'Macho yangu hayapo tena' - mwathiriwa wa shambulio la Israel akumbuka ujumbe uliompofusha Lebanon

Chanzo cha picha, Supplied
- Author, Carine Torbey
- Nafasi, Mwandishi wa Beirut, BBC Arabic
- Muda wa kusoma: Dakika 8
Nayfe huvaa miwani ya jua – si ili kujikinga na mwanga wa jua, bali kuwakinga wageni wasione macho yake, au mashimo yaliyosalia mahali macho yalipokuwa.
"Sehemu nyeupe za macho yangu, yaani sclera, hazipo tena," anasema. "Sehemu inayopokea nuru ndani ya jicho na neva zinazounganisha sehemu ya mbele ya jicho na ubongo zimeharibiwa kabisa."
Mwaka mmoja tangu shambulio la kifo lililotumia vifaa vya mawasiliano bila waya lililotekelezwa na Israel nchini Lebanon, BBC imezungumza na manusura na pia viongozi wa serikali kuhusu kilichotokea siku hiyo pamoja na athari zake za muda mrefu.
Ni tukio ambalo baadhi ya wanaharakati wanasema linaweza kuchukuliwa kama uhalifu wa kivita.
Katikati ya sebule ya Nayfe kuna picha yake ya kabla ya shambulio.
Anaonekana akiwa na macho makubwa meupe yenye nyusi zilizopangwa vizuri.
Anatabasamu kwa haya.
Mkono wake wa kushoto, ukiwa na vidole vilivyokunjwa, unaonekana kushikilia begi begani mwake.
Lakini leo, vidole hivyo havipo tena.
Uso wake umeharibika vibaya kiasi kwamba tulilazimika kuthibitisha na mama yake kuwa picha hiyo ni yake kweli.

Chanzo cha picha, Supplied
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa Nayfe mwenye umri wa miaka 29, tarehe 17 Septemba ilianza kama siku ya kawaida hadi ghafla, vifaa vya mawasiliano zilianza kulipuka mikononi mwa watu katika maeneo mbalimbali ya Lebanon.
Siku iliyofuata, vifaa vya mawasiliano aina ya walkie-talkie yaani simu za upepo navyo vililipuka katika shambulio linalofanana.
Matukio haya mawili yaliua angalau watu 37, wakiwemo watoto.
Takriban watu 3,000 walijeruhiwa vibaya na wengi wao wakiwa raia.
Nayfe ni mmoja wao. Alikuwa akifanya kazi katika Hospitali ya Saint George, iliyo karibu na Beirut, ambayo ni sehemu ya mtandao wa afya unaoendeshwa na Hezbollah.
Hezbollah ni kundi la Waislamu wa Kishia nchini Lebanon ambalo ni chama cha kisiasa, jeshi la wanamgambo, na pia linaendesha taasisi nyingi za kiraia zinazotoa huduma za afya na ustawi wa jamii.
Hezbollah ndilo lililolengwa na shambulio hilo.
Karibu saa tisa alasiri siku hiyo, Nayfe alikuwa ameanza zamu yake kama msimamizi katika idara ya usafi na usafishaji wa mazingira hospitalini.
"Kazi yangu ilikuwa kushughulikia wodi zote, si sehemu moja tu," anasema. "Hivyo mtu aliponihitaji, alinitumia ujumbe kupitia kifaa cha mawasiliano kisichokuwa na waya."
Nayfe alikuwa na kifaa hicho kila mara akiwa kazini. Alikuwa kazini kwa miezi minne tu, na alikuwa amepewa kifaa cha mawasiliano mpya siku 20 tu zilizopita.
Alipokuwa ofisini, kifaa hicho kilianza kutoa mlio wa tahadhari bila kukoma.
Kwa kawaida, Nayfe anasema, ujumbe ungekuja kwa namba, kisha angepiga simu ya mezani na kuuliza: "Sisi ni kutoka idara fulani, tunahitaji msaada."
Safari hii, alipoangalia kifaa hicho chake cha mawasiliano yaani pager, skrini ilikuwa na giza isivyo kawaida.
Akakileta karibu zaidi na macho ili asome ujumbe.
Hiyo ndiyo ilikuwa taswira ya mwisho aliyowahi kuona kabla kifaa kulipuka na kubadilisha maisha yake kabisa.

Chanzo cha picha, Supplied
Wakati huohuo, maelfu ya vifaa vya mawasiliano ya simu bila waya vingine vilianza kulipuka katika maeneo tofauti ya Lebanon na Syria.
Vyote vilikuwa vimenunuliwa na Hezbollah, ambayo inatambuliwa na Marekani, Uingereza na mataifa mengine kama kundi la kigaidi.
Hezbollah ni miongoni mwa mashirika yenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Lebanon, na katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, ilipata kura nyingi kuliko chama chochote kingine.
Vifaa hivyo vya mawasiliano ya simu bila waya vilisambazwa kwa wapiganaji wake pamoja na watumishi wa sekta zake za afya na kijamii.
Kwa muda mrefu, Hezbollah imekuwa ikiingiza vifaa, zana na silaha nchini Lebanon kupitia njia zisizo rasmi au bila usimamizi wa serikali.
Vifaa vya mawasiliano ya simu bila waya zilizowekwa mabomu zilipenyezwa kwa njia hiyohiyo.
Baadhi ya watu walipigwa na mabomu hayo wakiwa maeneo ya kawaida kama madukani, hospitalini, au hata wakiwa njiani.
Milipuko hiyo iliua, kujeruhi na kulemaza maelfu.
Ingawa kwa muda mrefu ilidhaniwa kuwa Israel ndiyo iliyohusika, waziri mkuu Benjamin Netanyahu alikiri hadharani kuwa Israel ilitekeleza shambulio hilo, miezi miwili baadaye, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari vya Israel.
Hadi sasa, serikali yake haijatoa kauli rasmi kuhusu uhalali wa shambulio hilo wala kujibu ombi la kutoa maoni.
Kwa mujibu wa maafisa wawili wa zamani wa ujasusi wa Israel waliouambia mtandao wa habari wa CBS, vifaa vya mawasiliano ya simu bila waya hizo ziliwekewa mabomu na kuuzwa kwa Hezbollah kupitia kampuni hewa, mojawapo ikiwa Hungary.
Walisema pia kuwa mpango wa kupenyeza vilipuzi katika simu za upepo yaani walkie-talkie ulianza miaka kumi kabla.

Chanzo cha picha, Houssam Shbaro/Anadolu via Getty Images
Wakati milipuko ilipokuwa inaanza, kikao cha baraza la mawaziri la Lebanon kilikuwa karibu kuanza.
Mawaziri, akiwemo aliyekuwa waziri mkuu Najib Mikati, walikuwa tayari kwenye makao makuu ya serikali walipoanza kupokea taarifa kuhusu shambulio hilo.
Miongoni mwa waliokuwepo ukumbini walikuwa mawaziri kutoka Hezbollah.
Mmoja wao alikuwa ameketi karibu na aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, Bassam Mawlawi.
Alipoulizwa iwapo kulikuwa na hofu ukumbini kwa sababu huenda baadhi ya mawaziri wa Hezbollah walikuwa na vifaa vya mawasiliano ya simu bila waya, Bwana Mawlawi alikataa pendekezo hilo kwa tabasamu ya upole.
"Sidhani kama mtu yeyote aliwauliza mawaziri [wa Hezbollah] kama walikuwa na kifaa cha mawasiliano ya simu kisicho na waya," anasema. "Pengine hata hawakujua."
Katika mahojiano yake ya kwanza na vyombo vya habari kuhusu siku hiyo, Bwana Mawlawi anakumbuka jinsi matukio yalivyotokea kwa haraka mno.
Anasimulia hofu iliyoikumba hata vikosi vya usalama.
Baada ya mashambulio ya simu za upepo yaani walkie-talkie, walikoma kutumia vifaa vyao kwa hofu kuwa navyo pia vinaweza kuwa na vilipuzi.
"Bila shaka kulikuwapo na tahadhari kwa watu waliokuwa wakitumia vifaa vya mawasiliano bila waya, hata ndani ya vikosi rasmi vya usalama," anasema.
"Hata katika Wizara ya Mambo ya Ndani, maafisa wetu walichukua tahadhari katika siku mbili zilizofuata mashambulio."
Wakati huo, hata maafisa wa usalama wa ngazi ya juu hawakuwa na picha kamili ya kiwango cha uvujaji wa usalama kilichotokea.
Mashambulizi hayo yamelaaniwa na kundi la wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wakiyaelezea kama ukiukwaji wa "kutisha" wa sheria za kimataifa.
Mashirika ya haki bado yanaitaka uchunguzi huru wa kimataifa.
"Mashambulizi yanaweza kuwa uhalifu wa kivita," anasema Ramzi Kaiss kutoka Human Rights Watch.
Anayataja mashambulio hayo kuwa "yasiyolenga walengwa moja kwa moja," jambo linalokinzana na sheria za kimataifa za kibinadamu, ambazo zinakataza matumizi ya vifaa vilivyowekewa mabomu kwa siri.
Bwana Kaiss anaongeza kuwa kutokana na mlipuko kutokea kwa wakati mmoja katika maeneo mengi, haingewezekana kuhakikisha kuwa vifaa vya mawasiliano ya simu zilikuwa mikononi mwa walengwa halisi wakati zilipolipuka.
"Tuliona watoto waliokuwa na kifaa cha mawasiliano ya simu bila waya ambao walijeruhiwa, waliouawa, pamoja na wahudumu wa afya," anasema.
Mwezi Aprili mwaka jana, baraza la mawaziri la Lebanon liliagiza wizara ya mambo ya nje kuwasilisha tamko rasmi kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), likiiomba iwe na mamlaka ya kuchunguza na kufungua mashitaka ya uhalifu wa kivita uliofanyika katika ardhi ya Lebanon kuanzia tarehe 7 Oktoba 2023.
Ingawa Lebanon si mwanachama wa ICC, ombi hilo lingeweza kutoa fursa ya mahakama hiyo kupata mamlaka ya kuchunguza uhalifu ndani ya kipindi kilichoainishwa.
Hata hivyo, uamuzi huo ulifutwa baadaye bila sababu rasmi kutolewa.
Inaaminika kuwa serikali ya Lebanon ilikabiliwa na shinikizo kutoka pande mbalimbali, na baadhi walieleza hofu kwamba mamlaka ya ICC yangeweza kuingia katika masuala ambayo serikali isingependa yashughulikiwe.
Wakati shambulio la vifaa vya mawasiliano ya simu bila waya lilipotokea, Lebanon ilikuwa tayari katika hali ya mvutano wa kijeshi wa kiwango cha chini kati ya Hezbollah na Israel, hali iliyochochewa na mashambulizi ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba.
Shambulio hilo lilikuwa ishara kwamba hali ilikuwa karibu kuzorota kwa kiwango kikubwa.
"Viashiria vilikuwa wazi kuwa awamu ya ghasia kubwa katika vita dhidi ya Lebanon ilikuwa inakaribia kuanza," anasema Bwana Mawlawi.
Usiku huo, hali katika hospitali mbalimbali nchini Lebanon ilikuwa ya kutisha kama mazingira ya janga.
Madaktari walitumia saa nyingi mfululizo, wengine hata siku nzima, wakifanya upasuaji wa dharura kwa manusura wa mashambulio.
Tulizungumza na Dkt. Elias Warrak, daktari bingwa wa macho mwenye uzoefu mkubwa, siku moja baada ya tukio.
Alisema kwamba katika usiku mmoja tu, aliondoa macho yaliyoharibika zaidi ya aliyowahi kufanya katika taaluma yake yote.
"Wagonjwa wengi walikuwa ni vijana wa umri wa miaka ishirini, na katika baadhi ya walioumia nililazimika kutoa macho yote mawili," alisema. "Katika maisha yangu yote, sijawahi kushuhudia hali kama ile."
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, karibu watu 500 walipata majeraha makubwa ya macho kutokana na shambulio hilo.
Nayfe hakujua kinachoendelea kote nchini.
Karibu siku 10 baada ya tukio, alikuwa bado hajitambui akiwa katika usingizi mzito wa dawa hospitalini Saint George.
Alipoamka, alikuwa na upungufu wa kumbukumbu.
Ilimchukua miezi kadhaa kuanza kukumbuka matukio ya kipindi kabla ya shambulio.
Matibabu yake yamekuwa marefu na ya maumivu makali.
Shirika moja linalohusiana na Hezbollah, linaloitwa "Wounded Foundation", ndilo linalogharamia upasuaji, upandikizaji wa ngozi, tiba ya mazoezi ya viungo na msaada wa afya ya akili anaouhitaji.
Nayfe ni mfuasi wa Hezbollah kama ilivyo kwa sehemu kubwa ya jamii ya Kishia nchini Lebanon.
Ni mhitimu wa saikolojia, pia ana vyeti vya programu za kompyuta na uhasibu.
Alipata kazi hospitalini baada ya kutafuta ajira kwa muda mrefu, hali inayodhihirisha changamoto za ajira kwa vijana wengi kutokana na hali mbaya ya kiuchumi nchini Lebanon.
Sasa, Nayfe hutumia siku zake akisubiri kati ya upasuaji mmoja hadi mwingine.
Mama yake ndiye anayemsaidia kazi nyingi za nyumbani, ambapo Nayfe hukaa muda mwingi.
Hata hivyo, anasema ameweza kupiga hatua kubwa kupitia tiba ya mazoezi ya viungo.
Licha ya mateso makubwa aliyoyapitia, bado ana tabasamu lenye haiba na wakati mwingine hufurahia kwa kicheko cha ghafla.
Anacheka sana alipoulizwa kama hospitali aliyokuwa akifanya kazi bado wanatumia kifaa cha mawasiliano ya simu bila waya.
"Hapana. Hebu fikiria kama bado wangekuwa wanazitumia," anasema huku akicheka.
Ni nini kinachompa moyo wa kuendelea?, aliulizwa.
"Imani," anajibu papo hapo.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












