Je, Taliban wanakiuka mafunzo ya Quran? Kwa nini elimu ya wanawake ni marufuku Afghanistan?

Chanzo cha picha, ADELA
"Sikuwa na hofu hata kidogo, kwa sababu nadhani mahitaji yangu ni ya haki," alisema msichana wa Afghanistan mwenye umri wa miaka 18.
Ndoto zake zilikatizwa wakati Taliban ilipopiga marufuku wanawake kutoka elimu ya juu.
Akiwa amekasirishwa na matarajio ya kupoteza maisha yake ya baadaye, mwanamke huyo (jina limebadilishwa kwa ajili ya usalama) alifanya maandamano ya ajabu ya peke yake mbele ya Chuo Kikuu cha Kabul, akinukuu aya za Qur'an.
Siku ya Jumapili, Desemba 25, Adela alikuwa amesimama mbele ya lango la chuo kikuu akiwa ameshikilia kadibodi iliyoandikwa neno "Iqra" - "Soma" kutoka kwenye Quran. Kwa mujibu wa Uislamu, neno hili ni amri ya kwanza iliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu kwa Mtume Muhammad.
"Mwenyezi Mungu ametupa haki ya kupata elimu. Tunapaswa kumwogopa Mwenyezi Mungu, sio Taliban ambao wanataka kuchukua haki zetu," aliiambia BBC.
Maandamano ya mtu mmoja
"Nilijua kwamba wanawatendea waandamanaji vibaya sana. Wanawapiga, wanatumia silaha wanatumia shoti za umeme na maji ya kuwasha dhidi yao. Lakini hata hivyo nilisimama kuwapinga," alisema Adela katika mahojiano na idhaa ya BBC nchini Afghanistan.

Chanzo cha picha, Adela
"Mwanzoni hawakunichukulia kwa uzito. Baadaye, mmoja wa watu wenye silaha aliniomba niondoke."
Mwanzoni, Adela alikataa kuondoka na kubaki pale alipokuwa, lakini bango lililokuwa mkononi mwake polepole lilivutia umakini wa walinzi wenye silaha waliokuwa karibu naye. Alishikilia bango hilo kwa nguvu na kumhutubia mwanachama wa Taliban.
Nilimuuliza: "Je, huwezi kusoma nilichoandika?" Hakusema chochote, hivyo Adela akaendelea: "Je, huwezi kusoma neno la Mungu?"

Chanzo cha picha, ADELA
"Alikasirika na kunitisha." Bango lilichukuliwa kutoka kwake na ilimbidi kuondoka kama dakika 15 baada ya maandamano yake pekee.
Wakati akipinga, dada yake alikuwa ameketi kwenye teksi na kuchukua picha na video za maandamano hayo. "Dereva teksi alikuwa akiwaogopa sana Taliban. Alimuomba dada yangu Sun aache kupiga picha. Akamtaka ashuke kwenye gari ili kusiwe na tatizo."
Kuongezeka kwa vikwazo dhidi ya wanawake
Baada ya kuondoka kwa haraka kwa vikosi vya kimataifa vinavyoongozwa na Marekani, Taliban walirejea madarakani nchini Afghanistan mwezi Agosti 2021.

Chanzo cha picha, AFP
Baada ya yote, walikataza wasichana kwenda shule za sekondari.
Septemba mwaka huu, waliwapiga marufuku wasichana kusoma baadhi ya masomo na kuwaambia kuwa wanaweza kuchagua vyuo vikuu vya mkoa wao pekee.
Mnamo Desemba 20, waliwapiga marufuku wanawake kutoka elimu ya juu, na kusababisha kulaaniwa kimataifa, na siku chache baadaye pia waliwapiga marufuku kufanya kazi katika mashirika ya ndani na ya kimataifa yasiyo ya kiserikali.
Tangu wakati huo, wanawake, hasa wanafunzi wa vyuo vikuu, wamekuwa wakiandamana kupinga marufuku ya elimu.
Baadhi yao wanaimba kauli mbiu "Wanawake, maisha, uhuru" iliyoenezwa katika maandamano ya hivi karibuni nchini Iran.
Maafisa wa Chuo Kikuu cha Kabul, ambako vitivo vinne kwa sasa vinaongozwa na wanawake, waliiambia BBC kwamba maprofesa wa kike sasa wamepigwa marufuku kuingia chuoni hapo.
Wito kwa wanaume
Kupigana na Taliban sio rahisi kwa wanawake kama Adela. Anataka wanaume waonyeshe ujasiri huo huo, lakini itawagharimu.

Chanzo cha picha, SWAMINATHAN NATARAJAN
"Wakati wa maandamano yangu, kijana mmoja alijaribu kuchukua video ili kuniunga mkono. Alipigwa sana," Adela anakumbuka.
Profesa mmoja wa kiume alirarua diploma yake kwenye runinga ya moja kwa moja kwa kupinga, na vyanzo viliiambia BBC kwamba zaidi ya maprofesa 50 wa vyuo vikuu wamejiuzulu kwa maandamano.
Mwalimu aliyegoma aliiambia BBC kwamba aliondoa barua yake ya kujiuzulu baada ya kupigwa na Taliban.
Lakini Adela anaamini kwamba ni muhimu kwa wanaume wa Afghanistan kujiunga na mapambano haya. "Sasa nchini Afghanistan, kuna wanaume wachache sana wanaotuunga mkono.
Nchini Iran, wanaume wanasaidia dada zao na kupigania haki za wanawake. Ikiwa tutatetea haki ya elimu kwa pamoja, tutapata mafanikio ya asilimia 100."















