Afghanistan: 'Wengi wetu tunaweza kuuawa - lakini tutashinda'

Chanzo cha picha, Getty Images
Asubuhi ya tarehe 30 Septemba, Mariam mwenye umri wa miaka 20 alikuwa akihangaika kufika katika kituo cha elimu cha Kaaj, katika eneo la Dasht-e-Barchi la Kabul, ambalo kwa kiasi kikubwa ni makazi ya watu wachache wa kabila la Hazara katika jiji hilo.
Wahida, rafiki yake wa karibu, alikuwa amempigia simu mapema asubuhi hiyo na kumwambia "Mbona bado umelala? Amka, tuna mtihani leo." Ulikuwa mtihani wa mazoezi katika maandalizi ya Concor, mtihani wa kujiunga na chuo kikuu nchini Afghanistan.
Wakati Mariam akielekea kituoni, Wahidah alimpigia simu tena kumtaka afanye haraka, akisema amemuwekea kiti. Saa 7:15 asubuhi, Mariam alipokuwa anawasili kituoni hapo alisikia mlio wa risasi.
"Kisha kulikuwa na mlipuko mbaya zaidi ambao sikuwahi kuusikia," anakumbuka. "Niliona wavulana wakikimbia nje ya kituo hicho, wakiruka ukuta wa mpaka wake. Sekunde chache baadaye, niliwaona wasichana wakikimbia pia. Wengi wao walijeruhiwa, wakiwa na damu usoni na katika nguo zao."
Mariam hakuruhusiwa kuingia katika kituo hicho lakini aligoma kwenda nyumbani. Aliendelea kumsubiri Wahidah atoke nje. Lakini hakutoka. Wahidah alikuwa miongoni mwa wanafunzi 45 wa kike waliouawa katika shambulizi hilo la kujitoa mhanga katika taasisi ya binafsi mnamo tarehe 30 Septemba.
"Alikuwa kama dada yangu. Tulifichiana siri zetu zote," Mariam anasema. "Wahidah hakukosa hata siku moja masomo ya maandalizi ya mtihani. Iwe mvua ilinyesha au theluji au kulikuwa na mafuriko, ingawa aliishi mbali zaidi na , alifika kila mara."

Chanzo cha picha, Getty Images
Siku hiyo ya Ijumaa asubuhi, babake Wahidah Mohammad Amir Hyderi alikuwa ameondoka kwenda dukani kwake mapema. "Sikumuona hata siku hiyo," anasema. "Alikuwa shujaa wa familia yetu, malaika wangu. Siku zote alifaulu shuleni. Na hata katika mtihani wa mazoezi mwezi uliopita, alikuwa mwanafunzi bora kati ya wanafunzi 650. Lakini sio tu kwamba alikuwa mwerevu, alikuwa mwenye tabia njema na mcha Mungu kiasi kwamba kila mtu katika jamii yetu alimpenda.
Kwa saa kadhaa baada ya mlipuko huo, Mohammad na Mariam walikwenda katika hospitali kadhaa wakimtafuta Wahidah. "Taliban hawakuturuhusu kuingia. Hatimaye katika hospitali ya Ali Jinnah, Mariam amelala ndani," Mohammad anasema, huku akilia akikumbuka siku hiyo. "Alitoka akilia na kwa uchungu dakika chache baadaye, akisema ameuona mwili wa Wahidah."

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tangu kundi la Taliban kunyakua mamlaka mwezi Agosti mwaka uliopita, wasichana wamezuiwa kwenda shule za sekondari katika sehemu kubwa ya Afghanistan, ikiwemo Kabul.
Wahidah alikuwa amemaliza shule ya sekondari mwaka jana, lakini alikuwa na wasiwasi kuhusu elimu ya dada zake wadogo. "Alikuwa ameanza kufundisha dada zake masomo yote yaliyofundishwa shuleni," Mohammad anasema.
Pamoja na vikwazo vya haki na uhuru wa wanawake kuongezeka chini ya Taliban, imekuwa wakati wa kukata tamaa kwa mamilioni ya watoto wa kike nchini humo.
"Kila nilipokuwa nikijisikia kukosa matumaini au sikuweza kupata motisha ya kusoma, niliishia kukosa masomo. Wahidah alikuwa akiniambia, 'nitakusaidia, usijali, lakini tafadhali njoo darasani," Mariam anasema.
Kwa wasichana wengi ambao wangekuwa katika shule za sekondari, vituo binafsi vya elimu ndio njia pekee ya wasichana hao kukamilisha siku na ndoto zao.
Afghanistan imeshuhudia mashambulizi mengi dhidi ya shule na maeneo ya elimu binafsi, hasa yale yanayotawaliwa na jamii ya Wahazara. Hakuna kundi hadi sasa ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo la Ijumaa iliyopita, lakini Jimbo la Khorasan la Kiislamu au ISKP - mshirika wa kikanda wa kundi la Islamic State - limedai kuwa ndilo lililohusika na mashambulizi ya awali.
Lengo la mashambulizi hayo ni kuwatisha, kuwavunja moyo na kuwakatisha tamii watoto wa kike wasishughulike na elimu.
'Nasubiri tu kituo kifunguliwe na nitarejea kwenye kozi yangu. Nilikuwa nahitaji motisha ya kuhudhuria masomo, lakini sasa ni dhamira na wajibu kwangu," Mariam anasema. "Lazima niendelee na elimu yangu, kwa ajili ya Wahidah, kwa Nazanin, Shabnam, Nargis, kwa Samira, kwa makumi ya marafiki zangu ambao waliuawa. Siku moja tutashinda."
Hana uhakika ni lini siku hiyo itakuja au kama itatokea katika maisha yake lakini ana uhakika itatokea hatimaye: "Labda wengi wetu tutauawa, lakini bila shaka tutashinda."












