Ni nini kinachojulikana kuhusu kifo cha jenerali wa Urusi katika shambulio linalodaiwa kufanywa na Ukraine Moscow?

h

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock

Maelezo ya picha, Vyanzo vya habari mjini Kiev vinasema Ukraine imemuua jenerali wa Urusi Igor Kirillov, ambaye aliuawa katika mlipuko mjini Moscow mapema Jumanne.
Muda wa kusoma: Dakika 5

Jenerali wa ngazi ya juu wa jeshi la Urusi na msaidizi wake wameuawa katika mlipuko mjini Moscow.

Luteni Jenerali Igor Kirillov, mkuu wa vikosi vya nyuklia, biolojia na kemikali (NBC), alikuwa kwenye mlango wa kuingia kwenye makazi ya watu mapema Jumanne (17/12) wakati kifaa kilichofichwa kwenye pikipiki kilipolipuka na kumuua, kulingana na Uchunguzi ya Urusi ilivyosema.

Kifaa hicho kiliripuka kwa mbali na kilikuwa na milipuko yenye uzito wa gramu 300, vyanzo vya usalama vya Urusi vimeliambia shirika la habari la serikali la Tass.

Vyanzo vya BBC katika wizara ya usalama nchini Ukraine vinasema nchi hiyo ilihusika na operesheni ya kumuua Kirillov mjini Moscow.

Kulingana nao, Kirillov alikuwa "mlengwa halali" kwa kuwa alikuwa mhalifu wa vita ambaye alitoa amri ya kutumia silaha za kemikali zilizopigwa marufuku dhidi ya jeshi la Ukraine.

Siku ya Jumatatu, wizara ya usalama ya Ukraine, inayojulikana kwa kifupi SBU, ilimshtaki Kirillov bila ya kuwepo, ikisema kwenye Telegram kwamba "anawajibika kwa matumizi makubwa ya silaha za kemikali zilizopigwa marufuku." Serikali ya Ukraine bado haijatoa tamko rasmi kuhusu kifo cha jenerali huyo.

Tayari alikuwa amewekewa vikwazo kutoka Uingereza na nchi nyingine kwa jukumu lake katika matumizi ya silaha za kemikali za Urusi.

Kamati ya uchunguzi ya Urusi, kwa upande wake, iliyaelezea mauaji ya Luteni Jenerali kama "kitendo cha kigaidi."

"Tukio hilo liliainishwa kama kitendo cha kigaidi, mauaji, usafirishaji haramu wa silaha na risasi," msemaji wa kamati hiyo Svetlana Petrenko alisema.

Mlipuko

h

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Mlipuko huo uliripotiwa kufichwa ndani ya pikipiki ya umeme

Mlipuko huo ulitokea katika eneo la makazi kusini mashariki mwa Moscow, takriban maili 4 (kilomita 6.5) mashariki mwa Kremlin.

Picha kutoka eneo la tukio zilionyesha mlango wa jengo hilo ukiwa umeharibiwa vibaya, huku kuta na madirisha kadhaa yakivunjwa. Mifuko miwili ya mwiili pia inaweza kuonekana mitaani.

Wakazi wanaoishi karibu na eneo la mlipuko waliliambia shirika la habari la AFP kwamba awali walidhani kelele kubwa walizosikia zilitoka katika eneo la ujenzi.

Mwanafunzi Mikhail Mashkov, ambaye anaishi katika jengo lililo karibu na mlango, alisema aliamshwa na "mlipuko mkubwa sana", akifikiri "kitu kimeanguka kwenye eneo la ujenzi", kabla ya kuangalia nje.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Olga Bogomolova aliripoti, kwa upande wake, kwamba alidhani kontena kutoka eneo la ujenzi lilikuwa limeanguka, lakini baadaye aligundua kuwa "ulikuwa mlipuko mkubwa sana", aliona "dirisha lililovunjika" na kugundua kuwa lilikuwa kitu kingine.

Kamati ya uchunguzi ya Urusi imesema "imefungua kesi ya jinai kuchunguza mauaji ya wanajeshi wawili."

"Wapelelezi, wataalam wa uchunguzi na huduma za uendeshaji wanafanya kazi katika eneo la tukio," walisema.

"Vitendo vya uchunguzi na shughuli za utafutaji wa kiutendaji zinafanywa kwa lengo la kubaini mazingira yote ya uhalifu."

Mashirika ya habari ya serikali ya Urusi yameripoti kuwa kifaa hicho cha kulipuka - ambacho kilimuua Kirillov, aliyekuwa na umri wa miaka 54, na msaidizi wake katika mtaa wa Ryazansky - kilikuwa na nguvu ya kulipuka sawa na kilikuwa na ukubwa wa 300

Waliongeza kuwa wataalamu wa mabomu na mbwa wa kupekua walikagua eneo hilo na hakuna milipuko mingine iliyopatikana.

Mauaji yamefanyika nchini Urusi hapo awali, lakini mashambulizi mjini Moscow ni nadra sana.

Vikwazo vya matumizi ya silaha za kemikali

g

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kirillov, 54, amehudumu katika majukumu mbalimbali katika Jeshi la Urusi linalohusishwa na vifaa au zana hatari.

Mwezi Oktoba, Uingereza iliweka vikwazo dhidi ya Kirillov, ikisema alikuwa amesimamia matumizi ya silaha za kemikali nchini Ukraine na alifanya kazi kama "msemaji muhimu wa taarifa za Kremlin". Vikwazo hivyo ni pamoja na kufungiwa kwa mali na marufuku ya kusafiri. Pia aliwekewa vikwazo na Canada na New Zealand.

Ukraine imemtuhumu Kirillov kwa kufanya uhalifu wa kivita. Shirika hilo la usalama limesema Urusi imetumia silaha za kemikali zaidi ya mara 4,800 chini ya uongozi wa jenerali huyo tangu uvamizi kamili wa Urusi mnamo Februari 2022. Moscow imekanusha madai hayo.

"Uchunguzi wa kabla ya kesi unaendelea ili kuandika ukweli mwingine wa ukiukwaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu," Ukraine ilisema Jumatatu.

Mwezi Mei, Marekani iliishutumu Urusi kwa kutumia silaha za kemikali kama "kitendo cha vita" nchini Ukraine, na ukiukaji wa sheria za kimataifa zinazokataza matumizi yake.

Kulingana na Ukraine, vikosi vya Urusi vilitumia ndege zisizo na rubani kuangusha silaha za kemikali kwa wanajeshi wa Ukraine.

Kanali wa Ukraine Artem Vlasiuk awali alisema kuwa zaidi ya wanajeshi 2,000 wa Ukraine walikuwa wametibiwa hospitalini kwa sumu ya kemikali wakati wa vita, na kwamba watu watatu walikufa.

Kremlin ilipuuzilia mbali madai hayo wakati huo kuwa "yasiyo na msingi."

h

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Urusi imefungua kesi ya jinai kuhusiana na mauaji ya Luteni Jenerali Igor Kirillov

Igor Kirillov alikuwa nani?

Igor Kirillov alikuwa Jenerali wa ngazi ya juu wa Urusi, mkuu wa majeshi ya ulinzi wa nyuklia, biolojia na kemikali. Aliteuliwa kuongoza NBC mwezi Aprili 2017.

Jenerali huyo alijulikana kwa taarifa zake za ziada katika wizara ya ulinzi ya Urusi, ambayo ilipelekea wizara ya mambo ya nje ya Uingereza kumuita "msemaji mkuu wa taarifa za uongo za Kremlin."

Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la Tass, alihudhuria Shule ya Juu ya Jeshi la Kostroma ya Ulinzi wa Kemikali. Amehudumu katika nafasi mbalimbali katika Jeshi la Urusi linalohusishwa na vifaa hatari, ikiwa ni pamoja na Kurugenzi ya Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Mionzi, Kemikali na Biolojia.

Kifo cha Kirillov kimekuja chini ya wiki moja baada ya mtaalamu maarufu wa silaha za Urusi kupigwa risasi karibu na nyumba yake mjini Moscow.

Vyombo vya habari vya Ukraine vimeripoti kuwa mauaji ya Mikhail Shatsky yalifanywa na idara ya ujasusi ya kijeshi ya Ukraine.

imetafsiriwa n Dinah Gahamanyi