Maswali yaibuliwa huku mtu aliyejihami kwa bunduki akishtumiwa kwa jaribio la kumuua Trump

Rais wa zamani Donald Trump yuko salama kufuatia jaribio la mauaji katika uwanja wake wa gofu wa Florida, na "mshukiwa wa tukio hilo " yuko kizuizini, mamlaka ya Marekani imethibitisha.

Muhtasari

  • Bakwata yaitaka serikali ya Tanzania kuchunguza mauaji na utekaji nyara
  • Nigeria: Wafungwa watoroka baada ya jela kusombwa na mafuriko
  • Biden asema Secret Service 'inahitaji msaada zaidi'
  • Trump aipongeza Secret Service kwa kumuokoa
  • Urusi itaeneza propaganda kuhusu mshukiwa wa jaribio la mauaji dhidi ya Trump - Ukraine
  • Mataifa ya Afrika Magharibi yanayoongozwa na majeshi kuzindua pasipoti mpya
  • Kesi ya Man City kuhusu ukiukaji wa sheria za ligi ya Premia yaanza
  • Mwimbaji wa Jackson 5, Tito Jackson aaga dunia akiwa na umri wa miaka 70
  • Mtangazaji wa zamani wa BBC Huw Edwards afikishwa mahakamani
  • Wanandoa walioshtakiwa kwa mauaji ya kijana ili kuiba mtoto waachiliwa huru
  • Ryan Wesley Routh: Mshukiwa wa jaribio la mauaji dhidi ya Trump ni nani?
  • Zelensky: Kwa sababu ya ukosefu wa silaha, Ukraine haiwezi kuandaa hata brigedi zinazohitajika
  • Mkuu wa misaada wa UN Gaza: Ulimwengu unawaangusha raia wasio na hatia
  • Video: Tazama polisi wakilizunguka gari la mshukiwa wa jaribio la mauaji ya Trump
  • Kamala Harris asema anashukuru Trump yuko salama
  • Mtuhumiwa alikuwa na shauku kuhusu msaada kwa Ukraine
  • Trump anusurika kwenye jaribio la mauaji Marekani

Moja kwa moja

Lizzy Masinga

  1. Kwaheri

    Na hadi hapo tunafika mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja leo.Tukutane tena kesho alfajiri panapo maajaliwa

  2. Mshukiwa katika jaribio la mauaji la Trump ashtakiwa kwa uhalifu wa kutumia bunduki

    Mshukiwa wa jaribio la muaji ta Donald Trump Ryan Routh, amefikishwa kortini na kusomewa mashtaka dhidi yake katika hafla iliyochukua chini ya dakika 10. Mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 58 aliletwa akiwa amevalia vazi la rangi ya bluu huku mikono yake ikiwa imefungwa mbele yake. Routh alizungumza na mtetezi wa umma kwa dakika kadhaa kabla ya kusikilizwa kwa kesi hiyo, akitabasamu na mara kwa mara hata akicheka wakati wakili alipokuwa akipitia utaratibu wa mahakama.

    Kesi ilipoanza, tulifahamu mashtaka ya shirikisho dhidi ya Routh - kumiliki bunduki ilhali yeye ni mhalifu aliyehukumiwa na kwa kuwa na yenye nambari iliyofichwa.

    Kosa la kwanza lina adhabu ya hadi miaka 15 jela, na la pili miaka mitano.

  3. Bakwata yaitaka serikali ya Tanzania kuchunguza mauaji na utekaji nyara

    Waziri Mkuu wa Tanzania akiwasili katika Baraza la Maulid mkoani Geita.

    Chanzo cha picha, Bakwata

    Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa Tanzania akiwasili katika Baraza la Maulid mkoani Geita.

    Baraza kuu la Waislamu nchini Tanzania, Bakwata, limetoa wito kwa serikali kuanzisha uchunguzi huru kuhusiana na matukio ya utekaji nyara na mauaji ya raia, vitendo vinavyodaiwa kutekelezwa na vyombo vya dola.

    Wito huo umejiri siku moja tu baada ya Baraza kuu la Maaskofu nchini Tanzania kutoa wito kama huo.

    Bakwata imesisitiza kuwa uchunguzi huo utabainisha wahusika wa visa hivyo katili.

    Akitoa kauli hiyo katika baraza la Maulid, katibu mkuu wa Bakwata Nuhu Mruma amesema serikali inapaswa kuchukua hatua za dharura ili kurejesha matumaini kwa raia.

    Katika siku za hivi karibuni,asasi za kiraia na wanasiasa hasa wa upinzani, wameshinikiza serikali ya Tanzania kuanzisha uchunguzi huru kutokana na mfululizo wa ripoti za watu kutoweka, kutekwa au hata kuuawa.

    Mapema mwezi huu, aliyekuwa Kada wa Chadema Ali Kibao, alitekwa na watu wasiojulikana na siku moja baadaye mwili wake ulipatikana umetupwa katika eneo la Ununioi jijini Dar es Salaam.

    Maelezo zaidi:

  4. Nigeria: Wafungwa watoroka baada ya jela kusombwa na mafuriko

    Video inaonyesha jinsi ukuta mmoja wa gereza ulivyobomolewa

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Video inaonyesha jinsi ukuta mmoja wa gereza ulivyobomolewa

    Mamlaka za Nigeria zinasema kuwa zaidi ya wafungwa 270 hawajulikani waliko baada ya kutoroka rumande wakati mafuriko makubwa yalipoharibu gereza moja katika moja mjini Maiduguri kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo.

    Kufikia sasa, saba kati yao wamerudi kizuizini.

    Mafuriko hayo yalisababishwa na kuporomoka kwa bwawa kufuatia mvua kubwa iliyonyesha.

    Takriban watu 30 wamefariki kutokana na mafuriko hayo na mamia ya wengine wamelazimika kuyahama makazi yao huko Maiduguri- mji mkuu wa jimbo la Borno.

    Gavana wa jimbo la Borno Babagana Zulum alielezea uharibifu huo kuwa ''mbaya sana.''

    Hii ni mara ya kwanza kwa mamlaka ya Nigeria kutangaza hadharani idadi ya wafungwa waliotoroka kizuizini.

    Idara ya Magereza ya Nigeria (NCoS) ilisema Jumapili kwamba baada ya kuta za gereza la ulinzi kuharibiwa, wafungwa walikuwa katika harakati za kuhamishwa na baadhi walifanikiwa kutoroka wakati wa "shughuli ya kuwamisha".

    Gavana Zulum hapo awali aliambia BBC kwamba baadhi ya waliotoroka ni wanamgambo wa kundi la la Boko Haram.

    Lakini haijabainika ni wangapi kati ya wafungwa hao waliotoroka wanahusishwa na kundi hilo kijihadi.

  5. Biden asema Secret Service 'inahitaji msaada zaidi'

    Biden

    Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock

    Rais wa Marekani Joe Biden amezungumza kwa mara ya kwanza na waandishi wa habari baada ya jaribio lingine la mauaji dhidi ya mtangulizi wake Donald Trump katika uwanja wake wa gofu mjini Florida.

    "Tunamshukuru Mungu," rais wetu wa zamani yuko salama, Biden alisema.

    Alipoulizwa ikiwa Huduma ya Secret Service inahitaji hitaji fedha au wafanyikazi zaidi, Rais Biden alisema kuna haja.

    "Lakini ukweli ni kwambai: Huduma hiyo inahitaji msaada zaidi," alisema.

    "Na nadhani Bunge linastahili kupatia kipaumbele mahitaji yao ikiwa kwa kweli wanahitaji maafisa zaidi wa huduma."

    Aliongeza: "Wanaamua ikiwa wanahitaji wafanyikazi zaidi au la."

  6. Trump aipongeza Secret Service kwa kumuokoa

    xx

    Chanzo cha picha, Reuters

    Idara ya Secret Service inayosimamia ulinzi wa viongoz wa kitaifa nchini Marekani imesifiwa na Donald Trump baada ya kuzuia kile FBI inachokiita jaribio la mauaji.

    Mshukiwa aliyejihami kwa bunduki - aliyetambuliwa na vyombo vya habari vya Marekani kama Ryan Routh - alionekana na maajenti katika vichaka vya uwanja wa gofu wa Trump Jumapili mchana huko Florida.

    Mgombea huyo wa urais wa chama cha Republican alikuwa akicheza umbali wa mita mia kadhaa

    Maafisa walimfyatulia risasi mshukiwa huyo ambaye alikimbia na kukamatwa baadaye.

    Akiongea na BBC, ajenti mmoja wa zamani alisema Huduma ya Secret Service ilikuwa na "siku njema", lakini akauliza ikiwa Trump alikuwa akipokea ulinzi wa kutosha kufuatia jaribio lingine la mauaji dhidi yake miezi miwili iliyopita.

    Tukio hilo lilisababisha kujiuzulu kwa mkurugenzi wa Secret Service.

    Soma pia:

  7. Urusi itaeneza propaganda kuhusu mshukiwa wa jaribio la mauaji dhidi ya Trump - Ukraine

    Trumpa na Mshukiwa

    Chanzo cha picha, Getty/Reuters

    Urusi itajaribu kueneza taarifa ghushi zinaihusisha Ukraine kwa jaribio la muuaji dhidi ya Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump mnamo tarehe 15 Septemba, mkuu wa Kituo cha Baraza la Usalama la Kitaifa na Kupambana na Taarifa za upotoshaji, Andriy Kovalenko, anasema kwenye mtandao wa Telegram.

    "Urusi inatumia jaribio lingine la mauaji ya Trump dhidi ya Ukraine kwenye vyombo vya habari. Vyombo vya habari vilielezea ukweli kwamba [Ryan] Routh; aliunga mkono Ukraine... "Kwa kuongeza, anahusishwa na shirika ambalo lilihusika katika utoaji wa silaha kwa Ukraine na Taiwan.

    Tukio hili tayari linageuka kuwa mada ya propaganda za Urusi. "Katika siku zijazo, adui atazindua nadharia kadhaa za njama kuhusu 'mbinu ya Ukraineni'.

    Bila shaka, haya yote ni uongo. Lakini makabiliano ya habari ni sehemu ya vita," anasema.

    Je, Trump anapaswa kupewa ulinzi zaidi?

    Trump hapati kiwango sawa cha ulinzi anachopata rais aliyepo madarakani, afisa wa usalama wa Kaunti ya Palm Beach Ric Bradshaw amedokeza.

    "Kama ingekuwa hivyo, uwanja huu wote wa gofu ungelikuwa umezingirwa na maafisa wa usalama," alisema.

    Lakini maajenti wawili wa zamani wa Secret Service walisema Trump anahitaji ulinzi zaidi kuliko marais wengine wa zamani, ikizingatiwa kwamba alikuwa akigombea tena Ikulu ya White House

    "Sasa tunapaswa kutathmini upya," Barry Donadio aliiambia BBC.

    "Je, wagombea hawa wote wanapaswa kupata kiwango sawa na cha ulinzi wa rais? Nadhani labda hilo ndilo jibu."

    Maelezo zaidi:

  8. Mataifa ya Afrika Magharibi yanayoongozwa na majeshi kuzindua pasipoti mpya

    TH

    Chanzo cha picha, AFP

    Nchi tatu za Afrika Magharibi zinazoongozwa na tawala za kijeshi zitazindua pasipoti mpya za kibayometriki "katika siku zijazo" kama sehemu ya kujiondoa kutoka kwa umoja wa kikanda wa Ecowas.

    Mali, Burkina Faso na Niger, ambazo viongozi wake wa kijeshi walichukua madaraka katika mfululizo wa mapinduzi kati ya 2020 na 2023, walitangaza mpango wao wa kuondoka kwenye umoja huo mnamo Januari.

    Kufuatia mapinduzi hayo, nchi za Afrika Magharibi ziliwawekea vikwazo wanajeshi hao, zikilenga kuwasukuma kurejesha utawala wa kiraia haraka.

    Lakini mataifa matatu ambayo sasa yanaunda Muungano wa Nchi za Sahel hadi sasa yamepinga wito huo, yakiamua kuimarisha muungano wao.

    "Katika siku zijazo, pasipoti mpya ya kibayometriki ya [muungano] itasambazwa kwa lengo la kuunganisha hati za kusafiria katika eneo letu la pamoja," kiongozi wa serikali ya Mali Kanali Assimi Goïta alisema katika hotuba yake ya televisheni siku ya Jumapili.

    Kanali Goïta, ambaye ni kaimu rais wa muungano wa Sahel, alizungumza siku moja kabla ya serikali za kijeshi kuadhimisha mwaka wa kwanza tangu wafanye uamuzi wa kuunda muungano wao wenyewe.

    Alisema pia walikuwa wakipanga kuzindua huduma ya pamoja ambayo itakuza "usambazaji wa habari kwa usawa katika mataifa yetu matatu".

    Burkina Faso ilikuwa imefichua mapema uamuzi wake wa kuzindua pasipoti mpya ya kibayometriki bila nembo ya Ecowas.

    Bado haijulikani jinsi pasi hizo mpya za kusafiria zitaathiri usafiri wa raia wao kwenda mataifa mengine ya Ecowas ambako walifurahia kusafiri bila visa kama wamiliki wa pasipoti ya kikanda ya mataifa 15.

    Mnamo Julai, wakuu wa serikali walisema walikuwa 'wameshaamua' kuhusu uamuzi wao huku wakiipa kisogo Ecowas.

    Walisema wanataka kujenga jumuiya ya watu huru kwa kuzingatia maadili ya Kiafrika na "mbali na udhibiti wa mataifa ya kigeni".

    Tangazo la hivi punde linakuja wakati Ecowas inajishughulisha na juhudi za kuyafanya mataifa matatu ya Sahel kurejea katika umoja huo.

    Ecowas hivi majuzi ilionya kuwa kurasimishwa kwa kundi lililojitenga kulileta hatari ya kusambaratika kwa eneo hilo na kuzidisha ukosefu wa usalama.

  9. Kesi ya Man City kuhusu ukiukaji wa sheria za ligi ya Premia yaanza

    xx

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kesi ya kusikilizwa kwa mashtaka 115 dhidi ya Manchester City kwa madai ya kukiuka kanuni za fedha za Ligi Kuu ya Uingereza inaanza leo.

    City walishtakiwa na kupelekwa kwa tume huru mnamo Februari 2023 kufuatia uchunguzi wa miaka minne. Inadaiwa City ilikiuka sheria zake za kifedha kati ya 2009 na 2018.

    City inakanusha vikali mashtaka yote na wamesema kesi yao inaungwa mkono na "ushahidi wa kina usiopingika". Ligi ya Premia inadai City ilikiuka sheria zinazohitaji klabu kutoa "taarifa sahihi za kifedha zinazotoa mtazamo wa kweli na wa haki wa hali ya kifedha ya klabu".

    Maelezo haya yalihusu mapato ya klabu, ambayo yanajumuisha mapato ya udhamini na gharama za uendeshaji.

    Pia imewashutumu mabingwa hao wa Ligi Kuu kwa kutotoa ushirikiano. Uchunguzi wa Ligi ya Premia ulipoanza, City ilisema madai hayo ni "uongo kabisa" na kwamba madai hayo yaliyochapishwa awali katika gazeti la Ujerumani Der Spiegel yalitokana na "udukuzi haramu na uchapishaji nje ya muktadha wa barua pepe za City".

    City wameshinda mataji manane ya ligi, vikombe vingi na Ligi ya Mabingwa tangu klabu hiyo iliponunuliwa 2008 na Kundi la Abu Dhabi United. "Inaanza hivi karibuni na tunatumai itakamilika hivi karibuni," meneja wa City Pep Guardiola alisema Ijumaa. “Natarajia uamuzi huo.

  10. Mwimbaji wa Jackson 5, Tito Jackson aaga dunia akiwa na umri wa miaka 70

    Tito Jackson ni kaka wa marehemu Michael Jackson

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Tito Jackson, aliyekuwa mmoja wa kundi la Jackson 5 pop na kaka yake marehemu Michael Jackson, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 70, vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti.

    Sababu rasmi ya kifo bado haijabainishwa. Tito alitumbuiza katika ensemble maarufu na kaka yake Jackie, Jermaine, Marlon na Michael, ambaye aliaga dunia mnamo 2009.

    Hivi karibuni alikuwa Munich kabla ya onesho ambalo kundi hilo lilipaswa kutoa.

    Steve Manning, rafiki wa muda mrefu wa familia ya Jackson na meneja wa zamani wa familia ya Jackson, aliiambia Entertainment Tonight kwamba Jackson aliaga dunia siku ya Jumatatu.

    Habari hizo zilithibitishwa katika chapisho la Instagram na wana watatu wa Jackson, Taj, Taryll na TJ Jackson, ambao wenyewe walikuwa wasanii watatu wa R'n'B/pop, 3T, miaka ya 1990.

    “Tumeshtuka, tumehuzunishwa na kuumizwa moyo,” waliandika. "Baba yetu alikuwa mtu wa ajabu ambaye alijali kila mtu na ustawi wao."

    Waliendelea: "Atamkosa sana. Itakuwa milele 'Tito Time' kwetu. "Tafadhali kumbuka kufanya yale ambayo baba yetu alihubiri kila wakati na hiyo ni 'Tupendane'. Tunakupenda Baba." Vibao vya Jackson 5 vilijumuisha ABC, The Love You Save na I Want You Back.

  11. Mtangazaji wa zamani wa BBC Huw Edwards afikishwa mahakamani

    .

    Chanzo cha picha, PA Media

    Maelezo ya picha, Huw Edwards akiwasili mahakamani

    Mtangazaji wa zamani wa BBC Huw Edwards anafikishwa mahakamani asubuhi ya leo, ambapo anaweza kuhukumiwa kwa mashtaka yanayohusisha picha zisizofaa za watoto.

    Mnamo Julai, msomaji huyo wa zamani wa habari alikiri kuwa na picha 41 kama hizo, ambazo zilitumwa kwake kwenye WhatsApp.

    Umri uliokadiriwa wa watoto katika picha nyingi ulikuwa kati ya 13 na 15, lakini mmoja alikuwa na umri wa kati ya saba na tisa.

    Atafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Westminster saa 10:00 saa za Uingereza. Anaweza kuhukumiwa, au kesi inaweza kupelekwa katika mahakama ya juu zaidi.

    Adhabu zinazowezekana ni pamoja na kifungo cha hadi miaka mitatu jela, au anaweza kupokea agizo la jumuiya kwa sharti kwamba atapitia mpango wa matibabu ya wahalifu wa ngono.

  12. Wanandoa walioshtakiwa kwa mauaji ya kijana ili kuiba mtoto waachiliwa huru

    TH

    Chanzo cha picha, Mahakama Kuu ya New South Wales

    Katika siku ya baridi kali mnamo Juni 2002, msichana mwenye ulemavu wa kiakili alitoweka kutoka New South Wales Riverina bila kujulikana.

    Tangu wakati huo, siri ya kile kilichotokea kwa Amber Haigh imevutia eneo kubwa la kilimo la Australia, kutokana na madai ya kushangaza: kwamba mtoto wa miaka 19 aliuawa na baba wa mtoto wake wa miezi mitano na mke wake, kwa ili waweze kumchukua mtoto wake.

    Miongo miwili baadaye, Robert na Anne Geeves - wote 64 - walishtakiwa kwa mauaji yake, lakini Jumatatu waliachiliwa huru .

    Jaji Julia Lonergan aligundua kuwa waendesha mashtaka wameshindwa kuthibitisha madai yao, akisema: "Kesi haziamuliwi kwa uvumi au tuhuma."

    Geeveses ndio watu wa mwisho wanaojulikana kumuona Amber akiwa hai. Kwa muda mrefu wamesema kuwa walimshusha kwenye kituo cha treni kilomita 300 (maili 186) kutoka nyumbani kwao Kingsvale - ambapo watatu hao walikuwa wakiishi wakati huo - ili aweze kumtembelea babake aliyekuwa akiugua tarehe 5 Juni.

    Licha ya uchunguzi wa kina wa polisi, uchunguzi wa kina, na zawadi ya dola milioni kwa habari, mwili wake haujawahi kupatikana.

    Waendesha mashtaka walitegemea ushuhuda wa mashahidi na mamia ya hati kuunga mkono nadharia yao - kwamba Geeveses "walimdanganya" Amber kuwa na mtoto wa Robert, na kisha kumuua wakati hakutaka kuachilia malezi.

    Mahakama ilisikia wanandoa hao walikuwa na mtoto wa kiume mtu mzima - ambaye hapo awali alichumbiana na Amber - lakini mwanzoni mwa miaka ya 2000 bado "walitamani sana" mtoto mwingine, baada ya kuvumilia kuharibika kwa mimba mara kadhaa na kujifungua mtoto aliyekufa.

    Hata hivyo, upande wa utetezi ulisema kuwa tuhuma za kumuua Amber ili kuiba mtoto wake hazikuwa na msingi wowote, na kwamba uchunguzi wa wawili hao ambao wamekaa gerezani kwa miaka miwili wakisubiri kusikilizwa kwa kesi hiyo ulikuwa na dosari tangu mwanzo.

  13. Ryan Wesley Routh: Mshukiwa wa jaribio la mauaji dhidi ya Trump ni nani?

    Routh

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mshirika wa BBC nchini Marekani, CBS News, amemtaja mshukiwa huyo kuwa Ryan Wesley Routh, akinukuu vyanzo rasmi, lakini ni nini zaidi tunachojua kumhusu?

    BBC Verify imepata wasifu kwenye mitandao ya kijamii unaolingana na jina hilo, zinaonesha alitoa wito kwa wapiganaji wa kigeni kwenda Ukraine kupigana dhidi ya vikosi vya Urusi.

    Routh, ambaye hakuwa na uzoefu wa kijeshi, aliliambia gazeti la New York Times mwaka 2023 kwamba alisafiri hadi Ukraine mara tu baada ya uvamizi wa Urusi mwaka 2022 kutafuta askari wa kijeshi kati ya wanajeshi wa Afghanistan waliokimbia Taliban.

    "Askari, tafadhali msinipigie simu. Bado tunajaribu kuifanya Ukraine iwakubali wanajeshi wa Afghanistan na tunatumai kuwa na majibu katika miezi ijayo... tafadhali kuwa na subira," aliandika kwenye Facebook mwezi Julai.

    Ripoti za awali zinaonesha Routh alikuwa na rekodi ya uhalifu na, kulingana na vyanzo vya CBS, alishtakiwa na kutiwa hatiani kwa makosa mengi ya uhalifu, ikiwa ni pamoja na kubeba silaha.

    Akizungumza na vyombo vya habari vya Marekani, mtoto wa kiume wa Bw Routh, Oran, alimtaja kuwa "baba mwenye upendo na anayejali".

  14. Zelensky: Kwa sababu ya ukosefu wa silaha, Ukraine haiwezi kuandaa hata brigedi zinazohitajika

    Zelensky katika mahojiano

    Chanzo cha picha, YouTube/@Zelenskyy_President

    Rais Volodymyr Zelensky aliiambia CNN katika mahojiano kwamba kutokana na kucheleweshwa kwa uwasilishaji wa silaha, Ukraine bado haijaweza kuandaa hata brigedi nne kati ya 14 zinazohitajika.

    "Kwanza, kila kitu kinakwenda polepole sana. Pili, tunahitaji brigedi 14 kuwa tayari. Hadi sasa, hatujapata brigedi yoyote kutoka kwa mfuko huu, hatujaandaa hata nne," rais wa Ukraine alisisitiza, akijibu swali la kwa nini.

    Kukubalika kwa vifurushi vya misaada kutoka Marekani na Ulaya hakujatafsiriwa kwa kiasi cha kutosha cha risasi kwa Ukraine. Zelensky alisisitiza kuwa katika kipindi cha miezi minane ya kusubiri uamuzi chanya kutoka kwa Bunge la Marekani kuhusu msaada kwa Kyiv kwa kiasi cha dola bilioni 61, Ukraine ilitumia hifadhi zake zote za risasi zilizopo.

    "Tulitumia kila tulichoweza. Tulihamisha tulichonacho kwenye hifadhi na kile tulichonacho kwenye maghala au kwenye brigedi za akiba tunazohitaji sasa," rais alisema.

    Forbes iliandika kwamba brigedi mpya zinazoundwa kama sehemu ya Vikosi vya Ulinzi vya Ukraine hazina silaha za kisasa, na lazima ziwe na silaha kutoka kwenye hifadhi za Sovieti.

    Unaweza kusoma;

  15. Mkuu wa misaada wa UN Gaza: Ulimwengu unawaangusha raia wasio na hatia

    Sigrid Kaag alizuru Gaza mwezi huu baada ya kupewa jukumu la kuboresha utoaji wa misaada inayohitajika haraka

    Chanzo cha picha, UN

    Afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia misaada Gaza ameambia BBC kwamba jumuiya ya kimataifa kwa pamoja inawaangusha raia wasio na hatia katika eneo hilo.

    Sigrid Kaag, ambaye aliteuliwa miezi tisa iliyopita kuboresha utoaji wa misaada inayohitajika haraka, alisema ripoti anayopaswa kutoa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo itakuwa "mbaya sana". Alielezea hali katika eneo hilo kama "janga kubwa". "Hatukidhi mahitaji, achilia mbali kujenga matarajio na matumaini kwa raia wa Gaza."

    Katika mahojiano nadra, Mratibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Utekelezaji wa masuala ya kibinadamu na Ujenzi mpya huko Gaza alisema mifumo ya kutoa msaada, ikiwa ni pamoja na njia nyingi za ardhini na baharini hadi Gaza sasa iko tayari.

    Na "UN inafanya kazi usiku na mchana na watu wanahatarisha maisha yao siku hadi siku".

    Lakini aliita Gaza "mahali pasipo salama zaidi duniani kufanya kazi". Alisema anasikitika kwamba "hakuna mengi zaidi yanayoweza kuboreshwa" hadi kuwe na usitishaji mapigano na kuachiliwa kwa mateka wa Israeli bado wanazuiliwa huko.

    Bi Kaag alisema kwamba kile kinachojulikana kama "kuondoa mzozo", kuhakikisha misheni ya misaada inaweza kuendelea kwa usalama, ilikuwa ikishindwa: "Haifanyi kazi, au haifanyi kazi vya kutosha, kufanya shughuli hizo kuwezekana."

    Wiki iliyopita Umoja wa Mataifa ulisema msafara wake mwingine wa misaada uliokuwa ukielekea kaskazini mwa Gaza ulizuiliwa na wanajeshi wa Israel, na shirika la Ulinzi la Raia la Hamas la Gaza lilisema shule ya Umoja wa Mataifa inayofanya kazi kama makazi ililengwa na shambulio la anga la Israel na kuua watu 18.

    Umoja wa Mataifa umesema wafanyakazi wake sita walifariki.

    Israel ilishutumu Hamas kwa kutumia kituo hicho kama "kituo cha amri na udhibiti" na kusema wapiganaji wa Hamas walikuwa miongoni mwa waliouawa.

    Unaweza kusoma;

  16. Video: Tazama polisi wakilizunguka gari la mshukiwa wa jaribio la mauaji ya Trump

    Maelezo ya video, Polisi walizunguka gari la mshukiwa wa jaribio la mauaji ya Trump karibu na uwanja wa gofu
  17. Kamala Harris asema anashukuru Trump yuko salama

    .
    Maelezo ya picha, Donald Trump na Kamala Harris

    Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris ametoa taarifa kamili zaidi kufuatia jaribio la kutaka kumuua mpinzani wke katika uchaguzi ujao Donald Trump, akishukuru kwamba yupo salama.

    "Nimesikitishwa sana na uwezekano wa jaribio la mauaji la rais wa zamani Trump leo," Harris alisema katika taarifa hiyo, iliyotolewa kupitia Ikulu ya White House.

    "Tunapokusanya ukweli, nitakuwa wazi: Ninalaani ghasia za kisiasa. Sote lazima tufanye sehemu yetu kuhakikisha kwamba tukio hili halisababishi vurugu zaidi." Ninashukuru kwamba Rais wa zamani Trump yuko salama.

    Ninaipongeza Huduma ya jinai ya Marekani na washirika kwa kutekeleza sheria na umakini wao.

    Kama Rais Biden alivyosema, Utawala wetu utahakikisha Huduma ya jinai ina kila rasilimali, uwezo, na hatua za ulinzi zinazohitajika kutekeleza dhamira yake muhimu.

    Hapo awali Harris alituma ujumbe kwenye Twitter akisema "ghasia hazina nafasi Marekani".

  18. Mshukiwa alitaka kuisaidia Ukraine

    Polisi

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ryan Wesley Routh, mshukiwa aliyetajwa na vyombo vya habari vya Marekani kuhusiana na jaribio la kumuua Donald Trump, aliliambia gazeti la New York Times mwaka 2023 kwamba alitaka kusaidia juhudi za vita nchini Ukraine, na alikuwa anataka kuajiri wanajeshi wa Afghanistan waliotoroka Taliban.

    Katika mahojiano kwa njia ya simu na jarida hilo la nje, Routh alisema wanajeshi kadhaa wameonesha nia.

    Pia alisema alipanga kuwahamisha kutoka Pakistan na Iran hadi Ukraine, katika visa vingine kinyume cha sheria.

    "Labda tunaweza kununua pasipoti kupitia Pakistan, kwa kuwa ni nchi fisadi," alisema. Routh pia aliiambia NYT wakati huo kwamba alikuwa Washington kukutana na Tume ya Usalama na Ushirikiano ya Marekani huko Uropa "kwa saa mbili" kusaidia kushinikiza msaada zaidi kwa Ukraine.

    Routh anaonekana kujishughulisha na juhudi za kuajiri hadi hivi karibuni mwezi Julai.

    Chapisho moja la Facebook kutoka Julai lilisomeka kwa sehemu: “Askari, tafadhali msinipigie simu. Bado tunajaribu kuifanya Ukraine kukubali wanajeshi wa Afghanistan na tunatumai kuwa na majibu katika miezi ijayo… tafadhali kuwa na subira.”

  19. Trump anusurika jaribio jingine la mauaji

    Trump

    Rais wa zamani Donald Trump yuko salama kufuatia jaribio la mauaji katika uwanja wake wa gofu wa Florida, na "mshukiwa wa tukio hilo " yuko kizuizini, mamlaka ya Marekani imethibitisha.

    Maafisa wa usalama waliona mtutu wa bunduki likipenya kwenye vichaka na kumfyatulia risasi, maafisa walisema.

    FBI ilisema Trump alikuwa umbali wa yadi 300-500 (m 275 hadi 455) wakati huo.

    Bunduki ya aina ya AK47 na upeo, pamoja na mikoba miwili na kamera ya GoPro, vilipatikana baadaye kwenye eneo la tukio.

    Shahidi aliripoti kumuona mshukiwa akikimbia kutoka kwenye vichaka na kurukia gari nyeusi aina ya Nissan baada ya maafisa hao kumfyatulia risasi mara kadhaa.

    Shahidi huyo alipiga picha gari hilo na nambari ya usajili na ilizuiliwa baadaye katika Kaunti ya Martin, kaskazini mwa klabu hiyo.

    "Tuliwasiliana na Ofisi ya Sheriff wa Kaunti ya Martin, tukawajulisha, na wakaona gari na kulivuta na kumzuia mtu huyo," Sheriff Ric Bradshaw wa Kaunti ya Palm Beach alisema.

    "Baada ya hapo, tulimchukua shahidi aliyeshuhudia tukio hilo, tukampandisha hadi pale na akajitambulisha kuwa ni mtu ambaye alimuona akikimbia kutoka kwenye kichaka, ambaye aliruka ndani ya gari,"alisema.

    Katika barua pepe kwa wafuasi wake, Trump alisema yuko "salama na mzima".

    "Hakuna kitakachonipunguza kasi," aliandika. "Sitasalimu amri kamwe!"

    Tukio hilo linakuja takribani miezi miwili baada ya mtu mwenye silaha kujaribu kumuua Trump katika mkutano wa hadhara huko Butler, Pennsylvania, akimpiga sikioni.

    Unaweza kusoma;

  20. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu