Video zilizohakikiwa zinavyoelezea jinsi kifo cha Igor Kirillov kilivyotokea

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Matt Murphy, Richard Irvine-Brown, Thomas Spencer & Joshua Cheetham
- Nafasi, BBC Verify
- Muda wa kusoma: Dakika 5
BBC Verify imekuwa ikichambua video na picha kutoka mitandao ya kijamii kutoka Moscow ili kujaribu kupata uhalisia wa picha wazi zaidi ya mlipuko uliomuua Jenerali Luteni Igor Kirillov wa Urusi na msaidizi wake.
Vyanzo vya habari Ukraine vinasema walifanya shambulio dhidi ya kamanda huyo wa juu, ambaye ni mkuu wa vikosi vya nyuklia, biolojia na kemikali (NBC} , nchini Urusi tangu 2017.
Alikuwa amewekewa vikwazo na Uingereza mwezi Oktoba na akakosolewa kama "kasuku katika habari za kupotosha kuhusu Kremlin".
Jenerali Luteni Kirillov alikuwa akiondoka katika jengo la kisasa la ghorofa katika sehemu ya kusini-mashariki ya Moscow mapema Jumanne wakati kifaa kilichofichwa kwenye skuta iliyoegeshwa kililipuka, kulingana na Kamati ya Uchunguzi ya Urusi - ambayo ni sawa kimamlaka na FBI ya Marekani.
Picha zilizothibitishwa na BBC Verify zinaonyesha watu wawili wakitoka kwenye jengo kabla ya mlipuko karibu na mlango.
Mavazi yao yana rangi ileile na yale ya maiti zilizopigwa picha baada ya mlipuko.
Skuta inaonekana ikiwa imeegeshwa kando ya mlango.
Hakuna kinachoonekana baada ya mlipuko, na picha zilizobaki zimefunikwa na vifusi kutoka kwa mlipuko.

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/SHUTTERSTOCK
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika video nyingine zilizochambuliwa na BBC Verify, mabaki ya skuta ya umeme yanaonekana yakiwa yameanguka kati ya vifusi na maiti mbili na mlango ulioharibiwa.
Picha ya karibu ya skuta, iliyothibitishwa kwa kulinganisha na vifusi, inaonyesha kuwa iko katika hali nzuri - isipokuwa sehemu ya usukani ambayo haionekani.
Wataalamu kutoka Janes - shirika la uchunguzi la binafsi linalotumia vyanzo wazi - waliliambia BBC Verify kwamba picha zinaonyesha kuwa mlipuko ulisababishwa na kilipuzi kilichotengenezwa kwa mkono (IED), badala ya silaha za kawaida.
"Kutoka kwa picha zilizopo za skuta, inaonekana kuwa bado iko kamili, hivyo athari inaonekana kuwa ni mivunjiko badala ya mlipuko mkubwa," alisema msemaji wa shirika hilo.
IED ni aina ya bomu "lililotengenezwa nyumbani" ambalo linaweza kuwa la aina mbalimbali na mara nyingi linatengenezwa na vifaa rahisi vinavyoweza kupatikana - kama vile misumari, kioo au vipande vya chuma - kulingana na Idara ya Usalama ya Marekani.
David Heathcote, meneja wa ujasusi kutoka kwa wachambuzi wa usalama McKenzie Intelligence, pia alikubali kuwa kifaa hicho kilionekana kuwa IED.
"IED zinaweza kutengenezwa kwa makusudi ili kuonekana kama kitu cha kila siku ambacho hakionekani kuwa cha ajabu," aliiambia BBC Verify. "Katika kisa hiki inaonekana kuwa kifaa kilifichwa ndani ya skuta, pengine kama kilipuzi kinachotumiwa na jeshi (lakini sio lazima) Semtex, badala ya kilipuzi cha kutengezewa nyumbani."
Aliongeza kuwa shambulio hilo linaonyesha "nguvu ya hali ya juu na linaweza kuwa limetayarishwa kwa miezi kadhaa," jambo ambalo lingehitaji "angalizo kubwa la mtu anayelengwa kabla ya shambulio."
Vyombo vya habari vya Urusi vimekuwa vikiripoti kuwa bomu lilikuwa limefungwa kwenye usukani wa skuta.

Chanzo cha picha, Telegram
Pia vyanzo vimeripoti, wakinukuu vyanzo vya vyombo vya usalama, kwamba mlipuko ulitengenezwa kwa kutumia njia ya kudhibiti kwa mbali.
Heathcote alikubaliana na tathmini hiyo, akisema kuwa ishara ya redio kutoka kwa simu au kifaa cha gari ingeweza kuwa kigezo cha mlipuko.
"Aliyetekeleza shambulizi atalazimika kuweka macho kwenye kifaa na atabonyeza kitufe ili kuanzisha mlipuko wakati mlengwa halali yupo karibu," aliiambia BBC Verify. "Ukaribu wa shambulio na kifaa unategemea ukaribu wa transimita inayotumika."
Vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vilisema mwanzoni kuwa Kifaa hicho kililipuka kwa mbali na kilikuwa na milipuko yenye uzito wa gramu 300, kisha baadaye kurekebisha takwimu hiyo hadi kilo 1, wakinukuu data kutoka kwa vyombo vya usalama.
Aliyeshuhudia mlipuko huo ameonyesha vyombo vya habari vya Urusi picha za kile alichosema ni vifusi vya mlipuko vilivyokuwa vimeanguka kwenye ghorofa yake inayozunguka mtaa wa tukio.
BBC Verify inaonyesha hizi kwa wataalamu wa silaha ili kusaidia kubaini kama vinaweza kuwa vimetoka kwa kifaa hicho.
Kwa mujibu wa wawekezaji, jengo la ghorofa alikouawa Jenerali Luteni Kirillov ni jipya na lilimalizika mwaka 2019.
Ghorofa hizo ni za kiwango cha juu, na baadhi zinapatikana kwa takribani paundi 153,540 mtandaoni.
Katika video zilizothibitishwa na BBC, kundi dogo linaonekana likikusanyika karibu na maiti, ambazo ziko kwenye eneo lililojaa theluji.
Magari ya huduma za dharura pia yanaonekana kwenye video.
Video zote mbili zilirekodiwa kwenye mtaa ukielekea kaskazini kuelekea Ryazansky Prospekt, Moscow, na kuibuka kwenye mitandao ya kijamii asubuhi ya Jumanne.
Zinaonyesha uharibifu katika mlango wa jengo, ikiwa ni pamoja na matofali kutawanyika na milango iliyofunguka, umbali kidogo kutoka kwa maiti.
Video nyingine imeonyesha mng'ao mkali kidogo kutoka kwenye kamera.
Nguvu ya mlipuko ilivunja theluji kutoka kwa magari yaliyoegeshwa karibu na jengo hilo.
Takriban ghorofa 10 nyingine kwenye mtaa huo wa mkasa zimeathiriwa na mlipuko, haya ni kwa mujibu wa mtandao wa Telegram wa Urusi Mash.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












