Tunachofahamu kuhusu mashambulizi mapya ya Urusi nchini Ukraine

Matokeo ya shambulio la Urusi katika mkoa wa Odessa

Chanzo cha picha, t.me/dsns_telegram

Muda wa kusoma: Dakika 5

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Urusi ilianzisha shambulia lake nchini Ukraine siku ya Jumatatu asubuhi kwa kutumia zaidi ya makombora mia moja na takribani ndege mia moja zisizo na rubani.

Kulingana na habari za hivi karibuni, watu watano waliuawa. Mamlaka ya Ukraine inasema mgomo huo wa pamoja ulilenga vituo vya nishati kote nchini.

"Hili lilikuwa mojawapo ya mashambulio makubwa zaidi kwa pamoja. Zaidi ya makombora mia moja ya aina tofauti na takribani 'shahid' mia moja. Na kama mashambulio mengi ya awali ya Urusi, hili ni baya sana, likilenga miundombinu muhimu ya kiraia," Zelensky. alisema.

Kulingana na yeye, shambulio hilo lilikuwa "katika mikoa yetu mingi, kutoka Kharkiv na Kyiv hadi Odessa na mikoa ya magharibi." "Kwa bahati mbaya, kuna majeruhi," rais wa Ukraine aliongeza.

Kwa mujibu wa mamlaka, takribani watu watano waliuawa katika mikoa ya Volyn, Zhitomir, Zaporizhia, Dnipropetrovsk na Kharkiv. Kuna majeruhi 20 wanaojulikana.

Kukatika kwa umeme na uhaba wa maji kuliripotiwa katika miji mingi, pamoja na sehemu za Kyiv. Urusi ilishambulia nishati au miundombinu mingine muhimu katika takribani mikoa 10, Reuters ilihesabu. Vyanzo vingine vinasema 15.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilithibitisha kwamba asubuhi ya Agosti 26, vikosi vya jeshi la Urusi vilianzisha "mashambulizi makubwa ya silaha za masafa marefu za anga na baharini" na kushambulia ndege zisizo na rubani kwenye miundombinu muhimu ya nishati ambayo inadaiwa kuunga mkono eneo la kijeshi na viwanda la Ukraine.

Kulingana na Wizara ya Ulinzi ya Urusi, malengo yalikuwa vituo vya umeme katika mikoa ya Kyiv, Vinnytsia, Zhitomir, Khmelnytskyi, Dnepropetrovsk, Poltava, Nikolaev, Kirovograd na Odessa.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mamlaka ya Urusi pia iliripoti mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Ukraine huko Saratov na eneo jirani ya Engels, ambapo kuna kambi ya ndege ya washambuliaji wa masafa marefu, ambayo hutumiwa kuishambulia Ukraine, vyombo vya habari vya Ukraine vinaripoti.

Urusi iliongeza kwa kasi mashambulizi kwenye gridi ya nishati ya Ukraine mwezi Machi, huku Rais Putin akihusisha hili na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Ukraine kwenye viwanda vya kusafishia mafuta vya Urusi na bohari za mafuta.

Shambulio jipya kubwa dhidi ya Ukraine lilikuwa kali zaidi katika wiki kadhaa ambazo wanajeshi wa Ukraine wamekuwa wakifanya mashambulizi katika eneo la Kursk, Reuters inaripoti.

Waziri Mkuu wa Ukraine Denis Shmyhal alisema kwamba adui "alitumia aina mbalimbali za silaha: UAVs, makombora ya cruise, Kinzhals."

Vyombo vya habari vya Ukraine viliripoti kuwa kituo cha kuzalisha umeme cha Kiev kilipigwa.

Jarida la Forbes la Ukraine, likitoa mfano wa chanzo, inaandika kwamba jeshi la Urusi "lililenga" kituo cha umeme wa maji, na linanukuu mkuu wa "Kituo cha Kupambana na taarifa za uongo" Andrey Kovalenko: "Kuhusu bwawa la nguvu ya umeme ya Kyiv, hakuna vitisho Haiwezekani kuiharibu kwa makombora. Haifai kulinganisha na eneo la Kherson, kulikuwa na mlipuko kutoka ndani.

Utawala wa kijeshi wa kikanda unaripoti tu kwamba vinu viwili vya nishati katika mkoa wa Kyiv viliharibiwa, ni zipi haswa, hazijaainishwa. Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, nyumba 22 za watu binafsi ziliharibiwa kutokana na kuanguka kwa vifusi.

Wakazi wa Kyiv

Chanzo cha picha, Yan Dobronosov/Telegraph

Poland ilitangaza kuwa kitu kiliingia kwenye anga ya nchi hiyo mapema Jumatatu asubuhi.

"Uwezekano mkubwa zaidi ilikuwa ndege isiyo na rubani, kwani njia na kasi ya ndege zinaonesha kuwa hakika halikuwa kombora," msemaji wa amri ya operesheni Jacek Goryszewski aliiambia Reuters.

Alisema wanajeshi walikuwa wakitafuta kitu hicho na bado haijawezekana kusema ikiwa ni cha Urusi au Kiukreni.

Jiografia ya shambulio jipya la Urusi ilikuwa pana. Mikoa ambayo vifaa vya umeme au miundombinu muhimu ilishambuliwa ni pamoja na mikoa ya Rivne na Volyn kaskazini-magharibi mwa Ukraine, mkoa wa Khmelnytsky kusini magharibi mwa nchi, mkoa wa Zhytomyr kaskazini, mkoa wa Lviv magharibi, na Dnipropetrovsk. Mikoa ya Kirovohrad na Vinnytsia katikati mwa Ukraine, mkoa wa Zaporizhia kusini mashariki na mkoa wa Odessa kusini.

Takribani saba kati ya mikoa hii ina miundombinu ambayo imeharibiwa kuharibiwa, kulingana na mamlaka, Reuters inabainisha.

Katika mkoa wa kaskazini-mashariki wa Sumy, ambapo Ukraine ilianzisha uvamizi wake wa Urusi mnamo Agosti 6, kituo cha miundombinu ya reli kiliharibiwa, kulingana na taarifa kutoka kwa mamlaka (hakuna maelezo mengine yaliyotolewa).

Huko Lutsk katika mkoa wa Volyn, jengo la ghorofa liliharibiwa katika shambulio, mamlaka iliripoti mtu mmoja alikufa na watano kujeruhiwa

Chanzo cha picha, t.me/dsns_telegram

Jeshi la anga la Ukraine limesema Urusi ilitumia mabomu 11 ya masafa marefu ya Tu-95 na silaha nyingine katika shambulio hilo kubwa.

Iligundua silaha 236 za mashambulizi ya anga, makombora 127 na droni 109 za mashambulizi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, makombora 102, likiwemo moja la Kinzhal, na ndege zisizo na rubani 99 zilidunguliwa.

Waandishi wa BBC waliripoti mawimbi kadhaa ya milipuko huko Kyiv, mifumo ya ulinzi wa anga ilipunguza shabaha za angani walipokuwa wakikaribia mji mkuu.

Kulingana na utawala wa kijeshi wa jiji hilo, takribani ndege 20 zisizo na rubani zilidunguliwa walipokuwa wakikaribia Kyiv.

Watu walijificha kwenye treni. Kwa jumla, tahadhari ya uvamizi wa anga katika jiji hilo ilidumu kwa saa nane na nusu.

Hakuna uharibifu katika mji mkuu wa Ukraine, lakini matatizo ya umeme na usambazaji wa maji yameanza katika Kyiv na miji mingine.

Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov alitoa wito kwa washirika kuondoa vikwazo dhidi ya vituo vya kijeshi vya Urusi baada ya mashambulizi mapya makubwa ya Urusi.

"Wananchi waliteseka, nyumba ziliharibiwa, miundombinu muhimu iliharibiwa. Hii inathibitisha tena kwamba ili kushinda tunahitaji uwezo wa masafa marefu na kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya vituo vya kijeshi vya adui. Ukraine inaandaa majibu," Interfax-Ukraine inamnukuu waziri huyo.

Urusi na Ukraine zote mbili zinakana kuwalenga raia makusudi. Kila upande unasema mashambulizi yake yanalenga kuharibu miundombinu muhimu kwa juhudi za vita vya mwingine.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga