Miungano inayobadilika kila mara ambayo ilichochea sarakasi ya kuondolewa madarakani kwa Naibu Rais Kenya

Muda wa kusoma: Dakika 6

Na Anne Soy

Naibu mhariri wa BBC Afrika, Nairobi

th

Chanzo cha picha, AFP

Kumpoteza naibu wako miaka miwili tu baada ya kuchaguliwa kwa tikiti ya pamoja kunaweza kuonekana kuwa pigo kubwa kwa rais, lakini sio wakati huu nchini Kenya.

Mara tu Rigathi Gachagua alipoonekana kumhujumu William Ruto, alichukua hatua ya haraka kumwondoa mshirika wake aliyeshikilia nafasi ya pili uongozini.

Alikuwa amejionea jinsi tofauti kati ya viongozi wawili wa juu nchini Kenya zinaweza kulemaza serikali baada ya kutofautiana na bosi wake wa zamani Uhuru Kenyatta.

Mabadiliko ya kisiasa ambayo hayajawahi kushuhudiwa nchini Kenya, yakionyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni, huenda yalionekana kuwa ya mpangilio kwa mtazamaji wa nje.

Mchakato wa kumfungulia mashitaka umekuwa ukifuatiliwa na watu wengi kwa mvuto huku mabunge mawili, mahakama na hatimaye afisi kuu za uongozi zitekeleza majukumu yao kwa kufuata utaratibu uliowekwa wa kisheria.

Lakini kwa Wakenya wengi, imekuwa ni hali ya juu iliyoibua maoni makali kutoka kote nchini.

Hapo awali kulikuwa na hali ya usaliti na kutamaushwa hasa kutoka eneo analotoka Gachagua katika Mlima Kenya, lakini kufikia Ijumaa asubuhi hali hii ilibadilika na hali kukubali matokeo kwani mtu aliyechaguliwa kuchukua nafasi yake, Kithure Kindiki, anatoka eneo hilo pia.

Unaweza Pia Kusoma
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Eneo la Mlima Kenya lilichangia pakubwa katika ushindi wa Ruto dhidi ya Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga katika uchaguzi wa urais wenye ushindani mkali mwaka wa 2022.

Odinga alikuwa akigombea na aliyekuwa Waziri wa Sheria mwenye nguvu, Martha Karua, anayetoka eneo hilo, na kuungwa mkono na Kenyatta, rais aliyekuwa anamaliza muda wake ambaye pia anatokea Mlima Kenya .

Lakini katika kipute hicho, Ruto, akiwa na Gachagua, alishinda kura nyingi za eneo hilo la nchi.

Kwa muktadha, siasa za Kenya kwa kiasi kikubwa zinaendeshwa na kanda - wengine wanaweza kusema kambi za kikabila na Mlima Kenya unabeba takriban robo ya kura za nchi.

Haishangazi kwamba marais watatu kati ya watano tangu uhuru - Jomo Kenyatta, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta - walitoka eneo hilo. Hii ndiyo sababu wagombea wawili wa juu katika uchaguzi uliopita wa urais - Ruto na Odinga - walichagua wagombea wenza kutoka huko, huku wote wawili wakitoka maeneo mengine ya nchi .

Kulihamakisha eneo hilo kwa hivyo kunaweza kuwa kujiua kisiasa kwa rais katika muhula wake wa kwanza.

Lakini majaribio ya Gachagua ya kutaka kuwa na ushawishi wa kisiasa wa eneo hilo ndio sumu iliyoua taaluma yake ya siasa .

Alishutumiwa na bunge kwa, miongoni mwa mambo mengine, kuendeleza siasa za mgawanyiko wa kikabila wakati alitarajiwa kuwa kielelezo cha muungano wa kitaifa.

Alibuni msemo wa “usiguze mlima”, akijifanya mlinzi mkali wa eneo la Mlima Kenya na lango kuu kuelekea huko.

Kanda za video zilichezwa wakati wa kesi ya kuondolewa kwake madarakani ambazo ilimwonyesha akipendekeza kuwa serikali ingeyapa kipaumbele maeneo ambayo yalikuwa yamepigia kura kuiunga mkono serikali ya sasa, ingawa Ruto pia alikuwa ametoa kauli sawa na hiyo.

Wabunge kutoka maeneo mengine walishutumu vikali hisia kama hizo.

Ruto alikaa kimya huku naibu wake akichukuliwa hatua ya kuondolewa madarakani ,licha ya maombi ya rais kuingilia kati, ikiwa ni pamoja na Gachagua hata kuomba msamaha "ikiwa [Gachagua] alimdhulumu".

Kulikuwa na mfano wa hivi majuzi wa machafuko yaliyotokea wakati rais na naibu wake walipokosana.

Wakati wa muhula wa pili wa Kenyatta, Ruto, aliyekuwa naibu wa rais wakati huo, alilalamika kutengwa na kunyanyaswa.

Taswira ya kuwa mwathiriwa ilimfanya ahurumiwe na wengi, ikiwa ni pamoja na katika ngome ya kisiasa wa rais wa wakati huo.

Lakini alihitaji zaidi ya huruma ili kushinda uchaguzi wa urais wa 2022 - ilimbidi amchague mgombea mwenza wake kutoka Mlima Kenya.

Huku wengi wakitarajia rais angemchagua mshirika wake wa muda mrefu, profesa wa sheria Kithure Kindiki, Ruto aliwashangaza wengi alipoamua kumteua aliyekuwa mbunge wa wakati huo Rigathi Gachagua.

Kindiki alikuwa tayari anajulikana sana nchini Kenya, akiwa amewahi kuwa naibu spika kabla ya kuondolewa wadhifa huo katika makabiliano ya Kenyatta dhidi ya washirika wa Ruto.

Wabunge wa chama cha Ruto walimpigia kura nyingi Kindiki, mara tatu walisema, alipotaka kuwahusisha katika mchakato wa kumchagua mgombea mwenza. Gachagua aliibuka wa pili lakini, mwishowe, alikuwa chaguo la Ruto.

Yeye kuteuliwa sasa katika nafasi hiyo, kwa hivyo, sio jambo la mshangao.

Kwamba anatoka "mlimani", ingawa kutoka kabila dogo, imesaidia kutuliza hisia za hasira na usaliti.

Wenyeji wengi waliozungumza kwenye televisheni wamekuwa wakitaka kukubaliwa kwa chaguo la rais ili kuepuka kugawanya eneo hilo.

Haya ndiyo yote yanayohusiana nayo - kusonga mbele na uchaguzi ujao ikiwa imesalia miaka mitatu tu.

Lakini bila shaka bado itapunguza uungwaji mkono wa rais katika Mlima Kenya.

v

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Raila Odinga alishindwa katika uchaguzi mgumu na William Ruto miaka miwili tu iliyopita lakini wawili hao sasa wameunda muungano.

Mafanikio ya mchakato huu pia yameegemea pakubwa ushirikiano mpya wa Ruto na adui yake mkubwa katika uchaguzi uliopita, Odinga, ambaye wabunge na maseneta wa chama chake walipiga kura kwa wingi kumuondoa Gachagua afisini.

Bunge pia lilimteua mshirika wa karibu wa Odinga, wakili mkuu James Orengo, kuongoza timu yake ya mawakili wakati wa kesi ya kumtimua Gachagua .

Kulikuwa na mshikamano wa maslahi hapa, bila shaka. Lakini inaweza kugeuka na kuwa sumu kwa Ruto.

Iwapo urafiki huo utadumu ni jambo lisilotabirika. Lakini ni sifa ya hali ya kisiasa ya Kenya inayobadilika kila mara.

Kwa sasa, Ruto amewateua wanachama wanne wakuu wa chama cha Odinga kwenye baraza la mawaziri na anamuunga mkono kwa nafasi yenye ushawishi ya mwenyekiti ajaye wa tume ya Umoja wa Afrika.

Wanaume hao wawili wana historia ndefu ya kisiasa pamoja kama washirika au wapinzani.

Katika uchaguzi wa urais wa 2002, Ruto alimuunga mkono Kenyatta huku Odinga akimuunga mkono Kibaki ambaye alishinda.

Miaka mitano baadaye, utiifu ulibadilika huku Ruto akiunga mkono Odinga na Kenyatta kumuunga mkono rais anayemaliza muda wake, Kibaki, katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali wa 2007 ambao ulisababisha ghasia nchini kote.

Ruto na Kenyatta baadaye walishtakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa madai ya kuhusika katika mapigano huku wakiunga mkono pande zinazopingana.

Lakini katika chaguzi mbili zilizofuata za 2013 na 2017, waligombea kwa tiketi ya pamoja na kumshinda Odinga.

Kesi dhidi yao katika ICC hatimaye zilitupiliwa mbali kwa kukosa ushahidi.

Ushirikiano wowote unawezekana katika siasa za Kenya, haijalishi ni jambo gani lisilowezekana katika macho ya mtu wa nje.

Viongozi wote wa kitaifa wanajaribu kuweka kambi zao za kikanda au kikabila zitumike kama chambo wakati wa kutafuta ushirikiano na mbinu ya kushinda uchaguzi wa kitaifa.

Ruto na Odinga kwa muda mrefu wamejitahidi kufikia hilo, baada ya kujiunga na siasa katika ujana wao.

Wote wawili wana wafuasi waaminifu - kama muungano wao wa hivi majuzi unavyoonyesha huku wafuasi wa Odinga wakibadilika na kumuunga kikamilifu mwanasiasa waliyempinga vikali takriban miaka miwili iliyopita.

Gachagua alitarajia kupata hadhi sawa, lakini azma yake kwa sasa imemchoma.

Anapinga kuondolewa kwake ofisini kortini na ikifaulu, bado inaweza kumpa maisha ya kisiasa. Ikiwa sivyo, sheria inamzuia kuwania wadhifa huo kwa takribani miaka 10.

Siasa za aina hii ni mchezo mrefu. Akiwa na umri wa miaka 59, Gachagua amechelewa kuingia kwenye uwanja wa kisiasa na hatma yake haijulikani.

Anaweza kusahaulika kisiasa au bado anaweza kurejea uwanjani - kama mpinzani wa Ruto au hata mshirika wake.

Licha ya kile kinachoonekana kama talaka chungu, huku rais akiendelea mbele na hali ya kawaida hakuna mtu nchini Kenya atakayeshangaa kumuona wakipeana mikono na kutabasamu kwenye televisheni ya taifa na naibu wake wa zamani aliyeachana naye.

Mandhari ya kisiasa ya Kenya kama tetemeko la ardhi - miamba inayoshikilia msingi inabadilika kila mara na chochote kinawezekana.

Unaweza Pia Kusoma

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah