Ukraine yasema ilipigana na wanajeshi wa Korea Kaskazini kwa mara ya kwanza

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanajeshi wa Korea Kaskazini wamepambana na wanajeshi wa Ukraine kwa mara ya kwanza, maafisa wakuu wa Ukraine wamefichua.
Katika mahojiano na shirika la utangazaji la Korea Kusini KBS, Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov alisema "kundi dogo" la wanajeshi wa Korea Kaskazini lilishambuliwa.
Kiongozi wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambaye hapo awali alilaani kutojibu kwa nchi za Magharibi kuhusu wanajeshi wa Korea Kaskazini, alisema "vita hivi vya kwanza na Korea Kaskazini vinafungua sura mpya ya ukosefu wa utulivu duniani".
Seoul, hata hivyo, ilisema "haiamini [wanajeshi wa pande zote mbili] kushiriki katika mapigano ya moja kwa moja", lakini kwamba kulikuwa na "tukio" lililohusisha idadi ndogo ya wanajeshi wa Korea Kaskazini "karibu na mstari wa mbele".
Ukraine inasema kuwa takribani wanajeshi 11,000 wa Korea Kaskazini walikuwa katika eneo la mpaka la Kursk, ambako wanajeshi wa Ukraine wamejikita.
Katika wiki za hivi karibuni, ujasusi wa Korea Kusini na Marekani pamoja na Nato umesema kuwa wameona ushahidi wa wanajeshi wa Korea Kaskazini kuhusika katika vita vya Urusi.
Lakini Moscow na Pyongyang hadi sasa hazijajibu moja kwa moja tuhuma hizo.















