Mambo matano katika uchunguzi wa Secret Service baada ya kushambuliwa Trump

m

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ronald Rowe alieleza kuwa tukio la shambulizi katika mkutano wa Butler liliakisi kushindwa kwa Secret Service
    • Author, Bernd Debusmann Jr
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Kaimu Mkuu mpya wa Secret Service ya Marekani amesema "alikosa usingizi" kutokana na kushindwa kwa ulinzi kulikosababisha jaribio la kumuua Donald Trump, wakati wa kikao cha maswali siku ya Jumanne.

Katika kikao hicho cha Baraza la Seneti la Marekani kilichochukua saa kadhaa, Ronald Rowe na Naibu Mkurugenzi wa FBI, Paul Abbate walieleza kuhusu uchunguzi unaoendelea, walichojifunza kuhusu muuaji huyo, na kushindwa kwa usalama.

Ushuhuda wa Rowe mbele ya jopo la pamoja la kamati ya Ndani ya Usalama ya Seneti na Mahakama, unajiri wiki moja baada ya mtangulizi wake, Kim Cheatle, kulazimishwa kujiuzulu.

Cheatle alikosolewa na Democrats na Republican kwa jinsi Secret Service, ilivyoshughulikia ulinzi Julai 13 huko Butler ambapo mtu mmoja alikufa, huku Trump na wengine wawili wakijeruhiwa, na kutokuwa na uwezo wa kujibu maswali mbele ya Kamati ya Uangalizi ya Bunge wiki iliyopita.

Majibu ya watu hao wawili katika kikao cha Jumanne yalikuwa mazuri zaidi kuliko yale yaliyotolewa hapo awali. Na Rowe alijaribu kuwahakikishia Maseneta juu ya mipango mipya ya kushughulikia matundu katika usalama.

Ulinzi wa anga

Mojawapo ya mapungufu yaliyotajwa ni kwamba Secret Service haikupeleka mfumo wa ulinzi wa anga, kabla ya mkutano.

Ikiwa wangepeleka, wangegundua ndege isiyo na rubani iliyokuwa ikiendeshwa na mshambuliaji Thomas Matthew Crooks, kabla ya mkutano huo.

Rowe anasema maafisa wa Secret Service kutoka Pittsburgh - ndio waliokuwa na jukumu kwa kiasi kikubwa la kudhibiti eneo la mkutano huko Butler.

Mawasiliano ya maafisa

Ingawa hakuweza kufichua maelezo mengi kwa sababu ya unyeti wa kazi ya Secret Service, Rowe alisema, maafisa anaowasimamia tayari wanashughulikia mapungufu yaliyotambuliwa katika usalama.

Rowe aliongeza "hatasubiri" uchunguzi ukamilike ili kuhakikisha "haturudii makosa hayo."

Alielezea nia ya kurekebisha jinsi Secret Service inavyowasiliana na polisi wa ndani kabla na wakati wa hafla.

Maafisa wanasema sehemu kubwa ya mawasiliano yao kwenye mkutano wa Butler yalifanyika kupitia ujumbe mfupi wa simu, jambo ambalo linaweza kuchangia mkanganyiko juu ya ripoti za mtu anayeshuku.

Rowe anasema wasiwasi kuhusu Crooks huenda ulikwama au kufichwa katika mawasiliano ya maafisa wa jimbo na wa ndani.

"Ni jambo nzuri [kwamba] kulikuwa na mlolongo wa mawasiliano ya jumbe fupi. Lakini mawasiliano hayo yanapaswa kuenea, kupitia redio ili kila mtu awe na ufahamu. Nataka watu watumie redio."

Alifikaje na bunduki kwenye paa?

k

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wachunguzi bado hawajabaini ni nini kilimsukuma Matthew Thomas Crooks kumshambulia Trump

Mojawapo ya mambo yasiyoeleweka ni jinsi Crooks alivyoweza kufika na bunduki kwenye paa la jengo na kumpiga risasi Trump waziwazi.

Sio Rowe wala Abbate aliyeweza kujibu swali hilo.

"Hatuna ushahidi wa uhakika jinsi alivyofika na bunduki hiyo huko," Abbate alisema, ingawa maafisa wanaamini ilikuwa kwenye mkoba aliokuwa nao kwenye mkutano huo.

Kulingana na Abbate, bunduki "ingekuwa inaonekana" kama ingekuwa kwenye begi. Hakuna mtu yeyote aliyeona bunduki iliyofungwa kamili kwenye mkoba. Bunduki hiyo isingetosha kwenye mkoba huu na isionekane."

Video mpya iliyoibuka inamuonyesha Crooks akichukua begi kutoka kwenye gari lake muda mfupi kabla ya kupanda juu ya paa na kufyatua risasi nane kwenye jukwaa la Trump.

"Inawezekana aliikongooa bunduki na kuitia kwenye begi na kuiunganisha tena. Hiyo ni moja ya nadharia ambazo tunaziangalia," anasema Abbate.

Sababu ya kufanya shambulio

Licha ya kufanya mamia ya mahojiano na kutazama video nyingi, wachunguzi bado hawajaweza kueleza sababu ya Crooks kwenda kwenye mkutano huo na kufyatua risasi.

Abbate alifichua kwamba wachunguzi wamegundua akaunti ya mtandao wa kijamii ambayo wanaamini inaweza kuwa na uhusiano na Crooks - ugunduzi ambao unaweza kutoa mwangaza kuhusu mtazamo wake.

Akaunti hiyo, inayojumuisha zaidi ya machapisho 700, ni ya 2019 na 2020.

Abbate aliongeza machapisho hayo, yanayohusishwa na Crooks, yanaonekana kuakisi chuki dhidi ya Wayahudi, wahamiaji, kuhimiza vurugu za kisiasa, na ni machapisho ya itikadi kali."

"Wakati timu ya upelelezi ikiendelea na kazi ya kuhakiki akaunti hii ili kubaini ikiwa kweli ni ya Crooks, ni muhimu kutambua kuwa kazi yetu inaendelea na ni ya muhimu."

Kufutwa Kazi

Wakati uchunguzi wa kilichotokea ukiendelea, baadhi ya wabunge kwenye kikao hicho walieleza wazi kuwa wanatarajia hatua za ziada za kinidhamu zichukuliwe.

Kwa mfano, Seneta wa Republican wa South Carolina, Lindsey Graham, alisema "njia bora ya kuhakikisha halitokei tena ni kuwafuta kazi maafisa, ili wale wanaokuja watambue kuna athari ukifanya makosa".

Rowe alisema hatakimbilia hukumu, lakini aliahidi "watu watawajibishwa."

"Ikiwa kulikuwa na ukiukwaji wa sera, watu hao watawajibishwa," alisema. "Watawekwa kwenye meza yetu ya adhabu, ambayo itajumuisha kufutwa."

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi