Vita vya Ukraine: Vinakaribia mwisho au kuzaa vita mpya?
Na Yusuph Mazimu
Nairobi, Kenya

Chanzo cha picha, Getty Images
Mzozo kati ya Urusi na Ukraine ulianza Februari 2014, baada ya Urusi kuikalia kimabavu Crimea na kuzuka kwa mapigano mashariki mwa Ukraine katika eneo la Donbas.
Kwa miaka kumi, mgogoro huu umekuwa ukihusisha vikosi vya waasi wanaotaka kujitenga vinavyoungwa mkono na Urusi kwa upande mmoja, na Ukraine kwa upande mwingine.
Hata hivyo, hali ilichukua sura mpya mnamo Februari 2022, wakati Urusi ilipoanzisha uvamizi wa kijeshi mkubwa dhidi ya Ukraine. Vita hivyo vimechukua zaidi ya miaka mitatu sasa, na viongozi wa dunia wanakutana tena kutafuta suluhu.
Mkutano wa wiki hii wa dharura wa viongozi wa Ulaya huko Paris Ufaransa, unagubikwa na hofu kwamba Marekani inasonga mbele na mazungumzo ya amani na Urusi bila kushirikisha Ulaya.
Marekani, kupitia maafisa wake wa ngazi ya juu, inatarajiwa kukutana na wawakilishi wa Urusi nchini Saudi Arabia ili kujadili kumaliza vita. Licha ya madai kwamba Ukraine imealikwa kushiriki, Rais Volodymyr Zelensky amesema nchi yake haijapokea mwaliko wowote rasmi.
Je, mkutano huu wa viongozi wa dunia utaleta mwisho wa vita au ni mwanzo wa mgawanyiko mpya kati ya Marekani na Ulaya kuhusu jinsi ya kushughulikia mgogoro wa Ukraine?
Ushirikiano wa Ulaya na Marekani uko rehani?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Marekani imekuwa kinara wa kusaidia Ukraine tangu uvamizi wa Urusi mwaka 2022, lakini sasa kuna dalili kwamba Washington inataka kufanikisha mazungumzo ya amani kwa njia yake. Mjumbe maalum wa Marekani kwa Ukraine, Keith Kellogg, ameeleza kuwa mazungumzo ya awali yalishindwa kwa sababu "watu wengi walihusishwa," akidokeza kwamba Marekani inapendelea njia ya moja kwa moja kati yake na Urusi.
Mtazamo huu unapingwa na viongozi wa Ulaya, ambao wanahisi kwamba Ukraine na mataifa ya bara hilo yanapaswa kuwa sehemu ya mazungumzo yoyote kuhusu mustakabali wa vita. Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer, amesisitiza kuwa huu ni "wakati wa kipekee kwa usalama wa taifa" na kwamba Ulaya inapaswa kuchukua nafasi kubwa zaidi ndani ya NATO.
Hili linaibua swali muhimu: Je, Ulaya ina nguvu za kutosha kushinikiza Marekani kufuata mkakati wa pamoja? Ikiwa Marekani itaendelea na mazungumzo yake na Urusi bila kushirikisha washirika wake wa Magharibi, inaweza kudhoofisha uaminifu ndani ya NATO na kuashiria mgawanyiko mkubwa wa kidiplomasia.
Je, makubaliano ya amani yanakaribia au ni mtego mwingine?

Chanzo cha picha, Getty Images
Historia ya juhudi za amani kati ya Ukraine na Urusi si ya kutia moyo. Makubaliano ya Minsk ya mwaka 2015, ambayo yalifikiwa kwa upatanishi wa Ufaransa na Ujerumani, yalishindwa kumaliza mapigano mashariki mwa Ukraine. Badala yake, yalimpa Urusi muda wa kuimarisha vikosi vyake kabla ya kuanzisha uvamizi mkubwa mwaka 2022.
Hofu kama hizo zinajitokeza tena kuhusu mazungumzo yanayopangwa kati ya Marekani na Urusi. Ikiwa Ukraine haitakuwa sehemu ya mazungumzo hayo, kuna uwezekano mkubwa kwamba makubaliano yoyote yatakayofikiwa hayatazingatia kikamilifu maslahi yake.
Rais Zelensky amesisitiza kwamba amani yoyote inapaswa kujumuisha urejeshaji wa maeneo yote ya Ukraine, ikiwa ni pamoja na Crimea, ambayo Urusi iliikalia kimabavu mwaka 2014. Hata hivyo, Marekani inaonekana kuwa na mtazamo tofauti, ikiashiria kuwa baadhi ya madai ya Ukraine si ya kimsingi katika kufanikisha amani ya haraka.
Ikiwa Marekani na Urusi zitafikia makubaliano bila kushirikisha Ulaya au Ukraine, kuna hatari ya historia kujirudia ambapo Urusi inaweza kutumia muda huo kujipanga kwa vita vingine katika siku za usoni.
Mustakabali wa Vita: Mwisho unakaribia au vita vipya vinazaliwa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Ingawa mkutano wa Paris unalenga kuimarisha mshikamano wa Ulaya kuhusu Ukraine, kuna dalili za mgawanyiko mkubwa kati ya Marekani na washirika wake wa Magharibi.
Sir Keir Starmer anatarajiwa kukutana na Rais Trump mwishoni mwa mwezi huu ili kuwasilisha mtazamo wa Ulaya kuhusu Ukraine. Pia, viongozi wa Ulaya wanapanga mkutano mwingine na Rais Zelensky baada ya mkutano huo, ili kuhakikisha kuwa Ukraine haiachwi peke yake katika juhudi za kusaka amani.
Swali kubwa linalosalia ni: Je, juhudi hizi za Ulaya zitakuwa na uzito wa kutosha kuzuia Marekani kuamua mustakabali wa Ukraine bila wao?
Ikiwa Marekani itaendelea na mkakati wake wa peke yake, Ulaya inaweza kulazimika kuimarisha uwezo wake wa kijeshi na diplomasia ili kuhakikisha kuwa haitegemei Marekani katika maamuzi muhimu ya usalama. Hii inaweza kuwa mwanzo wa mpangilio mpya wa kisiasa na kijeshi duniani, ambapo Ulaya inachukua nafasi kubwa zaidi katika masuala yake ya usalama.
Lakini ikiwa mkutano huu utazaa matunda na Marekani, Ulaya, na Ukraine wakaungana katika msimamo wa pamoja, basi kuna uwezekano mkubwa wa kufanikisha makubaliano ya amani yanayoweza kudumu.
Kwa sasa, bado ni mapema kusema kama mkutano huu utakuwa hatua ya mwisho kuelekea amani au ni mwanzo wa mgogoro mpya wa kisiasa na kidiplomasia kati ya Marekani, Ulaya, na Ukraine. Lakini jambo moja liko wazi: Hatima ya vita vya Ukraine itaamua mustakabali wa usalama wa Ulaya kwa miaka mingi ijayo.
Imehaririwa na Ambia Hirsi












