Homa ya Mapafu: Ufahamu kwa kina ugonjwa huu uliomsumbua Papa Francis

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis ameifariki dunia Jumatatu ya Pasaka, Aprili 21, 2025, akiwa na umri wa miaka 88 katika makazi yake katika Casa Santa Marta, Vatican.
Kifo cha Papa kimekuja chini ya saa 24 baada ya kujitokeza kwenye Uwanja wa St Peter's Square mjini Vatican kwa ajili ya Jumapili ya Pasaka.
Kabla ya kifo chake Papa Francis aligundulika na homa ya mapafu katika mapafu yake yote mawili na hali yake bado ni "mbaya," kwa mujibu wa taarifa ya Vatican.
Kwa zaidi ya miezi miwili tangu Februari, 14, kiongozi huyo alikuwa amelazwa akisumbuliwa na maambukizi ya njia ya upumuaji na alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Gemelli, Rome.
Vatican ilisema kuwa uchunguzi wa CT scan kwenye mapafu ulibaini kuwa Papa Francis alikuwa na tatizo hilo (Nimonia ya pande mbili kwa lugha nyingine) katika hatua za awali, hali inayohitaji matibabu zaidi.
Katika taarifa kadhaa, Vatican ilieleza kuwa hali ya Papa Francis ilikuwa ikibadilika na kuwa "mbaya", huku vipimo vya damu vikionyesha kuwa ana tatizo dogo pia la figo.
Sasa katika makala hii, tutafafanua zaidi kuhusu ugonjwa huu uliomsumbua Papa.
Homa ya Mapafu au Pneumonia ni nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Homa ya mapafu au nimonia ni maambukizi yanayosababisha uvimbe kwenye mifuko ya hewa (alveoli) ndani ya mapafu. Mifuko hii ya hewa inaweza kujaa maji au usaha, na kusababisha dalili kama:
- Kukohoa huku ukitoa makohozi yenye ute au usaha
- Homa
- Kutetemeka na kuhisi baridi kali
- Maumivu ya mwili
- Kuchanganyikiwa
- Kupumua kwa shida
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Nimonia inaweza kusababishwa na viumbe vidogo kama bakteria, virusi au fangasi.
Viumbe hivi vinaweza kuenea kwa njia ya matone kutokana na kukohoa au kupiga chafya, au kwa kugusa uso wenye vijidudu kisha kugusa mdomo, pua, au macho.
Kwa Papa Francis alikuwa na tatizo hili ambalo ni "bilateral" ikimaanisha kwamba maambukizi yameathiri mapafu yote mawili, badala ya pafu moja tu.
Hata hivyo, watafiti wa Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Sydney, Australia wanaamini kuwa kuwa na homa ya mapafu katika mapafu yote mawili haina maana kwamba maambukizi ni mabaya zaidi kwa kila mgonjwa.
Mwaka 2021, kulikuwa na takribani visa milioni 344 vya watu wenye ugonjwa huu duniani, ambapo milioni 2.1 kati ya visa hivyo, vilisababisha vifo.
Kati ya vifo hivyo, 502,000 vilikuwa vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano, kwa mujibu wa Utafiti wa Kimataifa wa Mzigo wa Magonjwa (Global Burden of Disease Study).
Katika mwaka huohuo, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), maambukizi ya njia ya chini ya upumuaji yalikuwa sababu ya tano ya vifo duniani, baada ya magonjwa ya moyo, COVID-19, kiharusi, na ugonjwa sugu wa kupumua (COPD).
Jinsi ya kuugundua homa ya mapafu na watu walio hatarini zaidi

Chanzo cha picha, Getty Images
Daktari anaposhuku mgonjwa ana homa ya mapafu au nimonia, anaweza kuagiza kufanyika kwa vipimo vya damu ili kuthibitisha uwepo wa maambukizi na kujaribu kutambua chanzo chake, ingawa mara nyingine haiwezekani kubaini chanzo hasa.
Mionzi ya X-ray ya mapafu inapendekezwa ili kubaini eneo lililoathiriwa, pamoja na uchunguzi wa makohozi au sampuli kutoka puani ili kutambua aina ya vimelea vinavyosababisha maambukizi.
Kiwango cha oksijeni mwilini pia hupimwa kwa kutumia 'pulse oximetry', kwa kuwa nimonia inaweza kuathiri uwezo wa mapafu kuingiza oksijeni ya kutosha kwenye damu.
Nimonia inaweza kuwa hatari kwa yeyote, lakini wazee wa umri wa Papa Francis wako katika hatari zaidi.
Wataalamu wa afya wanabainisha kuwa umri ni miongoni mwa vihatarishi vikubwa vya kupata maambukizi makali, hasa kwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 65 na watoto chini ya miaka miwili.
Mbali na umri, vihatarishi vingine ni pamoja na:
- Uharibifu wa mapafu kutokana na maambukizi ya awali
- Magonjwa ya muda mrefu ya mapafu kama emphysema na COPD
- Uvutaji sigara
- Kinga ya mwili iliyo dhaifu
Kwa upande wa Papa Francis, mbali na umri wake mkubwa, historia yake ya maradhi ya kupumua ikumueka katika hatari zaidi.
Katika ujana wake, alipatwa na kitu kinachoitwa kitaalamu pleurisy, hali inayosababisha uvimbe kwenye utando wa mapafu (pleura).
Kutokana na ugonjwa huo, sehemu ya pafu lake iliondolewa kwa upasuaji, hali iliyomfanya kuwa katika hatari kubwa zaidi ya maambukizi ya njia ya upumuaji.
Papa alilazwa hospitalini mnamo Februari 14 kwa matibabu ya 'bronchitis', ambao ni uvimbe wa njia za hewa (bronchi) zinazopeleka hewa kwenye mapafu. Uchunguzi zaidi ukaonyesha kuwa alikuwa pia na nimonia iliyoathiri mapafu yote mawili.
Alianza kuhisi dalili siku chache kabla ya kulazwa na alilazimika kuwaachia maafisa wake wasome hotuba alizoziandaa katika matukio ya hivi karibuni.
Matibabu ya Homa ya Mapafu

Chanzo cha picha, Getty Images
Ikiwa nimonia inasababishwa na bakteria, hutibiwa kwa antibiotiki.
Ikiwa imesababishwa na virusi, hutibiwa kwa dawa za antiviral, ingawa mara nyingi hazina ufanisi mkubwa.
Ikiwa haijulikani ni aina gani ya bakteria inayosababisha ugonjwa, mgonjwa anaweza kupewa antibiotiki za wigo mpana na zenye kukabiliana na aina mbalimbali ya vidudu hivyo.
Kwa wagonjwa wanaolazwa hospitalini, matibabu hujumuisha:
- Dawa za sindano (infusion)
- Tiba ya oksijeni
- Mazoezi ya kifua (physiotherapy) kusaidia kutoa majimaji yaliyokusanyika kwenye mapafu, hasa kwa wagonjwa wasio na uwezo wa kujisogeza
Vatican hapo awali ilitangaza kuwa maambukizi ya awali ya Papa Francis ni "polymicrobial", ikimaanisha kuwa yamesababishwa na mchanganyiko wa vijidudu tofauti.
Kutokana na hali hiyo, matibabu yake yanahitaji umakini zaidi, na anapewa antibiotiki pamoja na 'corticosteroids, ambazo ni dawa za kupunguza uvimbe.
Imetafsiriwa na Yusuph Mazimu na kuhaririwa na Ambia Hirsi












