Hezbollah yatangaza kulipua kituo cha jeshi la wanamaji la Israel na uwanja wa ndege wa kijeshi

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Hezbollah imetangaza siku ya Ijumaa kuwa imerusha makombora katika kambi ya jeshi la wanamaji la Israel na uwanja wa ndege wa kijeshi karibu na mji wa Haifa, kwa mara ya pili katika muda wa chini ya saa 24, huku kukiwa na makabiliano ya wazi kati ya pande hizo mbili kwa muda wa wiki saba.

Kundi hilo limesema katika taarifa yake kwamba wapiganaji wake walilenga kambi ya wanamaji ya Stella Maris, iliyoko kaskazini-magharibi mwa Haifa, kwa "msururu wa makombora ", ambayo ilisema ni pamoja na uchunguzi wa majini na ufuatiliaji.

Katika taarifa ya pili, chama hicho kiliripoti kwamba kililenga kambi ya Ramat David na uwanja wa ndege, kusini mashariki mwa Haifa, kwa msururu wa "makombora yenye ubora."

Alisema kuwa mashambulizi hayo mawili yalikuja "kujibu mashambulizi na mauaji yaliyofanywa na adui wa Israel" nchini Lebanon

Baada ya takriban mwaka mmoja wa kushambuliana kwa makombora katika mpaka wa Lebanon na Israel, Israel ilianza, kampeni kali ya anga dhidi ya maeneo ya Hezbollah katika vitongoji vya kusini mwa Beirut na kusini na mashariki mwa Lebanon.

Tarehe 30 ya mwezi huo, ilitangaza kuanza kwa mashambulizi machache ya ardhini kusini mwa nchi hiyo, ambapo inaanzisha mashambulizi na kujihusisha katika mapigano na Hezbollah.

Ongezeko la mashambulizi ya hivi punde limesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,600 nchini Lebanon, kati ya jumla ya zaidi ya 3,000 waliouawa na mashambulizi ya jeshi la Israel tangu mapigano yalipoanza kati ya Hezbollah na Israel Oktoba 8, 2023.

Hezbollah ilisema inakaribisha juhudi zozote za kusitisha vita, lakini "haiweki matumaini yoyote katika utawala maalum wa Marekani" kuhusu usitishaji mapigano nchini Lebanon.

Kauli hii imetolewa na Ibrahim al-Moussawi, mwanachama wa Kambi ya Uaminifu ya Hezbollah kwa Muqawama katika bunge la Lebanon alipokuwa akijibu swali kuhusu ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa rais wa Marekani.

Ushindi wa Trump unaweza kuwakilisha mabadiliko katika chama kilicho madarakani, "lakini Israel inafuata karibu sera sawa," Moussawi alisema na kuongeza: "Tunataka kuona hatua, na tunataka kuona maamuzi yakichukuliwa.

Pia unaweza kusoma

Ndege za kivita za F-15 za Marekani zawasili Mashariki ya Kati

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Jeshi la Marekani lilitangaza kuwasili kwa ndege za kivita za F-15 katika eneo la Mashariki ya Kati, wiki moja baada ya Washington kutangaza kutumwa kwa uwezo wa ziada wa kijeshi katika eneo hilo kama onyo kwa Iran.

Jeshi lilisema ndege hiyo, ambayo kwa kawaida huwa nchini Uingereza, iliwasili katika eneo la Kamandi Kuu ya Marekani.

Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilitangaza wiki iliyopita kwamba itatuma Makombora, wapiganaji, ndege za kujaza mafuta kutoka angani hadi angani na meli za ulinzi wa anga katika Mashariki ya Kati.

Pentagon ilionya wakati huo kwamba "ikiwa Iran au washirika wake watatumia wakati huu kulenga wanajeshi wa Marekani au maslahi katika kanda, Marekani itachukua hatua zote muhimu ili kujilinda."

Kwa upande wake, Ikulu ya White House ilisema, kupitia msemaji wake, kwamba Rais Biden ataendelea kutafuta suluhu nchini Lebanon kabla ya kuondoka madarakani Januari.

Awali, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken amekuwa akifanya vikao na idara mbalimbali kwa siku mbili ili kujadili kazi inayoisubiri idara hiyo katika muda wa siku 74 zijazo, hadi Januari 20.

Kupitia msemaji wake, Blinken alisisitiza katika vikao hivyo kuwa anakusudia kutumia muda uliobakia ofisini kwake ili kupata maendeleo yanayoonekana katika masuala kadhaa muhimu, ikiwa ni pamoja na kukomesha vita Lebanon na Ghaza.

Matukio ya mashambulizi Lebanon

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Jeshi la Lebanon limesema raia watatu waliuawa katika shambulizi la anga la Israel karibu na mji wa kusini wa Sidon ambalo lililenga gari wakati likipita kwenye kituo cha ukaguzi cha jeshi siku ya Alhamisi. Shambulizi hilo la anga pia limewajeruhi wanajeshi watatu wa Lebanon na wanajeshi wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa UNIFIL.

Jeshi la Lebanon limeongeza kuwa, wanajeshi waliojeruhiwa wa UNIFIL ni wa kikosi cha Malaysia, na kwamba walijeruhiwa wakati magari yao yakipita karibu na kituo cha ukaguzi wakati wa uvamizi huo.

Walinda amani watano waliowasili hivi karibuni walijeruhiwa katika shambulio la ndege isiyo na rubani karibu na msafara wao huko Sidon, kusini mwa Lebanon, UNIFIL ilisema katika taarifa, na kuongeza kuwa majeraha yao yalikuwa madogo na walitibiwa papo hapo.

Majeruhi katika upande wa jeshi la Israeli

.

Chanzo cha picha, Reuters

Jeshi la Israel lilisema wanajeshi watano kutoka Brigedi ya Nahal waliuawa na 16 kujeruhiwa katika vita kusini mwa Lebanon katika wiki za hivi karibuni, kulingana na taarifa iliyotolewa Alhamisi.

Katika muktadha unaohusiana, Idhaa ya 12 ya Israel iliripoti kwamba ving'ora vya mashambulizi ya anga vilisikika katika maeneo makubwa ya Haifa, Acre na miji mingine ya jirani, na makombora ya kuzuwia yalionekana katika anga ya eneo hilo.

Channel 12 iliongeza kuwa jengo la Haifa liliharibiwa na vifusi, na uharibifu pia ulionekana katika eneo la maegesho huko Kiryat Yam, karibu na Haifa.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na kuchapishwa na Seif Abdalla