Vladimir Demikhov: Mwanasayansi wa Soviet aliyeushangaza ulimwengu kwa majaribio ya mbwa wenye vichwa viwili

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka 1959, mwanasayansi wa Soviet, Vladimir Demikhov, alimwalika mpiga picha wa Jarida la LIFE, Howard Zochurek kumpiga picha yeye na msaidizi wake, Dk Vladimir Goriainov, wakifanya upasuaji wa mwisho, wa kuunda mbwa mwenye vichwa viwili .
Demikhov alielezea mbwa mwenye umri wa miaka 9 ambaye mwili wake ndio utatumika na mwingine mdogo, ambaye kichwa chake ndio kitapandikizwa kwenye mwili wa mbwa mkubwa.
Makala iliyoandikwa na mwandishi wa Moscow Edmund Stevens katika gazeti, ilielezea kwa undani upasuaji wa saa tatu na nusu.
"Kwanza, walichanja chale chini ya shingo ya mbwa mkubwa, na kufichua mshipa wa shingo, na sehemu ya uti wa mgongo ...
"Mwili wenye kichwa na migu tu wa mbwa mdogo uliwekwa kwenye meza ya upasuaji karibu na mbwa mkubwa. Na wakafanya operesheni na kisha wakashona ngozi. Na upasuaji ukaisha."
Picha za rangi nyeusi na nyeupe, ambazo zilionekana katika toleo la Julai 1959 la gazeti la Life, zilionyesha operesheni ya kutisha.
Kiumbe huyo aliishi kwa siku nne.
Maono ya Demikhov

Chanzo cha picha, Getty Images
Hakuwa mbwa wa kwanza wa Dk. Demikho mwenye vichwa viwili. Tayari alikuwa amefanya jaribio hilo mara 23 kwa viwango tofauti vya mafanikio. Moja ya uumbaji wake uliishi kwa siku 29.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Napata hisia mchanganyiko ninapoona picha hizo kwa sababu ni wanyama ambao, kwa maneno rahisi, waliteswa," anasema Igor Konstantinov, daktari maarufu wa kimataifa wa upasuaji wa moyo na mishipa ambaye alihitimu huko St. Petersburg na kufanya kazi katika Hospitali ya Watoto ya Royal huko Melbourne, Australia.
Demikhov aliliambia jarida la Life, lengo la majaribio yake lilikuwa kuonyesha kwamba kupandikiza tishu na viungo vyenye afya ni jambo linalowezekana.
Leo, upandikizaji ni jambo la kawaida, lakini haikuwa hivyo hadi mwishoni mwa miaka ya 1960 ambapo upandikizaji wa ini na moyo ulifanyika kwa mafanikio.
Lakini kwa wale waliosoma makala ya jarida la Life katika miaka ya 1950, maono ya Demikhov juu ya upandikizaji wa vchwa viwili yalionekana kama ya kutisha.
"Tutaanza kwa kuwa na benki ya tishu," daktari wa Soviet alimweleza mwandishi wa gazeti la Moscow.
"Hatimaye itajumuisha kila sehemu ya mwili wa binaadamu; konea, mboni za macho, maini, figo, mioyo na hata miguu.
"Kila kitu kitawekwa kwenye jokofu. Tutakapokuwa tayari, mwathirika wa ajali ataletwa na jeraha la baya. Na tutampatia kiungo muhimu kutoka katika benki yetu. Ikiwa upandikizaji utafanikiwa, ataishi. Ikiwa haujafanikiwa, tutafanya kwa mwingine."
Majaribio mengine

Chanzo cha picha, Getty Images
Demikhov alizaliwa 1916 kutoka familia masikini. Baba yake alikufa katika Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Urusi na mama yake alidhamiria watoto wake watatu wapate elimu nzuri.
Alisoma Biolojia katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Moscow, na kuhitimu kwa daraja la juu mwaka 1940. Miaka 20 mbele, ndipo alipoanza majaribio kuhusu upandikizaji.
Mbali na mbwa wake wenye vichwa viwili, alifanya tafiti pia. Mwaka1937, Demikhov aliunda kifaa cha kwanza cha kusaidia moyo .
Mapema 1946, alifanya upandikizaji wa vingo vya ndani ya mwili kwa wanyama, ikiwemo moyo na mapafu. Majaribio ya kwanza kufanikiwa ya upandikizaji kwa wanyama.
Pia alifanya operesheni ya kwanza ya mishipa ya kusukuma damu moyoni na upandikizaji wa kwanza wa ini, miongoni mwa mambo mengine.
"Ni ngumu sana kuelewa ni kwanini, alikuwa na msukumo huu wa ajabu wa kupandikiza vingo, licha ya maafa yote ya kiuchumi katika nchi yake na vita vya kutisha," anasema Konstantinov.
"Ninaweza tu kukisia kwamba alitaka kufanya jambo kubwa kwa nchi yake na kwa manufaa ya ubinadamu. Nadhani, hili ndilo jambo ambalo lilikuwa muhimu kwake."
Mchango wake

Chanzo cha picha, Getty Images
Mchango wa Demikhov katika upandikizaji ni mkubwa sana. Dk Christian Barnard, aliyefanya kazi ya kwanza ya kupandikiza moyo wa mwanadamu duniani, alimwita "baba wa upandikizaji wa moyo na mapafu."
Lakini mbwa wake wenye vichwa viwili waliharibu sifa yake yake, haswa katika nchi yake.
"Maafisa walimtangaza kuwa mzushi, na majaribio yake yalipigwa marufuku," anasema Konstantinov.
"Alilazimika kufanya kazi katika Idara ya Upasuaji ambayo iliongozwa na Alexander Vishnevsky, ambaye alikuwa daktari mkuu wa upasuaji wa jeshi la Soviet.
"Kwa hivyo alilindwa na jeshi la Urusi ili aweze kuendelea na majaribio yake.
"Lakini naweza kukuambia kama mwanafunzi wa matibabu katika Umoja wa Kisovieti na kisha Urusi, sikuwahi kusikia juu ya Demikhov. Jina lake halikutajwa," anasema mtaalamu huyo ambaye alihitimu kutoka Chuo cha Tiba cha Kijeshi huko Saint Petersburg, Urusi, 1992.
Lakini katika maeneo mengine, mafanikio yake yanapendwa.
"Anastahili sifa miongoni mwa madaktari bingwa wa majaribio ya upasuaji. Hajatambulika kama inavyotakiwa," liliandika jarida la The Annals of Thoracic Surgery mwaka wa 1994.
Katika mwaka wa kifo chake, alitambuliwa nchini Urusi na akapewa heshima ya juu. Dk Demikhov alikufa akiwa na umri wa miaka 82 mwaka 1998 katika nyumba yake nje kidogo ya Moscow.
"Kila kitu alichofanya kilikuwa kwa manufaa ya wagonjwa duniani kote, moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, wamefaidika na majaribio yake," anasema Konstantinov.
"Jambo la muhimu zaidi, aliweza kuwashawishi watu waliomfuata kwamba jambo lisilowezekana linawezekana."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












