Afghanstan: Taliban yafunga vyuo vikuu kwa wanawake

Chanzo cha picha, Getty Images
Taliban imetangaza kufungwa kwa masomo ya vyuo vikuu kwa wanawake nchini Afghanstan kulingana na barua ya wizara ya elimu ya juu.
Waziri anasema hatua hiyo inachukuliwa hadi taarifa nyingine itakapotolewa baadaye.
Taarifa hiyo ya wizara ya elimu ya juu pia inawazuia wanawake kupata elimu rasmi, kwa sababu tayari walikuwa wamezuiwa kuhudhuria masomo ya sekondari
Mwanafunzi mmoja mjini Kabul ameiambia BBC kwamba amekuwa akilia tangu aliposikia taarifa hiyo.
Miezi mitatu iliyopita maelfu ya wasichana na wanawake walifanya mtihani wa kujiunga na Chuo Kikuu kote nchini Afghanistan.
Lakini masharti yaliwekwa kote kuhusu masomo ambayo wangeyapata, huku wakiwekewa masharti magumu kabisa ya kujiunga na vitivo vya sayansi ya mifugo, uhandisi, uchumi na kilimo pamoja na uandishi wa habari.
Baada ya Taliban kuchukua mamlaka mwaka jana, vyuo vikuu vilianzisha ubaguzi wa kijinsia katika vyumba vya madarasa na milango ya kuingia vyuoni.
Wanafunzi wanawake walikuwa wakifundishwa tu na maprofesa wanawake pekee au wakufunzi wa kiume wa umri wa juu.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Akijibu kuhusu marufuku ya sasa, mwanafunzi mmoja wa kike aliiambia BBC kwamba alifikiri Taliban walikuwa wanahofia wanawake na mamlaka yao.
"Wamekata daraja pekee ambalo lingeniunganisha na hali yangu ya baadaye ‘’, alisema.
"Ninaweza kusema vipi? Ninaamini kwamba ningeweza kusoma na kubadili hali yangu ijayo au kuleta mwangaza kwa maisha yangu lakini wameuharibu."
Sekta ya elimu ya Afghanistan iliathiriwa pakubwa baada ya Taliban kuchukua utawala na kumekuwa na wasomi wachache waliopata mafunzo baada ya kuondoka kwa vikosi vilivyoongozwa na Marekani mwaka jana.
Mwanamke mwingine alizungumzia kuhusu "kupitia magumu mengi sana" alipojaribu kuendelea na elimu yake baada ya Taliban kuchukua mamlaka ya nchi.
Aliiambia BBC: "Tulipigana na makaka zetu, na mababa zetu, na jamii na hata na serikali.
"Tulipitia hali ngumu ili tuweze tu kuendelea na elimu yetu.
Wakati ule walau nilikuwa mwenye furaha kwamba ningeweza kuhitimu Chuo kikuu na kuafikia ndoto zangu. Lakini, sasa ninawezaje kujishawishi mwenyewe?"
Uchumi wa Afghanistan umekuwa ukitegemea kwa kiasi kikubwa misaada ya kigeni, lakini mashirika ya misaada kwa sehemu na baadhi kwa uangalifu mkubwa – yameondoa usaidizi wake katika sekta ya elimu baada ya Taliban kukataa kuwaruhusu wasichana kusoma elimu ya sekondari.
Waalimu wengi waliobaki hawalipwi kwa miezi kadhaa. Hatua za hivi punde huenda zinaibua hofu zaidi katika jamii ya kimataifa.
Marekani na mataifa mengine ya Magharibi walikuwa wameboresha elimu kwa wanawake nchini Afghanistan jambo ambalo Taliban ilipewa kama sharti la kutambuliwa rasmi kwa serikali yao.
Naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Robert Wood amelaani hatua za hivi karibuni za Taliban.
"Taliban hawawezi kutarajia kuwa wajumbe halali wa jamii ya kimataifa hadi watakapoheshimi haki za Waafghanistani wote ," alisema.
" Hasa haki za binadamu na haki za kimsingi za uhuru wa wanawake na wasichana."
Katika mwezi wa Novemba, mamlaka zilipiga marufuku wanawake kufika katika bustani za mji mkuu Kabul, zikidai kuwa sheria za Kiislamu hazikuwa zinafuatwa pale.

Chanzo cha picha, Getty Images
Suala linaigawanya Taliban
Uchambuzi na Yogita Limaye, Mwandishi wa BBC wa Kusini mwa Asia
Kumekuwa na uvumi kwa mwezi mzima sasa kwamba serikali ya Taliban itapiga marufuku elimu ya chuo kikuu kwa wanawake.
Mwanafunzi mmoja wa kike alibashiri hili wiki kadhaa zilizopita . "Siku moja tutaamka na watasema wasichana wamepigwa marufuku kusoma katika vyuo vikuu ," alikuwa amesema.
Na kwahiyo huku Waafghanistan wengu huenda walitarajia kwamba hivi karibuni zaidi au baadaye uamuzi huu utachukuliwa, bado umekuja kama wa kushitua.
Mwezi uliopita wanawake walizuiwa kwenda kwenye bustani za miji, katika maeneo ya mazoezi ya mwili (gym) na vidimbwi vya kuogelea .
Mwezi Machi mwaka huu, selikali ya Taliban haikutekeleza ahadi yake ya kufungua shule za sekondari kwa ajili ya wasichana.
Kutokana na mazungumzo na viongozi wa Taliban kwa kipindi cha mwaka uliopita , ni ushahidi kwamba kuna kutoelewqana ndani ya Taliban kuhusu suala la elimu ya wasichana.
Bila kurekodiwa, baadhi ya wajumbe wa Taliban wamekuwa wakirudia mara kwa mara klusema kuwa wanamatumaini na wanafanya juhudi za kujaribu na kuhakikisha wasichana wanapata elimu.
Wasichana waliruhusiwa kufanya mtihani wa kuhitimu masomo ya sekondari wiki mbili zilizopita, katika majimbo 31 kati ya 34 ya Afghanistan, ingawa hawajahruhusiwa kuwa shuleni kwa zaidi yam waka mmoja.
Hilo lilitoa tumaini dogo, ambalo kwa sasa limetoweka.















