Jinsi Ukraine Ilivyoweza kumuuwa Jenerali wa ulinzi wa Urusi Huko Moscow

Jenerali Igor Krylov alikuwa kamanda wa vikosi vya ulinzi vya nyuklia, kibaolojia na kemikali vya Urusi

Chanzo cha picha, Russian Ministry of Defens

Maelezo ya picha, Jenerali Igor Krylov alikuwa kamanda wa vikosi vya ulinzi vya nyuklia, kibaolojia na kemikali vya Urusi
    • Author, Zhanna Bezpiatchuk, Ilya Barabanov, Tom Santorelli
    • Nafasi, BBC World Service
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Vyanzo vya BBC katika huduma za usalama na ujasusi za Ukraine vimedhibitisha kuwa maajenti wa mashirika haya wanatekeleza operesheni dhidi ya vikosi vya kijeshi vya Urusi na maafisa wakuu waliohusika katika vita "popote pale maadui wa Ukraine wanapokuwa."

Maeneo haya ni pamoja na maeneo ya Ukraine yanayoshikiliwa na vikosi vya Urusi, ardhi ya Urusi, na maeneo mengine nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Ivan Stopak, mtaalamu wa kijeshi na afisa wa zamani wa Huduma ya Usalama ya Ukraine, mauaji ya Jenerali wa ngazi ya juu wa jeshi la Urusi, Igor Krylov, kwa kutumia kifaa kinachoshukiwa kuwekwa kwenye skuta, ni hatua inayofanana kwa ujasiri na shambulizi la Mossad kwa Hezbollah kwa kutumia kifaa cha pager.

"Huduma za ujasusi za Ukraine zililazimika kuchagua namna ya kummaliza Igor kati ya kumshambulia kwa risasi, kumlipua, au kumtilia sumu," aliongeza Stopak.

Pia unaweza kusoma:

Orodha ya malengo

Alisema kuwa kutoka kwa mtazamo wa Huduma ya Usalama ya Ukraine, mtu yeyote aliyehusika katika maandalizi, mipango, msaada, na utekelezaji wa uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine anaweza kuzingatiwa kuwa mlengwa halali.

Orodha ya wanaolengwa iliyochapishwa na huduma za ujasusi za Ukraine inajumuisha majina ya majenerali wa Urusi na makamanda wa vikosi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Jeshi la Anga la Urusi, ambalo linashambulia miji ya Ukraine na miundombinu ya nishati.

Hata hivyo, wakati Huduma ya Usalama inapoamua kumlenga mtu fulani, inatathmini kwa makini mambo kama vile ufanisi wake na umuhimu wake.

"Operesheni hii ni kazi ya kitaalamu sana. Operesheni kama hii inapaswa kufanywa na timu ya watu kadhaa," alisema Stopak kwa BBC.

"Wanapaswa kuwa wamepata taarifa kuhusu jenerali akiwa na silaha, wakiwa na taarifa kuhusu watu wake wa karibu, na uwezekano kwamba anafuatiliwa na huduma ya usalama ya Urusi."

Majasusi wanapaswa kujitolea katika misheni ya siri wakiwa waangalifu wasijulikane na kukamatwa wakiwa na mabomu mitaani Moscow au kugunduliwa na kamera za ufuatiliaji zilizowekwa – na zaidi ya hayo, wanahitaji pia kutoa njia salama ya kutoroka haraka.

"Afisa wa ujasusi aliyekuwa na jukumu la kupanga operesheni kama hizi aliniambia kuwa anapotuma watu wake kwenye misheni kama hii, dakika 20 ni sawa na siku tatu. Ni hatari sana na inawaumiza sana wote waliohusika."

Taarifa potofu na feki

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Jenerali Mkuu Igor Krylov, kamanda wa vikosi vya ulinzi wa kemikali vya Urusi, alikuwa mlengwa muhimu sana kwa huduma ya ujasusi ya Ukraine.

Jumatatu, Huduma ya Usalama ya Ukraine ilimtuhumu Krylov mwenye umri wa miaka 54 kwa kutumia silaha za kemikali zilizozuiliwa, akisema alikuwa "na jukumu katika matumizi ya silaha za kemikali zilizozuiliwa kwa wingi.

" Huduma hiyo ya usalama ilidai kuwa Urusi ilitumia silaha za kemikali zaidi ya mara 48,000 chini ya uongozi wa jenerali huyo.

Mnamo Oktoba, Uingereza iliweka jina la Krylov kwenye orodha ya vikwazo, ikisema aliongoza katika matumizi ya silaha za kemikali nchini Ukraine na alikuwa "meneja mkubwa wa upotoshaji wa taarifa za Kremlin."

Hata hivyo, Moscow inakanusha mashtaka haya.

Krylov pia aliongoza moja ya kampeni maarufu za upotoshaji dhidi ya Ukraine tangu kuanza kwa mzozo.

Anajulikana zaidi kimataifa kwa madai yake kwamba Magharibi inajaribu kutumia silaha za kibayolojia zisizo za kawaida dhidi ya Urusi.

Krylov alidai kuwa "Makao Makuu ya jeshi la Marekani inajaribu kuingiza makundi ya wanyama wadogo waliobeva virusi vya HIV na homa ya manjano" ndani ya Urusi, na pia alidai kuwa makundi ya "mbu wa vita" wanaobeba virusi mbalimbali wangesambazwa ili kuambukiza raia wa Urusi.

Alikuwa akishutumu Marekani kwa "kuandaa janga jipya kwa kutafuta mabadiliko ya virusi" na kupanga "kutekeleza kitendo cha uchochezi nchini Ukraine kwa kutumia vitu vyenye sumu na kisha kuilaumu Urusi."

Krylov alitoa madai yasiyo na msingi kuhusu maabara nyingi za kibayolojia alizodai Marekani ilikuwa ikijenga katika nchi mbalimbali za Umoja wa Kisovyeti wa zamani, na alishtumu Marekani kwa kuzuia uchunguzi kuhusu chanzo cha janga la Covid-19.

Alikuwa na tabia ya kutoa tuhuma nyingi.

Hakuna kamanda wa matawi ya majeshi ya Urusi aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari kama alivyofanya yeye.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, Igor Krylov alikuwa akipanga kufanya mkutano mwingine na waandishi wa habari siku aliyouawa.

Jenerali Igor Krylov alikuwa mbele ya jengo la makazi wakati kifaa kilichofichwa kwenye skuta kililipuliwa kwa mbali

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Jenerali Igor Krylov alikuwa mbele ya jengo la makazi wakati kifaa kilichofichwa kwenye skuta kililipuliwa kwa mbali

Hatima ya Putin kutokana na mkasa huu

Ukweli ni kwamba vyanzo vya kuaminika katika huduma ya ujasusi ya Ukraine vilikiri kuhusika na shambulizi hilo katikati ya mji mkuu wa Urusi inadhihirisha kujiamini kwao kuwa maajenti wao walifanikiwa kupata njia salama za kutoroka.

Huduma za ujasusi kwa kawaida huwa polepole kukubali kujihusisha na operesheni ili kuepuka kuongeza hatari kwa maajenti wao.

Mauaji ya jenerali yalifanyika siku moja baada ya mkutano wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi ambapo Rais Vladimir Putin na Waziri wa Ulinzi Andrei Belousov walizungumza kuhusu kuharakisha hatua ya jeshi la Urusi kuelekea ushindi katika vita na Ukraine.

Tukio hili pia lilitokea siku moja kabla ya kipindi cha kila mwaka cha Rais Putin cha "Direct Line" ambapo anatarajiwa kuwahakikishia raia wa Urusi kuwa mambo yanaenda vizuri na kuwa vikwazo vya Magharibi vitasaidia nchi kuendelea.

Stupak, afisa wa zamani wa ujasusi, alisema kuwa mauaji haya hayataathiri mwelekeo wa vita katika mstari wa mbele karibu na Pokrovsk, ambapo vikosi vya Urusi vinaendelea na mashambulizi - lakini yatafanya maneno ya Putin kuonekana kupoteza nguvu kwa raia wa Urusi na yanaweza kusababisha operesheni za kulipiza kisasi huko Kiev.

''Hili ni pigo kubwa zaidi kwa Urusi. Nafikiri maafisa wa huduma ya usalama wa Urusi hawatalala usiku huu, wakiulizwa mara kwa mara na wakuu wao: Jinsi gani jambo kama hili lilivyotokea Moscow?"

Mada zinazofanana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid