Trump anataka amani huku raia wa Ukraine wakiingiwa hofu

Chanzo cha picha, BBC/Matthew Goddard
- Author, James Waterhouse
- Nafasi, Mwandishi wa Ukraine
- Akiripoti kutoka, Malokaterynivka
- Muda wa kusoma: Dakika 4
''Sina mpango wowote wa siku za usoni,'' anasema Oleksandr Bezhan, akiwa amesimama mbele ya chumba ambacho kimebanwa na kufuli kilichoganda, eneo alikuwa akifanyia biashara yake ya kuuza samaki katika ukingo wa mto Dnipro kaskazini mwa Ukraine.
''Nikijipata nimeamka asubuhi, huwa nina amini riziki yangu ipo''.
Malokaterynivka ni eneo lililoko kilomita 15 yaani maili 9 Kaskazini mwa eneo la vita la Ukraine mkoa wa Zaporizhzhia.
Iwapo mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kusitisha mapigano utakuwa wenye ufanisi, eneo la Malokaterynivka linatumai litakuwa eneo bora.
Nilizuru eneo hili mwaka 2023, wakati Ukraine ilikuwa imeanzisha mapigano na Urusi.
Wakati huo UKraine ilionekana kuwa na nafasi nzuri ya kushinda vita hivi , hakika ilishinda vita vya Kyiv na kudhibiti maeneo mengine.
Lakini baada ya miezi 18, Urusi ilijibu mashambulizi hayo vikali na kufikia sasa Urusi inaonekana kudhibiti mapigano hayo.
Eneo hili ambalo vita vinaendelea linaonekana, lakini mto ambao ulikuwa tegemeo kwa wengi haupo tena.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakati eneo lililodhibitiwa na Urusi bwawa la Kakhovka iliharibiwa, eneo hili liligeuka kuwa uwanja mkubwa wa vichaka.
Mazingira haya yanaakisi hali ya kutokuwa na uhakika ambayo Ukraine inajikuta nayo.
Ikulu ya White House inataka kumaliza vita, lakini si jambo rahisi kama kupuliza kipenga cha kumaliza mechi.
"Endapo eneo linalopiganiwa litageuzwa kuwa mpaka, itakuwa hatari… mapigano yanaweza kuzuka wakati wowote," anasema Oleksandr.
Mto unaoonekana unaweka mpaka kati ya eneo letu na eneo linaloshikiliwa na Urusi.
Jua la mbali linang'aa juu ya kiwanda cha nishati cha nyuklia cha Zaporizhzhia, ambacho kiko chini ya udhibiti wa Moscow tangu 2022.
Ukraine na Marekani zote zinataka amani, lakini makubaliano yanaishia hapo.
Dhamira ya Washington kuhusu amani, pamoja na ukweli wa vita, ina maana kwamba Urusi huenda ikaendelea kushikilia maeneo ya Ukraine ambayo imeteka.
Ukraine inahitaji hakikisho la usalama linaloweza kuzuia vikosi vya uvamizi kuvuka mto.
Hata hivyo, Donald Trump amekataa mpango wa Kyiv ya kujiunga na muungano wa NATO akielekeza umakini wake kwa Urusi.
Baada ya kushuhudia na kuripoti kuhusu mapambano ya Ukraine kwa zaidi ya miaka mitatu, hii ni hali ngumu kwa nchi hiyo.
Kuna hisia za kutapeliwa. Wanazuoni wanamshutumu Rais Zelensky au sera mpya za nje za mshirika wake mkubwa.
"Mipaka haitategemea sisi," anasema Oleksandr. "Inaweza kutofanikiwa, lakini Seoul iko umbali wa kilomita 30 kutoka Korea Kaskazini, na wao kwa namna fulani wanaishi na kustawi."

Chanzo cha picha, BBC/Matthew Goddard
Changamoto ya Malokaterynivka ya kupata madhumuni mapya iko katikati ya mustakabali wa Ukraine.
Na wakati wanasiasa wanazungumza kuhusu mazungumzo, wananchi wa Ukraine wanaendelea kupigana na wengine kufa.
Wanavijiji wanakusanyika kwa ajili ya mazishi ya askari mmoja wa kijiji, ambaye pia anaitwa Oleksandr.
Nusu ya makaburi yaliyoko maziarani ni mapya.
Sherehe hiyo haiwezi kudumu zaidi ya dakika 25 kutokana na tishio la mashambulizi ya roketi.
Wazungumzaji wanajificha na kujilinda wakati wenzake wanapopiga saluti kwa bunduki.
"Siwezi kuwa na matumaini kwa mapumziko ya vita," anasema mkewe, Natalya, ingawa bado anataka kuaminishwa mambo yatakuwa sawa.
"Wanaendelea kutuma vijana wetu zaidi na zaidi katika vita hivi vinavyoendelea. Ningependekeza wapate suluhu ya vita hivi haraka iwezekanavyo."
Kando na mto kuna reli isiyotumika inayozungukwa na nyaya za stima.
"Hii ni kuzuia mawakala wa Urusi kusababisha uharibifu kwenye reli," anasema Lyudmyla Volyk, ambaye ameishi Malokaterynivka maisha yake yote.
Treni zilikuwa zikisafiri hadi Crimea kusini.
"Tunatumai kwamba siku moja itarudishwa," anasema mzee huyo mwenye umri wa miaka 65, kwa matumaini.
"Na siku moja tutaenda Crimea."
Miaka kumi na moja ya utawala wa Urusi kwenye rasi hiyo inafanya kuwa vigumu kuamini usalama na utulivu utarejea.

Chanzo cha picha, BBC/Matthew Goddard
Rais Zelensky anasisitiza kwamba hatosaini makubaliano ambayo hayashirikishi Ukraine, hivyo je, Lyudmyla anamwamini kupata makubaliano ambayo yatamlinda?
"Tunataka kuamini," anajibu baada ya kupumua kwa nguvu.
Ikiwa Donald Trump ataleta amani kwa Ukraine, itakubaliwa na wengi.
Tunatamani usiku tulale bila kelele, mlio wa risasi na wanajeshi wetu warejee nyumbani wakiwa salama.
Lakini kwa sasa, hali yoyote ya utulivu itachukuliwa kwa haraka na maswali yasiyojibiwa kuhusu jinsi mapumziko ya vita yatadumu na nani atayatekeleza.
Kyiv itaona ukosefu huu wa maelezo kuhusu yaliyomo kwenye makubaliano ya kusitisha vita kama fursa ya kupigania.
Tatizo kwa Ukraine ni kwamba, Urusi pia itafanya hivyo.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi












