Bowen: Zelensky katika hali ngumu mpya baada ya mazungumzo ya simu ya Trump-Putin

..

Chanzo cha picha, Reuters

Muda wa kusoma: Dakika 6

Marekani iko chini ya mamlaka mpya. Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, anajiunga na orodha inayokua ya washirika wa Marekani wanaogundua kuwa dunia chini ya Donald Trump haina uhakika na inaweza kuwa hatari zaidi kwao.

Ni wazi ilikuwa taarifa mbaya kwa Zelensky kusikia tangazo la kushtukiza kutoka kwa rais Trump kwamba alimpokea Rais wa Urusi, Vladimir Putin, kwenye mazungumzo ya dakika 90 kwa njia ya simu, ambayo itafuatiwa na mkutano wa ana kwa ana, labda nchini Saudi Arabia.

Baada ya Putin, Ikulu ya White House ilimpigia simu Zelensky. Akizungumza na waandishi wa habari nchini Ukraine asubuhi iliyofuata, Zelensky alikubali ukweli kwamba Putin alipokea simu ya kwanza, "ingawa kwa ukweli, si jambo la kufurahisha sana."

Kilichomshangaza zaidi Zelensky ni kwamba Trump, ambaye alimpigia simu baada ya kuzungumza na Putin, alionekana kumtazama, kwa kiwango kidogo, kama muhusika mdogo katika mazungumzo ya amani. Mojawapo ya ndoto zake nyingi za kutisha lazima iwe ni wazo la Trump na Putin kujaribu kutatua mustakabali wa Ukraine bila mtu mwingine yeyote katika mazungumzo.

Aliwaambia waandishi wa habari kwamba Ukraine "haitaweza kukubali makubaliano yoyote" yatakayofanywa bila ushiriki wake.

Alisema ni muhimu kwamba "kila kitu kisiende kulingana na mpango wa Putin, ambaye anataka kuhakikisha mazungumzo yanakuwa ya upande mmoja."

..

Chanzo cha picha, EPA

Rais Zelensky anajiandaa kuelekea kwenye mkutano wa usalama wa Munich, unaoanza Ijumaa, ambapo atajaribu kuwahamasisha washirika wa Ukraine. Anakabiliwa na mkutano mgumu na makamu wa rais wa Trump, JD Vance, ambaye alikuwa mmoja wa wakosoaji wakali wa msaada wa Joe Biden kwa Ukraine.

Hoja ambayo Zelensky atakutana nayo kutoka kwa Wamarekani ni kwamba Ukraine inashindwa katika uwanja wa vita na inahitaji kukabiliana na ukweli kuhusu kinachofuata. Atasema kwamba Ukraine inaweza kushinda - kwa msaada sahihi.

Nayo Umoja wa Ulaya pia ina wasiwasi. Baada ya kukutana na kumpongeza waziri wa ulinzi wa Ukraine, Rustem Umerov, mkuu wa sera za kigeni wa EU, Kaja Kallas, aliandika katika mtandao wa kijamii X kwamba Ulaya lazima iwe na jukumu kuu katika mazungumzo yoyote. "Kipaumbele chetu sasa lazima kiwe kuimarisha Ukraine na kutoa msaada thabiti wa kiusalama," Kallas alisema.

..
Maelezo ya picha, Maeneo ya Ukraine kwa sasa yaliyoko chini ya udhibiti wa Urusi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Zelensky anajua kwa maumivu kwamba wakati washirika wake wa Ulaya wanaonekana kuwa thabiti zaidi kuliko Wamarekani, Marekani bado inabaki kuwa na nguvu kubwa zaidi ya kijeshi duniani. Aliliambia Guardian wiki iliyopita kwamba "dhamana za usalama bila Marekani si dhamana halisi za usalama."

Kwa pamoja, washirika wa Ulaya wametoa pesa zaidi kwa Ukraine kuliko Marekani. Lakini Wamarekani wana silaha na mifumo ya ulinzi wa angani - kama vile betri za makombora ya Patriot zinazolinda Kyiv - ambazo Ulaya haiwezi kuzitoa.

Putin atafurahia kwamba anapata maisha rahisi zaidi kuliko alivyokuwa nayo kutoka kwa Biden. Rais wa zamani wa Marekani alimtaja Putin, pamoja na mambo mengine, kama "mhalifu mkuu," "mwanafalsafa mkatili," na "dikiteta muuaji" na kukata mawasiliano baada ya uvamizi wa kijeshi wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari 2022.

Ili kuonyesha kuwa kila kitu kimebadilika, Trump alifuatilia tathmini nzuri ya mazungumzo yake na Putin aliyofanya jana kwa chapisho la kutia moyo asubuhi kwenye jukwaa la mtandao wa kijamii Truth Social, akirejelea "mazungumzo aliyofanya na Urusi na Ukraine jana." Kulikuwa na "uwezekano mzuri wa kumaliza vita hivyo vya kutisha, vyenye umwagaji damu mkubwa!!!"

Putin si tu amerejea katika mazungumzo na nchi yenye nguvu zaidi duniani. Pamoja na Trump, anaweza sasa kujiona kama mwenye mamlaka wa mwisho katika vita aliyoanzisha alipovunja sheria za kimataifa kwa uvamizi wa kijeshi nchini Ukraine karibu miaka mitatu iliyopita.

Katika Ikulu ya White House, Trump alionekana kupendekeza kwamba idadi kubwa ya waliokufa na kujeruhiwa katika jeshi la Urusi ilitoa aina fulani ya uhalali kwa madai ya Putin ya kuendelea kudhibiti ardhi ya Ukraine na hata ile iliyochagua kujiunga nayo.

"Waliichukua ardhi kubwa na walipigania ardhi hiyo," Trump alisema. Kuhusu Ukraine, "baadhi yake itarudi."

..
Maelezo ya picha, Ukraine kabla ya uvamizi kamili wa Urusi mnamo 2022
Unaweza pia kusoma

Matamshi ya waziri wake wa ulinzi, Pete Hegseth, katika mkutano wa NATO mjini Brussels yalikuwa ya moja kwa moja zaidi. Alitaka Ukraine iwe "huru na yenye mafanikio." Lakini "lazima tuanze kwa kutambua kwamba kurudi kwenye mipaka ya kabla ya 2014 ya Ukraine ni lengo lisilowezekana."

"Kufuatilia lengo hili lisilo na uhalisia kutaongeza vita na kusababisha mateso zaidi."

Trump bado yuko kwenye upande rahisi wa kile kinachoweza kuwa changamoto kubwa ya kidiplomasia. Kujigamba kwamba ana ufunguo wa kumaliza vita vya Urusi na Ukraine ni jambo moja. Kufanya hilo litimie ni jambo lingine.

Tangazo lake kabla ya mazungumzo yoyote na Urusi kuanza kwamba Ukraine haitajiunga na NATO wala kupata ardhi yake yote iliyokamatwa limekosolewa sana kama mwanzo mbaya kutoka kwa mtu anayejiita kuwa mfanyabiashara bora zaidi duniani.

Mwanadiplomasia mkongwe wa Uswidi na mwanasiasa, Carl Bildt, alichapisha kauli ya dhihaka kwenye mtandao wa X.

"Ni hakika kuwa ni mbinu ya kibunifu katika mazungumzo kutoa makubaliano makubwa sana hata kabla ya kuanza. Hata Chamberlain hakufikia kiwango cha chini kiasi hicho mwaka 1938. Munich ilimalizika vibaya hata hivyo."

Bildt alichapisha picha ya waziri mkuu wa Uingereza wakati huo, Neville Chamberlain, aliporejea kutoka Munich mwaka 1938, akipunga mkono baada ya makubaliano maarufu na aliyofanya na Adolf Hitler - ambayo yaligharimu na kusababisha kugawanywa kwa Czechoslovakia na kusababisha vita vya pili vya dunia.

Baada ya uvamizi wa kijeshi wa Ukraine mwaka 2022, Vladimir Putin alitazamwa na magharibi kama tishio jipya kwa amani ya Ulaya. Mbinu ya Trump kwake ni tofauti sana.

Lazima ajaribu kuziba pengo kati ya mitazamo ya Putin na Zelensky, ambayo ni tofauti kabisa.

..

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Madai ya Ukraine hayatakubaliwa na Moscow, na Trump ameashiria kuwa hayaungi mkono pia

Lengo lililotangazwa na Zelensky ni kurejesha maeneo yaliyopotea ya Ukraine, ambayo ni takriban theluthi moja ya ardhi yote ya nchi hiyo. Pia anataka Ukraine kuwa mwanachama kamili wa NATO.

Putin anasisitiza kwamba mkataba wowote wa amani utahitaji Ukraine kukabidhi ardhi ambayo Urusi imechukua, pamoja na maeneo ambayo haijaiteka, ikiwemo jiji la Zaporizhzhia lenye wakazi zaidi ya laki tano. Ukraine pia itakuwa na hadhi ya kimataifa ya kutokuwa na upande, kutokuwepo na silaha na haitaji kujiunga na NATO.

Madai ya Ukraine hayatakubalika na Moscow, na Trump ameshaonyesha kuwa hayapendi pia.

Lakini matakwa ya Urusi ni sharti, sio pendekezo la kweli la amani. Trump, anapenda mikataba inayohusisha mali halisi. Lakini Putin anataka zaidi ya ardhi. Anataka Ukraine irejee kwenye uhusiano ilio kuwa nao na Kremlin wakati ilikuwa sehemu ya Umoja wa Kisovieti. Ili hilo litimie, Ukraine itabidi ipoteze uhuru wake na mamlaka yake kitaifa.

Biden alitoa msaada wa kutosha kwa Ukraine, kwa kuwa alichukulia vitisho vya Putin vya kutumia silaha za kinyuklia kama vitisho vya kweli ikiwa NATO itaingilia kati. Trump lazima awe na ufahamu kuhusu hatari ya nyuklia, lakini pia anaamini kuwa kuunga mkono Ukraine bila kikomo ni mkataba mbaya kwa Marekani, na anaweza kuboresha zaidi.

Kwa Ulaya, labda atawalazimisha kukabiliana na utofauti mkubwa kati ya ahadi zao za kijeshi kwa Ukraine na uwezo wao wa kijeshi. Nchi pekee zinazounga mkono kauli zao hadharani kuhusu tishio kutoka kwa Urusi ni Poland na mataifa ya Baltic kwa kuongeza matumizi ya jeshi kwa kiwango kikubwa.

Wakati Urusi ikiendelea kusonga mbele katika uwanja wa vita mashariki mwa Ukraine, huu ni wakati mgumu zaidi ambao Zelensky atakutana nao tangu miezi ya giza na kukata tamaa mwanzoni mwa vita, wakati Ukraine ilipojibu mashambulizi ya Urusi dhidi ya Kyiv.

Huu pia ni wakati wa maamuzi kwa washirika wa Ukraine wa upande wa magharibi. Wanakutana na maamuzi magumu ambayo hayafai kucheleweshwa tena.

Unaweza pia kusoma

Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Dina Gahamanyi