Marekani yaongeza msukumo katika juhudi za usitishaji mapigano kati ya Hezbollah na Israel
Juhudi za kusitisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah zimeongezeka, huku mjumbe wa Marekani akitarajiwa kurejea Lebanon kwa mazungumzo kuhusu uwezekano wa makubaliano.
Muhtasari
- Watu 10 wameuawa katika shambulio la usiku dhidi ya Sumy, maafisa wa Ukraine wasema
- Malal:Sikutarajia haki za wanawake zingepotea haraka hivyo
- Mtangazaji wa redio wa Australia amekamatwa dhidi ya madai ya unyanyasaji wa kingono
- Majirani wa Nordic wasambaza ushauri mpya wa kujiokoa wakati wa vita
- Msemaji wa Hezbollah ameuawa katika shambulizi la Israel mjini Beiru
- Takriban watu 34 wameuawa katika shambulizi la Israel kaskazini mwa Gaza
Moja kwa moja
Na Yusuf Jumah,Mariam Mjahid & Rashid Abdallah
Marekani inaipeleka dunia mahali hatari - Mwanasiasa wa Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Mbunge mmoja wa Urusi, Maria Butina, ameiambia BBC kwamba Marekani inatumia Ukraine na, katika mchakato huo, inazidisha mzozo kati yake na Urusi.
Ulimwengu hauhitaji "kuongezeka kwingine kwa vita," aliongeza, "hatua nyingine ya kuelekea, uwezekano, wa vita vya tatu vya dunia."
"Na wakati Marekani inacheza michezo ya kisiasa, kwa kweli wanaisukuma dunia kwenye mstari mwekundu hatari sana," Butina alionya.
Anaongeza kuwa ni jaribio la "kuongeza mgogoro kadri iwezekanavyo ili Trump asiweze kutimiza ahadi ya kusimamisha vita."
Unaweza kusoma;
Marekani yaongeza msukumo katika juhudi za usitishaji mapigano kati ya Hezbollah na Israel

Chanzo cha picha, EPA
Juhudi za kusitisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah zimeongezeka, huku mjumbe wa Marekani akitarajiwa kurejea Lebanon kwa mazungumzo kuhusu uwezekano wa makubaliano.
Haya yanajiri huku kukiwa na ongezeko la mashambulizi ya anga ya Israel kote nchini.
Kuongezeka kwa mapigano wiki iliyopita, ambayo yamewaua makumi ya watu nchini Lebanon, kunaonekana kuna lengo la kuishinikiza Hezbollah na serikali ya Lebanon kukubali makubaliano ya kumaliza migogoro huo uliodumu kwa mwaka mmoja.
Rasimu ya makubaliano hayo iliwasilishwa wiki iliyopita na balozi wa Marekani nchini Lebanon kwa Spika wa Bunge la Lebanon Nabih Berri, ambaye ameungwa mkono na Hezbollah kufanya mazungumzo.
Maelezo ya makubaliano hayo bado hayajafichuliwa lakini katika kile kinachoonekana kama ni dalili ya maendeleo ya mazungumzo hayo, Amos Hochstein, ambaye anaongoza juhudi za kidiplomasia za utawala wa Biden, alitarajiwa kurejea Beirut siku ya Jumanne.
Israel imeongeza mashambulizi yake ya angani kusini mwa Lebanon, ambako pia inafanya uvamizi wa ardhini katika bonde la Bekaa Mashariki na Beirut.
Unaweza kusoma;
Je,wandani wa rais mteule Trump wana maoni gani kuhusu Ukraine?

Chanzo cha picha, Getty Images
Donald Trump anatarajiwa kurejea Ikulu ya White House katika muda wa miezi miwili pekee.
Tayari amesema ananuia kumaliza vita nchini Ukraine kwa haraka - bila kutaja jinsi anavyopanga kufanya hivyo na anaweza kusitisha matumizi ya makombora mara tu atakapoingia madarakani.
Rais mteule wa Marekani Trump bado hajasema kama ataendeleza sera mpya ya makombora ya Biden, lakini baadhi ya washirika wake wa karibu tayari wameikosoa.
Donald Trump Jr, mtoto wa kiume wa Trump, aliandika kwenye mtandao wa kijamii: "Majeshi ya kijeshi ya viwanda yanaonekana kutaka kuanzisha Vita vya Tatu vya Dunia kabla ya baba yangu kupata nafasi ya kurejesha amani na kuokoa maisha."
Wengi wa maafisa wakuu wa Trump, kama vile Makamu wa Rais mteule JD Vance, anasema Marekani haipaswi kutoa msaada wowote zaidi wa kijeshi kwa Ukraine.
Lakini wengine katika utawala ujao wa Trump wana maoni tofauti. Mshauri wa Usalama wa Kitaifa Michael Waltz amedai kuwa Marekani inaweza kuharakisha uwasilishaji wa silaha kwa Ukraine ili kuilazimisha Urusi kufanya mazungumzo.
Rais mteule atachukua uamuzi gani kuhusu vita vinavyoendelea kati ya Ukraine na Urusi haijulikani. Lakini wengi nchini Ukraine wanahofia kwamba atakatiza usafirishaji wa silaha, ikiwa ni pamoja na ATACMS.
Unaweza kusoma;
Waliopoteza maisha kariakoo wafikia 16, tume yaundwa kutathimini ubora wa majengo

Chanzo cha picha, Ofisi ya Waziri Mkuu
Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema idadi ya waliopoteza maisha katika ajali ya kuanguka kwa jengo la ghorofa eneo la kariakoo nchini Tanzania imefikia 16.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo alipokuwa akihutubia wananchi kwenye viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam, alipokuwa akiongoza shughuli ya kuaga miili ya waliopoteza maisha.
Amesema athari ya kuanguka kwa ghorofa ni pamoja na kuharibika kwa mali nyingi, majeruhi wengi na mbaya zaidi ni vifo, ambapo amesema mpaka sasa waliookolewa wakiwa hai wamefikia watu 86.
Majeruhi walifikishwa kwenye hospitali mbalimbali za jijini na wengi wao wameruhusiwa huku watano wakiwa chini ya uangalizi wa karibu.
''Kutokana na athari hizi serikali imeendelea kuchukua hatua kunusuru maisha ya wenzetu ambapo shughuli za uokoaji zinaendelea''
''Kazi hiyo isisimame, usiku na mchana mpaka tuhakikishe mtu wa mwisho anaokolewa'' alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Serikali imesema inaendelea kugharamia matibabu kwa walioathirika, kwa kutoa mahitaji na gharama za mazishi kwa marehemu wote.
Bw. Majliwa amesema serikali itafanya uchunguzi maalumu kujua chanzo cha ajali na kumsaka mmiliki wa jengo ili kuisaidia polisi kwenye uchunguzi.
Imeunda tume ya watu 19 ili kuyapitia majengo yote ya maghorofa ili kujua ubora wa majengo na kuishauri serikali nini ifanye baada ya uchunguzi.
Mamia wajitokeza kutoa heshima za mwisho kwa waliofariki kariakoo Tanzania

Chanzo cha picha, EAGAN SALLA/BBC
Watanzania wamejitokeza kuaga miili ya waliopoteza maisha katika ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa katika soko kuu Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Hii leo miili imewasili katika viwanja vya mnazi mmoja kwa ajili ya kuagwa rasmi na mamia ya watu waliojitokeza viwanjani hapo.
Maelezo ya video, Mamia wajitokeza kutoa heshima za mwisho kwa waliofariki kariakoo Tanzania 
Chanzo cha picha, EAGAN SALLA/BBC

Chanzo cha picha, EAGAN SALLA/BBC

Chanzo cha picha, EAGAN SALLA/BBC

Chanzo cha picha, EAGAN SALLA/BBC
Biden 'anauchochea moto' mzozo, Urusi yasema

Chanzo cha picha, Getty Images
Iwapo makombora yaliyotolewa na Marekani yatarushwa hadi ndani kabisa ya Urusi, Moscow italiona shambulio hilo kama si la Ukraine, bali kutoka Marekani yenyewe, taarifa kutoka Kremlin asubuhi ya leo inasema.
Inaongeza kuwa Urusi na Putin wameweka wazi misimamo yao, na kwamba uamuzi wa Marekani unaonesha kiwango kipya cha ushiriki wa Washington katika mzozo huo.
Taarifa hiyo zaidi ilisema ni "dhahiri" kwamba utawala wa Biden unaomaliza muda wake unakusudia kuchukua hatua za kuongeza "mafuta kwenye moto" na kuchochea kuongezeka zaidi kwa mvutano.
Unaweza kusoma;
Marekani inaona matumizi ya wanajeshi Korea Kaskazini nchini Urusi ni ''kuzidisha mzozo''

Chanzo cha picha, Korean Central News Agency
Inafahamika kuwa uamuzi wa Rais Biden wa kuiruhusu Ukraine kushambulia eneo la Urusi kwa makombora ya Marekani ni jibu la moja kwa moja kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini wanaopigana pamoja na vikosi vya Urusi.
Mapema mwezi huu, maafisa wa Ukraine walifichua kuwa wanajeshi wao walipigana na wanajeshi wa Korea Kaskazini katika eneo la Kursk nchini Urusi.
Mnamo Juni, Korea Kaskazini na Urusi zilitia saini mkataba wa ulinzi wa pande zote, ikimaanisha kuwa watasaidiana ikiwa watashambuliwa.
Katika mazungumzo ya nadra ya simu na Rais wa Urusi Vladimir Putin siku ya Ijumaa, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alimwambia Putin moja kwa moja kwamba ushiriki wa Korea Kaskazini ulikuwa "ongezeko kubwa" la mzozo.
Unaweza kusoma;
Ukraine tayari imepata makombora ya ATACMS - na imeyatumia

Chanzo cha picha, Vikosi vya Wanajeshi vya Ukrain
Marekani kwa mara ya kwanza iliipatia Ukraine makombora ya ATACM zaidi ya mwaka mmoja uliopita - lakini yatumike tu ndani ya ardhi ya Ukraine.
Ukraine imetumia makombora ya masafa marefu yaliyotolewa na Marekani, yenye masafa ya hadi kilomita 300 (maili 186), huko Berdyansk na Luhansk mashariki mwa nchi hiyo, pamoja na Crimea.
Moscow ilitwaa Crimea kinyume cha sheria mwaka 2014 na ni nchi chache tu zinazotambua peninsula hiyo kama eneo la Urusi.
Kwa hivyo haikuangukia chini ya matakwa ya Marekani kwamba Ukraine ijizuie kutumia silaha zilizotolewa na Washington kushambulia eneo la Urusi.
Ufaransa na Uingereza pia zimetoa mchango wa makombora, yanayojulikana kama Stormshadows, chini ya vizuizi sawa na kwamba yatumike tu ndani ya eneo la Ukraine.
Vizuizi hivyo sasa vinatarajiwa kuondolewa
Kufikia sasa, Putin hajasema lolote

Chanzo cha picha, Reuters
Wanasiasa wa Urusi walijibu kwa hasira ripoti kwamba Rais Biden ameiruhusu Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu ya Marekani kushambulia ndani ya Urusi.
Mbunge wa Urusi Leonid Slutsky, mkuu wa chama kinachounga mkono Kremlin Liberal-Democratic Party, alitabiri kwamba "itasababisha kuongezeka kwa hali mbaya, na kutishia matokeo mabaya".
Seneta mwandamizi wa Urusi Vladimir Dzhabarov aliiita "hatua isiyo na kifani kuelekea Vita vya Tatu vya dunia".
Lakini cha muhimu sana katika Urusi ya Vladimir Putin ni kile anachosema Vladimir Putin.
Na, hadi sasa, hajasema chochote.
Yeye hata hivyo alisema mengi kabla. Katika miezi ya hivi karibuni, Kremlin imefanya ujumbe wake kwa nchi za Magharibi kuwa wazi: msifanye hivi, msiondoe vikwazo juu ya matumizi ya silaha zenu o za masafa marefu, msiruhusu Kyiv kushambulia ndani ya eneo la Urusi na makombora hayo.
Mnamo Septemba Rais Putin alionya kwamba ikiwa hii itaruhusiwa kutokea, Moscow itachukulia kama "ushiriki wa moja kwa moja" wa nchi za Nato katika vita vya Ukraine.
Unaweza pia kusoma
Watu 11wameuawa katika shambulio la usiku dhidi ya Sumy, maafisa wa Ukraine wasema

Chanzo cha picha, Sumy prosecutor's office
Watu 11 waliuawa, wakiwemo watoto wawili, wakati kombora la Urusi lilipopiga kitongoji cha makazi yenye watu wengi katika mji wa kaskazini-mashariki wa Sumy usiku kucha, kulingana na maafisa wa Ukraine.
Watu wengine 55 walijeruhiwa katika shambulio hilo, wakiwemo watoto wanane, Huduma ya Dharura ya eneo hilo la Ukraine inasema.
Takriban majengo 10 ya ghorofa na magari yaliharibiwa, baraza la jiji la Sumy linaripoti.
Ukraine yasema ilidungua droni nane za Urusi usiku
Kikosi cha anga cha Ukraine kilitungua ndege nane kati ya 11 zilizorushwa usiku kucha, Jeshi la Wanahewa la Ukraine limesema.
Ndege zisizo na rubani za Shahed - zinazojulikanapia kama "kamikaze" drones - zilipigwa risasi juu ya mikoa ya Poltava, Kharkiv, Cherkasy, Chernihiv na Kyiv , wakati nyingine tatu zilitajwa kama 'zilizopotea'
Urusi pia ilishambulia eneo la Sumy nchini Ukraine kwa makombora mawili ya balistiki ya Iskander-M na kombora la Kh-59, jeshi la anga linaongeza.
Unaweza pia kusoma
Malal:Sikutarajia haki za wanawake zingepotea haraka hivyo

Chanzo cha picha, Picha za Getty
Risasi ilishindwa kumnyamazisha, sasa Malala Yousafzai anapaza kupigania haki za wanawake Afghanistan.
Baada ya miaka miwili tangu Taliban iteke Afghanistan ,haki za wanawake zimepuuzwa mno kiasi cha kwamba ni marufuku kwa wanawake kuimba.
Malala amewahi kujipata mashakani katika himaya ya kundi la Taliban mpakani Pakistan,kufuatia waasi walio na misimamo mikali kuwashambulia na kumpiga risasi akiwa katika basi la shule.
Mabadiliko yanayoendelea kushuhudiwa Afghanistan kama sio ukatili pia kinachomtamausha Malala ambaye alinusurika kupigwa risasi 2012 amejipata akifanya kampeini ya usawa.
"Sikutarajia haki za wanawake hazitatiliwa maanani haraka hivyo," Malala ameiambia idhaa ya BBC ya Asia Mwaka 2021,kundi la Taliban ilirejea madarakani Afghanistan ,miaka 20 baada ya uvamizi ulioongozwa na marekani kuondoa utawala wa Taliban kufuatia shambuiza la 9/11.
Tangu wakati huo wanawake nchini Afghanistan wamekumbana na vikwazo vikali chini ya sheria za maadili za Taliban.
Sheria hizi zinahusisha kanuni za mavazi ,ambazo zinawalazimisha wanawake kuvaa mavazi kamili ya kujisitiri,na pia zinakataza wanawake kusafiri bila msimamizi wa kiume au kuwaaangalia wanaume machoni isipokuwa wanahusiana kifamilia au ndoa.
Shirika la Umoja wa mataifa limeelezea sheria kama hizi ni kama “ubaguzi wa kijinsia”mfumo wa unaguzi wa kijamii na kiuchumi unaotokana na jinsia.
Licha ya mazingira kama haya, wanawake wa Afghanistan wanaendelea kupinga na kupigania haki zao, mara nyingi wakihatarisha maisha yao.
Malala Yousafzai, ambaye anajulikana katika filamu Bread & Roses, anasisitiza ujasiri wa wanawake hawa na anatoa wito wa msaada wa kimataifa na shinikizo kwa Taliban kurejesha haki za wanawake.
Filamu hii inatilia mkazo mapambano na ujasiri wa wanawake wa Afghanistan, huku Malala akielezea matumaini kwamba ujasiri wao utaongeza mshikamano na hatua ya kimataifa.
Unaweza pia kusoma
Mtangazaji wa redio wa Australia amekamatwa dhidi ya madai ya unyanyasaji wa kingono

Chanzo cha picha, Getty Images
Mtangazaji maarufu wa redio wa Australia, ambaye pia alikuwa mkufunzi wa timu ya Wallabies, Alan Jones, amekamatwa baada ya uchunguzi wa kina kufanywa kuhusu madai ya unyanyasaji wa kingono.
Maafisa wa polisi wa New South Wales wamesema kuwa wajasusi kutoka kitengo cha kulinda watoto dhidi ya unyanyasaji walimkamata mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 83, aliyekuwa akiishi katika eneo la Sydney Circular Quay, jumatatu asubuhi, kabla ya kutekeleza msako nyumbani kwake.
Kikosi cha kufuatilia kesi hiyo kilianzishwa mwezi Machi ili kuchunguza tuhuma za unyanyasaji wa kingono na vurugu za kimwili zilizodaiwa kufanywa kati ya mwaka 2001 na 2019, kulingana na ripoti zao.
Bwana Jones ni miongoni mwa watangazaji maarufu wa Australia na awali alikanusha mashitaka dhidi yake, baada ya tuhuma hizo kuripotiwa katika gazeti la Sydney Morning Herald mwaka 2023.
Kulingana na kamishna wa polisi wa NSW, Karen Webb, wanatarajia waathiriwa zaidi kuwasilisha ripoti za unyanyasaji dhidi ya Jones, kama ilivyokuwa kwa kesi za aina hiyo.
Bwana Jones pia amekuwa akishtakiwa kwa makosa ya kuharibu majina ya watu mara kadhaa. Maafisa wa polisi wanatarajiwa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na kesi hiyo wakati wowote kutoka sasa.
Majirani wa Nordic wasambaza ushauri mpya wa kujiokoa wakati wa vita

Chanzo cha picha, TT News Agency/AFP
Jumatatu hii, mamilioni ya Waswidi wataanza kupokea nakala fupi ya kuwashauri jinsi ya kujiandaa na kuvumilia iwapo vita vitatokea au majanga ya dharura.
Nakala hii, inayoitwa “Iwapo Majanga au Vita Vitatokea,” imetengenezwa upya baada ya miaka sita, kutokana na tahadhari ya utovu wa usalama kutoka serikali ya Stockholm, ikielezea ongezeko la mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine. Ukubwa wa nakala hii ni mara mbili ya ile ya awali.
Nchi jirani kama Finland pia imechapisha ushauri mitandaoni kwa raia wake kuhusu jinsi ya kukabiliana na kujiandaa iwapo vita vitazuka.
Vilevile, raia wa Norway wametolewa nakala zinazowaasa kujiandaa na kujisimamia kwa wiki moja iwapo hali itachafuka, vita, au majanga mengine.
Uswidi ilijiunga na muungano wa kijeshi wa NATO, kama vile Finland, baada ya Moscow kupanua mipaka ya vita mwaka 2022. Norway ilikuwa mwanachama mwanzilishi wa muungano wa ulinzi wa magharibi.
“Tumesambaza nakala milioni 2.2, kila familia iliyoko Norway ikipokea ushauri huu,” alisema Tore Kamfjord, msimamizi wa kampeni ya kujilinda na kujiandaa kikamilifu katika Idara ya Ulinzi wa Raia wa Norway (DSB).
Soma zaidi
Msemaji wa Hezbollah ameuawa katika shambulizi la Israel mjini Beirut

Chanzo cha picha, Reuters
Msemaji wa Hezbollah Mohammed Afif ameuawa katika shambulizi la Israel mjini Beirut ,mauaji hayo yakithibitishwa na mkuu wa wanajeshi wa Lebanon.
Shambulio liligonga makao makuu ya chama cha kisiasa cha Baath katika eneo lina watu wengi la Ras al-Naba jumapili hii ni kulingana na vyanzo vya habari vinavyomilikiwa na serikali ya Lebanon.
Afif ambaye ni mmoja wa wachache waliobakia wa kundi hilo alionekana mara ya mwisho jumatatu wiki jana akitoa taarifa katika kongamano la mashinani kusini mwa Beirut ambako kundi hilo limekita kambi.
Shambulio hili limeuawa watu 4 na kujeruhi 14 linajiri kufuatia kampeni ya Israel dhidi ya Hezbollah ambayo imeongezeka tangu mwishoni mwa mwezi Septemba.
Shambulio hili linaonekana kama sehemu ya mkakati wa Israel wa kulenga Hezbollah zaidi ya viongozi wa kijeshi.
Zaidi ya watu 3,400 wameuawa nchini Lebanon tangu Israel ilipoanza kuzidisha mashambulizi yake kufuatia msaada wa Hezbollah kwa Hamas.
Vita hivi imesababisha zaidi ya watu milioni 1.2 kukimbia makwao.
Soma zaidi
Takriban watu 34 wameuawa katika shambulizi la Israel kaskazini mwa Gaza

Chanzo cha picha, Getty Images
Mashambulizi ya anga ya Israel kwenye jengo la ghorofa tano la makazi huko Beit Lahia kaskazini mwa Gaza yamesababisha vifo vya takriban watu 34, shirika la ulinzi wa raia la eneo hilo linasema.
Shirika hilo, lililonukuliwa na AFP, lilisema wengi wa waliofariki ni wanawake na watoto, huku makumi ya watu wakihofiwa kuwa chini ya vifusi. Watu saba pia walijeruhiwa.
Jeshi la Israel limesema limekuwa likishambulia maeneo ya wanamgambo kaskazini mwa Gaza, ikiwemo Beit Lahia, katika jaribio la kuwazuia Hamas kujipanga upya.
Kwingineko, katikati mwa Gaza mashambulizi matatu tofauti dhidi ya kambi za wakimbizi yamesababisha vifo vya watu 15, huku wengine watano wakiuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Israel huko Rafah kusini, ulinzi wa raia uliongeza.
"Uwezekano wa kuokoa waliojeruhiwa unapungua kwa sababu ya ufyatuaji risasi unaoendelea na mizinga," msemaji wa ulinzi wa raia Mahmud Bassal alisema.
Kilichosalia kwenye jengo la makazi huko Beit Lahia ni rundo la vifusi, na saruji iliyovunjika na vipande vya chuma vilivyosokotwa vinavyotoka kwenye magofu.
Mwanamume mmoja, ambaye familia yake iliishi katika jengo hilo, lakini alikuwa anakaa mahali pengine, alisema, akinukuliwa na AFP: "Sote tulifikiri kwamba kifo kilikuwa karibu."
"Eneo lote lilikuwa linatetemeka."
Jeshi la Israel lilisema mashambulizi yake kaskazini mwa Gaza - yaliyoanzia Jabalia na kuzidishwa hadi Beit Lahia - yalihusisha mashambulizi kadhaa usiku kucha kwa kile ilichokiita "lengo la kigaidi katika eneo hilo".
Iliongeza katika taarifa kwamba "kumekuwa na juhudi za kuendelea kuwaondoa raia kutoka eneo la vita ".
Lakini wakazi wengi wa eneo hilo hawataki kuacha nyumba zao. Bw Bassel alisema familia sita ziliishi katika jengo lililoharibiwa huko Beit Lahia.
Mwanamke mmoja katika eneo hilo alielezea hasira yake kwa BBC News.
"Tumewakosea nini watu, tumewasababishia madhara gani? Tumefanya kosa gani, tunakaa majumbani mwetu, mbona mnatufukuza?"
Unaweza pia kusoma
Hujambo na Karibu
Karibu tena kwa matangazo yetu ya moja kwa moja leo Jumatatu tarehe 18 Novemba ,2024.

