Tunachofahamu kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza makubaliano ya kusitisha mapigano ya miezi 13 kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Lebanon wanaoungwa mkono na Iran la Hezbollah.
Katika taarifa ya pamoja, Marekani na Ufaransa zimesema makubaliano hayo yatasitisha mapigano nchini Lebanon na "kuilinda Israel dhidi ya tisho la Hezbollah na makundi mengine ya kigaidi".
Haya ndiyo tunayojua kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyomo kwenye taarifa rasmi na ripoti za vyombo vya habari.
Mkataba wa kusitisha mapigano unakusudiwa kuwa wa kudumu
Rais wa Marekani Joe Biden amewaambia waandishi wa habari kwamba makubaliano hayo "yamepangwa kuwa usitishaji wa kudumu wa mapigano".
Chini ya masharti ya usitishaji mapigano, zaidi ya siku 60 Hezbollah itaondoa wapiganaji wake na silaha kutoka eneo la mstari wa Buluu - mpaka usio rasmi kati ya Lebanon na Israel na mto Litani, uliopo takriban kilomita 30 kaskazini.
Wapiganaji wa Hezbollah watachukuliwa na vikosi vya jeshi la Lebanon katika eneo hilo, ambao watahakikisha kuwa miundombinu au silaha zinaondolewa na kwamba haiwezi kujengwa upya, kwa mujibu wa afisa wa ngazi ya juu wa Marekani.
Katika kipindi hicho cha siku 60, Israel itaondoa hatua kwa hatua vikosi vyake vilivyosalia na raia, Biden alisema, akiongeza kuwa itawawezesha raia wa pande zote mbili za mpaka kurejea majumbani mwao.

Wanajeshi 5,000 wa Lebanon watachukua nafasi ya Hezbollah
Jeshi la Lebanon linatarajiwa kupeleka wanajeshi 5,000 kusini chini ya makubaliano hayo, kwa mujibu wa afisa wa Marekani.
Hata hivyo, maswali bado yanabaki kuhusu jukumu lao katika kutekeleza usitishaji mapigano, na iwapo watakabiliana na Hezbollah iwapo itahitajika, jambo ambalo linaweza kuzidisha mvutano katika nchi ambayo mgawanyiko wa kidini ni mkubwa.
Jeshi la Lebanon pia limesema halina rasilimali - fedha, nguvu kazi na vifaa - kutimiza majukumu yake chini ya makubaliano hayo, ingawa tatizo hilo linaweza kupunguzwa na michango kutoka kwa washirika wa kimataifa wa Lebanon.
Lakini maafisa wengi wa nchi za magharibi wanasema Hezbollah imedhoofishwa na kwamba huu ni wakati wa serikali ya Lebanon kurejesha udhibiti wa maeneo yote ya nchi hiyo.

Chanzo cha picha, Reuters
Nani atafuatilia utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mkataba huo unafuatia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1701, ambalo lilimaliza vita vya mwaka 2006 kati ya Israel na Hezbollah.
Chini ya azimio la 1701, maeneo ya kusini mwa Litani yanapaswa kuwa huru na bila silaha isipokuwa zile za serikali ya Lebanon na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa (Unifil).
Lakini pande zote mbili zililaumiana kuhusu ukiukaji wa azimio hilo.
Israel inasema Hezbollah iliruhusiwa kujenga miundombinu mikubwa katika eneo hilo, wakati Lebanon inasema ukiukaji wa Israel ulijumuisha ndege za kijeshi katika eneo lake.
Mara hii, Marekani na Ufaransa zitajiunga na utaratibu uliopo wa safari, ambao unahusisha kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa mataifa (Unifil), Lebanon na Israeli, ambao utafuatilia ukiukaji wa makubaliano, afisa mwandamizi wa Marekani alisema.
"Hakutakuwa na wanajeshi wa Marekani katika eneo hilo, lakini kutakuwa na msaada wa kijeshi kwa majeshi ya Lebanon, kama tulivyofanya katika siku za nyuma. Lakini katika hilim jeshi la Lebanon litashirikiana na jeshi la Ufaransa , "alisema afisa huyo.
Akielezea wasiwasi wa Israel, Biden alisema: "Hezbollaha haitaruhusiwa kujenga upya miundombinu ya kigaidi kusini mwa Lebanon ."
Israel inadai haki ya kujibu mashambulizi
Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu amesema Israel "itadumisha uhuru kamili wa kijeshi" nchini Lebanon "kwa uelewa kamili wa Marekani".
"Kama Hezbollah itakiuka makubaliano na kujaribu kujipa silaha, tutashambulia. Ikiwa itajaribu kujenga upya miundombinu ya kigaidi karibu na mpaka, tutashaimbulia. Ikiwa itarusha roketi, ikiwa itachimba handaki, ikiwa italeta lori lililobeba roketi, tutashambulia," alisema.
Biden aliunga mkono mtazamo huo, akiwaambia waandishi wa habari: "Ikiwa Hezbollah au mtu mwingine yeyote atavunja makubaliano hayo na kuwa tisho la moja kwa moja kwa Israel, basi Israel ina haki ya kujilinda kwa mujibu wa sheria za kimataifa."
Lakini pia alisema makubaliano hayo yanaunga mkono uhuru wa Lebanon.
Madai ya Israel ya haki ya kushambulia hayaaminiki kuwa sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano kwa sababu yalikataliwa na Lebanon. Ili kulishughulikia suala hilo, ripoti za vyombo vya habari zilisema kwamba Marekani itatoa barua inayounga mkono haki ya Israel ya kuchukua hatua.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi












