Wanajeshi wa Korea Kaskazini Nchini Urusi: Wanapigana lakini je, Watahepa? au Kusaliti wajibu

Marekani na Ukraine zinadai kuwa wanajeshi wa Korea Kaskazini wanapigana na Wanajeshi wa Ukraine katika eneo la Kursk

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Marekani na Ukraine zinadai kuwa wanajeshi wa Korea Kaskazini wanapigana na Wanajeshi wa Ukraine katika eneo la Kursk
    • Author, Jean Mackenzie
    • Nafasi, Mwandishi BBC Seoul
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Anapokumbuka miaka yake katika jeshi la Korea Kaskazini, kitu cha kwanza anachosema Han-eul ni hisia za njaa – njaa isiyokoma na inayochosha.

Katika mwezi wake wa kwanza wa utumishi, alipoteza kilo 10: wanajeshi walilishwa mahindi pekee yaliyochanganywa na kabichi iliyojaa uvundo.

Baada ya miezi mitatu ya mafunzo, karibu kikosi chake chote kilikuwa kimechoka kupita kiasi, na kulazimika kutumwa kwenye kituo maalum cha kurekebisha hali ya afya ili waweze kurejesha uzito wa mwili.

Baadaye, walipotumwa kulinda mpaka na Korea Kusini, walibadilishiwa mlo na kuwa mchele.

Hata hivyo, vitengo vya nyuma vilifanikiwa kuiba posho za mchele kabla haujawafikia wanajeshi, wakichanganya mchanganya mchele kidogo uliobaki.

Kwa wakati huo, Han-eul anasema, kikosi chake kililishwa vizuri zaidi kuliko vingine - mbinu inayotumika na uongozi wa Korea Kaskazini kuzuia kutoroka. Hata hivyo, hii haikumzuia Han-eul mwenyewe.

Mnamo 2012, alikimbia kwa hatari kubwa kupitia eneo lisilo la mtu kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini.

Hadithi zake za uzoefu, pamoja na za wanajeshi wengine waliokimbia kutoka Korea Kaskazini, zinatoa mwanga kidogo kuhusu hali ya wanajeshi elfu kadhaa wa Korea Kaskazini waliotumwa kwenye mistari ya mbele katika vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.

Wakati wa kutoroka kwake mwaka wa 2012, Haneul alikuwa akihudumu katika askari wa mpakani wakilinda eneo lisilo na wanajeshi.

Chanzo cha picha, BBC/Hosu Lee

Maelezo ya picha, Wakati wa kutoroka kwake mwaka wa 2012, Haneul alikuwa akihudumu katika askari wa mpakani wakilinda eneo lisilo na wanajeshi.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Inaaminika kwamba Pyongyang ilituma takriban wanajeshi 11,000 kwenda Urusi kusaidia vikosi vya Urusi kuvamia na kuidhibiti sehemu ya mkoa wa Kursk ambao Ukraine ilichukua katika shambulio la ghafla mnamo Agosti.

Wiki hii, Seoul, Washington, na Kyiv waliripoti kwamba "idadi kubwa" ya wanajeshi wa Korea Kaskazini walishiriki katika mapigano katika mkoa wa Kursk, huku maafisa wa Korea Kusini wakisema kwamba "zaidi ya wanajeshi mia moja" walikuwa wameuwawa au kujeruhiwa (hata hivyo takwimu hizi hazijathibitishwa na vyanzo vingine).

Wanajeshi waliosaliti huduma na wataalamu wengine wa kijeshi waliozungumza na BBC wanatahadharisha kwamba vitengo hivi havipaswi kupuuziliwa mbali.

Kwa mujibu wa taarifa za ujasusi za Korea Kusini, wengi wa wanajeshi waliotumwa Urusi kutoka DPRK ni wanachama wa vitengo maalum vya kushambulia na wanajulikana kwa "ari ya kupigana vita," ingawa "hawana ujuzi wa hali ya juu wa vita vya kisasa."

Ni wanaume warefu na wenye miili imara pekee wanaochaguliwa kwa vitengo vya kushambulia, anasema Lee Hyun-sung, aliyewafundisha wanajeshi wa Korea Kaskazini katika vitengo maalum mwanzoni mwa miaka ya 2000 kabla ya kutoroka mwaka 2014.

Alifundisha wanajeshi hao mbinu za sanaa za kijeshi, kutupa visu, na mbinu za kutengeneza silaha za makali kutoka kwa vyombo vya chakula na vifaa vingine vya jikoni.

Ingawa wanajeshi wa vitengo maalum hupitia mafunzo makali zaidi kuliko vitengo vya kawaida vya Korea Kaskazini, hata hivyo, wanajeshi wengi mara nyingi wanakosa lishe ya kutosha hadi kufikia uchovu wa kupindukia.

Video iliyovuja, inayodhaniwa kunaswa Urusi, inaonyesha wanajeshi wachanga na dhaifu, anasema Han Eul, kinyume kabisa na picha za wanajeshi wa Korea Kaskazini kama zinavyoonyeshwa katika video za uenezi wa Propaganda kutoka Pyongyang, ambapo wanajeshi wanavunja vipande vya barafu na kupasua minyororo ya chuma kwa mikono yao.

Kwa mujibu wa Han Eul, alifyatua risasi tatu tu katika kipindi chote cha utumishi wake wa kijeshi, wakati wa mafunzo yake pekee ya silaha.

Uzoefu wake wa vita unajumuisha tukio moja ambapo mkulima aliyekuwa na njaa alijiingiza kwenye sehemu ya eneo lisilo na ulinzi wa kijeshi ambalo lililindwa na kikosi cha Han Eul, akitafuta matunda ya kula.

Han Eul anasema alipuuzilia mbali amri kali ya kuua mtu aliyejiingiza bila idhini au kutomruhusu mtu huyo aondoke, akiamua kumtahadharisha asirejee kosa hilo tena na aondoke mara moja.

Mwanzoni mwa miaka ya 2000, Lee Hyun-sung alikuwa mwalimu wa vikosi maalum vya Korea Kaskazini

Chanzo cha picha, BBC/Hosu Lee

Maelezo ya picha, Mwanzoni mwa miaka ya 2000, Lee Hyun-sung alikuwa mwalimu wa vikosi maalum vya Korea Kaskazini

Kwa kuzingatia siri kubwa inayozunguka DPRK na upungufu wa taarifa zinazotoka nchini humo kuelekea ulimwenguni, ni vigumu kusema ni kiasi gani jeshi la nchi hiyo limebadilika katika kipindi cha miaka 10 tangu kutoroka kwa Han-eul.

Inaonekana kwamba kiongozi Kim Jong-un ameielekeza sehemu kubwa ya rasilimali za nchi (ambazo tayari ni chache sana) si katika kisasa na kuimarisha jeshi la kawaida, bali katika kuendeleza mpango wa makombora na kutengeneza silaha za nyuklia.

Mwingine aliyetoroka, Ryu Sung-hyun, ambaye alikimbia mwaka 2019, anasema miaka mitatu ya kwanza katika jeshi ni ngumu sana, hata kwa wale waliobahatika kufuzu na kujiunga na vitengo maalum.

Sasa akiwa na umri wa miaka 28, alitumia miaka saba katika jeshi la anga la Korea Kaskazini, akihudumu kama dereva.

Anasema hali imekuwa mbaya zaidi kadri miaka ilivyopita, na mchele umeondolewa: "Wanajeshi hutumwa kwenye milima kwa siku chache na kiasi kidogo cha mchele, na wanaambiwa kuwa hiyo ni sehemu ya kozi ya kuishi."

Kwa kuwa wanajeshi wanahudumiwa kwenye maeneo ya milimani ya Peninsula ya Korea, wanajeshi wasaliti wanajiuliza kama wanajeshi wa Korea Kaskazini wataweza kuzoea mapigano katika mazingira mapya - kwenye mitaro kwenye maeneo tambarare karibu na Kursk.

Pia ni muhimu, anasema Ryu, kukumbuka kwamba wanajeshi wa vitengo vya kushambulia hawakufunzwa awali kwa ajili ya mapigano ya mstari wa mbele: "Kazi yao ni kuvamia mipaka ya adui, na kuleta machafuko ndani ya ardhi ya adui."

Ingawa, anaongeza, Kim Jong-un hakuwa na chaguo lingine isipokuwa kutuma vitengo maalum kwenda Urusi – kwa maana ya kwamba, wanajeshi wa vitengo vya kawaida hutumia sehemu kubwa ya huduma yao wakifanya kazi za ujenzi, kilimo au kukata kuni.

Ili kuepuka kudhalilisha sifa za Korea Kaskazini huko Moscow, Kim Jong-un alilazimika kutuma wapiganaji ambao walikuwa na uwezo wa kuonyesha angalau kiwango cha msingi cha mafunzo ya kijeshi.

Ryu anasema kuwa kama sehemu ya mafunzo yao ya kujifunza kujiokoa, wanajeshi hupelekwa milimani kwa siku kadhaa wakiwa na mchele mdogo.

Chanzo cha picha, BBC/Maxine Collins

Maelezo ya picha, Ryu anasema kuwa kama sehemu ya mafunzo yao ya kujifunza kujiokoa, wanajeshi hupelekwa milimani kwa siku kadhaa wakiwa na mchele mdogo.

Vikwazo vya lugha pia vinaongeza changamoto nyingine.

Habari za ujasusi za kijeshi za Ukraine hivi karibuni ziliripoti kwamba tatizo la mawasiliano lilisababisha wanajeshi wa Korea Kaskazini walipiga risasi kimakosa kwenye kikosi cha Urusi, na kuua wanane.

Hii inaweza kutoa picha kwamba wanajeshi wa Korea Kaskazini huko Ukraine ni "nyenzo za vita tu", ishara ya juhudi za kutokata tamaa kwa Rais Putin kutafuta watu wapya kwa ajili ya mahandaki katika mkoa wa Kursk.

Hata hivyo, wafichuzi ambao ni wanajeshi wa zamani wa Korea Kaskazini wanaamini kwamba hitimisho hili ni potofu.

Uaminifu wa dhati wa wapiganaji kwa utawala na ari yao ya mapigano inaweza kubadilisha upungufu wao mwingi.

"Zaidi ya wanajeshi wa kushambulia wanatoka katika familia za wafanyakazi au za mashamba ya ushirika, ni waaminifu kwa chama na hutii amri bila kuuliza maswali," anasema Han Eul, ambaye baba yake na binamu yake walihudumu katika vitengo maalum.

Mafunzo makali ya kisiasa, ambayo kimsingi ni ubongo wa kisiasa, yanayotolewa kila asubuhi yatasaidia wanajeshi kujiandaa kisaikolojia kwa huduma nchini Urusi, anasema Lee.

Ana uhakika kwamba kadri muda unavyosonga, wanajeshi wa Korea Kaskazini "watakuwa wamezoea hali za vita, watakuwa wamejifunza kupigana, na watapata njia za kuishi."

Picha zilizotolewa na vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini mnamo Machi 2024 zinaonyesha mafunzo ya vikosi maalum

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Picha zilizotolewa na vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini mnamo Machi 2024 zinaonyesha mafunzo ya vikosi maalum

Ingawa hakuna aliyewauliza wanajeshi wa Korea kuhusu maoni yao kuhusu kutumwa Urusi, kwa maoni ya Ryu, wengi wao wangeenda huko kwa hiari yao wenyewe.

Kwa wale wenye malengo ya kimaisha, hii ni fursa nzuri ya kupiga hatua katika taaluma zao.

Na kwa kuzingatia ugumu wa utumishi wa kijeshi nchini Korea Kaskazini, wengi wao huenda watashukuru hata kupata fursa ya kusafiri nje ya nchi kwa mara ya kwanza.

"Nadhani wako na ari zaidi ya kupigana kuliko wanajeshi wa Urusi," anasema.

Na anakubali kwamba kama angelikuwa katika nafasi ya wanajeshi hawa, yeye mwenyewe asingekataa misheni kama hiyo.

Kamanda wa zamani wa vitengo maalum vya jeshi la Korea Kusini, Chun In-bum, anakubaliana na tathmini za wafichuzi

"Kwamba wanajeshi hawa hawana chakula na mafunzo haimaanishi kuwa hawawezi kupigana. Uzoefu wa mazingira utaanza haraka. Hawawezi kupuuziliwa mbali chini ya hali yoyote."

Ingawa wanajeshi 11,000 huenda wasilete tofauti kubwa katika vita katika mahandaki vinavyotisha—na baadhi ya makadirio yanaonyesha kwamba Urusi inapoteza zaidi ya wanajeshi 1,000 kila siku—wataalamu na maafisa wanaamini kwamba matumizi yao yatakuwa na manufaa zaidi ya hapo.

Kwa nadharia, Pyongyang inaweza kutuma takriban wanajeshi 60,000 kwa huduma ya Moscow, au hata 100,000 kama wangehitajika.

Katika hali kama hiyo, Chun In-bum anaamini, wingi wa nguvu kazi unaweza kubadilika kuwa ubora, hivyo msaada wa Pyongyang unaweza kuwa muhimu sana.

Kwa mujibu wa wanajeshi wa zamani wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un anaweza kwa urahisi kubali hasara kubwa kati ya wafanyakazi wake: hili halitakuwa na athari yoyote kwa uthabiti wa utawala wake.

"Hutuma hasa wanajeshi ambao hawana ushawishi au uhusiano wa juu – kwa uwazi, wale ambao wanaweza kutumika kama sadaka kwa urahisi," anasema Han Eul.

Anakumbuka aliguswa kujua kwamba kikundi chake cha awali hakikuwa na mtu yeyote kutoka familia zenye cheo cha juu au ushawishi.

"Hapo ndipo nilijua kuwa sisi tunatumiwa."

Pia hamtarajii upinzani mkubwa kutoka kwa familia za wanajeshi waliokufa, kwani watasherehekewa kama mashujaa.

"Familia nyingi zilipoteza watoto wao katika jeshi," anasema, akitolea mfano binamu yake wa pili ambaye alikufa kwenye vita.

Badala yake, mama yake alipokea barua ya shukrani kutoka kwa mamlaka ikisifu mchango wa kishujaa wa mtoto wake katika ushindi.

Je kutakuwa na wanajeshi watakaotoroka?

Uaminifu wa dhati wa wanajeshi wa Korea Kaskazini na familia zao kwa utawala na ideolojia rasmi unaweza kuharibu matumaini ya Waukraine na Wakorea Kusini kwamba wengi wao wangeweza kutoroka mara tu walipoingia kwenye mapigano halisi.

Kyiv na Seoul tayari wamejadili kufanya operesheni za shinikizo la kisaikolojia kwenye mstari wa mbele ili kuwashawishi Wakorea wajiunge.

Hata hivyo, inaonekana hawana simu za mkononi.

Kwa mujibu wa taarifa za ujasusi za Ukraine, hata wanajeshi wa Urusi wanachukuliwa simu zao kabla ya kukutana na vitengo vya Korea Kaskazini.

Hivyo, mbinu zinazoweza kutumika kwa ajili ya kutoa dosari kwa maadili ya wanajeshi wa Korea Kaskazini ni pamoja na kutangaza ujumbe wa uenezi kupitia spika za sauti au kutoa vipeperushi kutoka kwandege zisizo na rubani.

Ryu na Han Eul walikubaliana kutoroka baada ya kusoma uenezi wa Kusini mwa Korea unaopinga utawala wa Kim Jong-un.

Hata hivyo, wote wana mashaka makubwa kama mbinu hizi zitafanikiwa mbali na nyumbani.

Kwao, inachukua muda mrefu kwa mwanajeshi kuleta hamu ya kutoroka na ujasiri wa kutoroka.

Han Eul pia anadhani kwamba maafisa walipewa amri ya kuua yeyote atakayejaribu kutoroka.

Anakumbuka jinsi wenzake walivyomfyatulia risasi bila aibu alipokuwa akikimbia kupitia eneo lisilo na ulinzi wa kijeshi.

"Risasi kumi na mbili zilipiga kwa kasi takriban mita moja juu ya kichwa changu," anakumbuka.

Kuwakamata wanajeshi wa Korea Kaskazini pia kunaweza kuwa kazi ngumu kwa Jeshi la Ukraine.

Nchini Korea Kaskazini, kukamatwa – yaani, kujisalimisha kwa adui – ni aibu mbaya kuliko kifo.

Ili kuepuka hili, wanajeshi wanatishwa kujitoa maisha yao.

Ryu anakumbuka wimbo maarufu wa kijeshi uitwao "Hifadhi Risasi Yako ya Mwisho": "Unafundishwa kuweka risasi mbili daima: moja kwa adui na moja kwako mwenyewe."

Hata hivyo, mkufunzi wa zamani wa Vitengo Maalum, Lee, amejitolea kusaidia. Amejitolea kwenda mstari wa mbele kuzungumza na wanajeshi moja kwa moja.

"Ni vigumu wao kuanza kutoroka kwa wingi baada ya hii, lakini inafaa kujaribu," alisema. "Sauti ya mtu aliye hai, anayejulikana – kama yangu na Wakoreno wengine – inaweza kuwa na athari muhimu ya kisaikolojia kwao."

Han Eul anatumai kuwa watarudi nyumbani Korea Kaskazini. Anajua kuwa jamaa zake wengi huenda wamo kati ya wanajeshi waliotumwa kusaidia Urusi.

"Natumai tu watarudi salama."

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid