Mshauri wa Trump asema lengo la Ukraine lazima liwe amani na si kutwaa tena eneo

Mshauri mkuu wa rais mteule Donald Trump anasema utawala ujao utazingatia kufikia amani katika vita vya Ukraine badala ya kushinda eneo la nyuma.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Dinah Gahamanyi

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo haya ya moja kwa moja, shukran kwa kuwa nasi lakini kumbuka unaweza kufuata taarifa zetu zaidi kwenye Chaneli yetu ya WhatsApp:

    Bofya hapa ili kujiunga na chaneli yetu ya WhatsApp ikiwa unatumia simu yako ya mkononi au Wavuti ya WhatsApp.

    h
  2. Marekani 'haitakubali kuwepo kwa Hamas nchini Qatar'

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Qatar ni taifa dogo lakini yenye ushawishi ni mshirika mkuu wa Marekani na ina kambi kubwa ya kikosi chake cha anga

    Maafisa wakuu wa Marekani wameripotiwa kusema kuwa Washington haitakubali tena uwepo wa wawakilishi wa Hamas nchini Qatar, wakilishutumu kundi hilo la Palestina kwa kukataa mapendekezo ya hivi karibuni ya kufikia usitishaji vita vya Gaza na makubaliano ya kutekwa.

    Katika maelezo mafupi kwa shirika la habari la Reuters, maafisa hao wamesema kuwa serikali ya Qatar imekubali kuwaambia Hamas kufunga ofisi yake ya kisiasa siku 10 zilizopita.

    Hamas wamekuwa na msingi wa kisiasa huko Doha tangu 2012, ikiripotiwa kuwa ni kwa ombi la utawala wa Obama, oili kuruhusu mawasiliano na kundi hilo.

    Taarifa hizo zimekanushwa kwa BBC na maafisa wa Hamas; Qatar bado haijatoa maoni.

    Taifa hilo dogo lakini lenye ushawishi mkubwa la Ghuba ni mshirika mkuu wa Marekani katika eneo hilo.

    Ni mwenyeji wa kambi kuu ya jeshi la anga la Marekani na imeshughulikia mazungumzo mengi magumu ya kisiasa, pamoja na Iran, Taliban na Urusi.

    Kando na Marekani na Misri, Waqatari pia wamekuwa na jukumu kubwa katika duru za mazungumzo ambayo hayajafanikiwa hadi sasa ya maafikiano na usitishaji mapigano katika vita vya mwaka mzima kati ya Israel na Hamas huko Gaza.

    Unaweza pia kusoma:

  3. Vita vya Ukraine: Mshauri wa Trump asema lengo la Ukraine lazima liwe amani na si kutwaa tena eneo

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Trump amekuwa akisema mara kwa mara kipaumbele chake ni kumaliza vita

    Mshauri mkuu wa rais mteule Donald Trump anasema utawala ujao utazingatia kufikia amani katika vita vya Ukraine badala ya kurejesha tena eneo lililotwaliwa.

    Bryan Lanza, ambaye ni mtaalamu wa mikakati wa chama cha Republican, aliiambia BBC kuwa utawala wa Trump utamwomba Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kutoa maoni yake kuhusu "maono ya kweli ya amani".

    "Na ikiwa Rais Zelensky atakuja mezani na kusema, sawa tunaweza kuwa na amani ikiwa tu tuna Crimea, anatuonyesha kuwa hayuko makini," alisema.

    Urusi ilitwaa rasi ya Crimea mwaka wa 2014. Miaka minane baadaye, ilianzisha uvamizi kamili wa Ukraine na kutwaa eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

    Trump tayari amezungumza na Zelensky tangu kushinda uchaguzi wa Marekani - wawili hao walipiga simu siku ya Jumatano huku bilionea Elon Musk pia akishiriki.

    "Yalikuwa mazungumzo mafupi na Musk, lakini yalikuwa mazungumzo mazuri na Trump, yalichukua takriban nusu saa," chanzo katika ofisi ya rais wa Ukraine kiliiambia BBC.

    "Hayakuwa mazungumzo kwa kweli kuhusu mambo muhimu sana, lakini kwa ujumla yalikuwa ya kusisimua na ya kupendeza."

    Trump amekuwa akisema mara kwa mara kipaumbele chake ni kumaliza vita na kudhibiti matumizi ya rasilimali za Marekani.

    Unaweza pia kusoma:

  4. Je, Urusi inamtazamia Trump kumaliza vita Ukraine?

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Duru ndani ya serikali ya Urusi zinaendelea kutathmini namna gani ushindi wa Donald Trump utakavyoathiri vita nchini Ukraine.

    Shirika la Habari la Urusi, Interfax limeripoti kuwa naibu waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Sergei Ryabkov, amesema kwa sasa Moscow na Washington "zinapeana ishara kuhusu Ukraine" kwa kupitia mawasiliano ya siri.

    Kiongozi huyo amesema pia hakuna matayarisho yalionza kufanyika juu ya mazungumzo ya simu baina ya Rais Vladimir Putin na rais mteule Trump, lakini amedokeza kuwa Urusi ipo tayari kumsikiliza mapendekezo ya Trump ya namna ya kumaliza mzozo wa Ukraine.

    Hata hivyo, Ryabkov ametahadharisha kuwa mapendekezo mengi ya Trump kufikia sasa yanaonekana kuwa kama ahadi za kampeni.

    "Nafikiri baadhi ya ujumbe wake… kuhusu maazimio ya haraka sana juu ya kumaliza kinachoendela Ukraine hayana uzito… zaidi ya kuwa ni njia ya kujipatia umaarufu wakati wa kujiandaa na uchaguzi."

    Unaweza pia kusoma:

  5. Vita vya Ukraine: Urusi yadungua droni 50 za Ukraine

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wizara ya Ulinzi ya Urusi inasema kuwa ndege za Ukraine 50 zisizo na rubani zimedunguliwa Jumamosi usiku katika maeneo saba ya Urusi.

    Kulingana na jeshi la Urusi, droni hizo 28 zilipigwa risasi juu ya mkoa wa Bryansk, 12 juu ya mkoa wa Kursk, nne juu ya mkoa wa Novgorod, mbili juu ya mkoa wa Smolensk, mbili katika mkoa wa Tula, na mbili kila moja juu ya mikoa ya Oryol na Tver.

    Gavana wa mkoa wa Kaluga, Vladislav Shapsha,- aliandika katika chaneli yake ya telegraph kwamba nyaya za umeme ziliharibiwa kwa sababu ya mlipuko wa droni.

    Mkuu wa mkoa wa Tula, Dmitry Milyaev, kwa upande wake anasema kwamba uchafu wa droni uliharibu " taa za nyumba moja ya kibinafsi

  6. Tazama: Jinsi ujumbe uliofichwa ndani ya chupa kwenye mnara baada ya miaka 132 ulivyopatikana

    Maelezo ya video, Mhandisi Ross Russell alipata barua hiyo katika chupa iliyoandikwa mwaka 1892

    Wahandisi wamepata chupa yenye ujumbe wa miaka 132 ndani kabisa ya kuta za mnara wa taa unaofahamika kama Corsewall Lighthouse kusini mwa Uskochi. Ugunduzi wa aina hii unasemekana kuwa ''hutokea mara moja moja maishani''

    Soma zaidi:

  7. Watu 25 wauawa katika mlipuko wa bomu Pakistani

    f

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Takriban watu 200 walikuwa katika kituo cha Quetta wakati mlipuko huo ulipotokea

    Watu takriban 25 wameuawa katika mlipuko wa bomu kwenye stesheni ya treni katika jimbo la Balochistani, nchini Pakistani.

    Makumi ya watu wengine wamejeruhiwa kufuatia mlipuko huo uliotokea wakati treni yenye abiria wengi ya asubuhi ilipokuwa ikijiandaa kuondoka kwenye stesheni ya Quetta.

    Kundi la wanamgambo la Balochistan Liberation Army, limekiri kutekeleza shambulio hilo ambalo tathmini ya polisi inaonesha lilikuwa ni la kujitoa mhanga.

    Kumeshuhudiwa ongezeko na mashambulizi katika jimbo hilo katika siku za hivi karibuni. Kundi hilo linapigania uhuru na udhibiti wa rasilimali wa jimbo hilo.

    Kwa mujibu wa kamishna wa jiji, watu 25, akiwemo aliyejitoa mhanga, waliuawa katika mlipuko huku takribani watu 50 wakijeruhiwa.

    Afisa mwandamizi wa polisi Muhammad Baloch amesema inashukiwa kuwa aliyejitoa mhanga alivaa vilipuzi vyenye kilo baina ya sita mpaka nane.

    Raia wa kawaida na wanajeshi ni miongoni mwa watu waliouawa na kujeruhiwa katika shambulio hilo, afisa huyo ameiambia BBC

    Video zilizochapishwa mitandaoni zinaonesha wakati mlipuko huo ukitokea mapema asubuhi ya leo, huku kukiwa na makumi ya watu wakiwa katika harakati za kuabiri treni.

    Abdul Jabbar ni miongoni mwa majeruhi waliofikishwa katika Hospitali ya Kiraia. Alisema kuwa alikuwa akiingia kituoni, akiwa amenunua tikiti kutoka kwa ofisi ya uhifadhi, mlipuko ulipotokea.

    "Siwezi kuelezea hofu niliyokumbana nayo leo, ilikuwa kana kwamba siku ya hukumu imefika," alisema.

  8. Marekani yamshtaki mwanamume mmoja kwa madai ya njama ya Iran ya kumuua Trump

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Serikali ya Marekani imemfungulia mashtaka raia mmoja wa Afghanistan kuhusiana na njama ya Iran ya kutaka kumuua Donald Trump kabla ya kuchaguliwa kuwa rais ajaye.

    Siku ya Ijumaa wizara ya sheria ya nchi hiyo ilifichua mashtaka dhidi ya Farhad Shakeri, 51, ikidai kuwa madai alipewa jukumu la "kuandaa mpango" wa kumuua Trump.

    Serikali ya Marekani inasema Bw Shakeri hajakamatwa na inaaminika kuwa yuko Iran.

    Iran ambayo ilieleza madai hayo kuwa "hayana msingi kabisa".

    Katika malalamishi ya jinai yaliyowasilishwa katika mahakama ya Manhattan, waendesha mashtaka wanadai kuwa afisa mmoja katika jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran alimwelekeza Bw Shakeri mnamo Septemba kubuni mpango wa kumuua Trump.

    "Wizara ya sheria imeshtaki mtu wa utawala wa Irani ambaye alipewa jukumu na serikali la kupanga mtandao wa washirika wa uhalifu ili kuendeleza njama za mauaji ya Iran dhidi ya watu inaowalenga , akiwemo Rais mteule Donald Trump," Mwanasheria Mkuu wa Marekani Merrick Garland alisema katika taarifa yake.

    Watu wengine wawili pia walishtakiwa kwa kupewa kazi ya kumuua mwandishi wa habari wa Marekani ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa Iran.

    Walitambuliwa kama Carlisle Rivera, anayejulikana pia kama "Pop", 49, kutoka Brooklyn, na Jonathon Loadholt, 36, kutoka Staten Island.

    Wawili hao walifikishwa mahakamani katika Wilaya ya Kusini mwa New York siku ya Alhamisi na wanazuiliwa huku wakisubiri kusikilizwa kwa kesi.

    Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Esmaeil Baghaei amesema shutuma sawa na hizo za majaribio ya kuwaua marais wa Marekani zilitolewa siku za nyuma jambo ambalo Iran ililikanusha na kuendelea kusema kuwa ni uongo.

    Unaweza pia kusoma:

  9. Vita vya Ukraine: Musk ashiriki katika mazungumzo ya kwanza kati ya Trump na Zelensky baada ya uchaguzi

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alizungumza na Rais mteule wa Marekani Donald Trump kwa njia ya simu Jumatano jioni, muda mfupi baada ya chama cha Republican kushinda uchaguzi.

    Shirika la Axios limechapisha makala kama saa moja iliyopita ambapo vyanzo viwili visivyojulikana vilielezea jinsi mazungumzo yalivyoendelea. Axios linaandika kwamba vyanzo vilifahamika yaliyomo kwenye mazungumzo kwa undani.

    Je, yapi yaliyozungumziwa?

    • Mazungumzo hayo yalichukua dakika 25, na, bila kutarajia, pia yalijumuisha mfanyabiashara Elon Musk, ambaye alimuunga mkono Trump kikamilifu wakati wa kampeni ya uchaguzi.
    • Baada ya Zelensky kumpongeza Trump kwa ushindi wake, rais huyo mteule alijibu kuwa ataendelea kuiunga mkono Ukraine, lakini hakuingia kwa undani.
    • Sio vyanzo viwili, bali ni vyanzo vitatu vilivyothibitisha kuwa Zelensky alihisi mazungumzo yalikwenda vizuri na hivyo wasiwasi wake kuhusu ushindi wa Trump haukuongezeka, kulingana na mpatanishi mmoja wa Axios baada ya mazungumzo, "Zelensky aliachwa bila hisia za kukata tamaa."
    • Musk, kwa upande wake, alisema ataendelea kuiunga mkono Ukraine kwa kuipatia njia ya kufikia vituo vya mawasiliano vya satelaiti vya Starlink. Amekuwa na utata kuhusu hili siku za nyuma . Musk alikataa kutoa maoni yake juu ya taarifa za vyanzo kuhusu maudhui ya mazungumzo hayo.

    Zelensky alikutana na Trump huko New York mnamo Septemba. Tangu wakati huo, wasaidizi wake wamedumisha mawasiliano na Trump, ambaye amezungumza hadharani kuhusu Ukraine na rais wake wakati huu.

    Unaweza pia kusoma:

  10. Pelosi anamlaumu Biden kwa kushindwa kwa Democrat katika uchaguzi huku lawama zikiongezeka

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Spika wa zamani wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi amesema Wademokrat wangeweza kufanya vyema katika uchaguzi wa Jumanne iwapo Rais Joe Biden angejiondoa katika kinyang'anyiro hicho mapema.

    Pelosi - mmoja wa wanasiasa wenye nguvu huko Washington - aliliambia gazeti la New York Times kwamba "kama rais angetoka mapema, kungeweza kuwa na wagombea wengine katika kinyang'anyiro hicho".

    Matamshi yake ni lawama za hivi punde zaidi kutoka kwa Wanademocrat baada ya chama hicho kushindwa kuingia Ikulu ya White House na uwezekano wa mabunge yote mawili ya Congress mnamo Jumanne.

    Pelosi anaripotiwa kuwa aliongoza msukumo wa chama cha Democrats kumtimua Biden, ambaye aliishia kuondoka kwenye kinyang'anyiro hicho mwishoni mwa Julai baada ya wiki za shinikizo kufuatia matokeo duni ya mdahalo dhidi ya Donald Trump.

    Biden alipomaliza kampeni yake, alimuidhinisha haraka Makamu wa Rais Kamala Harris kuchukua nafasi yake. Alishindwa vibaya na Rais mteule Trump siku ya Jumanne.

    Pelosi aliliambia gazeti la New York Times: "Matarajio yalikuwa kwamba, kama rais angejiondoa, kungekuwa na mchujo wazi."

    Uchaguzi wa mchujo wa wazi ungehusisha idadi ya wagombea wa Democtrat wanaoshindana kuchaguliwa na wajumbe wa chama kumrithi Biden.

    Pelosi amesema kuwa Harris angefanya vyema katika mchakato wa msingi kama huu na ingemfanya "kuwa na nguvu zaidi mbele".

    "Lakini hatujui hilo. Hilo halikufanyika. Tunaishi na kile kilichotokea,"

    "Na kwa sababu rais aliidhinisha Kamala Harris mara moja, hiyo ilifanya iwe vigumu kuwa na mchujo wakati huo. Kama ingekuwa mapema zaidi, ingekuwa tofauti."

    Unaweza pia kusoma:

  11. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya mubashara jumamosi hii ya tarehe 09.11.2024, tukikuletea habari za kikanda na kimataifa