Shambulio la Moscow: Tunabainisha ukweli kuhusu madai ya Urusi kuhusu shambulio hilo

H
    • Author, Olga Robinson, Shayan Sardarizadeh & Paul Brown
    • Nafasi, BBC Verify

Urusi imekuwa ikiilaumu Ukraine mara kwa mara kwa shambulio baya katika ukumbi wa tamasha la Moscow wiki iliyopita, licha ya kundi la Islamic State (IS) kudai kuhusika na Ukraine kukanusha.

Kupitia taarifa za maafisa wa Urusi, ripoti za vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, BBC Verify inachunguza jinsi kampeni ya kuilaumu Kyiv ilivyofanyika.

Shutuma za awali

Shutuma zilitolewa mara tu baada ya ripoti za awali za shambulio la Jumba la Jiji la Crocus kuibuka kwenye mitandao ya kijamii siku ya Ijumaa.

Wanablogu kadhaa wanaoiunga mkono Kremlin wanaochapisha kwenye programu ya kutuma ujumbe Telegram walilaumu Ukraine kwa zaidi ya saa moja.

Mchambuzi anayeiunga mkono Urusi Sergey Markov, kwa mfano, alisema saa 1825 GMT washambuliaji walionekana kama "waislamu wenye itikadi kali", lakini akaongeza, bila ushahidi, kwamba shambulio hilo "linawezekana lilipangwa kutoka Kyiv".

Dakika 40 baadaye (1903 GMT), gazeti la kitaifa la Moskovsky Komsomolets, lilimnukuu mtaalamu wa kijeshi Roman Shkurlatov akisema huenda shambulio hilo lilipangwa kwa msaada wa Idara ya Usalama ya Ukraine na ujasusi wa kijeshi.

Na mnamo 1927 GMT, Rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev aliapa kulipiza kisasi ikiwa Ukraine ilihusika.

Madai bandia ya kuhusika

Saa chache baadaye, saa 2213 GMT, NTV, moja ya chaneli kuu za Runinga za Urusi, ilirusha kipande cha video, ikidai kwamba ilionesha afisa mkuu wa Ukraine akithibitisha kuhusika kwa nchi yake.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika video, Oleksiy Danilov anaonekana kusema: "Ni furaha huko Moscow leo, nadhani ni furaha sana. Ningependa kuamini kwamba tutapanga furaha hiyo mara nyingi zaidi."

Lakini BBC Verify imethibitisha kuwa kipande hicho cha video ni hariri ya mahojiano mawili ya TV ya Kiukreni yaliyotangazwa wiki iliyopita.

Zote mbili zinaweza kupatikana kwenye YouTube. Ya kwanza ni mahojiano na Danilov tarehe 19 Machi. Nyingine ilichapishwa siku tatu mapema na inamuangazia mkuu wa ujasusi wa kijeshi wa Ukraine, Kyrylo Budanov.

Nukuu ya Danilov ambayo inaonekana kwenye video ya NTV haiwezi kusikika katika mahojiano ya awali.

Uchambuzi wa sauti, uliofanywa kwa BBC Verify na Kikundi cha Utafiti wa Teknolojia ya Uchunguzi wa Juu katika Chuo Kikuu cha Liverpool John Moores, unasema sauti hiyo ilibadilishwa katika video ya NTV.

Pengo katika data ya masafa ya sauti inaonesha kuwa sauti imehaririwa.Hatahivyo, watafiti hawawezi kuwa na uhakika kwamba sauti ilitolewa na AI.

BBC Verify pia imepata habari iliyopachikwa katika faili ya sauti inayopendekeza kuwa imewekwa kupitia programu ya uhariri.

'Dirisha' la kuvuka

Rais Putin alisema washambuliaji hao walinaswa walipokuwa wakijaribu kukimbilia Ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images

Shutuma rasmi iliyotolewa katika hotuba ya Vladimir Putin siku ya Jumamosi.

Rais wa Urusi alisema washambuliaji walinaswa walipokuwa wakijaribu kukimbilia Ukraine, ambapo "dirisha la kuvuka mpaka lilitayarishwa kwa ajili yao".

Hata hivyo, Urusi haijawasilisha ushahidi wa "dirisha" kuruhusu washambuliaji kupitia.

Ingawa BBC Verify haiwezi kuthibitisha kwa kujitegemea ni wapi washukiwa walikuwa wakielekea, tumethibitisha video kadhaa na picha zao wakikamatwa. Na licha ya madai ya Putin, kukamatwa kwa watu hao kulifanyika mbali sana na mpaka wa Ukraine.

Kwa kulinganisha maelezo ya mazingira, tunajua washukiwa wawili waliokamatwa walirekodiwa katika takribani maili 90 (145km) kutoka mpaka wa Ukraine.

Wakati Ukraine imekanusha kuhusika kwa vyovyote vile, utekelezaji wa shambulio umedaiwa na kundi la Islamic State (IS) kupitia shirika lake la habari linalojiita Amaq.

Ushahidi unaoonekana, unaosambazwa na IS, ni pamoja na picha ya washambuliaji wanne wakiwa na nyuso zo zenye ukungu.

Maelezo mengi, kama vile vipengele vya ukumbi wa tamasha na bunduki zinazotumiwa na wavamizi zinalingana na video zilizoibuka mtandaoni wakati wa shambulio hilo.

Lakini pamoja na ushahidi, Urusi inaendelea kuishutumu Ukraine.

Margarita Simonyan, mhariri mkuu wa mtandao wa TV wa Urusi RT (hapo awali ulijulikana kama Russia Today), alisema kwenye X washambuliaji hawakutoka IS kwa sababu hawakuwa wamevaa fulana za kujitoa mhanga na "hawakuwa na nia ya kufa".

Lakini wakati IS imeonya mara kwa mara washambuliaji dhidi ya kukamatwa wakiwa hai, washambuliaji wa kundi hilo walitoroka hapo awali.

Kwa mfano, mwishoni mwa 2022 mmoja wa wapiganaji waliohusika katika shambulio kwenye hoteli huko Kabul alifanikiwa kutoroka na baadaye kutekeleza shambulio la kujitoa mhanga, kulingana na vyombo vya habari vya IS vilivyonukuliwa na BBC Monitoring.

Tunachojua kuhusu watuhumiwa

Washambuliaji waliendesha gari nyeupe aina ya Renault, ambayo inalingana na gari lililoonekana kwenye video tofauti iliyotumiwa wakati wa kukimbia kutoka eneo la ukumbi wa tamasha, kabla ya kuzuiliwa.

Kulingana na naibu wa Jimbo la Duma la Urusi Alexander Khinshtein, mwanaume mmoja alikamatwa karibu na gari hilo, huku wengine watatu wakikimbilia msituni karibu na kuzuiliwa kufuatia msako.

Silaha na pasipoti za Tajik zilipatikana kutoka kwenye Renault, Bw Khinshtein aliongeza.

Siku ya Jumapili, picha zilichapishwa za wanaume hao wakisindikizwa katika mahakama ya Moscow. Waliitwa na mamlaka ya Urusi kama: Dalerdzhon Mirzoyev, Saidakrami Murodali Rachabalizoda, Shamsidin Fariduni na Muhammadsobir Fayzov.

IS ilitoa video inayowaonesha washambuliaji hao wanne wakiwa na nyuso zao kuwa na ukungu

Chanzo cha picha, AMAQ

Katika picha iliyotolewa na IS, watatu kati ya washukiwa hao wanaonekana wakiwa wamevalia t-shirt ya rangi ya kahawia, fulana ya kijani kibichi na polo ya kijivu.

Shati hizi zinaonekana kufanana na zile zilizovaliwa na washukiwa watatu wakati wa kukamatwa kwao.

Kwa mfano, nembo mbili kwenye fulana ya rangi ya kahawia isiyokolea inayovaliwa na mtu anayeitwa Rachabalizoda pia zinaonekana kwenye video iliyotolewa na IS. Pia anajitambulisha kwa jina moja wakati wa mahojiano yaliyofuata.

Mshukiwa Mirzoyev, ambaye shati lake halionekani kwenye picha ya IS, alizuiliwa akiwa amevalia shati la mikono mirefu ya kijani, jeans ya bluu na mkanda mweusi. Nguo hizi tatu ilivaliwa na mtu mwenye bunduki kwenye video ya IS.

Je, madai ya IS ya kuhusika ni ya kweli kwa kiasi gani?

Kuwepo kwa video yenye picha za hali ya juu iliyorekodiwa na washambuliaji wakati wa kutekeleza mauaji hayo, matumizi yao ya kauli mbiu zilizozoeleka miongoni mwa washambuliaji wa IS kwenye video hiyo, na usambazaji wake kupitia chaneli rasmi za vyombo vya habari vya IS ni sawa na utaratibu wa kundi hilo.

Maelezo ya video, Washukiwa wa shambulio la ukumbi wa tamasha la Urusi wakifikishwa katika mahakama ya Moscow

Picha ya mmoja wa washambuliaji ndani ya Jumba la Jiji la Crocus zaidi ya wiki mbili kabla ya shambulio hilo imechapishwa na vyombo vya habari vya Urusi, ikionesha kuwa ilikuwa imepangwa mapema.

IS mara nyingi husubiri uthibitisho wa hatima ya washambuliaji kabla ya kutoa madai. Mshambuliaji akifa, huzuia mashirika ya kijasusi kutoa taarifa.

Kwa hivyo madai ya kuhusika wakati wahalifu walikuwa bado wapo si ya kawaida, na inaonesha nia ya IS kuthibitisha jukumu lake.

Hii sio mara ya kwanza kwa IS kulenga Urusi. Mashambulizi mengine mawili makubwa yalitokea mwaka wa 2015 na 2018, pamoja na mashambulizi mengine ya katika miaka ya hivi karibuni.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga