Tunachojua kufikia sasa kuhusu 'jaribio la mauaji la Trump'

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alikimbizwa hadi kwenye eneo salama siku ya Jumapili baada ya kile shirika la ujasusi la Marekani -FBI lilichokitaja kama jaribio la mauaji katika uwanja wake wa gofu wa Florida.
Tukio hilo limetokea miezi miwili tu baada ya jaribio lingine la mauaji dhidi yake huko Butler, Pennsylvania, ambapo Trump alipigwa risasi sikioni wakati wa mkutano wa kufanya kampeni.
Maelezo bado yanajitokeza kuhusiana na tukio la hivi punde. Lakini haya ndio tunayojua kufikia sasa.
Mshukiwa alioneka vipi?
Tukio hilo lilitokea katika Klabu ya Kimataifa ya Gofu ya Trump iliyopo West Palm Beach, Florida takriban dakika 15 kutoka makazi rasmi ya Trump katika jumba lake la Mar-a-lago.
Mshambuliaji huyo alionekana na maafisa wa usalama wanaomlinda Trump , ambao walikuwa wakifanya ukaguzi wa kiusalama huku Trump akicheza.
Mawakala hao kwa kawaida huenda kwenye shimo moja mbele ya alipo Trump, kulingana na polisi.
Mtutu wa bunduki – ambao hapo awali ulielezewa kama wa aina ya AK-47 na afisa wa utawala wa Kaunti ya Ric Bradshaw – ulionekana kwenye kichaka kilichopo kando ya uwanja.
Wakati huo Trump alikuwa karibu umbali wa yadi 300-500 (272-557m) kutoka kwa mshukiwa , alisema.
Afisa wa usalama "alikabiliana mara moja" na mshukiwa huyo, ambaye alitoroka, afisa wa utawa wa eneo Bradshaw alisema.
"Huduma ya ujasusi ilifanya kile ambacho kilipaswa kufanyika."

Je mtuhumiwa alikamatwa vipi?
Maafisa wa usalama walifyatua risasi nne hadi tano walipomuona mtu aliyekuwa na bunduki .
Mshukiwa alidondosha bunduki na kutoroka kwa gari, na pia kuacha mikoba miwili ( begi dogo), kifaa kilichotumika kuweka silaha na kamera ya kulenga shabaha (GoPro), alisema afisa utawala wa eneo, Bradshaw.
Mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo alisema alimuona mtu huyo akikimbia kutoka kwenye kichaka hadi kwenye gari jeusi aina ya Nissan, afisa utawala wa eneo alisema. Shahidi huyo alichukua picha ya gari hilo na kuikabidhi kwa vyombo vya sheria.
Mshukiwa alikamatwa na polisi akiendesha gari kuelekea kaskazini kwenye barabara kuu ya I-95 baada ya kuvuka hadi Kaunti ya Martin takriban kilomita 55 (maili 34) kutoka kwenye uwanja wa gofu wa Trump.
Vyanzo kadhaa vya usalama vimeliambia shirika la habari la CBS News, ambalo ni mshirika wa BBC wa Marekani, kwamba jina la mshukiwa ni Ryan Wesley Routh.
Ryan Routh ni nani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Maelezo juu ya historia ya mshukiwa yanaendelea kujitokeza taratibu.
Akizungumza na vyombo vya habari vya Marekani, mtoto wa kiume wa Bw Routh, Oran, alimtaja kuwa "baba mwenye upendo na anayejali".
"Sijui ni nini kimetokea huko Florida, na nafikiri ni uzushi , kwa sababu kwa taarifa chache nilizozisikia haionekani kama mtu ninayemjua mimi alifanya kitu chochote cha wazimu, mbali na vurugu. ," Oran alisema katika taarifa kwa CNN.
BBC Verify imepata wasifu wa mitandao ya kijamii unaoendena na jina hilo. Unaonyesha kuwa Routh alitoa wito kwa wapiganaji wa kigeni kwenda Ukraine kwa ajili ya vita dhidi ya vikosi vya Urusi.
Pia kuna ujumbe wa kuunga mkono Palestina, kuunga mkono Taiwan na dhidi ya Uchina kwenye wasifu wake, pamoja na madai juu ya "vita vya kibaolojia" vya Uchina na kuhusu kurejea kwa virusi vya Covid-19 kama "shambulio".
Bw Routh, ambaye hakuwa na uzoefu wa kijeshi, aliliambia gazeti la New York Times mwaka wa 2023 kwamba alisafiri hadi Ukraine mara tu baada ya uvamizi wa Urusi mwaka 2022 kutafuta wanajeshi walioajiriwa miongoni mwa wanajeshi wa Afghanistan waliokimbia Taliban.
"Pengine tunaweza kununua baadhi ya pasipoti kupitia Pakistan, kwa vile ni nchi fisadi," alisema.
Bw Routh pia aliliambia gazeti la Times kwamba alikuwa na mkutano mjini Washington DC na Tume ya Usalama na Ushirikiano ya Marekani barani Ulaya "kwa saa mbili" ili kusaidia kupata uungwaji mkono zaidi kwa Ukraine.
Anaonekana kuhusika katika juhudi za kuajiri hivi majuzi katika majira ya joto, akiandika kwenye Facebook mwezi Julai: "Askari, tafadhali msinipigie simu. Bado tunajaribu kuifanya Ukraine iwakubali wanajeshi wa Afghanistan na tunatumai kuwa na majibu katika siku zijazo, miezi ... tafadhali kuweni na subira."
Ripoti za mapema zinaonyesha kuwa Bw Routh alikuwa na rekodi ya uhalifu.
Kulingana na vyanzo vya CBS, Ryan Routh alishtakiwa na kuhukumiwa kwa makosa mengi ya uhalifu katika Kaunti ya Guilford huko North Carolina kati ya 2002 na 2010.
Makosa hayo ni pamoja na kubeba silaha iliyofichwa, kukataa kukamatwa na askari polisi, kuendesha gari kwa leseni iliyofutwa, kupatikana na mali ya wizi na kugonga na kutoroka na gari.
Nini kilitokea kwa Trump?
Trump hakujeruhiwa wakati wa tukio hilo.
Muda mfupi baada ya tukio hilo kuthibitishwa na timu yake ya kampeni, chama cha Republican kilitoa taarifa kwenye orodha yake ya uchangishaji iliyosomeka: "Kulikuwa na milio ya risasi katika eneo langu, lakini kabla ya uvumi kuanza kuenea, nilitaka usikie hii kwanza: NIKO SALAMA NA SALAMA".
Trump alitoa ushuhuda wake kwa mtangazaji wa kituo cha utangazaji cha Fox News Sean Hannity, ambaye alisimulia tukio hilo hewani Jumapili.
"Walikuwa kwenye shimo la tano, walikuwa karibu kupiga mpira wa gofu," Bw Hannity alisema.
Rais huyo wa zamani alisikia "pop pop, pop pop", alisema. "Ndani ya sekunde chache, Maafisa wa usalama walimvamia rais [na] kumfunika."
Aliongeza kuwa gari lililoimarishwa kwa chuma hivi karibuni lilimpeleka Trump kwenye eneo salama.
Nini kitatokea baadaye?
Wakati wa mkutano huo wa habari na kiongozi wa utawala wa eneo, Jeffrey Veltri kutoka Ofisi ya FBI Miami Field alisema ofisi hiyo inaongoza uchunguzi ikishirikiana pamoja na mashirika mengine ya utekelezaji wa sheria.
"Tumetuma rasilimali kadhaa, zikiwemo timu za uchunguzi, timu ya kukabiliana na janga, mafundi wa mabomu na – maafisa wa kushughulikia majibu ya ushahidi," Veltri alisema, akiongeza kuwa "rasilimali kamili za FBI" pamoja na Huduma ya ujasusi ya Marekani, Palm Beach.
Ofisi ya afisa wa utawala wa eneo na ofisi ya utawala wa Kaunti ya Martin zilihamasishwa kufanya uchunguzi wa tukio hilo.
Ikulu ya White House ilisema Rais Joe Biden na Makamu wa Rais Kamala Harris, ambaye ni mgombea urais wa chama cha Democratic, wamefahamishwa kuhusu tukio hilo na wamefarijika kujua kwamba yuko salama.
"Nimesikitishwa sana na uwezekano wa jaribio la mauaji la Rais wa zamani Trump leo," Harris alisema katika taarifa.
Viongozi kutoka katika jopokazi la wabunge wa vyama viwili lililoundwa kuchunguza jaribio la mauaji la Julai 13 huko Pennsylvania walisema wanashukuru rais huyo wa zamani hakudhurika, "lakini wanasalia na wasiwasi mkubwa kuhusu ghasia za kisiasa na kulaani vikali" tukio hilo.
Mbunge wa chama cha Republican Mike Kelly na wa Democrat Jason Crow walisema jopo kazi limeomba mkutano na huduma za ujasusi ili kuelewa "kilichotokea na jinsi maafisa wa usalama walivyoshughulikia" tukio hilo.
Afisa wa huduma za ujasusi Rafael Barros aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumapili kuwa hatua zimechukuliwa tangu jaribio la awali la mauaji na "kiwango cha tishio ni kikubwa".
Bw Routh anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Jumatatu, katika mahakama ya Kaunti ya Palm Beach karibu na Mar-a-Lago.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Seif Abdalla












