Rais Museveni azungumzia kuzuiliwa kwa Besigye

Museveni amesisitiza kwamba uwajibikaji lazima uwe kipaumbele badala ya maoni ya kisiasa.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri.

  2. Waingereza washtakiwa kwa ujasusi nchini Iran

    .

    Chanzo cha picha, Familia

    Waingereza waliozuiliwa Craig na Lindsay Foreman wameshtakiwa nchini Iran kwa kosa la ujasusi, shirika la habari la mahakama nchini humo limesema.

    Bw na Bi Foreman walikamatwa mwezi Januari lakini habari za kuzuiliwa kwao, kwa tuhuma za usalama ambazo hazijatajwa, ziliibuka wiki iliyopita.

    Msemaji wa mahakama Asghar Jahangir alisema kwamba wanandoa hao, wote wenye umri wa miaka 52, "waliingia Iran kwa kisingizio cha kutalii" na "kukusanya habari katika mikoa mingi ya nchi".

    Wawili hao walihama kutoka East Sussex na kuanza maisha mapya huko Andalucia, Uhispania, mnamo 2019 na walikuwa wamejitokeza kwenye kipindi cha Channel 4's A New Life in the Sun mnamo 2022 ili kuonyesha maisha yao kama wahamiaji.

    Wenzi hao walikuwa wamesafiri kwa pikipiki kuzunguka ulimwengu na walikuwa wamepanga kukaa Iran kwa siku tano.

    Bw na Bi Foreman walikuwa wakielekea Australia katika safari yao duniani kote na walikuwa wamevuka Iran kutoka Armenia tarehe 30 Desemba na walikuwa wakipanga kuwa Pakistan ifikapo tarehe 4 Januari.

    Katika msururu wa ujumbe kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kuzuiliwa, wenzi hao walielezea furaha yao ya kuwa Iran.

    Lindsay Foreman, aliye na shahada ya udaktari katika saikolojia, alisema "alikuwa na wakati mzuri sana".

    Mumewe Craig, ambaye ni seremala, alizungumza kuhusu "watu wa kupendeza" kwenye "nchi inayovutia".

  3. Mazungumzo ya Marekani-Urusi yapiga 'hatua ya kwanza' katika safari ndefu na ngumu ya kumaliza vita vya Ukraine - Rubio

    .

    Chanzo cha picha, RUSSIAN FOREIGN MINISTRY PRESS/HANDOUT/EPA-EFE/REX/Shutterstock

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov, ambaye alikuwa sehemu ya ujumbe wa Riyadh, ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba Urusi na Marekani zimekubaliana kuweka mazingira ya kurejesha ushirikiano kikamilifu kati ya mataifa hayo mawili.

    Katika mkutano wa wanahabari, waziri wa Marekani Marco Rubio huko Riyadh mapema alasiri hii - alikuwa akizungumza pamoja na mjumbe wa Mashariki ya Kati Steve Witkoff na mshauri wa usalama wa kitaifa Mike Waltz.

    "Lengo la mkutano wa leo" lilikuwa kufuatilia mazungumzo ya simu ya Rais wa Marekani, Donald Trump na Rais wa Urusi Vladimir Putin wiki iliyopita.

    Rubio alikuwa na "uhakika" kuwa Urusi ilikuwa "tayari kuanza mazungumzo yenye tija" kumaliza mzozo wa Ukraine.

    Soma zaidi:

  4. Bei za chakula zapanda ghafla katika mji wa Bukavu

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Na Alfred Lasteck

    BBC, Nairobi

    Bei ya Vyakula zinaelezwa kupanda kwa kasi katika jiji la Bukavu, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, baada ya waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda kuliteka jiji hilo wiki iliyopita.

    Kupanda kwa ghafla kwa bei za bidhaa kunahusishwa na uporaji mkubwa wa maduka, masoko na maghala ya mashirika ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu.

    Hata hivyo waasi wa M23 wanaripotiwa kuanza kuelekea maeneo mengine baada ya kuteka jiji la Bukavu, ambao ni mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kusini. Wiki chache zilizopita walishika udhibiti wa jiji lenye utajiri wa madini la Goma, katika Jimbo la Kivu Kaskazini mashariki ya Congo.

    Wakazi wa Bukavu wameiambia BBC kuwa masoko mengi hayana vyakula, lakini hata kile kinachopatikana ni kwa bei ya juu.

    Mkazi mmoja alisema, “Wengi wetu hatuwezi kutoka nje ya nyumba, bado kuna hofu, lakini pia bei za chakula zimepanda kwa sababu ya uporaji na uharibifu wa maduka na masoko hivi karibuni...

    "...katika muda wa siku tatu tu, kila kitu kimepanda mara tatu ya bei ya kawaida. maharagwe yalikuwa yakiuzwa kuanzia faranga 3,000 (pauni 0.83), sasa ni faranga 12,000 (pauni 3.32). Alhamisi iliyopita sukari iliuzwa faranga 500 (pauni 0.14), sasa ni faranga 12,000 (pauni 3.32). Hali ni mbaya sana hapa,” alisema mkazi huyo.

    Pia alisema kuwa tangu mapigano yalipoanza Goma, watoto wake na wengine wengi katika kijiji chao hawajaenda shule.

    Mfanyabiashara mmoja katika mji huo alisema karibu kila kitu kilichokuwa dukani kwake kiliibiwa na kilichobaki kwa udogo ni bidhaa zisizo za chakula.

    Kutokana na mapigano yaliyotokea mwishoni mwa wiki, benki zote mjini Bukavu zimefungwa.

    Jumatatu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lililaani uporaji wa tani 7,000 za chakula cha msaada mjini Bukavu.

    Soma zaidi:

  5. Baadhi ya wanajeshi wa Israeli wasalia Lebanon baada ya muda wa mwisho wa kuondoka

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Israel imeondoa vikosi vyake kutoka kusini mwa Lebanon isipokuwa katika maeneo Matano pekee, shirika la habari la serikali ya Lebanon linasema.

    Kujiondoa kwa Israel ni sehemu muhimu ya usitishaji mapigano uliomaliza mzozo wa mwaka mzima na wapiganaji wa Kishia wa Hezbollah.

    Mawaziri wa Israel walisema baadhi ya wanajeshi watasalia ndani ya Lebanon ili kulinda jamii za kaskazini mwa Israel.

    Ikijibu, Lebanon ilisema Israeli lazima ijiondoe kabisa. Ilisema itachukulia "kuendelea kuwepo kwa Israeli katika eneo lolote la ardhi ya Lebanon kama uvamizi".

    Usitishaji vita unaitaka Israeli iondoke na jeshi la Lebanon kuchukua nafasi ya makundi yote yenye silaha kusini mwa Mto Litani, yapata kilomita 30 kaskazini mwa Israeli.

    Hezbollah ndiyo ilikuwa yenye nguvu kubwa katika eneo hilo kwa miongo kadhaa, lakini iliharibiwa vibaya katika mzozo huo, ambao ulikuwa mbaya zaidi kupigana na Israeli tangu kundi hilo la wanamgambo kuanzishwa mwaka 1982.

    Mamlaka ya Lebanon inasema zaidi ya watu 3,960 - wengi wao raia - waliuawa wakati wa uhasama, na wengine milioni moja walifukuzwa kutoka maeneo ambayo Hezbollah ilikuwa na uwepo mkubwa.

    Mamlaka ya Israel inasema zaidi ya wanajeshi 80 wa Israeli na raia 47 waliuawa. Takriban raia 60,000 walitimuliwa kutoka kaskazini mwa Israel.

    Wengi wa wale waliokimbia makazi yao nchini Lebanon wamerejea nyumbani, Umoja wa Mataifa unasema, wakati ni wachache tu kati ya wale waliokimbia makazi yao nchini Israeli wamefanya hivyo, kulingana na ripoti.

    Soma zaidi:

  6. Wanakijiji wauawa huko Sudan, wanaharakati wanasema

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Zaidi ya raia 200 wasiokuwa na silaha wameuawa katika vijiji kadhaa nchini Sudan kwa muda wa siku tatu na kikosi cha kijeshi cha Rapid Support Forces (RSF) ambacho kinahusika katika mzozo wa kikatili na wanajeshi, shirika la kutetea haki za binadamu la eneo hilo limesema.

    Mtandao wa Wanasheria wa Dharura ulisema mashambulizi hayo yalitokea al-Kadaris na al-Khelwat kuelekea kaskazini mwa jimbo la White Nile - maeneo ambayo wanajeshi hawakuwapo.

    Wapiganaji wa RSF walihusika na visa vya watu "kunyongwa, utekaji nyara, raia kupotea na uporaji wa mali", mtandao huo uliongeza.

    RSF, ambayo ilishirikiana na jeshi kabla ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuanza Aprili 2023, haijatoa maoni yoyote kuhusu madai hayo.

    Wawili hao walikuwa wameingia madarakani pamoja katika mapinduzi - lakini walitofautiana kuhusu mpango unaoungwa mkono kimataifa kuelekea utawala wa kiraia.

    Baadhi ya viongozi wakuu wa RSF kwa sasa wako nchini Kenya ambapo wanatarajiwa kutangaza mipango ya kuunda serikali yao katika maeneo wanayodhibiti.

    Wachambuzi wanaonya kuwa hatua hiyo inaweza kuzidisha mgawanyiko nchini Sudan.

    Soma zaidi:

  7. RSF na washirika wake kusaini makubaliano ya kuanzisha utawala pinzani

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Gen Mohamed Hamdan Dagalo (kushoto) na Gen Abdel Fattah al-Burhan (kulia) wote wanaongoza vikosi vyenye nguvu

    Vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) vinasema itasaini makubaliano ya kisiasa na vikundi vya kisiasa vya washirika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, siku ya Ijumaa.

    Vikundi hivyo vimekusanyika ili kurasimisha "Makubaliano ya kisiasa kwa ajili ya Serikali ya Amani na Umoja", ambayo wanasema itawezesha kuunda serikali sawia katika maeneo yanayodhibitiwa na RSF.

    Mshauri wa kisiasa wa RSF Basha Tabiq alithibitisha kwenye mtandao wa X, "shughuli za hafla hiyo zilianza mnamo Februari 18 na zitaendelea kwa siku mbili, na makubaliano ya kisiasa kusainiwa siku ya mwisho, yatakayojumuisha ushiriki na uwepo muhimu wa kidiplomasia na kimataifa."

    Ushirikiano huo ni pamoja na vikundi vya raia wa Sudan, kisiasa na wenye silaha, ambao wanataka kuanzisha "serikali ya amani na umoja" katika mikoa inayodhibitiwa na RSF.

    Vikundi muhimu, kama vile Sudan Revolutionary Front (SRF), muungano wa vikundi vya zamani vya waasi vya Darfur, na washiriki wa zamani wa serikali ya kiraia waliopinduliwa na mapinduzi ya kijeshi ya 2021, wanahusika.

    Hata hivyo, Sudan National Umma Party (NUP), moja ya vyama vya zamani vya siasa nchini humo, vimepinga hatua hiyo.

    Serikali ya Kenya imekosolewa kwa kuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo.

    Mkuu wa Jeshi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, amelaani hatua hiyo.

    Shinikizo la RSF kuwa na serikali pinzani kunasababisha wasiwasi juu ya kutokuwa na utulivu wa muda mrefu na mgawanyiko zaidi nchini Sudan, ambao umeingizwa katika vurugu na machafuko ya kisiasa tangu mzozo huo ulipoanza Aprili 2023.

    Soma zaidi:

  8. Rais Museveni azungumzia kuzuiliwa kwa Besigye na hali yake ya afya

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais Yoweri Museveni ameangazia suala la kukamatwa na kuzuiliwa kwa kiongozi wa upinzani Dr. Kizza Besigye, na kusisitiza kuwa lile ambalo linafaa kupewa kipaumbele ni hukumu itolewe kwa haraka wala sio suala la miito ya maridhiano au msamaha.

    Museveni alisisitiza kwamba uwajibikaji lazima uwe kipaumbele badala ya maoni ya kisiasa.

    "Nimeona wasiwasi wa Waganda juu ya kuzuiliwa kwa Dk. Besigye kwa makosa makubwa ambayo anadaiwa alikuwa amepanga," alisema Museveni.

    ‘’Ikiwa unataka nchi thabiti, swali sahihi zaidi linapaswa kuwa: Kwa nini Dk. Besiggye alikamatwa?’’ Museveni alisema. Jibu la hilo ni kesi yake imalizwe kwa haraka ili ukweli ujitokeze.’’

    Museveni aliendelea kwenye taarifa yake na kusema kuwa, ‘’vinginevyo, itakuwa kuendeleza ukosefu wa usalama ambao ni hatari sana kwa nchi.’’

    Kuhusiana na afya ya mwanasiasa Kizza Besigye, Rais Museveni amesema kuwa kuna hospitali ya umma gerezani na kuwa wahudumu wa afya wa kibinafsi wa Kizza Besigye wamekuwa wakimtembelea na kuongeza kuwa ikiwa kuna haja ya huduma yoyote ya ziada ya matibabu, serikali itashauriwa.

    ‘’Katika hili, Dk Besigye, alikuwa kwenye mgomo wa kutokula. Hiyo ni sehemu ya sababu ya yeye kuwa dhaifu kunakoonekana kwenye picha zilizoko magazeti. Je! huo sio ulaghai usio na msingi?''

    Haya yanajiri baada ya familia ya Besigye kuibua wasiwasi kufuatia kupokea ujumbe kutoka idara ya magereza ya Uganda iikiitaka familia hiyo itume daktari binafsi wa Besigye.

    Kupitia mtandao wa kijamii wa X mbunge wa Buhweju nchini Uganda, Francis Mwijukye alifafanua kwamba Besigye aliyekuwa akitumia kiti cha magurudumu alipelekwa kwenye hospitali iliyoko kwenye jengo la kibiashara linaloitwa Bugolobi village Mall.

    Mwanasiasa huyu amewekwa gerezani baada ya kusomewa mashtaka ya kumiliki silaha katika mahakama ya kijeshi ya Uganda.

    Katika taarifa ya leo, Museveni amezungumzia kucheleweshwa kwa kesi ya Besigye amayo imehamishwa kutoka mahakama ya kijeshi hadi ya kiraia.

    ‘’Ni nani anayechelewsha kesi? Mahakama ndio uliogundua mapungufu katika mahakama ya kijeshi na wakaagiza kuhamishwa kwa kesi hiyo hadi Mahakama za Kiraia,’’ Museveni alisema.

    Besigye, aliyekuwa daktari wa binafsi wa Rais Yoweri Museveni, alikamatwa katika mazingira ya kutatanisha mnamo mwezi Novemba mwaka jana jijini Nairobi pamoja na msaidizi wake wa kisiasa, Obeid Lutale.

    Soma zaidi:

  9. Ukraine yatikiswa na shambulizi la usiku kucha

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Usiku wa kuamkia leo, vikosi vya ulinzi vya anga vilidungua ndege 103 kati ya 176 zilizorushwa na Urusi, Jeshi la Wanahewa la Ukraine linasema.

    Zilidunguliwa katika mikoa kadhaa, ikiwa ni pamoja na Kyiv, ambapo moshi ulionekana ukipanda juu ya jiji.

    Siku ya Jumatatu jioni, wakaazi wa Kyiv waliagizwa na meya kujilinda.

    Uharibifu uliripotiwa huko Kirovohrad, Kharkiv, Kyiv na Cherkasy.

    Ndege nyingine zisizo na rubani 67 zilipotea kwenye anga, jeshi la anga linaongeza.

    Soma zaidi:

  10. 'Alikufa kwa kuiba chokoleti': Wapakistani wajawa na ghadhabu kwa kifo cha mjakazi mtoto

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wanandoa kaskazini-mashariki mwa Pakistan wamezuiliwa kwa madai ya kumuua msichana wa miaka 13 ambaye aliwafanya kazi kama mjakazi, kwa madai kuwa ameiba chokoleti.

    Msichana huyo aliyefahamika kwa jina moja tu, Iqra, alifariki dunia kutokana na majeraha mengi katika hospitali hiyo Jumatano iliyopita. Uchunguzi wa awali wa polisi ulisema aliteswa.

    Kisa hicho kilichotokea Rawalpindi kimezua hasira na ujumbe mwingi wa alama ya reli #JusticeforIqra ukiwa na makumi ya maelfu ya maoni, na kusababisha mijadala kuhusu ajira ya watoto na unyanyasaji wa wafanyikazi majumbani.

    Sheria zinazohusiana na ajira ya watoto zinaweza kutofautiana nchi hadi nchi, lakini watoto walio na umri wa chini ya miaka 15 hawawezi kuajiriwa kama wafanyikazi wa nyumbani katika jimbo la Punjab.

    "Niliumia sana alipofariki," babake Iqra, Sana Ullah, aliambia BBC.

    Alisema kuwa alipokea simu kutoka kwa polisi kuhusu Iqra Jumatano iliyopita. Alipokimbilia hospitali alimuona Iqra akiwa amelala kitandani ilhali hajitambui. Alifariki dakika chache baadaye.

    Iqra alianza kufanya kazi kama mjakazi kuanzia akiwa na umri wa miaka minane. Babake, mkulima mwenye umri wa miaka 45, alisema alimtuma kufanya kazi kwa sababu alikuwa na deni.

    Baada ya kufanya kazi kwa waajiri wachache, alienda kufanya kazi kwa wenzi hao miaka miwili iliyopita, ambao wana watoto wanane wao wenyewe. Alikuwa akipata takriban £23 ($28) kwa mwezi.

    Polisi walisema Iqra alikuwa akituhumiwa kuiba chokoleti za waajiri wake, na kuongeza kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa Iqra aliteswa.

    Polisi pia wanasema kulikuwa na ushahidi wa unyanyasaji wa mara kwa mara. Picha na video zilizopatikana na BBC zilionyesha miguu na mikono yake imevunjika mara kadhaa, pamoja na jeraha kubwa kichwani mwake.

    Uchunguzi wa maiti unafanywa ili kutathmini kiwango kamili cha majeraha yake, na polisi wameambia BBC kwamba walikuwa bado wanasubiri ripoti ya mwisho ya matibabu.

    "Moyo wangu unalia machozi ya damu. Ni wangapi... wanafanyiwa ukatili majumbani mwao kila siku kwa kazi ndogo ndogo ya maelfu kadhaa tu?" mwanaharakati Shehr Bano aliandika kwenye mtandao wa X. "Ni kwa muda gani maskini wataendelea kuzika mabinti zao kwa namna hii?"

    Wengine wameeleza kuwa mauaji yake yalisababishwa na jambo dogo sana.

    "Alikufa kwa chokoleti?" aliuliza mtumiaji mmoja wa Pakistani kwenye X.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Watoto wanyimwa haki ya kupata elimu ya msingi huku mzozo ukizidi Congo - UNICEF

    Katika baadhi ya mataifa elimu ya bure inakabiliwa na changamoto zikiwemo uhaba wa bidhaa msingi kama walimu wa kutosha, vitabu, madawati na hata vyoo

    Chanzo cha picha, TONY KARUMBA

    Maelezo ya picha, Katika baadhi ya mataifa elimu ya bure inakabiliwa na changamoto zikiwemo uhaba wa bidhaa msingi kama walimu wa kutosha, vitabu, madawati na hata vyoo

    Huku vita vikichacha na wakaazi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wakikimbia makwao, Shirika la kimataifa la kuhudumia watoto duniani UNICEF limetoa wito wa hatua za dharura ili kuokoa mwaka wa masomo kwa maelfu ya watoto.

    Hata kabla ya mzozo huu kuongezeka, mfumo wa elimu mashariki mwa DRC ulikuwa ukikumbwa na changamoto kubwa kutokana na idadi kubwa ya wakimbizi.

    Zaidi ya watu milioni 6.5, wakiwemo watoto milioni 2.6, wameathiriwa na uhamaji katika eneo hilo.

    Vita kali tangu mwanzo wa mwaka zimewalazimu zaidi ya shule 2,500 kufungwa katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, pamoja na shule zilizozungukwa na wakimbizi.

    Shule nyingi zimeharibiwa, na zilizosalia kubadilishwa kuwa makazi, na watoto 795,000 sasa wanakosa elimu – ongezeko kutoka 465,000 mwezi Desemba 2024 haya ni kwa mujibu wa UNICEF.

    Ikiwemo mkoa wa Ituri, zaidi ya watoto milioni 1.6 mashariki mwa DRC hawana nafasi ya kusoma.

    “Hii ni hali ya dharura kwa watoto,” alisema Jean Francois Basse, Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC.

    Ingawa shule za Goma zilifunguliwa tarehe 9 Februari, idadi ya wanafunzi waliorejea ilikuwa ndogo, na wazazi wakisema hali ya usalama bado ni hatarishi.

    Wakati mizozo inapozuka, shule zinasaidia kudumisha utulivu na kutoa ulinzi kwa watoto dhidi ya hatari za kuajiriwa na makundi ya kijeshi na unyanyasaji wa kingono.

    Kulingana na UNICEF Shule pia zinatoa msaada wa kisaikolojia kwa watoto waliokutana na madhila wanapoenda kupata elimu ya msingi.

    Kama sehemu ya ombi lake la misaada ya kibinadamu, UNICEF inahitaji dola milioni 52 za Marekani ili kukidhi mahitaji ya elimu ya watoto 480,000.

    UNICEF pia inatoa wito kwa pande zinazohusika katika mzozo kuheshimu taasisi za elimu na mali nyingine za kiraia, kulingana na wajibu wao chini ya sheria za kimataifa. Vile vile wanajeshi wanaopigana wametakiwa kutovamia au kuendesha shughuli yoyote katika taasisi za elimu.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Mgogoro wa Sudan: RSF na washirika wake wajiandaa kuwa na serikali mbadala

    gg

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kiongozi wa wanamgambo wa (RSF) Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti) amewasili jijini Nairobi ili kusimamia saini ya katiba itakayozalisha serikali mbadala nchini Sudan, hatua ambayo wataalamu wanatahadharisha inaweza kusababisha mgawanyiko wa taifa hili lilo katika vita la kaskazini-mashariki mwa Afrika.

    Muungano wa makundi ya kiraia, kisiasa na ya kijeshi ya Sudan yanayoshirikiana na RSF unatarajiwa kusaini katiba hii leo katika mji mkuu wa Kenya kwa ajili ya “serikali ya amani na umoja” itakayoundwa baadaye mwezi huu katika maeneo yanayodhibitiwa na kikosi hiki cha RSF.

    Muungano huu unajumuisha Sudan Revolutionary Front (SRF), muungano wa makundi ya waasi wa zamani wa Darfur, na wanachama wa zamani wa serikali ya kiraia iliyokuwa ikiongozwa na jeshi na kupinduliwa mwaka 2021.

    Mpango wa kuanzishwa kwa utawala unaoshirikiana na RSF kama serikali mbadala ikitawala sambamba na jeshi la Sudan umeibua hofu kuhusu kugawanya taifa hili na kuchochea vita vya wenyewe kwa wenyewe kuchacha.

    Chanzo cha kidiplomasia kisichojulikana kilichonukuliwa na tovuti ya Beam Reports iliyomilikiwa na binafsi kilisema jana kuwa serikali inayoongozwa na jeshi ya Sudan ilikuwa ikishinikiza Nairobi kutoruhusu RSF kutangaza serikali mbadala kwenye ardhi ya Kenya, “na kusababisha hali ya machafuko” kuhusu mpango huo.

    Tangazo la RSF lilikuwa limetolewa awali kuwa litafanya mkutano huo jana lakini lilicheleweshwa hadi leo kutokana na changamoto za kiufundi.

    Mahusiano kati ya Sudan na Kenya yalikuwa yakianza kuboreka katika miezi ya karibuni kufuatia mvutano kuhusu urafiki wa Rais William Ruto na Hemedti, kulingana na gazeti huru la The Eastleigh Voice.

    Mkuu wa Jeshi Abdel Fattah al-Burhan amesema hatakubali mpango wa RSF kuunda serikali mbadala na kuwaonya vikali watakaounga hatua ya kikosi hicho kuwa hawatakuwa na nafasi katika siasa za nchi hiyo.

    “Nataka kutuma ujumbe kwa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kwamba watu wa Sudan hawatakubali serikali yoyote, iwe ni ya Hamdok [waziri mkuu wa zamani Abdalla Hamdok] au mtu mwingine yeyote kuwalazimishia,” alisema Burhan jana katika mkutano huko Port Sudan.

    Hamdok anayeongoza muungano wa kisiasa wa Sumud, ulioanzishwa baada ya muungano mkubwa wa Sudan wa kupinga vita na kuunga mkono demokrasia, Taqaddum, kugawanyika katika makundi mawili tarehe 10 Februari kufuatia tofauti kubwa kuhusu uundaji wa serikali mbadala inayoshirikiana na RSF.

    Sumud inakanusha kuunga mkono RSF na pia haitambui serikali inayoongozwa na Burhan.

    Pia unaweza kusoma;

  13. Wataka kumuondoa Rais kwa kuitangaza sarafu ya $LIBRA kwenye mtandao wa X

    Milei

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Argentina, Javier Milei, anakabiliwa na wito wa kuondolewa madarakani pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na uhamasishaji wake wa sarafu ya kijigitali (cryptocurrency) kwenye mitandao ya kijamii.

    Milei alichapisha kwenye X, awali Twitter, kuhusu sarafu ya $LIBRA Ijumaa, akiwa ameeleza kwamba itasaidia kufadhili biashara ndogo ndogo na kampuni changa.

    Akatoa mpaka na njia ya namna ya kununua sarafu hiyo, jambo hilo lilisababisha bei yake kupanda ghafla. Lakini ndani ya masaa machache, alifuta chapisho hilo na thamani ya sarafu hiyo ikaporomoka, na hivyo wawekezaji kupoteza sehemu kubwa ya fedha zao.

    Baadhi ya wanasiasa wa upinzani katika Bunge wanasema wanapanga kuanzisha taratibu za kumuondoa madarakani Milei, huku mawakili wakisema wamewasilisha malalamiko ya ulaghai katika mahakama ya jinai ya Argentina Jumapili.

    Watu wengine mtandaoni wamemlaumu Milei kwa kitendo kinachojulikana kama "rug pull," ambapo waendelezaji wa safaru za mtandaoni huvutia wanunuzi, kisha kusitisha shughuli za biashara na kutoboa fedha zilizokusanywa kutokana na mauzo.

    Waliongeleza kuwa kiunganisho (link) kilichotumika kununua sarafu hicho kilikuwa na maneno ambayo rais hutumia katika hotuba zake.

    Hata hivyo, ofisi ya rais ya Argentina ilisema Jumamosi kuwa uamuzi wa kufuta chapisho huo ulikuwa wa kuzuia minong'no kufuatia mwitikio wa umma juu ya alichokifanya. Taarifa hiyo ilisema Milei hakuwa amehusika katika maendeleo ya cryptocurrency, na kwamba Ofisi ya kupambana na Rushwa ya serikali itachunguza na kuamua kama kuna yeyote aliyefanya makosa, ikiwa ni pamoja na rais mwenyewe.

    Wapinzani wa kisiasa wa Milei wametumia fursa hii kumkosoa. Rais wa zamani, Cristina Fernández de Kirchner, ambaye kwa sasa yuko upande wa upinzani, alimkosoa vikali akimwita "mdanganyifu wa crypto" katika chapisho lililotazamwa mara 6.4 milioni.

    Kwa upande wake, muungano mkuu wa upinzani wa nchini homo ulisema utawasilisha ombi la kumuondoa madarakani rais huyo. Pia, Esteban Paulón, mwanachama wa Chama cha Waisocialisti cha upinzani, alisema katika chapisho kwenye mtandao wa X kwamba naye atawasilisha ombi la kuanzisha taratibu za kuondolewa madaraka.

  14. Macron ateta kwa simu na Trump na Zelensky kuhusu Ukraine

    Emmanuel Macron with European Council President Antonio Costa and European Commission President Ursula von der Leyen

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amesema kuwa amezungumza na Rais wa Marekani Donald Trump na na mwenzake wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ili kuwafahamisha kuhusu yaliyojiri kwenye mkutano wa viongozi wa Ulaya uliofanyika jana huko Paris.

    Viongozi wa Uingereza na wa EU walikutana kwenye mkutano wa dharura kuhusu Ukraine hapo jana. Hatujui ni nini kilijadiliwa, lakini ripoti zinaonyesha kwamba nchi zilizoshiriki zilikuwa zimegawanyika kuhusu kama Ulaya itawapeleka wanajeshi wa amani huko Ukraine iwapo kutakuwa na makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Akiandika kwenye X mapema Jumanne, Macron alisema kuwa makubaliano ya amani "yanapaswa kuja pamoja na dhamana thabiti na zenye uaminifu za usalama kwa wa Ukraine."

    "Tutashirikiana pamoja Ulaya, Marekani, na Ukraine," alisema Macron. "Hii ndiyo ufunguo."

    Ikulu ya Marekani, White House ilielezea simu hiyo kama ya urafiki na Macron, wakati Zelensky alisema walikubaliana kwamba dhamana yoyote ya usalama kwa Ukraine inapaswa kuwa "thabiti na ya kuaminika."

  15. Urusi yasema Ulaya haina nafasi katika mazungumzo ya amani ya Ukraine

    Waziri wa masuala ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Waziri wa masuala ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov

    Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amesema Ulaya haina umuhimu wowote katika makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Ukraine huku viongozi wa Ulaya wakimaliza mkutanao wao jana Paris.

    ‘’Sijui ni kwanini wanataka kuwa katika mazungumzo ya maridhiano, ikiwa watadokeza mawazo ya ujanja juu ya kufungia mzozo wakati wao wenyewe, kwa desturi, na tabia zao, wana nia ya kuendeleza vita, basi kwa nini tuwaalike huko?" Lavrov asema.

    Lavrov alitoa kauli hiyo alipokuwa akijiandaa kuelekea Saudi Arabia ambapo atakutana na mwenzake wa Marekani Marco Rubio kujadili vita vya Ukraine na kurekebisha mahusiano yaliyopwaya kati ya Moscow na Washington.

    Kwa upande wa Ulaya, viongozi wamekubaliana kuwekeza zaidi katika ulinzi wa bara hilo na kudhihirisha nia na umuhimu wa kushirikishwa kwenye mchakato wa amani katika mzozo kati ya Urusi na Ukraine.

    Waziri mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer amesema kuwa makubaliano yoyote ya amani nchini Ukraine yatahitaji msaada wa Marekani ili kuhakikisha Urusi haivamii nchi hiyo Jirani.

    Akizungumza katika kongamano la viongozi wa Ulaya lililoandaliwa Paris aliapa kutuma vikosi vya kijeshi Ukraine kudumisha amani ikiwa ni hatua muhimu ya kutekeleza makubaliano ya amani.

    Akieleza kuwa atakapokutana na Rais Trump wiki ijayo atazungumza kwa mapana kuhusu makubaliano yakusistisha mapigano Ukraine.

    Naye Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisisitiza kuwa mazungumzo yakusitisha mapigano yatakuwa bure ikiwa kyiv haitahusishwa.

    Maafisa wa Marekani wamewaambia nchi za Ulaya kuhusu yaliyojadiliwa katika makubaliano, lakini hawatahusishwa moja kwa moja.

    Starmer pia ametoa hakikisho kuwa Marekani haitajiondoa Nato kama vle wengi walivyotarajia.

    Pia unaweza kusoma:

  16. Majeshi ya Israel 'yapuuza' ukomo wa kusalia Lebanon

    gg

    Chanzo cha picha, EPA

    Vikosi vya Israel vimeendelea kudhibiti maeneo ya Lebanon, huku muda wa vikosi hivyo kuondoka katika nchi hiyo ukifika kikomo.

    Chanzo cha kiusalama cha Lebanon kimetangaza kuwa kimeanza kujitayarisha kurejesha maeneo yaliyokuwa chini ya udhibiti wa Israel, huku muda wa vikosi hivyo kuondoka ukitamatika leo.

    Hata hivyo, Israel imesema haitatoa vikosi vyake kwa kwa wakati mmoja nchini Lebanon kwani vitaendelea kudhibiti baadhi ya maeneo yaliyopo mpakani, licha ya shinikizo kutoka kwa mataifa mengine kuwataka kutekeleza makubaliano ya kusitisha vita kikamilifu.

    Makubaliano ya kusitisha vita yaliyoanza tarehe 7 Novemba mwaka jana, yaliyosimamiwa na Marekani na Ufaransa, yaliagiza Israel iondoke kusini mwa Lebanon ndani ya siku 60, ambapo muda huo uliongezwa hadi tarehe 18 Februari 2025.

    Baadhi ya matakwa ya makubaliano hayo ni kwamba watakaomiliki silaha ni maafisa wa usalama pekee wa Lebanon, huku serikali ya nchi hiyo ikipiga marufuku kusambaza silaha au zana za vita kwa vikosi visivyo rasmi.

    Wakati wa mikutano ya amani, Rais wa Lebanon, Michel Aoun, alielezea wasiwasi wake kwamba huenda Israel haitaondoa vikosi vyake vyote nchini humo na aliiomba jamii ya kimataifa kuingilia kati ili kuwajibisha Israel.

    Kwa upande wa Israel, wamesema itakuwa vigumu kwao kuruhusu Hezbollah kuwa na silaha, hasa katika maeneo yaliyo mpakani.

    Ingawa vikosi vya kijeshi vya Israel vimeondoka katika maeneo ya magharibi ya Lebanon, bado vimejikita katika baadhi ya vijiji vya kusini na yanaendelea kushambulia kwa mabomu kila siku.

    Haya yanajiri wakati Lebanon inajiandaa kwa mazishi ya viongozi wao wakuu kama vile Hassan Nasrallah na Hashem Safieddine mwishoni mwa wiki.

    Mashirika ya kibinadamu hata hivyo yameonya kwamba uharibifu mkubwa wa miundombinu unaoshuhudiwa nchini Lebanon unachochea wakaazi kuogopa kurejea makwao.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Marekani na Urusi zaanza mazungumzo ya kumaliza vita Ukraine

    Ukraine

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mazungumzo kati ya ujumbe wa Urusi na Marekani yameanza huko Saudi Arabia, kwa ajili ya kutafuta suluhu na kumaliza vita vya Ukraine.

    Kwa upande wa Marekani unasisitiza kwamba mazungumzo ya leo sio kuanza makubaliano, lakini ni kufanyia kazi iwapo Urusi "ina dhamira ya dhati" ya kumaliza vita vya Ukraine.

    Urusi inasema kipaumbele chake ni kuboresha mahusiano yake na Marekani.

    Mkutano huu ni wa ndani na haifahamika utachukua muda gani.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, Balozi wa Marekani katika Mashariki ya Kati, Steve Witkoff, na Mshauri wa Usalama wa Taifa, Mike Waltz, wote wamewasili katika nchi hiyo ya Ghuba kwa ajili ya mazungumzo ya awali.

    Kwa upande wa Urusi, Waziri wa mambo ya nje, Sergei Lavrov, pamoja na mshauri wa Rais Vladimir Putin, Yuriy Ushakov, wanashiriki katika mazungumzo hayo, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Urusi.

    Ukraine

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Wawakilishi wa Marekani na Urusi wakiwa kikaoni, Riyadh

    Watendaji hao wanawawakilisha Trump na Putin, kufuatia mazungumzo ya awali kwa njia ya simu kati ya viongozi hao yaliyofanyika wiki iliyopita. Baada ya mazungumzo hayo Trump alisema anatarajia kukutana na Vladimir Putin "hivi karibuni."

    Hata hivyo Ukraine haijaalikwa kushiriki katika mazungumzo haya yanayofanyika Riyadh, jambo ambalo limezua wasiwasi miongoni mwa viongozi wa Ulaya. Kuhusu hilo, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Rubio alisema mazungumzo hayo yatakuwa "ya kweli" ikiwa yataanza rasmi, lakini akasisitiza kuwa "hatujafikia hatua hiyo bado."

    Rubio pia alisema hatarajii mazungumzo haya kumaliza vita mara moja.

  18. 80 wanusurika kifo katika ajali ya ndege Canada

    Ajali

    Mtoto mmoja na watu wazima wawili wamejeruhiwa vibaya katika ajali ya ndege iliyokuwa inatua katika uwanja wa ndege wa Toronto Pearson nchini Canada.

    Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha ndege ambayo inaonekana kupinduka chini juu, juu chini, bila ya kuwa na moja ya mabawa yake.

    Mamlaka za uwanja wa ndege wa Toronto Pearson zilisema ajali hiyo ilihusisha ndege ya Delta Air Lines 4819 iliyokuwa ikitoka Minneapolis, na kwamba "abiria wote na wafanyakazi wa ndege wamepatikana."

    Ndege hiyo ilikuwa na watu 80, wakiwemo abiria 76 na wafanyakazi wa ndege wanne, kama ilivyotangazwa na Delta. Abiria 22 kati yao ni Wacanada, wengine ni wa mataifa mbalimbali, alisema Ms. Flint.

    Majeruhi 18 wamepelekwa hospitali, kwa mujibu wa Shirika hilo.Miongoni mwao, waliojeruhiwa vibaya ni pamoja na mtoto mmoja, mwanamume wa miaka 60, na mwanamke wa miaka 40. Abiria 22 kati yao ni Wacanada, wengine ni wa mataifa mbalimbali, alisema Ms. Flint.

    Uwanja wa ndege ulifungwa muda mfupi baada ya tukio hilo, lakini safari za kuingia na kutoka Toronto Pearson ziliendelea tena baada ya saa kadhaa.

  19. Mzozo wa DRC: Watu 10,000 wakimbilia Burundi

    Wakimbizi

    Wakati mapigano yanaendelea katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambayo inapakana na Burundi, zaidi ya watu 10,000 wamekimbilia nchini Burundi, Wizara ya Mambo ya ndani ya Burundi imethibitisha.

    Katika mkutano na waandishi wa habari, Waziri Martin Niteretse alisema kuwa wengi wao wamewasili katika siku tatu zilizopita.

    "Tangu Jumapili tarehe 14 hadi Jumapili Februari 16, Burundi imepokea karibu wakimbizi 10,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo," alisema Niteretse.

    Wakimbizi hao wanavuka Mto Rusizi upande wa Cibitoke au kupitia Uvira, eneo la DRC lililo karibu na Gatumba nchini Burundi.

    Kwa mujibu wa waziri huyo, wakimbizi watapelekwa katika kambi za muda za Cibitoke na Gihanga katika mkoa wa Bubanza.

    Hata hivyo, baadaye watapelekwa katika kambi za wakimbizi zilizo mbali na mpaka kama vile Rutana na Ruyigi mashariki mwa nchi.

    Alisema kwa sasa kuna juhudi za kuwatenganisha raia wa kawaida, wanajeshi, na wale walio na matatizo ya kiafya.

    Mpaka sasa Burundi tayari inahifadhi wakimbizi zaidi ya 86,000 kutoka DRC.

    Pia unaweza kusoma:

  20. Natumai hujambo.