Je, Ukraine inaweza kumudu mwaka mwingine wa vita na Urusi?

FD
Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Ukraine
    • Author, Jonathan Beale
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Ukraine inapoteza ardhi yake katika vita. Wanajeshi wake wengi wamechoka baada ya miaka mitatu ya mapigano. Swali ni ikiwa nchi hii inaweza kustahimili mwaka mwingine wa vita?

Vikosi vya Ukraine vinavyopigana na Urusi huko mashariki, vinakaribia kuzingirwa katika mji wa Korakhove, ambao umekuwa eneo la mapigano makali katika wiki za hivi karibuni.

Kikosi cha "Black Pack" kinajaribu kuvizuia vikosi vya Urusi, ili visiuzingire mji wa Korakhove. Warusi wanakuja kutoka pand tatu.

Surtees, kamanda wa kikosi hiki mwenye umri wa miaka 31, alijiunga na jeshi baada ya uvamizi wa Urusi. Anasema mwanzoni alifikiri vita hivyo vingedumu kwa miaka mitatu. Lakini sasa anajitayarisha kiakili kwa miaka mingine kumi ya kupigana.

Wanafahamu nia ya Donald Trump ya kumaliza vita. Volodymyr Zelensky na Putin pia wametangaza utayari wao kwa mazungumzo, lakini inaonekana ni vigumu kufikiria makubaliano yanayotekelezeka.

Pia unaweza kusoma

"Vita viendelee"

T
Maelezo ya picha, Surtees anasema ana wasiwasi kuhusu matokeo ya mazungumzo ya amani

Ninapomuuliza kama anapendelea mazungumzo au kuendelea na vita, Surtees anajibu kwa uthabiti: "Kuendelea na vita."

Huu ni mtazamo ambao wanachama wengi wa kikosi chake wanao. Serhi, mpishi wa kundi hilo, anaamini mazungumzo hayo yatasimamisha vita kwa muda tu, "mzozo utaanza tena mwaka mmoja au miwili ijayo."

Anakubali kwamba hali ya sasa "si nzuri" kwa Ukraine. Lakini pia yuko tayari kuendelea na vita. Serhi anasema kuuawa ni "ni sehemu ya kazi."

David, mwimbaji katika kikosi hicho, anaamini kuwa Trump hatabiriki. "Trump anaweza kuwa mzuri sana au mbaya sana kwa Ukraine," anasema.

Kikosi hiki hupigana kwenye mstari wa mbele wiki moja na kupumzika wiki nyingine. Lakini wanaendelea na mazoezi hata wakiwa wamepumzika kwa sababu wanaamini yatawafanya kuwa na ari.

"Hatuwezi kuendelea na vita kwa miaka mingi"

TR
Maelezo ya picha, Dennis amejiunga na kikosi hiki kwa hiari kutoka Ujerumani

Dennis alijiunga na kikosi hiki hivi karibuni. Kwa hiari yake aliacha nyumba yake salama nchini Ujerumani na kujiunga na kundi hili.

"Nilijiuliza - ninaweza kuishi katika ulimwengu ambao Ukraine haipo?" Denis anakiri kwa huzuni kwamba Ukraine sasa inaonekana kushindwa, lakini anaongeza: "Ikiwa hatutajaribu, bila shaka tutashindwa. "Angalau nitakufa nikijaribu kupata ushindi, sio kukata tamaa na kukubali kushindwa."

Lakini tofauti na wengine, Denis anaamini Ukraine inapaswa kufikiria usitishwaji wa mapigano. Anaamini majeruhi kwa upande wa Ukraine ni wengi zaidi kuliko takwimu rasmi, ambazo zinasema ni zaidi ya 400 elfu waliokufa na kujeruhiwa.

"Nadhani askari wengi wameuawa au wamechoka sana," anasema. "Suala sio kwamba tunataka kusitishwa kwa mapigano, lakini ukweli ni kwamba hatuwezi kuendeleza na vita hivi kwa miaka mingi."

Umma unataka nini?

DFC
Maelezo ya picha, Maisha yanaendelea huko Dnipro
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Dnipro, jiji la tatu kwa ukubwa nchini Ukraine. Mji huu unalengwa mara kwa mara na makombora ya Urusi na droni. Ving'ora vinasikika mara kwa mara mchana na usiku. Katika wakati wa utulivu, Waukraine huenda kwenye ukumbi wa michezo.

Katika onyesho la alasiri ya leo ni onyesho la vichekesho liitwalo "Kaidash Family," bado kuna dalili ya vita. Kimya cha dakika moja kuwakumbuka waliokufa, na kufuatiwa na wimbo wa taifa wa Ukraine.

Ludmila anasema. "Tunapokea misaada, lakini haitoshi - ndiyo maana inatubidi tuketi kwenye meza ya mazungumzo."

"Hakuna suluhisho rahisi," anasema Ksenia. "Wanajeshi wetu wengi wameuawa. Walipigana kwa sababu moja - kuilinda ardhi yetu. Lakini nataka vita hivi viishe."

Tafiti pia zinaonyesha umma unataka mazungumzo ya amani.

Maombi mengi ya kusitisha mapigano yanatoka kwa wale ambao wamelazimika kukimbia maeneo ya vita. Katika makazi karibu na jumba la maonyesho, ambalo hapo awali lilikuwa bweni la wanafunzi, kikundi cha wanawake wazee wanne wanakumbuka nyumba walizoacha.

Valentina, mwanamke mwenye umri wa miaka 87, anasema walikuja hapa mikono mitupu, lakini wamepewa viatu, nguo na chakula. "Ni vizuri kuwa mgeni, lakini ni bora kuwa nyumbani," anasema.

dfv
Maelezo ya picha, Valentina na Maria wameacha nyumba zao katika maeneo ambayo sasa yanadhibitiwa na Urusi

Nyumba yake sasa iko katika eneo linalokaliwa na Urusi. Wanawake wote wanne wanataka mazungumzo ya amani. Lakini Maria, 89, anasema: "Sijui jinsi pande hizi mbili zinavyoweza kutazamana machoni baada ya moto huu mbaya waliousababisha."

"Sasa ni wazi kwamba hakuna upande unaoweza kushinda kijeshi, ndiyo maana tunahitaji mazungumzo," aliongeza.

Ikiwa mazungumzo ya amani yatafanyika, wanawake hawa wanaweza kulipa gharama kubwa zaidi - kwani Ukraine inaweza kulazimika kutoa baadhi ya maeneo yake ili kufikia amani.