Je, virutubisho hivi ndio siri ya ngozi nyororo?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Christine Ro
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Virutubisho vya collagen vinaweza kuifanya ngozi yako kuwa nyororo - lakini ushahidi wa hilo bado ni mdogo, kwa sababu ya kukosekana tafiti za kutosha.
Collagen inapigiwa upatu sana. Protini hii, ambayo ni muhimu kwa ngozi na viungo, inaelezwa kama tiba ya muujiza kwa kila kitu kutoka mikunjo ya uso hadi kukosa usingizi.
Uzalishaji wa collagen mwilini, kawaida hupungua kadiri unavyozeeka - iwe unailinda ngozi yako dhidi ya jua au la. Na collagen ndio imekuwa biashara kubwa.
Bryan Johnson, ni mjasiriamali wa teknolojia ambaye ametumia virutubisho hivyo. Anasema yeye hutumia gramu 25 za collagen kila siku.
Lakini collagen bado haieleweki vizuri. Ingawa kuna ushahidi kwamba ina faida za kiafya, lakini utafiti wa hilo bado ni mdogo. Je, ushahidi wa kisayansi unaendana na madai ya wauzaji wake?
Hakuna utafiti wa kutosha

Chanzo cha picha, Getty Images
Protini ya "collagen inapatikana katika tishu za wanyama," anabainisha Andrea Soares, mtaalamu wa lishe aliyesajiliwa huko Georgia, Marekani, ambaye ni sehemu ya mtandao wa Top Nutrition Coaching network, kampuni ambayo husaidia kuunganisha watu na wataalamu wa lishe katika eneo lao.
Bidhaa za Collagen hutokana na wanyama mbalimbali; ng'ombe, nguruwe, kuku na samaki. Na virutubisho hivyo pia hutengenezwa kutokana na mimea.
Mbali na aina mbalimbali za vyanzo vya collagen, virutubisho hivi vimeundwa katika aina tofauti, kutoka vinywaji, unga na vidonge.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa ujumla, madai mengi yanayotolewa kuhusu virutibisho hivi, hayaja chunguzwa ipaswavyo. Katika Mataifa ya Umoja wa Ulaya, "virutubisho vya collagen bado havijaidhinishwa rasmi kwa matumizi," anaelezea Leng Heng, afisa wa lishe ya binadamu katika Bodi ya Usalama wa Chakula ya Ulaya (EFSA).
EFSA ni bodo ya Umoja wa Ulaya, ambayo hutathmini hatari zinazohusiana na vyakula. Walipoangalia collagen, walihitimisha kuwa madai yaliyowasilishwa kuhusu virutubisho hivyo hadi sasa hayana ushahidi wa kutosha.
"Kuna ukosefu wa tafiti kwa wanadamu, watengenezaji wanategemea ushahidi kutoka kwa utafiti wa wanyama na maabara, ambao hauwezi kutabiri athari kwa wanadamu," anasema Heng.
Anasema madai kama vile collagen husaidia kudumisha unyororo wa ngozi, au inaboresha utendakazi wa viungo, bado hayajaonyeshwa vya kutosha na utafiti wa kisayansi.
Heng anasema, tafiti nyingi juu ya collagen zimefafadhiliwa na makampuni ya virutubisho hivyo au yaliyoidhinishwa na wafanyakazi wa makampuni haya. Migogoro ya maslahi inapaswa kutangazwa katika karatasi za utafiti, lakini hilo halifanyiki kila wakati.
Lakini hakuna hatari kubwa za kiafya za moja kwa moja za virutubisho hivi.
Kwa ajili ya ngozi, tishu na viungo

Chanzo cha picha, Getty Images
Daktari wa ngozi kutoka London Anjali Mahto, aliiambia BBC mwaka 2019, "kuna uthibitisho mdogo kwamba virutubisho hivyo vitastahamili mmeng'enyo wa chakula, na kuingia kwenye mkondo wa damu na kufika kwenye ngozi yako."
Protini yoyote inapofika tumboni - ikiwa ni pamoja na collagen - kawaida huvunjwa na kuwa asidi ya amino, ambayo hugeuzwa kuwa protini ambayo mwili unaihitaji kwa wakati huo.
Watumiaji wengi huona matokeo mazuri kwa ngozi zao. Na utafiti mmoja umegundua kuwa kolajeni ya hidrolisisi inaweza kuwa na faida kwenye ngozi , kama vile kuboresha unyevu. Lakini watafiti hao walihitimisha kwa kusema, utafiti zaidi unahitajika ili kudhibitisha hilo.
Lakini wataalamu wanasema ipo njia mbadala ya kuongeza ufanisi wa virutubisho vya collagen. Robert Erskine, mtaalamu wa fiziolojia ya mishipa ya fahamu katika Chuo Kikuu cha Liverpool, anasema mazoezi yanaweza kuchochea tishu za mwili kuzalisha upya kolajeni kuliko kawaida.
Katika utafiti mmoja, Erskine na wenzake kutoka vyuo vikuu vya Uingereza, kwa kutumi sampuli ya vijana, wanaume wenye afya nzuri, waligundua kuwa wanaume hao walizalisha kolajeni mpya zaidi walipokunywa mchanganyiko wa vitamini C na gramu 30 ya collagen hidrolisisi kabla ya mazoezi.
Katika utafiti mwingine wa Erskine, timu hiyo ilichunguza wanaume wa makamo kupitia njia hiyo hiyo. Waligundua kuwa kulikuwa na nyongeza ya collagen, lakini ndogo. Kwa hivyo, umri ni sababu katika uzalishaji wa collagen.
Tafiti nyingine imegundua kuwa virutubisho vya collagen hupunguza maumivu yanayohusiana na viungo. Lakini watafiti wanasema utafiti zaidi unahitajika.
Je, unapaswa kutumia collagen?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pamoja na kirutubisho chochote, kuna hatari ya mwingiliano na dawa zingine ambazo watu wanatumia, kwa hivyo wataalamu wanashauri mtu yeyote anayefikiria kutumia kirutubisho, kuzungumza na mtaalamu wa afya kwanza.
Kuongezeka utumiaji wa protini kama collagen kunaweza kuleta shida kwa watu walio na tatizo la figo au ini na kuathiri utenda kazi wa mwili, anasema Erskine.
Wengi wa watu wanavutiwa na virutubisho, baada ya kusikia matangazo ya vyombo vya habari au watu wanaowajua. Ni muhimu sana watu kukutana na wataalamu wa afya kwanza.
Kwa ujumla, kutokana na sababu nyingi, hakuna jibu moja la ikiwa collagen inafaa. Itategemea kwa nini unataka kuitumia, kwa muda gani unaweza kuendelea kuitumia, na jinsi inavyoweza kukupa majibu kwa afya yako.
Hatimaye, wanasayansi wanaeleza kwamba mamia ya pauni kwa mwaka zinazotumiwa kwa virutubisho vya collagen zinaweza kutumika kwa lishe bora zaidi, ambayo itaboresha afya yako
Mbali na vyakula vyenye lishe vya aina mbalimbali, mazoezi, kulala - vyote vina faida kubwa kwa afya ya ngozi. Ni kweli hayo yanaweza kukuchosha lakini yanaweza kuokoa pesa nyingi kwa muda mrefu.
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi












