Kwa nini Kenya inageukia mazao ya GMO kukabiliana na ukame
Na Richard Kagoe
BBC News, Nairobi

Wakati Kenya inapojiandaa kufanya biashara ya mazao yaliyotokana na mbegu kisaki za GMO, kuna upinzani kutoka kwa baadhi ya wakulima na makundi vya wanaharakati, ambao wanatilia shaka usalama wa mazao hayo.
"Unafanya kile tunachokula kuwa mbaya zaidi kuliko ilivyo," anamshtumu mkulima Eva Wanjiru.
Ana wasiwasi na ukweli kwamba wakulima wengi wa Kenya wataanza kutumia mbegu za kisaki za mahindi (GM) mapema mwaka ujao, baada ya serikali hivi majuzi kubatilisha marufuku ya miaka 10 dhidi ya mazao hayo.
Hata hivyo hakuna cha kuogopa linapokuja suala la kula vyakula vilivyokuzzwa kutokana na mbegu za kisaki (GMO) kwenye mwili wa binadamu, anasema Richard Oduor, profesa wa bioteknolojia katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.
"Hakuna ushahidi wa kisayansi unaohusisha vyakula vya GMO na saratani. Ninaona ni mjadala unaofaa kwa sababu kwa nini hatuna hofu kutumia insulini iliyobadilishwa vinasaba lakini hatuwezi tunaogopa vyakula vya GM kwa sababu ya athari ya kujitungia? Madai ambayo hayana msingi," aliiambia BBC.
Kwa hali yoyote, anasema, GMOs hufuatiliwa kwa karibu baada ya kutolewa.
Kenya kwa sasa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji unaosababishwa na kukosekana kwa mvua kwa misimu minne mfululizo, huku kukiwa na ukame mkali zaidi katika kanda ya Afrika Mashariki kuwahi kushuhudiwa katika miongo minne.
Hii inamaanisha kuwa mazao hayawezi kukua, na hivyo kutishia uwezekano wa kuzuka kwa baa la njaa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mbegu za GM ni zile ambazo zimebadilishwa vinasaba ili kutoa kile kinachoonekana kuwa sifa zinazohitajika kama vile ukame na kustahimili wadudu - na ni kutokana na ustahimilivu huu ndipo wengine wana maoni chanya zaidi kuliko Bi Wanjiru.
Wanasema kuondolewa kwa marufuku ya GMO kulichochewa na hitaji la kweli la kuhakikisha usalama wa chakula na kulinda mazingira.
"Mabadiliko ya hali ya hewa, ukali wa ukame na kuibuka kwa wadudu waharibifu kama vile viwavijeshi na vipekecha shina wa mahindi, na magonjwa ya mahindi kama vile lethal necrosis ni tishio kwa usalama wachakula, malisho ya [ng'ombe] na usalama wa lishe," alisema Dk Eliud Kireger, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo la Kenya.
Magonjwa na wadudu hawa huharibu zao la mahindi. Kwa mfano, viwavi jeshi hula mimea mingi wanapo mimea.
Wanasayansi wa masuala ya chakula pia wanasema teknolojia hiyo itapunguza utegemezi wa bara la Afrika katika uagizaji wa chakula kutoka nje kwa sababu itaongeza uzalishaji.
"Tunapaswa kukumbatia teknolojia na kuiona kama suluhu ya changamoto tunazokabiliana nazo zaidi ya matatizo," alisema Dkt Murenga Mwimali, kutoka Muungano wa Sayansi katika Chuo Kikuu cha Cornell nchini Marekani.
Kulenga chakula kikuu cha Kenya
Tathmini ya 2018 ya tafiti kuhusu mazao ya GMO iliashiria kuwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita mavuno kutokana na mbegu kisaki za mahindi ya GMO yameongezeka.
Mdhibiti wa teknolojia ya kibayoteknolojia nchini Kenya anasema kuna ushahidi kwamba gharama zinapunguzwa kwa sababu ya udhibiti bora wa magugu, utumiaji mdogo wa dawa za kukabiliana na wadudu na kupungua kwa nguvu kazi.
Kuondoa marufuku hiyo kunamaanisha kuwa wakulima wa Kenya sasa wanaweza kulima kwa uwazi mazao ya GM, pamoja na kuagiza chakula kutoka nje ya nchi na vyakula vya mifugo vinavyozalishwa kupitia kwa njia ya GMO, kama vile mahindi meupe ya GMO.
Mahindi ni chakula kikuu nchini Kenya, na hulimwa katika asilimia 90 ya mashamba yote ya Kenya.
Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Kenya, na kinatoa asilimia 80 ya ajira kwa wakazi wa mashambani.
Wakulima wa Kenya wanategemea mazao yao sio tu kwa mapato bali kama chanzo cha chakula kwa familia zao.

Bi Wanjiru amekuwa akifanya kilimo-hai kwa miaka mingi huko Kiangwaci eneo la Sagana, kilomita 110 (maili 70) kaskazini-mashariki mwa mji mkuu, Nairobi.
Hatumii dawa za kuua wadudu au mbegu chotara kwenye shamba lake la ekari moja.
Anaamini hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba mazao yanayokuzwa kupitia teknolojia ya GMO yatasaidia nchi kukabiliana na uhaba wa chakula.
"Wakulima wengi wanaopanda hizi GMO wanalalamika kuhusu wadudu na magonjwa. Mvua isiponywesha, bado wanalalamika kuhusu [jinsi] mazao yanavyoharibika shambani. Sidhani kama ni suluhu."
Pia kuna hofu kwamba wakulima wanaoanza kutumia GMO watategemea kampuni zinazouza mbegu hizo, na wataanza kutawala soko kwa maslahi yao badala ya wakulima wa kawaida wa Kenya.
'Sheria za kibabe'
"Kuruhusu makampuni haya kutawala soko la uzalishaji na uagizaji wa mazao muhimu kama vile mahindi kunaweza kuathiri maisha ya wakulima ambao wanazalisha takriban magunia milioni 40-45 ya mahindi kila mwaka nchini Kenya," alisema Claire Nasike, mwanasayansi wa mazingira katika shirika la Greenpeace Africa.
"Kuondoa marufuku ya GMO pia kutawaweka wakulima kwenye sheria kali za haki miliki zinazohusiana na hati miliki zinazomilikiwa na makampuni ya kimataifa ya GMO.
Mbegu ya GM ina hati miliki na hii inaweza kuwaingiza wakulima ambao mazao ya GM yamelimwa kwenye shamba lao katika migogoro ya haki miliki bila wao kujua," Bi Nasike iliendelea kusema.
Lakini Dkt Stephen Mugo, mkurugenzi wa Kituo cha Resilient Agricalture Africa, anahoji kuwa Kenya haitakuwa mateka wa mashirika ya kimataifa.
"Ni madai yasiyo na msingi kwa sababu Kenya ina uwezo wa kuendeleza mazao ya GM. Kampuni nyingi hukodisha teknolojia ambayo wao hutumia kuunda jeni mpya," alisema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Utafiti uliofanywa na shirika lisilo la kiserikali, Route to Food Initiative, mwaka jana ulionyesha kuwa 57% ya Wakenya hawataki mazao ya GMO, sasa watalazimika kushawishika.
Shirka la serikali lililopewa jukumu la kufanya usimamizi wa jumla na udhibiti wa uhamishaji, utunzaji na matumizi ya GMO linasema aina za mahindi zimefanyiwa majaribio na zipita tathmini za viwango vya usalama.
Maafisa wanasema hazina madharakwa afya ya binadamu.














