Vita vya Pili vya Dunia: “Nilisikia ving'ora na magoti yakaanza kutetemeka.”

cv

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Neville Chamberlain
    • Author, Greg McKevitt
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Uingereza iliingia vitani na Ujerumani ya Hitler tarehe 3 Septemba 1939. Ni miaka 21 tu ilikuwa imepita tangu Vita vya kwanza vya Dunia kuisha, na Waziri Mkuu wa Uingereza Neville Chamberlain alijaribu sana kuzuia vita vingine na Ujerumani.

Mwaka mmoja mapema, Chamberlain alidai "amani imepatikana" kupitia Mkataba wa Munich, wakati Uingereza na Ufaransa zilipomwacha Adolf Hitler aichukue Sudetenland kutoka Czechoslovakia, mradi tu hatojaribu kunyakua ardhi zaidi.

Mwezi Machi 1939, Hitler alivamia Czechoslovakia, akivunja masharti ya mkataba. Kisha Ijumaa tarehe 1 Septemba 1939, alianzisha mashambulizi makali dhidi ya Poland, jirani dhaifu wa Ujerumani. Hitler alipiga mahesabu kwamba washirika wa Poland, Uingereza na Ufaransa, zisingejibu chokochoko hizi mpya.

Lakini sera ya Chamberlain ya kumtuliza Hitler haikuwezakuleta ufanisi tena. Uingereza ilitoa makataa siku ya Jumamosi kwamba ikiwa Hitler hatoondoa majeshi yake, kutakuwa na vita. Mwisho wa onyo hili ni saa 05:00 asubuhi, siku ya Jumapili.

Pia unaweza kusoma

Tangazo la Vita

Dakika kumi na tano baadaye, Chamberlain aliketi mbele ya kipaza sauti cha BBC katika Chumba cha Baraza la Mawaziri huko 10 Downing Street, makazi yake rasmi. Mtangazaji wa BBC Alvar Lidell alikuwa pamoja naye.

Katika matangazo yake, Chamberlain alisema: “Ni pigo kubwa kwangu kwamba mapambano yote ya muda mrefu ya kupata amani yameshindwa. Uvamizi wa Hitler nchini Poland unaonyesha wazi hakuna nafasi ya kutarajia mtu huyu ataachana na tabia yake ya kutumia nguvu kupata atakacho - anaweza tu kuzuiwa kwa nguvu."

Wakati watu wakitafakari habari hii, matangazo yaliyofuata yalibadilisha maisha ya kila mtu. Sehemu zote za burudani kama vile sinema zilifungwa, na mikusanyiko mikubwa ya umma kama vile hafla za michezo pia ilipigwa marufuku.

"Beba barakoa yako ya gesi kila wakati. Hakikisha wewe na kila mwanakaya wako, haswa watoto wanaoweza kukimbia, majina na anwani zao vimeandikwa panapoonekana. Andika kwenye bahasha au kwenye lebo ya mizigo; sio kwenye karatasi ya kawaida ambayo inaweza kupotea. Ishonee lebo hiyo kwenye nguo za watoto wako mahali ambapo hawawezi kuiondoa.”

Ingawa wengi waliogopa habari za vita, Lakini maandalizi yalikuwa yameshafanywa kabla, wakati akifanya uchokozi. Maelfu ya watoto walihamishwa kutoka majiji na miji siku ya kabla ya tangazo.

Mwaka mmoja kabla, BBC ilitangaza mipango ya serikali ya kuchukua hatua za tahadhari za ulinzi. Pamoja na kuandikisha watu wa kujitolea katika vikosi vya ulinzi wa anga na ulinzi wa baharini, vipeperushi vilisambazwa juu ya nini cha kufanya wakati wa uvamizi wa anga, mitaro ilichimbwa kwenye bustani za mapumziko na barakoa za gesi zilisambazwa.

Aprili 1939, uandikishaji wa raia ulianzishwa. Kufikia wakati vita, zaidi ya vibanda milioni 1.5 vya chuma kwa ajili ya kutoa ulinzi wa mashambulizi ya angani, vilikuwa vimetolewa kwa ajili ya watu kuchimba na kuvizika kwenye bustani zao.

Kumbukumbu za watu

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ndani ya dakika chache baada ya Chamberlain kutangaza vita, ving'ora vilisikika London yote. Mwaka 1969, miaka 30 baadaye, BBC ilikusanya kumbukumbu za watu za wakati huo katika kipindi kilichoitwa, Where Were You on the Day War Broke Out? (Ulikuwa wapi Siku Vita Vilipoanza?)

Mwanamke mmoja alisema: "Nilisikia ving'ora vikilia na nilikuwa nikitetemeka magotini." Mwingine anakumbuka aliona wafanyakazi wa bandarini wakikimbia kuokoa maisha yao.

Mwanaume mmoja aliyekuwa nje wakati ving'ora vinalia alimuuliza mtu fulani kama angeweza kujificha katika kibanda cha chuma cha kujihifadhi, na kuambiwa hakuna nafasi. Alisema mwenye nyumba alimwambia: "Mimi ndiye pekee katika eneo hili niliyeamua kuwa na makazi ya kujificha. Mara tu king'ora kilipolia, majirani zangu wote walipanda juu ya uzio wa nyuma na kuingia kwenye makazi yangu. Watazame, wamejazana kama sungura."

Mwanaume mwingine alikiri kwamba alikuwa akicheza tenisi wakati wa ving'ora, "na tukakimbilia nyumbani haraka iwezekanavyo."

Ufaransa ilitangaza vita dhidi ya Ujerumani saa tano baada ya Uingereza. Rais wa Marekani Franklin D Roosevelt aliamua kutoegemea upande wowote, akihofia kuingia katika kile kilichoonekana kama mzozo wa Ulaya.

Katika moja ya matangazo, alisema: "Taifa hili litasalia kuwa taifa lisiloegemea upande wowote. Lakini siwezi kumtaka kila Mmarekani abaki asiegemea upande wowote katika mawazo pia.

Saa 12:00 jioni, Mfalme George VI alitangaza kutoka Buckingham Palace kwa raia wake nchini Uingereza na Jumuiya ya Madola, “watu wasimame imara na waungane katika wakati huu wa majaribu.”

Vita vyaingia England

Baada ya ving'ora vilivyosikika mjini London, kilichofuata nchini Uingereza katika muda wa miezi sita ni kipindi ambacho kilijuulikana kama Vita vya Phoney, ni mvutano mkali lakini hakuna mabomu yanayoanguka.

Kufikia mwishoni mwa chemchemi ya 1940, ni watu wachache tu ambao walikuwa bado wanabeba barakoa za gesi na vibanda vya kujikinga vilikuwa vimejaa maji.

Hadi tarehe 7 Septemba 1940 ndipo anga kusini mwa England ikaanza kupata giza, wanajeshi wa Ujerumani walianza mashambulizi mfululizo ya angani. Zaidi ya raia 40,000 waliuwawa kwa mabomu ya Ujerumani wakati wa miezi minane ya kutisha.

Chamberlain alijiuzulu kama waziri mkuu Mei 1940. Alikufa kwa saratani Novemba mwaka huo. Siku tatu baada ya kifo chake, mrithi wake Winston Churchill alitoa pongezi kwake katika Baraza la Commons.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah