika Mashariki ya Kati."

Chanzo cha picha, LOUAI BESHARA/AFP via Getty Images
Lakini mwezi mmoja tu baadaye, polisi walifanya ukatili dhidi ya maandamano ya amani, ya kuunga mkono demokrasia katika mji wa Deraa, na kusababisha mzozo uliogharimu maisha ya karibu watu nusu milioni na mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao.
Mwaka huo, jumuiya ya kimataifa ilianza kumtazama mke wa rais wa Syria kwa mtazamo tofauti.
Muda mfupi baada ya wasifu huo kuonekana kwenye Vogue, The New York Times iliripoti kwamba makala hiyo ilikuwa sehemu ya kampeni ya utawala wa Assad, ambayo ilijumuisha malipo ya $5,000 kwa mwezi kwa kampuni ya matangazo ya Marekani ambayo ilikuwa ikifanya kazi kama mpatanishi kati ya Vogue na Asma al. Assad.
Makala hayo yaliondolewa kwenye tovuti ya Vogue muda mfupi baadaye, na mhariri mkuu wa chapisho hilo, Anna Wintour, alitoa taarifa ya kulaani utawala wa Assad.
Ugonjwa
Akitoa maoni yake kwa mara ya kwanza juu ya ghasia mnamo Februari 2012, mke huyo wa rais alisimama kidete na mumewe.
"Rais ni rais wa Syria, si wa kikundi cha Wasyria, na mke wa rais anamuunga mkono katika jukumu hilo," ilisema taarifa kutoka ofisi yake kwa gazeti la Uingereza la The Times.
Mambo yalibadilika haraka kutokana na vita. Mnamo 2012, Umoja wa Ulaya ulimwekea vikwazo Asma, na kumpiga marufuku kusafiri na kufungia mali zake.
Lakini Asma alisisitiza juu ya kutoa taarifa zinazomuunga mkono mumewe na kuhakikisha kwamba amejitolea "kuwafariji" "wahaathiriwa wa ghasia."

Chanzo cha picha, LOUAI BESHARA/AFP via Getty Images
Katika mahojiano yake na televisheni ya Urusi mwaka 2016, Asma alisema alikuwa akitumia nafasi yake "kuandaa msaada kwa waliokimbia makazi na waliojeruhiwa, kwa askari wa Syria na familia za 'mashahidi' ambao wamekufa katika vita."
Mnamo mwaka wa 2018, viongozi wa Syria waliripoti kuwa Asma al Assad alikuwa akipokea matibabu ya saratani ya matiti.
Katika mahojiano na runinga ya serikali ya Syria mnamo 2019, alisema alikuwa amepona kutokana na kugunduliwa mapema.
Mnamo Mei 2024, rais wa Syria aliripoti kwamba alikuwa amepatikana na saratani ya damu.
"Taarifa hiyo ilisema Asma, mwenye umri wa miaka 48, angepitia utaratibu maalum wa matibabu ambao ungemtaka ajitenge, na kwa sababu hiyo angejitenga na shughuli za umma," shirika la habari la Reuters liliripoti.
Sasa yuko Moscow na mumewe na watoto watatu.
*Makala haya yalichapishwa awali tarehe 20 Oktoba 2016, yalihuishwa mwaka 2017 kufuatia wito wa kumvua Asma al Assad uraia wa Uingereza na kuanguka kwa utawala wa Bashar al Assad.
Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Seif Abdalla












