Ni nini kilitokea kwa wanawake ambao waliipinga Taliban?

Chanzo cha picha, Parwana Ibrahimkhail Nijrabi
Baada ya Taliban kuzuia uwezo wa wanawake wa Afghanistan kufanya kazi, kujifunza na kutoka hadharani, baadhi ya wanawake awali walikaidi sheria hizi mpya, wakiingia mitaani kuandamana.
Lakini hivi karibuni, wale waliokusanyika katika mji mkuu Kabul na miji mingine mikubwa kudai "chakula, kazi, uhuru" walihisi nguvu kamili ya Taliban.
Waandamanaji wanaiambia BBC kuwa walipigwa, walinyanyaswa, walifungwa jela na hata kutishiwa kuuawa kwa kupigwa mawe.
Tunazungumza na wanawake watatu ambao walipinga serikali ya Taliban baada ya kuanza kuweka vizuizi kwa uhuru wa wanawake baada ya Taliban kuchukua mamlaka tarehe 15 Agosti 2021.
Tarehe 14 Juni inaadhimisha siku 1000 za amri ya Taliban ambayo ilipiga marufuku wasichana kupata elimu zaidi ya mwaka wa sita.
Maandamano mjini Kabul

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati wanamgambo wa Taliban walipoteka Kabul tarehe 15 Agosti 2021, maisha ya Zakia yalianza kuporomoka.
Alikuwa mlezi wa familia yake kabla ya Taliban kurejea madarakani, lakini alipoteza kazi yake haraka baada ya kutwaa madaraka.
Wakati Zakia (jina bandia) alipojiunga na maandamano zaidi ya mwaka mmoja baadaye mnamo Desemba 2022, ilikuwa fursa yake ya kwanza kueleza hasira yake ya kupoteza haki ya kufanya kazi na elimu.
Waandamanaji walikuwa wakiandamana hadi Chuo Kikuu cha Kabul, kilichochaguliwa kwa "umuhimu wake wa mfano", lakini walisimamishwa kabla ya kufika wanakokwenda.
Zakia alikuwa akipiga kelele kwa sauti kubwa wakati polisi wa Taliban waliokuwa na silaha walipokomesha uasi wake wa muda mfupi.
"Mmoja wao alinyooshea bunduki yake mdomoni mwangu na kutishia kuniua pale pale ikiwa sitanyamaza," anakumbuka.
Zakia aliwaona waandamanaji wenzake wakiwa wamekusanyika kwenye gari.
"Nilipinga. Walikuwa wakipindisha mikono yangu," anasema. "Nilikuwa nikivutwa na Taliban ambao walikuwa wakijaribu kunipakia kwenye gari lao na waandamanaji wenzangu wengine."
Mwishowe, Zakia alifanikiwa kutoroka, lakini kile alichokiona siku hiyo kilimfanya kuwa na hofu kwa siku zijazo.
"Vurugu hazikuwa zikifanyika nyuma ya milango iliyofungwa tena," anasema, "zilikuwa zikifanyika katika mitaa ya mji mkuu Kabul mbele ya watu wote."
Kukamatwa na kupigwa
Mariam (si jina lake halisi) na mwanafunzi mwenye umri wa miaka 23 Parwanah Ebrahimkhel Najarabi walikuwa miongoni mwa waandamanaji wengi wa Afghanistan ambao walizuiliwa baada ya unyakuzi wa Taliban.
Akiwa mjane na mlezi pekee wa watoto wake, Mariam aliogopa kwamba hangeweza kuhudumia familia yake wakati Taliban ilipoanzisha sheria zinazozuia uwezo wa wanawake kufanya kazi.
Alihudhuria maandamano mnamo Desemba 2022. Baada ya kuona waandamanaji wenzake wakikamatwa, alijaribu kukimbia lakini hakutoroka kwa wakati.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Nilitolewa nje ya teksi kwa nguvu, wakapekua begi langu na kupata simu yangu," anakumbuka.
Alipokataa kuwapa maafisa wa Taliban nambari yake ya pasi, anasema mmoja wao alimpiga ngumi kali sana akafikiri kwamba ngoma ya sikio lake ilikuwa imepasuka.
Kisha wakapitia video na picha kwenye simu yake.
"Walikasirika na kunishika kwa kunivuta nywele," anasema. "Walinishika mikono na miguu na kunitupa nyuma ya gari aina ya Ranger."
"Walikuwa na jeuri sana na mara kwa mara waliniita kahaba," Mariam anaendelea. "Walinifunga pingu na kuniweka mfuko mweusi kichwani, sikuweza kupumua."
Mwezi mmoja baadaye, Parwanah pia aliamua kuandamana dhidi ya Taliban, pamoja na kundi la wanafunzi wenzake, kuandaa maandamano kadhaa.
Lakini hatua yao pia ilikabiliwa na kisasi cha haraka.
"Walianza kunitesa tangu waliponikamata", anasema Parwanah.
Alilazimishwa kuketi kati ya walinzi wawili wa kiume wenye silaha.
"Nilipokataa kukaa pale walinisogeza mbele, wakanifunika blanketi kichwani na kunielekezea bunduki na kuniambia nisisogee."
Parwanah alianza kuhisi "dhaifu na kama mfu anayetembea" kati ya watu wengi wenye silaha nzito.
"Uso wangu ulikuwa umekufa ganzi kwani walinipiga makofi mara nyingi sana. Niliogopa sana, mwili wangu wote ulikuwa ukitetemeka."
Maisha ya gerezani
Mariam, Parwanah na Zakia walikuwa wanafahamu kikamilifu madhara yanayoweza kutokea ya maandamano ya umma.
Parwanah anasema hakuwahi kutarajia Taliban "kumtendea kama binadamu". Lakini anasema bado alishangazwa na unyanyasaji wake.
Chakula chake cha kwanza gerezani kilimwacha katika mshtuko.
"Nilihisi kitu chenye ncha kali kikichoma mdomo wangu," anasema. "Nilipotazama, ulikuwa msumari nilitupa."
Katika milo iliyofuata, alikuta nywele na mawe.
Parwanah anasema aliambiwa atauawa kwa kupigwa mawe, huku wakimuacha akilia hadi usiku na kuota ndoto za kupigwa mawe akiwa amevalia kofia.
Msichana huyo mwenye umri wa miaka 23 alishtakiwa kwa kuendeleza uasherati, ukahaba na kueneza utamaduni wa kimagharibi na alikuwa gerezani kwa takribani mwezi mmoja.
Mariam aliwekwa kwenye kitengo cha ulinzi kwa siku kadhaa, ambapo alihojiwa huku akiwa amefunikwa mfuko mweusi kichwani.
"Niliweza kusikia watu kadhaa, mmoja alinipiga teke na kuuliza ni nani aliyenilipa kazi ya kuandaa maandamano," anakumbuka. "Mwingine alinipiga ngumi na kusema 'Unafanya kazi kwa ajili ya nani?'
Mariam anasema aliwaambia waliomhoji kuwa alikuwa mjane ambaye alihitaji kazi ya kuwalisha watoto wake wawili, lakini anasema majibu yake yalisababisha vurugu zaidi.

Chanzo cha picha, Parwana Ibrahimkhail Nijrabi
Kukiri na kuachiliwa
Parwanah na Mariam wote waliachiliwa tofauti kufuatia uingiliaji kati wa mashirika ya haki za binadamu na wazee wa eneo hilo, na sasa hawaishi tena Afghanistan.
Wote wawili wanasema walilazimishwa kutia saini maungamo ya kukiri hatia na kuahidi kutoshiriki katika maandamano yoyote dhidi ya Taliban.
Ndugu zao wa kiume pia walitia saini karatasi rasmi za kuahidi kuwa wanawake hao hawatashiriki maandamano yoyote zaidi.
Tuliweka madai haya kwa Zabihullah Mujahid, msemaji mkuu wa serikali ya Taliban, ambaye alithibitisha kuwa wanawake hao walikamatwa lakini akakanusha kuwa walitendewa vibaya.
“Baadhi ya wanawake waliokamatwa walijihusisha na vitendo ambavyo ni kinyume na serikali na dhidi ya usalama wa raia,” alisema.
Anapinga madai ya wanawake na anakanusha kutesa kulitumika: "Hakuna kupigwa katika jela yoyote ya Imarati ya Kiislamu na chakula chao pia kimeidhinishwa na timu zetu za matibabu."
Ukosefu wa vifaa vya msingi
Mahojiano ya Human Rights Watch na baadhi ya waandamanaji baada ya kuachiliwa kwao yalithibitisha madai yaliyosikilizwa na BBC.
"Taliban wanatumia kila aina ya mateso na hata kufanya familia zao kulipa maandamano haya, wakati mwingine wanawafunga na watoto wao katika hali mbaya," alisema Ferishtah Abbasi wa HRW.
Mtafiti wa Amnesty International Zaman Soltani, ambaye alizungumza na waandamanaji kadhaa baada ya kuachiliwa, alisema magereza hayana vifaa vya msingi.
"Hakuna mfumo wa kupasha joto wakati wa baridi, wafungwa hawapewi chakula kizuri au cha kutosha na masuala ya afya na usalama hayazingatiwi hata kidogo," Soltani alisema.
Kutamani maisha ya kawaida

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati wa kuchukua madaraka, Taliban walisema wanawake wanaweza kuendelea kufanya kazi na kwenda shule, na tahadhari kwamba hii inaweza tu kutokea kulingana na utamaduni wa Afghanistan na Sharia.
Wanaendelea kusisitiza kuwa marufuku ya shule kwa wasichana baada ya mwaka wa sita ni ya muda lakini hawajatoa dhamira thabiti ya kufungua tena shule za upili za wasichana.
Huko Afghanistan, Zakia alichukua nafasi moja zaidi na kuzindua kituo cha masomo ya nyumbani ili kusomesha wasichana wadogo. Hii pia ilishindwa.
"Wanahisi kutishwa na kikundi cha wanawake kukusanyika mahali mara kwa mara," anasema, sauti yake iliyojaa huzuni. "Taliban waliweza kufanya walichotaka. Mimi ni mfungwa katika nyumba yangu mwenyewe."
Bado anakutana na wanaharakati wenzake lakini hawapangi maandamano yoyote. Wanachapisha taarifa za mara kwa mara kwenye mitandao ya kijamii kwa kutumia jina bandia.
Alipoulizwa kuhusu ndoto zake kwa Afghanistan, anaangua kilio.
"Siwezi kufanya chochote. Hatupo tena, wanawake wanaondolewa katika maisha ya umma. Wasichana wenye umri wa zaidi ya miaka 12 bado hawawezi kwenda shule. Tulichotaka ni haki zetu za msingi, ilikuwa ni ombi kubwa kulidai?"
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












