Meli za kijeshi za Urusi zimeondoka katika kambi ya Syria huku kukiwa na shaka juu ya siku zijazo

sd

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kambi ya jeshi la wana maji Tarto imekuwa ni muhimu kwa nguvu za Urusi katika eneo hilo
    • Author, Matt Murphy & Josh Cheetham
    • Nafasi, BBC News World
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Vyombo vya majini vya Urusi vinaonekana vimeondoka kwa muda katika bandari yao kuu nchini Syria, picha za satelaiti zilizokaguliwa na BBC Verify zinaonyesha hilo, huku kukiwa na sintofahamu kuhusu mustakabali wa kijeshi wa Moscow nchini humo baada ya kuanguka kwa mshirika wake, Bashar al-Assad.

Picha zilizochukuliwa na Maxar tarehe 10 Disemba zinaonyesha baadhi ya meli zimeondoka kwenye kambi ya wanamaji ya Tartous tangu Jumapili na kwa sasa zimekaa nje ya bandari katika Bahari ya Mediterania.

Wakati huo huo, picha nyingine zilizopigwa siku hiyo hiyo zinaonyesha shughuli zikiendelea katika kambi kuu ya anga ya Urusi nchini Syria, Hmeimim, ndege zikionekana kwenye lami.

Siku ya Jumatatu, msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov alisema Moscow itaingia katika mazungumzo na serikali mpya kuhusu uwepo wa jeshi la Urusi katika siku zijazo.

"Kila kinachowezekana kinafanyika ili kuwasiliana na wale wanaohusika katika kuhakikisha usalama na, bila shaka, jeshi letu pia linachukua tahadhari zote muhimu," aliwaambia waandishi wa habari huko Moscow.

Hapo awali alisema ni "mapema" kutafakari juu ya mustakabali wa kambi hizo.

"Tunafanya mawasiliano na wale wanaoidhibiti Syria kwa sasa. Hilo ni muhimu kwa sababu tuna kambi zetu huko na ofisi yetu ya kidiplomasia [ubalozi]. Na bila shaka, kuhakikisha usalama wa vituo vyetu ni muhimu sana," aliwaambia waandishi wa habari.

Kambi ya Tartous

fd

Chanzo cha picha, Maxar/BBC

Kambi ya jeshi la majini ya Tartous ni kambi ya kikosi cha Bahari Nyeusi na ndio kambi pekee ya ukarabati na ujazaji mafuta ya Urusi katika Bahari ya Mediterania. Ilianzishwa na Umoja wa Kisovieti katika miaka ya 1970, ikapanuliwa na kufanywa ya kisasa na Urusi mwaka 2012 – pale Kremlin ilipoanza kuongeza uungaji mkono wake kwa serikali ya Rais Assad.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kambi hiyo inaziruhusu meli za Urusi kubaki katika Mediterania bila kulazimika kurudi kwenye bandari katika Bahari Nyeusi kupitia Mlango-Bahari wa Uturuki. Pia ni bandari yenye kina kirefu cha maji, kumaanisha inaweza kuwa na nyambizi za nyuklia za Moscow, kulingana na Taasisi ya Wanamaji ya Marekani.

Picha mpya za satelaiti zinaonyesha Moscow imeziondoa meli zake za kivita nje ya bandari kwa muda, umbali wa kilomita 13 (maili nane) kutoka pwani ya Syria.

Haijulikani ikiwa kuondoka kwao ni sehemu ya kujiondoa kwa kudumu kutoka Tartous au la. Katika wiki za hivi karibuni, picha za satelaiti zimeonyesha meli za Urusi zikiingia na kutoka bandarini.

Mike Plunkett mchambuzi wa masuala ya usalama katika shirika la Janes, anabainisha kuwa ingia toka ya meli za Urusi "ilifanywa ili kuhakikisha meli zao haziwezi kushambuliwa."

"Haijuulikana ikiwa walikuwa na wasiwasi kuhusu mashambulizi kutoka kwa waasi wa Syria au uharibifu kutokana na mashambulizi yoyote ya Israel dhidi ya mali za Syria huko Tartus," aliongeza.

Frederik Van Lokeren, nahodha wa zamani wa jeshi la wanamaji la Ubelgiji na mchambuzi, aliiambia BBC Verify, inaonekana meli za Urusi sasa ziko katika hali ya kusubiri huku Moscow ikijadili kuhusu hatua yake inayofuata.

"Wako katika hali ya sintofahamu kwa sasa, kwa sababu hawajui kabisa kitakachotokea," anasema Bw. Van Lokeren.

"Ni wazi, kwa kuwa wanakawia kuondoka, inaonekana Urusi haiko tayari kuondoa meli zake zote nje ya eneo hilo, na hilo linaweza kuwa ishara kwamba wanajadiliana na washirika wa kikanda ili kuona ni wapi wanaweza kupeleka meli hizi."

Wachambuzi wanasema ikiwa Urusi italazimika kufunga kambi ya Tartous, inaweza kuzipeleka meli hizo huko Tobruk nchini Libya. Eneo hilo linadhibitiwa na Marshal Khalifa Haftar anayeungwa mkono na Kremlin na tayari kuna kambi za ndege za Urusi.

Lakini kujiondoa Tartous kutakuwa na gharama kubwa, na Van Lokeren anasema hatua hiyo pia italeta meli za Urusi karibu na kambi za Nato, na kuzifanya ziwe rahisi kufuatiliwa. Kwa sasa, anasema, hakuna dalili kwamba Urusi inahamisha vifaa ili kujiondoa Tartous.

Kambi ya Hmeimim

DFC

Chanzo cha picha, Maxar/BBC

Tangu 2015 kambi ya anga ya Hmeimim imekuwa sehemu muhimu ya operesheni za Urusi kote Mashariki ya Kati na Afrika. Imetumika kufanya mashambulizi ya anga katika miji kote Syria kuunga mkono utawala wa Assad, huku pia ikitumika kusafirisha wakandarasi wa kijeshi hadi Afrika.

Picha za satelaiti zilizokaguliwa na BBC Verify zinaonyesha kuna ndege mbili kubwa - zilizotambuliwa na Janes kama ndege za usafiri za IL-76 - zikiwa bado zimekaa kwenye lami kwenye kambi hiyo Disemba 10. Helikopta pia imeonekana kwenye picha hiyo.

Janes inabainisha kuwa mifumo ya ulinzi wa anga kwenye kambi hiyo bado inaonekana katika kona ya kaskazini-magharibi.

Dara Massicot, mchambuzi katika Shirika la Carnegie kwa ajili ya Amani ya Kimataifa, anasema uhamishaji katika kambi ya anga utahusisha ndege kubwa na nyingi zaidi kuliko zile zinazoonekana kwenye picha za satelaiti, na kupendekeza kuwa Moscow haina mpango wa kuhama mara moja.

"Wakati majeshi ya Urusi yalipotumwa Syria 2015, kulikuwa na safari za ndege kubwa karibu 300 katika wiki mbili, na hiyo ilikuwa kabla ya upanuzi wa kambi hiyo," aliandika kwenye X.

Licha ya Urusi kuonekana kuendelea kubaki eneo hilo, lakini kuanguka kwa utawala wa Assad kunawakilisha pigo kubwa kwa matarajio ya Kremlin katika eneo hilo. Wakati wa ziara ya 2017 katika kituo cha anga cha Khmeimim, Rais Vladimir Putin aliweka wazi kwamba anakusudia uwepo wa Moscow uwe mradi wa muda mrefu.

Akitafakari juu ya hali hiyo, mwanablogu mashuhuri wa kijeshi anayeunga mkono Kremlin, Rybar alionya kwenye Telegram kwamba uwepo katika eneo hilo ni hatari kubwa.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla