Kurejea kwa Trump Ikulu kunaweza kubadilisha muelekeo wa vita vya Ukraine?

Chanzo cha picha, Reuters
Na Anthony Zurker
Katika maisha yake mafupi lakini yenye matukio mengi ya kisiasa, Donald Trump ameonyesha mara kwa mara tabia ya kumuonea huruma Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Katika kilele cha mkutano wa Urusi-U.S nchini Finland mnamo mwaka 2018, Trump aliamua kubeba maneno ya Putin na kupinga kwamba Urusi iliingilia uchaguzi wa Marekani wa mwaka 2016, na kupuuza kabisa ripoti za kijasusi za Marekani zilizoonyesha tofauti.
Iwapo Trump atarejea Ikulu ya White House, mtazamo huu chanya zaidi dhidi ya Urusi huenda ukawa tena msingi wa sera za kigeni za Marekani. Zaidi ya hayo, hilo huenda likaungwa mkono na wapiga kura wengi wa Republican na baadhi ya wanachama wa chama chake katika bunge la Congress.
Maoni yake katika mkutano na wapiga kura ulioandaliwa na CNN wiki hii kwa mara nyingine tena yaliwashawishi wale wanaotambua urafiki wake kwa Putin kwamba walikuwa sahihi.
Rais huyo wa zamani alisema anaweza kumaliza vita vya Ukraine ndani ya saa 24, ingawa hakusema kwa namna gani anaweza kufanya hivyo.
Alikataa kujibu swali la kama anataka Ukraine ishinde vita, na alilaumu gharama ya usaidizi wa kijeshi. "Hatuna hata silaha kwa ajili yetu wenyewe, na tunatoa nyingi (kusaidia Ukraine)," alisema, akishutumu nchi za Ulaya kwa kutochangia vya kutosha.
Trump kama Mpango mbadala wa Putin (Plan B)
Wakati bunge la Marekani limeidhinisha mabilioni ya dola za ufadhili kwa Ukraine kwa muda mrefu, akiwa rais, Trump anaweza kupunguza kasi au hata kukomesha uungwaji mkono huo.
Tayari alifanya hivi alipoongoza Ikulu ya White House: Bunge liliidhinisha usaidizi wa kijeshi, lakini yeye aliingilia kati.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baadhi ya wenzake wa chama cha Republican walikuwa wepesi kushutumu matamshi ya Trump kuhusu msaada wa silaha kwa Ukraine, lakini inawezekana - na hata kuna uwezekano - kwamba uungaji mkono wa Marekani kwa Kiev unaweza kukoma kabisa ikiwa Trump atachaguliwa tena Novemba 2024.
Angalau, usaidizi huu hautakuwa tena na masharti. Wala hakutakuwa na juhudi ambazo Washington imefanya hadi sasa kudumisha msimamo mmoja na washirika wa Ulaya katika masuala ya vikwazo dhidi ya Urusi.
Uingereza, ambayo inaongeza misaada yake kwenda Ukraine, ikiwa ni pamoja na utoaji wa makombora ya masafa marefu, wanahofia matokeo ya kusikitisha ya muhula mwingine mpya wa urais wa Trump.
Ikiwa Trump atasimamisha upelekaji wa silaha kwenda Ukraine (Kyiv), vita vitamalizika kwa kufuata masharti ya Urusi, ambayo ni jinamizi baya zaidi kwa nchi za Magharibi, Sir Alex Younger, mkuu wa zamani wa kijasusi wa Uingereza MI6, alisema.
"Putin hakuwa na mpango mbadala (Plan B) wakati alipoaivamia Ukraine, lakini sasa ni suala la kusubiri," Younger alisema.
Mwisho wa misaada - mwisho wa vita?
Umma wa Marekani hauungi mkono tena misaada kwenda Ukraine. Kura ya maoni ya Pew Research wiki hii ilionyesha kuwa Wamarekani zaidi wangependa kuona mamlaka za Marekani zikizingatia zaidi masuala ya ndani.
Lakini Jeffrey Treistman, profesa wa usalama wa taifa katika Chuo Kikuu cha New Haven huko Connecticut, hashawishiki kwamba mwisho wa misaada ya Marekani itamaanisha ni kushindwa kwa Ukraine. Kwa maoni yake, vita vinaweza kuendelea kwa miaka au miongo kadhaa.
"Waukraine, kwa sifa zao, wameonyesha dhamira ya ajabu ya kupigana na Warusi na kupinga uvamizi, hata wakati misaada [ya kimataifa] ilikuwa midogo mwanzoni mwa vita. Wana uwezo hata kama Marekani itaacha kuwasaidia,” Treitsman alisema.
Siku moja baada ya Trump kutoa maoni yake, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliiambia BBC kuwa hana wasiwasi wowote kuhusu uchaguzi wa Marekani wa 2024.
“Uchaguzi wa Marekani utafanyika baada ya mwaka mmoja, ni nani anayejua tutakuwa wapi sote. Ninaamini kufikia wakati huo tutakuwa tumeshinda (vita),” alisema na kuweka wazi kuwa haamini katika kudhoofisha uhusiano uliopo kati ya Ukraine na Marekani.












